Friday, 26 January 2018

NEC yatoa orodha ya wagombea wa udiwani



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa majina 27 ya wagombea udiwani walioteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwania nafasi hizo katika kata 10.

Uchaguzi mdogo katika kata hizo utafanyika Februari 17,2018 kutokana na baadhi ya madiwani kujiuzulu nyadhifa zao na vifo.

Katika uteuzi huo wanaume waliojitokeza kugombea nafasi hizo ni 24 na wanawake ni watatu.

Taarifa iliyotolewa na NEC leo Ijumaa Januari 26,2018 imesema wagombea wa kata nne waliteuliwa Januari 20 na wengine wa kata sita waliteuliwa Januari 24,2018.

Wagombea waliojitokeza kuwania udiwani katika kata ya Buhangaza iliyoko wilayani Muleba mkoani Kagera na vyama vyao ni Jenitha Tibihenda (CCM), Nelson Makoti (Chadema) na Grayson Aniceth (NCCR Mageuzi).

Katika Halmashauri ya Siha iliyoko mkoani Kilimanjaro ambako kuna kata tatu zitakazofanya uchaguzi mdogo, wagombea katika kata ya Gararagua ni Zakaria Lukumai (CCM) na Agness Lasway (Chadema). Kata ya Donyomuruak wagombea ni Lwite Ndossi (CCM) na Daniel Molle (Chadema), wakati katika kata ya Kashashi wagombea ni Suzan Natai (CCM) na Immanuel Saro (Chadema).

Mkoani Mwanza ambako kuna kata mbili, wagombea wa kata ya Kanbyelele iliyoko Halmashauri ya Misungwi ni Marco Yela (ACT Wazalendo), Daniel Makoye (CCM) na George Mhoja (Chadema). Kata ya Isamilo iliyoko wilayani Nyamagana wagombea ni Nyamasiriri Marwa (CCM), John Kisyeri (Chadema), Hashim Ramadhan (CUF), Georgina Kibendegele (DP) na Ramadhani Mtoro (UDP).

Kwenye kata ya Mitunguruni iliyoko wilayani Singida wagombea ni Abdallah Mkoko (CCM), Manase Kijanga (Chadema) na Abdallah Kinga (CUF).

Wagombea wa Kata ya Madanga iliyoko wilayani Pangani mkoani Tanga ni Mohamed Abdallah (ACT Wazalendo), Athuman Tunutu (CCM) na Swaibu Mwanyoka (CUF).

Mkoani Dodoma ambako pia kata mbili zitafanya uchaguzi, kata ya Manzase iliyoko wilayani Chamwino wagombea ni Amos Mloha (CCM), Alex Chalo (Chadema) na Ndahani Mazengo (Chaumma), wakati kata ya Kimagai wilayani Mpwapwa mgombea ni Noah Lemto aliyepita bila kupingwa.


Hospitali ya Bugando yanufaika na mashine za CT-SCAN


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amezindua huduma za mashine ya CT – SCAN katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando jijini Mwanza,ambazo zilisimama kwa muda wa miaka minne iliyopita, baada ya mashine iliyokuwepo awali kuharibika mwaka 2014.

Mashine hiyo ya kisasa,iliyonunuliwa nchini Ujerumani kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.7,imesimikwa na kufanyiwa majaribio na uhakiki kutoka tume ya mionzi Tanzania na kuthibitika kuwa na uwezo wa kufanya kazi ipasavyo.Mashine hiyo kwa mujibu wa daktari bingwa wa mionzi Dk.Godfrey Kasanga itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku.

Askofu wa jimbo katoliki la Geita,Mhashamu baba askofu Flavian Kasala,ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa bodi ya uendeshaji ya hospitali hiyo,Mhashamu Askofu Mkuu jimbo kuu la Mwanza Yuda Thadei Rwaichi,amewataka watumishi wa kitengo kitakachosimamia huduma za mashine hiyo kuitunza na kuacha kuihujumu.

Kwa upande wake,Mkurugenzi mkuu wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya ziwa Bugando Dk.Abel Makubi ameiomba serikali kuanzisha taasisi ya moyo katika hospitali hiyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wanaokwenda Dar es Salaam kutafuta matibabu ya moyo katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.


