Wednesday, 18 October 2017

Mtambo Wa kuchomea taka unavyohatarisha afya za wananchi Mkuranga,,,

Wakazi wa kijiji cha Dundani wilayani Mkuranga wako katika hatari ya kupata magonjwa yanayosababishwa na moshi mzito unaozalishwa na mtambo mkubwa wa kuchoma takataka za hospitali ulio jirani na makazi yao.
Uchunguzi wa Mwananchi umegundua kuwa mtambo huo mkubwa kuliko yote nchini kwa kazi hiyo ulijengwa kabla ya kufanyika kwa tathmini ya athari ya mazingira (EIA) na sasa umegeuka kero kwa wakazi hao. Mbali na uchomaji wa taka za hospitali, tanuru hilo linaloendeshwa na kampuni ya Safe Waste Incinerator linatumika pia kuchomea dawa zilizoisha muda wa matumizi na zile zinazogundulika kuwa si halisi (feki).
Kutokana na hali hiyo, wakazi wa Dundani wameziomba mamlaka zinazohusika kuingilia kati ili kunusuru afya zao na mazingira.
Kabla ya kiwanda hicho kuanza kuteketeza kiwango kikubwa cha taka hizo hakuna mkazi aliyehisi hatari iliyokuwa mbele, lakini sasa uteketezaji wa kiwango kikubwa umewafanya wakasirishwe.
Wakati mwekezaji huyo akijenga mtambo huo kati ya mwaka 2013 na 2014 hakukuwa na wakazi eneo hilo, lakini kwa sasa mtambo huo umezungukwa na makazi ya watu ambao sasa wanataka ama uhamishwe au zibuniwe mbinu mpya za kudhibiti moshi na harufu kali.
Kadhia hiyo imewaweka viongozi wa kisiasa na maofisa afya wilayani Mkuranga katika wakati mgumu kutokana na lawama za wananchi.
Malalamiko kila kona
“Hatujui hizi takataka ni kabila (aina) gani kwa sababu hatushirikishiwi na wala hajafika mwenye kiwanda kutuambia anachoma kitu gani,” alisema Mbarka Salumu mkazi wa Dundani.
“Ile harufu tunayoisikia ukisema ni mtu anachomwa ni sawa tu! Ukisema wadudu wanachomwa sawa! Na ukisema sumu inachomwa sawa tu kwa sababu ni harufu chafu kabisa.” Kwa mujibu wa Salumu, mtambo huo unapowashwa, moshi husambaa na kuingia mpaka ndani ya nyumba zao. “Tunataka tusaidiwe ili hii kero itutoke, ifike wakati huyu bwana atolewe sehemu hii ili tusidhurike,” anaongeza.
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linasema halijapokea taarifa rasmi kuhusu kero hiyo. “Hili tatizo tumelisikia juzi tu na ndio tunakwenda kukagua. Ni mpaka tutakapofika na kuona hali halisi ndipo nitakapokuwa katika nafasi ya kulizungumzia hili zaidi,” alisema ofisa wa NEMC, Alfred Msokwa.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ilimpa kibali mwekezaji kujenga mtambo huo, ambao hauwashwi kila siku kabla ya kufanyika kwa tathmini ya athari za mazingira. “Halmashauri zetu wakati mwingine huruhusu kujengwa kwa mitambo kama hii zikilenga kuongeza mapato na kusahau suala la mazingira na afya za watu. Wakati mwingine vibali vinatolewa katika ngazi ya halmashauri, halafu wanashindwa kuwasimamia,” alisema. Ofisa mmoja wa kampuni inayolalamikiwa aliyeomba kutotajwa jina, alisema wamepata malalamiko hayo kupitia vyombo vya habari, akisema ni “changamoto za kawaida katika biashara”.
“Tumepigiwa simu na watu kadhaa kutoka Mkuranga wakitaka tu-surrender documents (tusalimishe nyaraka). Tumewaandikia kutafuta muda mwafaka ili tukae na mamlaka zote husika na kuwajibu wanayoyataka kwetu kwa pamoja,” alisema ofisa huyo. Mkazi mwingine wa Dundani, Saidi Hamisi, alisema haelewi kinachochomwa.
“Ni kama (harufu) ya dawa za hospitali. Na watu ukiwauliza wengine wanasema zinachomwa simu za zamani, wengine wanasema dawa za hospitali zinazotoka Bohari Kuu, sasa hatuelewi ni kitu gani,” alisema. “Moshi ni mzito sana na harufu inayokuja inakuwa ya mchangayiko, sasa kwa kuwa lile bomba halijaenda juu sana ule moshi unaishia kusambaa chini.
“Kipindi alivyonunua huku palikuwa bado pori, kwa ushauri wangu kwa sababu huku mji umeshaingia basi hiki kiwanda kihamishwe au bomba liende hewani ili ule moshi unapotoka sisi tusiathirike.”
Kero ya moshi mzito na harufu kali imelalamikiwa pia na wanawake wakiwemo wajawazito.
“Harufu kama hii inatuumiza sana sisi wajawazito, tunaumia, tunaombwa tusaidiwe,” alilalamika mwanamke mjazito aliyeomba kutotajwa jina. Malalamiko ya mjamzito huyo yaliakisiwa pia na Rajma Saidi.
“Mtu unaweza kupika chakula na usikile kwa sababu harufu inayotoka huko ni mbaya kupita kiasi kwa hiyo tunakereka sana. Tunashukuru umefika ukatoe salamu huku hali si nzuri,” alisema Rajma
Ofisa msaidizi wa afya wilayani Mkuranga, Juma Shari alisema wamefuatilia malalamiko na kuthibitisha kuwa ni ya kweli.
“Kiwanda kipo kwa chini na maeneo ya makazi yako juu. Kwa hiyo katika uchomaji wao, moshi husambaa kwa urahisi zaidi kwenye eneo la makazi,” alisema Shari.

No comments:

Post a Comment