Friday, 20 October 2017

Nassari ashangaa kuwaona viongozi ofisini


Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema kuwa bado anashangaa kuendelea kuwaona ofisini viongozi ambao aliowataja kwenye ushahidi wa kutumia rushwa kununua madiwani wa Chadema mkoani Arusha kwani watakuwa na nafasi kubwa ya kuharibu ushahidi huo. Mh. Nassari amesema kwamba hofu yake kwa viongozi hao ni kwamba watakuwa na nafasi kubwa ya kuuharibu ushahidi huo kwa kuwa bado wamekalia madaraka hivyo wanaweza kufanya lolote kuhakikisha ushahidi ulioneshwa unaharibika ikiwa ni pamoja na upelelezi kufanyika kwa mashaka. "Kinachonishikisha ni kuendelea kuwaona viongozi wale bado wapo ofisini. Huko nyuma tumeona watu wakiwajibika kisiasa pale wanapopata tuhuma kuhusu rushwa, huwa wanawajibika au kuwajibshwa. Hapa naona inakuwa ngumu kidogo kuhusu upelelezi wa kesi hii kufanyika . Mfano tunaona sehemu kwenye video Mkurugenzi anasikika akieleza ni namna gani ataelekeza wale madiwani waanze kulipwa kidogo kidogo lakini bado yupo ofisini hii inanisikitisha kwani upelelezi unakuwa na mashaka kidogo" Nassari Aidha Nassari amesema ameshangazwa na kauli ya Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola kwamba yeye anaingilia upelelezi wao na kudai kwamba anachoamini yeye ni kwamba hajavunja sheria wala hajaingilia upelelezi wao kwani anachokifanya ni kuutaarifu umma kila hatua anayokua anaifanya. Nassari ameongeza kwamba kauli zinazotolewa na Mlowola kama zina lengo la kumtia hofu basi kwake hofu hiyo anaamini haitafanya kazi kwake kwani kama ni kuzungumza na wanahabari wakati akiwa anapeleka ushahidi hataacha kwani huwa hazungumzii ushahidi alioubeba bali huwa anazungumzia hatua anazopiga. Pamoja na hayo Nassari amesema hawezi kuzungumza kama haki itapatikana au la bali anachoamini Takukuru ni taasisi inayojitegemea hivyo hawataona haya kutenda haki ili ijulikane wateule wa rais wana hatia au vinginevyo.

No comments:

Post a Comment