Friday, 1 December 2017

Nafasi za kazi leo Dec 1

TBA yasimamia Tanesco kuondoa vifaa vyao



Dar es Salaam. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye amepewa kazi ya kubomoa jengo la Tanesco Ubungo, leo Ijumaa ameanza kusimamia shirika hilo litoe madirisha, vitu pamoja na viyoyozi ili waanze kazi ya kubomoa kama ilivyoagizwa na Rais John Magufuli.

TBA imechelewa kuanza ubomoaji wa jengo hilo baada ya Tanesco kuomba waondoe wenyewe madirisha, milango na AC, kazi ambayo amepewa kuifanya mpaka leo Ijumaa jioni kabla ya ubomoaji kuanza.

Akizungumza na gazeti hili leo Ijumaa wakati uondoaji wa madirisha ukiendelea, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga amesema kazi waliyonayo ni kubwa lakini wamejipanga kuikamilisha kwa wakati.

"Mpaka sasa hatujapata mchoro wa jengo hili baada ya kujengwa, tunachofanya ni kupima na kuchora ili kuepusha madhara. Unaweza ukakata bomba la gesi hapa ikawa shida tena," amesema Mwakalinga.


Amesema suala kubwa wanalolizingatia kwenye ubomoaji huo ni usalama na kwamba watatoa mafunzo maalumu kwa wafanyakazi kuhusu kujikinga wakati kazi hiyo ikiendelea.

Amebainisha kwamba watabomoa jengo la mbele pekee bila kuathiri lile la nyuma. Hata hivyo, amekiri kwamba jengo litakalobaki litakosa mwonekano mzuri kwa sababu sehemu ya mbele inayobeba sura ya jengo itakuwa imeondolewa.

"Tutatumia teknolojia mbili katika kubomoa jengo hili ambazo ni manual na mechanical. Tungeweza kutumia njia ya kulipua lakini tumeona itaathiri shughuli nyingine za kiuchumi," amesema.

Mwakalinga amesema athari zitakazojitokeza wakati wa ubomoaji ni kelele pamoja na vumbi. Amesema wamefanya tathmini ya jengo na kuangalia athari za mazingira na kujiridhisha kwamba ni chache.

Kuhusu gharama za ubomoaji, Mwakalinga amebainisha kwamba bado hawajakubaliana kuhusu hilo lakini watakaa na Tanesco kuzungumza kuhusu gharama hizo.

"Sheria ya manunuzi ya umma inasema ukishampa mtu kazi bila kutangaza tenda mnapata fursa ya kukaa na kujadili gharama wakati kazi inaendelea. Kwa hiyo, tutakaa na kuzungumzia hilo, hii ni taasisi ya umma na agizo limetoka kwa Rais," amesema Mwakalinga.

Mke wa Kafulila kafunguka



November 30, 2017 Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA Jesca Kishoa ambaye pia ni Mke wa Mbunge wa zamani Kigoma Kusini David Kafulila amekuwepo kwenye headlines kwa zaidi ya wiki moja baada ya Kafulila kuhamia CCM na kumuacha CHADEMA.

Kupitia page yake ya Instagram Jesca ameandika yafuatayo…

UCHAGUZI HUU WA UDIWANI UTOSHE 
KUTOA PICHA HALISI YA TAIFA HILI KWA SASA.

Mungu katunyima binadamu kujua siri nyingi za dunia hii ili turudi kwake na kumtambua yeye peke yake kama Mfalme wa ulimwengu.

Ametunyima kuchagua wazazi wa kutuzaa (maana uwenda wengine wangetaka kuzaliwa na watu wa aina ya Trump au Dangote,) ametunyima kuchagua wapi pa kuzaliwa (maana wengine uwenda wangetamani kuzaliwa ulaya na sio Tanzania)

Ametunyima kuchagua malezi ya kulelewa na ndio maana kwa mazingira yoyote watoto wamekuwa wakiishi kutegemeana na mazingira ya wazazi.

Lakini Mungu ametupa nguvu moja kubwa ambayo ikitumika vema huleta matunda mema na majibu ya mambo yote niliotaja juu, Mwenyezi Mungu katika maandiko matakatifu amezitambua Serikali za wanadamu na kupitia hizo endapo kutapatikana viongozi sahihi waliochaguliwa na wengi, ambao kwa uwingi huo ni alama au tafsiri ya chaguo la Mungu, hakika nchi itaneemeka na itatulia.

Ikiwa kinyume chake kwamaana ya alieshinda kuanzia mbinguni sie aliepewa ushindi duniani hakika mambo hugeuka kuwa laana na mateso kwa viumbe wa Mungu, Anguko la Madiwani au Wabunge wanaoshinda chaguzi sio la kwao peke yao na vyama vyao ni anguko la watu wa Mungu waliopaza sauti zao kwa unyenyekevu kupitia sanduku la kura.

