Tuesday, 23 January 2018

TIRA, IIT yaanzisha mfumo wa Kimtandao wa huduma za bima



Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) imeanzisha mfumo wa kimtandao wa huduma za bima kwa wateja wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Akizungumza Kamishna wa TIRA, Dk Baghayo Saqware amesema mfumo huo unazitaka kampuni kuweka taarifa kwenye mtandao kwa mizigo inayoingizwa kutoka nje ya nchi na bima wanazotoza.

Hatua hiyo imekuja baada ya marekebisho ya Sheria ya Bima inayowataka waagizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi kutumia kampuni za ndani za bima.

Kabla ya marekebisho ya sheria hiyo, waagizaji wa mizigo nchini waliweza kutumia kampuni za bima za nje ili kupata kinga ya bidhaa zao.

Akifungua mafunzo ya wadau wa bima kuhusu namna ya kutumia mfumo wa kusimamia ulipaji wa bima kwa mizigo na bidhaa kutoka nje, Dk Saqware amesema utarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa ajili ya mamlaka za serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Takwimu Taifa (NBS).

Amesema mfumo huo utasaidia kufahamu kama sekta ya bima inakua ukilinganisha na ukuaji wa uchumi.

Dk Saqware amesema mfumo huo utazirahisishia mamlaka za serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kupata taarifa za bima kwa urahisi.

Amesema kampuni za bima na mawakala wataoshindwa kutoa taarifa zao kwenye mfumo wa mtandao huo watakuwa wanavunja sheria za nchi na hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Amesema utumiaji wa kampuni za ndani za bima utasaidia kampuni za bima, madalali na mawakala kukua kibiashara na kuongeza mapato.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT), Bosco Bugali alisema mtandao huo pia utawasaidia wanaodai fidia kulipwa kwa haraka na kwa ufanisi kwani hawatahangaika kuwasiliana na kampuni za bima za nje ya nchi.

BREAKING NEWS: Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi wa halmashauri ya Butiama


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 23, 2018 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Butiama mkoani Mara Solomoni Ngiliule kuanzia leo kutokana na ubadhirifu wa fedha za Umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo ametangaza maamuzi hayo leo zikiwa zimepita siku tatu toka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa maagizo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.

Waziri Mkuu aliagiza kiongozi huyo kuchunguzwa kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwemo sh. milioni 12 walizotumia kuandaa profile ya Halmashauri hiyo huku fedha zingine ni pamoja na sh. milioni 70 za elimu maalumu, sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazikujulikani zimetumikaje.

Nafasi za kazi leo Jan 23

Salum Mwalimu:Nipo tayari kuwa mwendawazimu


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zanzibar Salum Mwalimu amefunguka na kudai yupo tayari kuwa mwendawazimu kwa kuwapigania wananchi wa jimbo hilo akiwa Bungeni.

Salum Mwalim ameeleza hayo ikiwa imepita siku moja tokea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuruhusu kuanza kwa kampeni rasmi za uchaguzi mdogo katika majimbo mawili ambayo ni Kinondoni na Siha.

"Nakwenda Bungeni kulia na kuwa mwendawazimu kwa ajili mahitaji ya watu wa Kinondoni, hakuna wa kunikataza kuongea jambo lolote ambalo litakuwa lina tija kwa watu wangu. Nitahakikisha narudisha heshima ya kinondoni", alisema Salum Mwalim.

Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni unatarajiwa kufanyika mwezi ujao (Februari 17, 2018) ili kuweza kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya chama cha wananchi (CUF), Maulid Mtulia aliyejiuzulu kiti na uanachama kwa chama hicho na nafasi zote za uongozi alizokuwa nazo hapo awali.

Msigwa aachiwa baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuchomwa nyumba kiongozi wa CCM


Jeshi la Polisi mkoani hapa lilimshikilia na kumuachia kwa dhamana Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa tuhuma za kuratibu matukio mawili ya kihalifu likiwamo la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Iringa Mjini, Alfonce Muyinga.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Julisu Mjengi amesema mbunge huyo alikuwa akitafutwa kwa muda akituhumiwa kuratibu utekelezwaji wa matukio mawili ya kihalifu likiwamo la Januari 17 la kuchomwa kwa nyumba aliyokuwa akiishi Muyinga.

Mjengi alitaja tukio la pili kuwa ni lile la Januari 15 la kubomolewa kwa nyumba ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwangata Chadema, Anjelus Mbogo aliyejizulu nafasi yake na kuhamia CCM.

