Monday, 16 October 2017

Waziri Mkuu Amewaonya Mawaziri,,,,,

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya mawaziri na kuwataka watumie madaraka yao kwa manufaa ya Taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Kassim Majaliwa amesema hayo leo Oktoba 16, 2017 alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na Makatibu Wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Aidha Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi na kamwe wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya Uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.”
Waziri Mkuu amesema Mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI Bw. Suileiman Jaffo pamoja na Manaibu wake Bw. Joseph Kandege na Bw. George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile.
Wengine ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu wake Bw. Jumaa Aweso, Waziri wa Viwanda na Biashara Bw. Charles Mwijabe na Naibu wake Mhandisi Stella Manyanya.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na Naibu wake Bw. Josephat Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake Bw. William Ole Nasha, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Ulega pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.

No comments:

Post a Comment