Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeboresha mfumo wa malipo ya ankara na kuanzia sasa wateja wa mita za kawaida na wanaoomba kuunganishiwa umeme watalazimika kufanya malipo kwa mfumo wa kielektroniki.
Evaristo Winyasi, kaimu meneja wa Tehama, utafiti na utengenezaji mifumo wa Tanesco amesema mfumo huo umeanza Desemba 14,2017 kwa mikoa minne ya shirika hilo iliyopo Dar es Salaam na Pwani.
Amesema lengo la mfumo huo ni kutekeleza kwa vitendo matakwa ya sheria iliyopitishwa na Bunge, hivyo shirika limejiunga na mfumo huo ili kuhudumia wateja kwa kutumia benki na mitandao ya simu.
“Tumeshaungana na mfumo wa malipo ya Serikali wa GPG katika benki za NMB, CRDB na NBC. Kila benki imetoa njia zote za malipo ikiwemo ATM na simu,” alisema Winyasi jana Ijumaa Desemba 15,2017.
Amesema wateja wa Tanesco watafanya malipo kwa kutumia mitandao ya simu ikiwemo Airtel Money, M-Pesa na Tigo Pesa.
Winyasi amesema mteja hawezi kukamilisha malipo pasipo kufika ofisi za malipo na kupewa deni analodaiwa likiwa limeambatana na kumbukumbu namba ambayo itatumika kulipia kwa mfumo wa kielektroniki.
Meneja Masoko wa Tanesco, Mussa Chowo amesema madhumuni ya kujiunga na mfumo huo wa Serikali ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya shirika.
Chowo amesema mfumo huo hautawahusu wateja wa mita za Luku. Amesema wataendelea kupokea malipo kwa wateja watakaolipia kwenye ofisi, huku wakipewa maelekezo na ukomo.
“Wiki tatu kutoka sasa; Januari (2018) kwa mikoa ya Dar es Salaam tutasitisha malipo kwenye ofisi na wateja watayafanya kupitia benki na mitandao ya simu,” amesema.
No comments:
Post a Comment