"Mchungaji Msigwa tulikuwa tukimtafuta kutokana na kuhusika kwake katika kuratibu matukio mawili ya kihalifu, lile la Januari 15 la kubomoa nyumba ya aliyekuwa diwani aliyehama Chadema na kujiunga na CCM pamoja na tukio la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Alfonce," amesema Mjengi na kuongeza;

"Na jana (Jumatatu) amejisalimisha mwenyewe hivyo tumemhoji hadi majira ya saa tatu usiku tulipomuachia kwa dhamana, taratibu nyingine zinaendelea na tutawajulisha pindi tukapozikamilisha," amesema

Msigwa amekuwa mtuhumiwa wa nne kukamatwa akihusisha na matukio hayo baada ya wiki iliyopita jeshi hilo kueleza kuwa linawashikiliwa watuhumiwa watatu kwa mahojiano kutokana na kuhusika na tukio la kuchoma nyumba ya aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM.

Mdee, Bulaya ‘wachomoka’ kifungoni


Kifungo walichokuwa wakitumikia wabunge wa Chadema, Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Halima Mdee (Kawe) cha kutokuhudhuria shughuli za Bunge kimemalizika na wamesema wamerejea na kasi ileile.

Wabunge hao waliadhibiwa kwa azimio la Bunge Juni 5 mwaka jana kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge ambayo ni jumla ya siku 47, waliyokosa ukiondoa shughuli zote za mikutano ya kamati za Bunge.

Adhabu hiyo ilikwenda sanjari na kulipwa nusu mshahara na posho kwa kipindi chote walichotumikia adhabu hiyo wakituhumiwa kudharau kiti cha spika.

Mikutano mitatu waliyoikosa ni wa bajeti uliokuwa ukiendelea, wa saba uliofanyika kati ya Septemba 5 hadi 15 na mkutano wa tisa wa Novemba 7 hadi 17.

Makato ya mshahara na posho yamebainishwa katika Kanuni 75 ya Bunge inayosema: “Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena katika sehemu yoyote ya ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”

Jana, kwa nyakati tofauti Bulaya na Mdee walizungumza na gazeti hili juu ya kurejea kwao, huku wakisema hawajutii kwa adhabu hiyo na hawatorudi nyuma au kutetereka katika kusimamia wanachokiamini.

“Nitaendelea kuwa Mdee yuleyule wa siku zote, kama walidhani wakinifungia mwaka nitabadilika. Hapana! Sitaraji kubadilika. Nimetumwa na wananchi wangu kusema ukweli na nitausema, sijaja kumpigia magoti mtu,” alisema.

Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), alisema wakati akitumikia adhabu hiyo amepata fursa ya kufanya shughuli kwa karibu za jimboni kwake na zile za Bawacha.

Naye Bulaya alisema: “Nimerudi bungeni tayari na leo (jana) nilihudhuria kamati yangu ya uwekezaji na mitaji.”

Alipoulizwa amejifunza nini kutokana na adhabu hiyo, alisema: “Bulaya wa kukosoa, Bulaya anayesimamia kile anachokiamini pasi na kuvunja sheria na taratibu hajabadilika, nitaendelea kuwakosoa.”

“Hata nilipokuwa natoka CCM kuja Chadema nilijua mambo kama haya ya kukamatana, kufungiana yatakuwapo kwa hiyo nilijipanga na wala hawanitetereshi, nimerudi na sitarudi nyuma,” aliongeza.

Mkhitaryan kusaidia matibabu kwa wenye Kansa


IKIWA ni saa chache baada tu ya kutua Arsenal akitokea Manchester United, Henrikh Mkhitaryan amesema atatumia jezi ya Man U ili kusaidia matibabu ya watoto wa Armenia walioathirika kwa saratani.
Mkhitaryan amekabidhiwa jezi ya Arsenal jana huku Sanchez akikabidhiwa jezi ya Man United United huku wakibadilishana miji kutoka London kwenda Manchester.

“Katika kuwashukuru wote waliochangia katika filamu ya simulizi yangu, nitatoa jezi la klabu ya Manchester United lililosainiwa na wachezaji ili kuwasaidia watoto wa Armenia walioathirika kwa saratani,”amesema Henrikh Mkhitaryan‏

Nyoso kupandishwa Kizimbani siku yoyote kuanzia Leo


Mlinzi wa timu ya Kagera Sugar Juma Said Nyosso anatarajiwa kupandishwa Mahakamani siku yeyote kutoka leo (Jumanne), kutokana na kutenda kosa la jinai wakati akitoka nje ya uwanja.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, RPC Agustine Ollom na kusema bado wanamshikilia mchezaji huyo wa Kagera na endapo watakapomaliza mahojiano naye wanatarajia kumpeleka Mahamakani kwa ajili ya mashtaka yake.