WOTE KWA PAMOJA TUKEMEE VIKALI UPINDISHAJI WA MATOKEO BILA KUJALI WEWE NI NANI NA UNA UHUSIANO GANI NA SIASA ZA NCHI ILI KULIOKOA TAIFA HILI.

Roho mtakatifu ana uwezo mkubwa na nafasi kubwa ya kunyoosha mambo sawasawa, ungana na mimi katika maombi maalum juu ya taifa hili usiku huu kabla hujalala popote ulipo – hayo ndio aliyoyaandika Jesca.


Wakwanza kupandikizwa Figo Muhimbili Aruhusiwa


Dar es Salaam. Mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prisca Mwingira  ameruhusiwa kurudi nyumbani leo Ijumaa baada ya kuwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari bingwa wa figo kwa siku 10.

Prisca (30) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mikese mjini Morogoro, amechangiwa figo na mdogo wake Batholomeo Mwingira (27).

Akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa mara baada ya kutoka chumba cha uangalizi maalum (ICU), Prisca ameishukuru Serikali kugharamia matibabu yake na kuiomba kuwekeza zaidi katika matibabu ya kibingwa ili kusaidia Watanzania wengi wasio na uwezo wa kufuata gharama nje ya nchi.

“Kwa kipekee napenda kumshukuru sana ndugu yangu, kaka yangu Batholomeo kwa kupenda niendelee kuishi. Madaktari bingwa wa figo Muhimbili tangu wamenipokea wamekuwa wakinipa matibabu mbalimbali, nimesafishwa damu kwa muda wa mwaka mmoja wamenishauri na mpaka katika matibabu ya kupandikiza figo nyingine,"


Serikali yakanusha haijatoa ruhusa chuo kikuu huria kutoa kozi ya foundation



Singida. Serikali imesema  haijatoa ruhusa  Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.

Baadhi ya mitandao imetoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: “Waziri Mkuu aruhusu kozi za 'Foundation' Chuo Kikuu Huria” kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu amesema  Serikali bado inafanyia maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.

“Kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” amesema

“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea kuiboresh’’amesema

Ameongeza kwamba ‘’ Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” amesema

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda amesema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi za Foundation katika chuo hicho.

“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” amesema Prof. Bisanda.

Hizi ndizo sababu za Wema Sepetu kutamani kufa


“Kuna muda mwingine huwa natamani Allah Subhannah Wata’allah anichukue tu…Ya Dunia ni mengi sana….Kuna muda mwingine ninakufuru Mwenyezi Mungu na kutamani labda hata nisinge-exist (nisingekuwepo)… Ila acha niendelee kumtegemea yeye…

“Kila jambo hutokea kwa sababu….Hili nalo litapita… I think I need a time off social media (Nafikiri nahitaji kupumzika kwenye mitandao ya kijamii) kwa mara nyingine tena…. Siwezi jamani…”

SABABU YA KWANZA

Katika uchunguzi uliofanywa na Ijumaa, umebaini moja ya sababu zilizompelekea bidada huyo kuanika waraka huo wa kifo ni pamoja na kesi yake ya madawa ya kulevya inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.

Tangu kesi yake hiyo ya kukutwa na kutumia madawa ya kulevya ilivyoanza mwanzoni mwa mwaka huu, Wema amekuwa mtu wa nenda rudi mahakamani ambapo mpaka sasa imetajwa tena Desemba 14, mwaka huu.

Kutokana na uwepo wa kesi hiyo, mara kwa mara amekuwa akiongelewa tofauti mitandaoni jambo linalomchafulia jina na heshima yake na kitendo hicho kinaonekana kumchosha na kuamua kutoa waraka huo mzito.

SABABU YA PILI

Sababu nyingine inayoonekana wazi imempelekea kuandika waraka huo ni ishu ya kisiasa inayoendelea ya wanachama wengi kuhama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alichopo yeye na mama yake, Mariam Sepetu na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uchunguzi umebaini kuwa, Wema na mama yake walipohamia Chadema walikuwa na imani kubwa ya kukiimarisha chama hicho, lakini kitendo cha baadhi ya wanachama kukihama chama hicho na kurejea CCM kimemkatisha tamaa na kumfanya awe njia panda na kushindwa kuamua kama abaki au aondoke.

SABABU YA TATU

Inaeleweka kuwa Wema hakuwa mtu wa kutulia na mpenzi mmoja na hiyo ilitokana na tabia za kila mwanaume anayekuwa naye katika mapenzi.

Katikati ya mwaka huu, Wema aliamua kuanzisha uhusiano na mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Bakari na baadaye picha za wawili hao wakiwa kimahaba zikavuja.