Wazazi wavamia shule kudai kurejeshewa michango yao


Baadhi ya wazazi katika halmashauri ya mji wa wa Mbinga mkoani Ruvuma wameshindwa kulielewa agizo la Rais John Magufuli la kufuta michango katika shule za msingi na sekondari na  kuvamia shule wakidai kurejeshewa michango yao.

Kufuatia hali hiyo Baraza la halmashauri ya mji wa Mbinga limeitisha kikao cha dharura kujadili changamoto hizo na nanmna ya kuzitatua huku Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Mbinga Donald Msigwa akiwataka madiwani kutopingana na agizo la Rais katika majadiliano hayo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mheshimiwa egno Kipwere amesema agizo la Rais halijahalalisha wananchi kudai kurejeshewa michango waliyochangia na halijafuta michango waliyokubaliana wenyewe kuchangia.

Wenger ajigamba kuhusu usajili wake


Kocha wa Arsenal Arsene Wenger amesema timu hiyo haitauza mchezaji bila kununua mchezaji huku pia akiongelea usajili wa Aubameyang kuwa bado haujakamilika.

Kocha huyo mkongwe ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa ripoti ya majeruhi na programu za timu kwa ujumla, ambapo amesisitiza nyota wake Olivier Giroud hauzwi kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa.

''Kwasasa hauzwi mchezaji yoyote bila kununua mchezaji wa kuchukua nafasi yake, tumemuuza Sanchez lakini tumempata Mkhitaryan hivyo timu iko vizuri na kikosi cha wachezaji waliopo'', amesema Wenger.

Pia Mfaransa huyo ameongeza kuwa milango pekeee itakayokuwa wazi ni kwa timu za vijana ambapo kuna baadhi watatolewa kwa mkopo na wengine watapandishwa kwenye kikosi cha wakubwa.

Kuhusu kumsajili nyota wa Gabon na Borussia Dortmund Pierre Aubameyang, Wenger amesema bado hawezi kusemea lolote kwasababu hakuna kilichokamilika na mchezaji huyo bado ni mali ya Dortmund.



Kumbe CCM wenyewe wanasubiri kuapishwa tu?

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amefunguka na kusema kuwa wagombea wa Ubunge kupitia chama chake katika uchaguzi wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha wanasubiri kuapishwa tu na kuingia bungeni.

Polepole amesema hayo alipokuwa akihojiwa na moja ya kituo cha habari na kusema kuwa kwa jinsi ambavyo wana CCM wamefanya kazi nzuri sana Kinondoni na Siha kuhakikisha wanawanadi na kuwauza wagombea wao hivyo wana uhakika wa kushinda uchaguzi huo kwa kishindo.

"Kwa utafiti tunaofanya na kazi nzuri tuliyofanya tunasubiri kutangazwa washindi katika majimbo yote mawili pale Kinondoni na Siha" alisisikika Polepole akisema

Mbali na hilo Polepole amekanusha chama hicho kuwa na mvurugano wa wenyewe kwa wenyewe kufuatia kusimamisha wagombea katika majimbo hayo ambao hawana muda mrefu katika chama hicho wakitokea upinzani na kusema kwa CCM kila mwanachama ana haki sawa na wanachama wengine.

Chama Cha Mapinduzi kimemsimamisha Maulid Mtulia kugombea Ubunge kwa jimbo la Kinondoni wakati katika jimbo la Siha kimemsimamisha Dk Godwin Mollel ambao wote walikuwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokea vyama vya upinzani, lakini walijivua uanachama kwenye vyama vyao na kujiunga na CCM.

Unaambiwa kesho Simba wataishangilia Yanga



Watani wa jadi Simba na Yanga, kesho Jumamosi watakuwa kitu kimoja kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaowakutanisha Azam na Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Watani hao watakuwa kitu kimoja kwani Simba inahitaji kuendelea kukaa kileleni bila ya wasiwasi, huku Yanga ikihitaji kuzisogelea timu zilizokuwa juu yake katika harakati zake za kutetea ubingwa wa ligi hiyo.

Kwenye msimamo wa ligi hiyo, Simba inaongoza ikiwa na pointi 32, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30, huku Yanga ikiwa na pointi 25 katika nafasi ya tatu.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, amesema: “Tumesikia Simba kesho watakuja kutushangilia, niseme tu hii si mara ya kwanza wao kutushangilia, wameshatushangilia mara nyingi, ni jambo jema, sisi ni watani wa jadi na hakuna uadui kati yetu.

