Friday, 20 October 2017

Yanga yaipiga mkwala stand UTD

KOCHA MSAIDIZI WA KLABU YA YANGA, SHADRACK NSAJIGWA.
KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema maandalizi waliyoyafanya kuelekea mchezo wao dhidi ya Stand United ni ya kiwango cha juu na wenyeji hao wasitegemee urahisi.
Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Kambarage, ulioko Shinyanga keshokutwa ili kusaka pointi nyingine muhimu za kutetea ubingwa wanaoushikilia.
Akizungumza na gazeti hili jana kutoka Tabora walipokuwa wameweka kambi ya muda kujiandaa na mchezo huo, Nsajigwa, alisema kuwa, wamejiandaa vizuri na mchezo wao wa kirafiki waliocheza juzi dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora umewaongezea nguvu.
“Tulijiwekea mikakati katika michezo miwili ule wa Bukoba na huu tunaokwenda kucheza Shinyanga, tuondoke na pointi zote sita, tumefanikiwa mchezo wa kwanza, tunaenda Shinyanga kukamilisha kile tulichokianza Bukoba,” alisema Nsajigwa.
Aliongeza kuwa wanajua watakutana na ushindani kutoka kwa wenyeji wao, ambao watataka kutumia vyema uwanja wa nyumbani, lakini wamejipanga kuondoka na ushindi.
Kuhusu wachezaji watakaoanza kwenye mchezo huo hasa kuepuka wale wenye kadi mbili za njano ambao wanaweza wakapelekea kuukosa mchezo dhidi ya Simba, Nsajigwa alisema suala lipo chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina.
“Tuna siku ya leo (jana) kesho (leo) na Jumamosi kuangalia nani ataanza kwenye mchezo wa Shinyanga, tunafahamu tunatakiwa kuwa na tahadhari, si tu kwa kadi lakini pia kuepuka wachezaji wetu wasiumie kwa sababu ya mchezo wa Oktoba 28, hilo suala linafanyiwa kazi,” alisema Nsajigwa.
Wachezaji wa Yanga ambao wana kadi mbili za njano na wako katika hatari ya kuikosa Simba kama wataonyeshwa kadi yoyote Jumapili ni Kelvin Yondani na Juma Abdul.

No comments:

Post a Comment