Wednesday, 18 October 2017

Kauli ya Lissu Baada ya kutoka ICU

Dar es Salaam. Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Alute Mughwai ameeleza jinsi alivyomtoa mdogo wake chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kile ambacho alikisema mara tu baada ya kutoka ndani kwa mara ya kwanza.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Alute amesema Lissu mara baada ya kutoka si yeye pekee alifurahi hata ndugu zake waliokuwapo walifurahia tukio hilo.
“Manesi walipanga kumtoa nje Jumamosi (Oktoba 14) na kwa kuwa Lissu alijua tunakwenda, aliwaeleza wasimtoe wasubiri ndugu zake tufike, nilikuwa mimi na ndugu wengine,” amesema Alute
“Ilipofika saa 10 jioni tulimtoa na mimi ndiye nilimtoa ICU, alifurahi na sisi tulifurahi kwa hatua hiyo,” ameongeza
Mwananchi lilipotaka kujua, Lissu baada ya kutoka nje alisema nini, Alute amesema, “alifurahi kwa mara ya kwanza kupigwa jua, alisema ni sawa na ukiwa mfungwa huoni jua, mawingu wala hupigwi upepo ule wa kawaida.
Alute amesema Lissu alikaa nje karibu nusu saa kisha akarudishwa wodini ambako ameleeza ingawa si ICU lakini ina ulinzi na ungalizi wa karibu na si kila mtu anaweza kumwona.
“Kama alivyosema Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema- Freeman Mbowe) jana, anaendelea vizuri na ana akili ziko timamu.”
Kuhusu mchakato wa kumpeleka nje ya Nairobi ambao familia itahusika zaidi, Alute amesema: “Mimi nilikuwa Nairobi, ndiyo narudi nitatoa maelezo ya kipi kitafuata baada ya kuwasiliana na ndugu.”
Amesema ndugu wapo sehemu mbalimbali kama Kenya, Australia, Marekani, Canada ambao watabidi wajadiliane kwanza ndipo watatoa taarifa ya kinachoendelea.

No comments:

Post a Comment