Monday, 16 October 2017

Ndege ya AirAsia yageuka na kurudi Australia baada ya hofu ya hitilafu

Ndege ya shirika la Indonesia ya AirAsia imelazimika kugeuka na kurudi Australia baada ya marubani kujulishwa kuwa kulikuwa na tatizo la hewa katika eneo la abiria la ndege hiyo.
Ndege hiyo ya QZ535, iliyokuwa safarini kwenda kisiwa cha Bali nchini Indonesia, ilirudi Australia dakika 25 baada ya kupaa siku ya Jumapili.
Airbus A320 iliyokuwa na abiria 151 ilitua salama kwenye uwanja wa Perth, AirAsia ilisema kuwa ndege hiyo ilikumbwa na matatizo ya kiufundi, huku vyombo vya habari nchini Australia vikisema kuwa ilionekana kushuka.
Kanda ya video iliyorekodiwa na kupeperushwa na vyombo va hahari, ilionyesha vifaa vya hewa vikining'inia kutoka kwa dari la ndege.
AirAsia iliwaomba msamaha abiria kwa tatizo lolote lililosababishwa na hitilafu hiyo.
Mwezi Juni ndege ya AirAsia iliyokuwa safarini kwenda Bali, ililazimika kurudi uwanja wa Perth baada ya hitilafu ya injini yake kusababisha ndege hiyo kutingishika kama mashine ya kuosha.
Mwezi Disemba mwaka 2014 ndege ya AirAsia ilianguka baharini na kuwaua watu wote 162 waliokuwa ndani yake

No comments:

Post a Comment