Bila kujua kitu, Wema aliona amepata sehemu ya kupumzikia na kwamba kwa Bakari angeweza kumfuta machozi yote kwa sababu alikuwa na kila alichokihitaji lakini hali ikawa tofauti ambapo jamaa huyo alikuja kukamatwa na kuwekwa nyuma ya nondo huko Mombasa, Kenya kwa kukutwa na madawa ya kulevya.

SABABU YA NNE

Sababu nyingine iliyopeleka kuchapa waraka huo wa kifo ni kitendo cha kupishana na madili baada ya kubainika kuwa ana kesi ya madawa ya kulevya.

Ikumbukwe kuwa, Wema alitakiwa kushiriki moja kati ya tamthiliya kubwa nchini itakayoanza kuonekana hivi karibuni akiwemo na Irene Uwota na Elizabeth Michael ‘Lulu’ lakini shavu hilo likapita pembeni baada ya kubainika kuwa kesi yake ya madawa itachelewesha zoezi la kuandaa kwa kuwa atakuwa anakosa muda wa kuhudhuria lokesheni.

SABABU YA TANO

Kwa muda mrefu amekuwa akiumizwa na maneno ya watu kumsema kushindwa kupata mtoto. Amekuwa akiandamwa mara kwa mara kila anapokuwa katika uhusiano wake kiasi cha kufikia hatua ‘kufeki’ kuwa amepata mimba.

Mara nyingi amekuwa akiposti picha za watoto na kuonesha hisia zake kwa uchungu kutokupata mtoto na pia alishawahi kuweka picha akiwa na mama yake na kuandika; “Ipo siku nami nitaitwa mama.”

Licha ya kufanya vyote hivyo, amekuwa mtu wa kuandamwa kwa kukejeliwa na matusi.

Hapa tumekuanikia kurasa za mbele na za nyuma za magazeti yote ya Tanzania leo, Dec 1, 2017. Ni yale ya Hardnews, Udaku na Michezo.


VIDEO: CUF ya Lipumba yatoa tamko


Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa chama cha wananchi (cuf) Jafari Mneke amesema kuwa mwaka 2015 vyama vya upinzani viliunganisha nguvu zao pamoja ili kufikia lengo la kuitoa CCM madarakani lakini mpango huo ulivurugwa na Chadema.
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI....USISAHAU KUSUBSCRIBE



Tanesco wathibitisha umeme kurejea



Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema huduma ya umeme imerejea saa 7.11 mchana nchi nzima isipokuwa mkoa wa Mbeya.

Huduma ya umeme ilikatika tangu jana katika mikoa yote iliyounganishwa katika gridi ya taifa.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa mchana, Desemba 1, 2017 na Kaimu Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Leila Mhaji imesema mkoa wa Mbeya ndiyo pekee ambao huduma hiyo haijarejea kutokana na hitilafu iliyopo katika njia ya Mufindi.

Amesema mafundi wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inarejea katika mkoa huo kama ilivyo kwenye mikoa mingine.

“Tutaendelea kuwajulisha mara huduma hiyo itakaporudi kwani mafundi wanaendelea na kazi,” amesema. Amesema mapema leo huduma hiyo ilianza kurejea katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Tanga

Aidha amewaomba radhi wateja kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Amesisitiza wananchi kutoshika wala kukanyaga waya uliokatika au kuanguka.

Mama Samia atoa neno kwa wasichana wanaojiuza




MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Desemba 1, 2017 amewaongoza wakazi wa Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijiji Dar.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Samia amewaasa vijana kuacha kujihusisha na ngono zembe ili kuepuka kuendelea kuambukizwa ukimwi na kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari duniani kote.

Aidha, Makamu wa Rais amewataka akina dada wanaofanya biashara za kuuza miili yao kingono (machangudoa) kuacha mara moja kwani kufanya hivyo kutapelekea kupoteza nguvu kazi la kesho.

Kitaifa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yamefanyika leo katika Mkoa wa Lindi ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaongoza Watanzania wote katika katika maadhimisho hayo..

Waziri Mwanjelwa amsimamisha kazi Ofisa wa Pareto



NAIBU Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa, amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kumsimamisha kazi Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, anayesimamia zao la pareto, Emmanuel Halinga ili kupisha uchunguzi.

Agizo hilo alilitoa juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Jojo, Kata ya Santilya akiwa kwenye ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM) na wananchi wote waliokuwapo kwenye mkutano huo wa hadhara kumrushia shutuma nzito na kumkataa mtaalamu huyo.