Wanaovamia Maeneo Ya Serikali Kukiona Cha Moto Dar


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka wananchi wanaopenda kuvamia maeneo ya Serikali yakiwemo maeneo ya shule kuacha na kuondoka mara moja kwani hatua Kali za kisheria  dhidi yao zitachukuliwa ikiwa pamoja na kufikishwa mahakamani.

Makonda amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, alipokuwa anazindua uezekaji paa wa Ofisi za Walimu katika shule ya Msingi Mapinduzi iliyopo katika manispaa ya Kinondoni  na kusema kuwa kutokana na shule kutokuwa na uzio watu  wamekuwa wakijiamulia kujenga au kufanya makazi katika maeneo ya shule kitendo ambacho si sahihi.

"Wale wanaojipangia kuhamia au kuvamia maeneo yaaliyo wazi ya Serikali yakiwemo maeneo ya shule, hospitali na mengineyo  na kufanya makazi  kuacha mara moja tabia hiyo kwani kwa kufanya hivyo hatua Kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kufikishwa mahakamani".Amesema Makonda.

Amesema watu wakihamia na kujenga maeneo ya shule watoto wao watasomea wapi hivyo tujiulize  kuvamia maeneo ya shule na kujenga ni kosa na wanaofanya hivi wachukuliwe hatua na kufikishwa mahakamani kwa yeyote atakaye uza au kununua maeneo hayo.
Aidha amesema wanaboresha mazingira ya kazi kwa walimu ikiwa ni kuendelea kusupoti kauli ya Rais Magufuli ya Mpango wa Elimu bure bila malipo wameamua kuboresha mazingira ya kazi kwa Walimu katika Mkoa huo kwa kujenga ofisi zipatazo 402,ambapo Leo Amezindu uzwkaji Paa katika ofisi hizo katika shule hiyo manispaa ya Kinondoni.

"Lazima mpishi awe anapika vizuri ili walaji waweze kula ivyo tunaboresha mazingira ya walimu wetu ili waweze kufanya kazi kwa uledi na ufanisi mkubwa ili watoto wetu waweze kufaulu vyema"Amesema

Kwa  upande Meya wa Mnispaa ya Kinondoni Mhe.Benjamani  Sitta memshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuangalia suala la Ofisi pamoja na nyumba za kwa Mkoa huo kwani ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa walimu walikuwa hawana ofisi kitendo kinachopelekea walimu kukaa chini ya miti na kufanya kazi zao.




VIDEO: Makonda Ampigia Debe Mtulia


Mkuu wa Wa Mkoa wa Dra es salaam Paul Makonda amewataka Wananchi katika jimbo la Kinondoni kuamchagua mgombea ambae atatekeleza ahadi na kero zao, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa anazindua uezekaji paa wa Ofisi za Walimu katika shule ya Msingi Mapinduzi iliyopo katika manispaa ya Kinondoni.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI.......USISAHAU KUSUBSCRIBE

Breaking News: Tido Mhando afikishwa kizimbani Leo


ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Tido Mhando amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar leo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa TBC.


Mourinho aongeza Mkataba Man U


Kocha Jose Mourinho sasa ataifundisha Manchester United hadi mwaka 2020.

Mourinho raia wa Ureno ameongeza mkataba huo wa miaka mitatu kwa mwaka mmoja zaidi.
Pamoja na kwamba mashabiki wamekuwa wana hofu huenda ataondoka lakini uongozi unaonekana kumuamini zaidi.

VIKOMBE ALIVYOBEBA AKIWA NA UNITED:

Community Shield (2016)
League Cup (2016-17)
Europa League (2016-17)

Huu ndio ujumbe wa Mh.Lema kwa Jaji Mkuu wa Tanzania


Baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Juma kuwataka wanasiasa na viongozi wa serikali wenye mamlaka ya kikatiba na sheria kutoingia utendaji wa Mahakama na kuheshimu Muhimili huo. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema Mahakama ambayo ni imara katika haki inawezaje kukubali kuingiliwa?.

Lema amemwambia Jaji Mkuu huyo kuwa Mahakama inapaswa kujitazama zaidi huku akimueleza kuwa Mahakama ikiyumba taifa limeyumba pia.

