Wednesday 18 October 2017

Nassari Awavimbia Takukuru......

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), amepinga onyo alilopewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) la kutoweka hadharani taarifa anazowafikishia kuhusiana na flashi za tuhuma za rushwa na kusisitiza kuwa hataacha kufanya hivyo.
Akizungumza jana ikiwa muda mfupi baada ya kupata taarifa za onyo alilopewa na Takukuru, Nassari alisema haoni kama anavunja sheria kwa kuuarifu umma juu ya kila hatua anayoichukua kuhusiana na taarifa za rushwa anazozifikisha Takukuru.
Hivi karibuni, kwa nyakati tofauti, Nassari amekuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea anavyofikisha taarifa Takukuru kuhusiana na kile anachodai kuwa ushahidi juu ya tuhuma za rushwa za baadhi ya viongozi mkoani Arusha.
Jana, Takukuru kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola, ilitoa onyo lililotajwa kuwa la nne kwa mbunge huyo kuhusu mwenendo wake wa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya tuhuma za rushwa anazowafikishia na kumtaka kukaa kimya wakati uchunguzi wa suala lake ukiendelea.
Nassari amekuwa akiwasilisha kwenye ofisi za Takukuru ‘flashi’ na CD zenye video anazodai zinaonyesha jinsi viongozi wa serikali jijini Arusha walivyokuwa wakiwashawishi kwa rushwa madiwani kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili wahamie Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Siwezi kukaa kimya. Nitaendelea kuzungumza na vyombo vya habari… wananchi wana haki ya kupata taarifa,” alisema Nassari kuiambia Nipashe jana baada ya kusikia onyo alilopewa na Takukuru.
Katika hoja yake, Nassari alidai kuwa aliamua kuwasilisha ushahidi Takukuru kuthibitisha madai yake kwamba kuna madiwani wawili wa Chadema waliotangaza kujiunga na CCM hivi karibuni walishawishiwa kwa rushwa.
Nassari aliwasilisha kile alichodai kuwa ni ushahidi wa vitendo vya rushwa kwa mara ya kwanza Oktoba 2, 2017 akisindikizwa na wabunge wenzake wa Chadema, Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Godless Lema (Arusha Mjini). Alienda tena Takukuru kuwasilisha ushahidi wake wa pili Oktoba 4, 2017 kabla ya juzi kuwasilisha ushahidi wake wa tatu.
ONYO LA TAKUKURU
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mlowola alisema wameshamwonya Nassari mara tatu juu ya kitendo chake cha kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza kile kinachojiri wakati wa mazungumzo kati yao na mbunge huyo.
Mlowola alimtaka mbunge huyo kukaa kimya na ‘akome’ kuzungumzia suala hilo kwenye vyombo vya habari kwa sababu vinginevyo, anaweza anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Kamishna Mlowola alisema:
"Oktoba 2 mwaka huu, Nassari akiwa na wabunge wenzake Mchungaji Peter Msigwa na Godbless Lema, walikuja ofisini kwetu. Wakatoa taarifa zao na tukapokea… na tukawaambia hicho kilichowasilishwa tutafanyia kazi.
"Lakini kwa mshtuko baada ya kupokea taarifa, tukashangaa wanaongea na waandishi wa habari kuhusu kilichojiri wakati awali tuliwaambia tukio hili wasilifanye kisiasa. Na tuliwaonya wasiongee na waandishi.”
Mlowola alisema kuwa kwa mara nyingine, Oktoba 4, 2017, Nassari alifika tena Takukuru na kutoa maelezo kwao na alipotoka ofisini kwao, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza yale yaliyojiri kwenye mazungumzo yao, licha ya ukweli kuwa awali walishamkanya aache kufanya hivyo.
Alisema Oktoba 16 (juzi), Nassari alifika tena katika ofisi za Takukuru kuwasilisha taarifa zingine na alipomaliza, alifanya kitendo kile kile cha kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza hatua ambazo zimeshanza kuchukuliwa, ijapokuwa alipewa angalizo kwa mara nyingin e la kutokufanya jambo hilo.
“Tunamwonya Nassari, ameshaleta taarifa kwetu na atuache tufanye kazi kwa mujibu wa sheria na siyo kutushinikiza,” alisema Kamishna Mlowola na kuongeza:
“Natoa onyo lingine… endapo ataendelea na tabia hii tutazingatia sheria na tutachukua sheria dhidi yake, bila kuathiri taarifa yake aliyotupa kuifanyia kazi."
Mlowola aliongeza kuwa Sheria ya Takukuru inawapa mamlaka ya kufanya kazi kwa uhuru bila ya shinikizo.
Alisema Takukuru inapokea taarifa zinazohusiana na rushwa au makosa ya rushwa kutoka vyanzo mbalimbali vikiwamo vya wazi na vya siri.
Alisema taarifa wanaipokea kutoka kwa mtu yeyote na anaweza kuwa mtakatifu, shetani, mwendawazimu au mwenye akili timamu, lakini hatua ya kwanza kwao inakuwa ni kupokea taarifa na mengine hufuata baadaye.
Alisema Takukuru inapopeleleza huwa inaangalia kama kuna kosa limetendwa na kufikishwa katika chombo kingine kilichotengwa ambacho ni mahakama kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
“Hatukutarajia kuwa na drama (maigizo) na watu wanapaswa kufahamu kuwa Nassari ameleta taarifa na siyo ushahidi… ushahidi una sifa zake,” alisema Kamishna Mlowola.
Alibainisha kuwa kifungu cha 37 cha makosa ya rushwa, kinaeleza kuhusu makosa ya jinai yanayoweza kutendwa na mtoa taarifa.
Alisema Nassari alikuwa ni mtoa taarifa na Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa na kwamba kinyume chake, Nassari amejionyesha mwenyewe katika vyombo vya habari kuwa ndiye aliyewapatia taarifa.
“Tunachokiona sisi hapo, Nassari na wenzake wanataka kulifanya suala hili kama la kisiasa badala ya sheria. Tuzingatie sheria. Chombo chenye mamlaka tukiache kifanye kazi yake,” alisema Kamishna Mlowola.
Alisema kuihusisha Takukuru katika malumbano na ulingo wa kisiasa si vizuri kwa kuwa jukumu la Takukuru siyo kufanya siasa.
Alisema uchunguzi unaweza kuonyesha kilichotokea katika tukio hilo ni kosa au siyo kosa kwa kuwa inawezekana kuna makosa yanafanyika mtu akadhani ni ya jinai, kumbe ni makosa ya kawaida ambayo yanahitaji utaratibu mwingine wa kuyashughulikia.

No comments:

Post a Comment