Dk. Mwanjelwa, alisema kuwa pamoja na zao hilo la pareto kuwa la kwanza kwa uzalishaji katika nchi za Afrika, huku likiwa la pili kwa uzalishaji duniani, lakini bado halijamkomboa mkulima nchini jambo ambalo linaonyesha namna ambavyo baadhi ya wataalamu wa kilimo wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Alisema kuwa wataalamu wa kilimo walipaswa kusimamia kwa kiasi kikubwa zao hilo kwani pato lake ni wastani wa tani 2,000 kwa mwaka sawa na Sh bilioni 12 hadi 14 na katika kipindi hiki bei ya kuanzia mkulima analipwa Sh 2,300 kwa kilo hadi 3,300 kulingana na ubora wa zao hilo.

Dk. Mwanjelwa, alitoa siku saba kwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini, Lucas Ayo, kutoa sababu za kwanini mnunuzi ni mmoja wa zao hilo jambo ambalo linaonyesha kuwa na harufu ya rushwa au kusababisha kudumaza soko la zao hilo kwa kuwa na mnunuzi mmoja asiyekuwa na ushindani.

“Mkishaanzisha tu vikundi vya vyama vya ushirika, mtoe taarifa mapema iwezekanavyo na Serikali kupitia mrajisi itatoa elimu ya ushirika,” alisema Dk. Mwanjelwa.

Ameagiza zao la pareto kuwa huru ili mkulima awe huru kuuza kwa mnunuzi anayemtaka kwani kwa sasa kuna mnunuzi mmoja tu ambaye anajipangia mwenyewe namna ya kununua zao hilo kwa gharama atakazo.

Rostam wakanusha kuimba matusi

Msanii wa muziki Bongo, Stamina amesema ngoma ya ‘Kiba_100’ haina matusi kama baadhi ya watu wanavyodai.                                                                                               

Kiba_100 ni ngoma ya Roma na Stamina (Rostam) ambayo kwa sasa inafanya vizuri. Akizungumza na XXL ya Clouds Fm Stamina amesema hata wale wanasema ngoma hiyo inastahili kufungiwa wanakosea.

“Ukisema hiki kitu kifungiwe, je kifungiwe kwa sababu gani ukiangalia hatuja tukana, hakuna tusi ambalo lipo cleared ambalo mtu anaweza kusema hili ni tusi, hakuna tusi tulilotukana” amesema Stm

“Sisi wenyewe katika uandishi tulifuata maadili ya kutofikisha vitu vingine kwa sababu ya ukali wa maneno, ukisema wimbo ufungiwe ni sawa na kusema niache kazi yangu ya muziki, halafu kuna kuwa hakuna uhuru wa msanii kwa sababu kuna vitu unashindwa kuvifikisha, kama umeongea kitu ambacho kina ukweli acha kifike” amesisitiza.

Kiba_100 ni ngoma ya pili kwa Rostam kutoa baada ya kufanya vizuri na ngoma ‘Hivi Ama Vile’.

Wachaga kuanza kuchunguzwa na TAKUKURU



Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro (Takukuru), imeanza kuchunguza utamaduni wa familia za kabila la Wachaga za kutumia majani kufunika au kumaliza kienyeji kesi zinazohusu ukatili wa kijinsia na mimba za wanafunzi.

Majani hayo maarufu kwa jina la Sale/Masale kwa mila na tamaduni za kabila la Wachaga, hutumika kuashiria amani, kuomba msamaha na kumaliza tofauti zao na mara nyingi hutumika pale kunapokuwa na matatizo baina ya pande mbili.

Ofisa wa Takukuru Wilaya ya humo, Denis Mazigo amefichua siri hiyo ya kuanza kwa uchunguzi dhidi ya mila hiyo wakati wa uwasilishaji ripoti ya Kamati ya Ulinzi wa Mtoto.

“Haliwezi kutangulizwa jani la sale peke yake, lazima kuna mazingira ya kutolewa kwa fedha kama rushwa, ndiyo msamaha uweze kukubalika.

"Sasa sisi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa tumeanza kufanyia kazi jambo hili, kwa sababu tumeona kesi nyingi za ukatili zikikwama huku zikiwa na ushahidi wa kutosha.” amesema Mazigo.

Wilshere hatihati kucheza Kombe la Dunia



Kocha wa timu ya Taifa ya England, Gareth Southgate amemuweka katika mazingira magumu kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Jack Wilshere.

Mchezaji huyo anasubiri simu ya kocha huyo wa timu ya Taifa ya England kumjumuisha katika kikosi cha Kombe la Dunia mwakani nchini Russia.

Ingawa Wilshere anajipa matumaini ya kuwemo katika kikosi hicho, lakini Southgate amemtaka kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Arsenal.

Mchezaji huyo anahaha kupata namba kikosi cha kwanza Arsenal, baada ya kurejea kutoka Bournemouth alikokuwa akicheza kwa mkopo.

“Simu yangu haikua wazi siku zote, Jack anatakiwa kupata nafasi Arsenal. Amesugua benchi katika mechi nyingi, hivyo napaswa kumchunguza, “alisema Southgate.