“Mh Jaji Mkuu kauli kuhusu wanasiasa na Watendaji wa Serikali kutokuingilia Mahakama ni kauli muhimu kwa wkt huu, lakini Mahakama ambayo ni imara ktk haki inawezaje kukubali kuingiliwa ?Mahakama inapaswa kujitazama zaidi.Mahakama ikiyumba Taifa linayumba,” ameandika Lema kwenye mitandao yake ya kijamii.

Jaji Ibrahimu alisema hayo, January 23 mwaka huu jijini Dar es salaam, wakati akifafanua siku ya maadhimisho ya siku ya sheria nchini yatakayoadhimishwa Februali Mosi Mwaka huu.

Nelly atetewa na Mpenziwe kuhusu kesi ya ubakaji

Msanii wa muziki nchini Marekani Nelly, huwenda akapona katika sakata linalomkabili la kumfanyia unyanyasaji wa kingono binti mmoja wakatiwa tour yake mwaka 2017.

Mpenzi wa msanii huyo Shantel Jackson, ameeleza kuwa mwanadada anayedai kubakwa na rapper huyo sio kweli kwani hata yeye alikuwepo katika eneo la tukio hilo ila alikuwa chumba cha kubadilishia nguo.

“Ni kweli mimi na Nelly tulikoseana ila hawezi kufanya tendo la ubakaji,” ameeleza mrembo huyo.

Monique Greene  ndiyo  mrembo anayedai kufanyiwa ubakaji na rapper huyo katika gari  la Tamasha maeno ya Washington, na sasa wanawake wengine wawili wameibuka na kudai kufanyiwa kitendo kama hicho na msanii huyo.

Maelezo ya mpenzi wa Nelly, Shantel Jackson:

Wanaume watatu waliokunywa dawa za kuongeza nguvu za kiume walazwa hospitali



Wanaume watatu waliokunywa dawa za kuongeza nguvu za kiume huko nchini Zambia  wamejikuta wakilazwa hospitali baada ya kuanza kutapika nakuharisha mfululizo baada ya kutumia dawa hizo.

Vyombo vya habari nchini Zambia vimeeleza kuwa wanaume hao walilazwa kwa makosa kwenye vituo vya zahanati za kuhudumia wagonjwa wa kipindu pindu wakidhaniwa kuwa wanaugua kipindu pindu hadi baadaye walipokuja kukiri kuwa walikunywa dawa za kuongeza nguvu za kiume na ndio zimepelekea waharishe na kutapika.

Kwa mujibu wa mtandao wa The Mast Online wa nchini humo umeeleza kuwa wanaume hao walikuja kubainika kuwa hawaugui kipindupindu wakati Kiongozi Mkuu wa Jimbo la Mashariki nchini Zambia, Chanda Kasolo alipotembelea kujua idadi ya wagonjwa juzi (Jumatano) katika Hospitali ya Katete jimboni humo..

“Mpaka kufikia jana kulikuwa na kesi mbili za wagojwa waliolazwa kutoka Lusaka, hivyo idadi ya wagonjwa imeongeka kutoka 24 hadi 26 jambo ambalo limeongeza hofu kwenye jamii yetu. Na kingine cha kushangaza jana tumepata wagonjwa wengine watatu kutoka Katete eneo ambalo halijawahi kupatwa kabisa na kipindu pindu lakini baada ya  uchunguzi wa madaktari tumebaini kuwa Wagonjwa hao hawakuwa wanaugua Kipindu Pindu,“amesema Kasolo na kuelezea kilichowakumba.

“Baada ya majibu ya vipimo kupatikana , inaonekana kuwa wanaume hao walikutwa na mchanganyiko wa pombe, vyakula na dawa za kienyeji ambazo zilisababisha mchafuko wa mfumo wa chakula na hivyo ikahusishwa na kipindupindu lakini baada ya kuwauliza maswali, baadaye walikiri kuwa walikunywa dawa ya kuongeza nguvu,”amesema Kasolo.

Hata hivyo tayari wanaume hao wamehamishwa kwenye hospitali hiyo inayolaza wagongonjwa wa kipindu pindu na kulazwa kwenye hospitali ya kawaida.

Mpaka sasa vifo vya watu wapatao 70 vimeripotiwa kutokea tangu mwaka jana kwa kesi za ugonjwa wa kipindu pindu .

Mwishoni mwa mwaka jana Rais wa Zambia, Edgar Lungu alitangaza kuwa ugonjwa huo ni janga la taifa huku akitaka kila mwananchi kuwajibika kwa usafi.