"Bado mtuhumiwa yuko mahabusu anaendelea kuhojiwa na yule majeruhi yupo hospitali kwa hiyo tunategemea madaktari wakatakavyo kuwa wamepita hii 'round' ya asubuhi watatupa hali yake jinsi anavyoendelea. Juma Nyoso amefanya kosa la jinai hivyo sisi tutampeleka Mahakamani mapema itakavyowezekana na huko ndipo itakapojulikana kama alitenda kosa au laa na mwisho kutolewa adhabu juu yake", alisema RPC Agustine Ollom.

Juma Said Nyosso alikamatwa jioni ya jana (Jumatatu) baada ya mechi kumalizika dhidi ya Simba katika dimba la Kaitaba ambapo wachezaji wa Kagera Sugar walikuwa wanaelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa bahati mbaya mmoja ya mashabiki inasemekana alimpulizia vuvu zela Nyosso ndipo naye alipompiga shabiki huyo mpaka kupoteza fahamu.

Wafanyakazi walipwa mshahara wa matofali badala ya pesa


Wafanyakazi katika kiwanda cha matofali kusini mashariki mwa China wanaokidai kiwanda hicho mishahara yao yenye thamani ya $14,050, wamelipwa matofali, inaripotiwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari Xinhua, takriban wafanyakazi 30 wa kiwanda hicho huko Nanchang, katika jimbo la Jiangxi , walikubali kulipwa matofali 290,000 badala ya mshahara wanaodai.

Gazeti la Jiangxi Daily linaripoti kuwa wafanyakazi hao , wote wakiwa ni wahamiaji , wametoka katika eneo la milima la jimbo la Yunnan kuini magharibi, na hawakuwa na namna ili kuishi kwa "kutumia mishumaa na kuwasha kuni moto ili kupunguza baridi ".

Baada ya chama chao cha wafanyakazi kuingilia kati na kwa usadizi wa mahakama, wafanyakazi hao walikubali kupokea matofali hayo kutoka wamiliki wa kiwanda badala ya mshahara wao ambao hawajalipwa.

Xinhua linasema kuwa waajiri wao, ambaye hakutajwa jina katika vyombo vya habari, bado anajaribu kutafakari namna ya kuwalipa, tofuati iliosalia ya Yuan 10,000 wanaodai wafanyakazi hao.

Taarifa hii imezusha mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii China, huku wengi wakielezea wasiwasi wao kuhusu ni kwanini mara kwa mara wafanyakazi wa vijijini wahamiaji ndio hulipwa kidogo kidogo?

Wengine wametania wakisema hali imekuwa mbaya kiasi cha matofali kuonekana kuwana thamani sawana fedha.

Je wewe ungekubali kulipwa mshahara wako kwa bidhaa nyingine yoyote kando na pesa taslimu?

Kamanda wa Polisi aweka bayana chanzo cha aliyegongwa na Ndege


KAMANDA wa Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, Matanga Mbushi, ameweka bayana chanzo cha mwanamke aliyegongwa na ndege ya Fastjet jijini Mwanza na kufariki dunia kuwa alikuwa na matatizo ya akili.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda Mbushi alisema hadi sasa wameshindwa kubaini jina la mwanamke huyo ambaye alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na ndege.

Ajali hiyo ilitokea katikati ya wiki iliyopita usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ulioko wilayani Ilemela.

Ndege hiyo ilimgonga mwanamke huyo akiwa anavuka kwenye njia ya kurukia ndege  wakati ndege hiyo yenye namba za usajili 58S-EJE190 ikiwa kwenye mwelekeo wa kuruka.

Alipoulizwa jana kama mwanamke huyo amefahamika na hatua gani zinachukuliwa ili tukio hilo lisitokee tena, Kamanda Mbushi alisema wanaopaswa kuzungumzia hilo ni Mamlaka ya Usalama wa Anga (TCAA).

“Yule mwanamke bado hatujapata jina lake, lakini inavyoonekana kuwa alikuwa na matatizo ya akili,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita, Kamanda huyo alisema wakati ndege hiyo ikiwa kwenye mwelekeo wa kuruka, mwanamke huyo alikuwa anakatiza kwenye njia ya ndege ndipo alipogongwa na kufa papo hapo.

“Ndege hii ilikuwa kwenye mruko wa futi 148 tokea pointi 12 kuelekea pointi 30 ikiwa na abiria 89 waliokuwa wakitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam,” alisema.

Alisema pamoja na ajali hiyo, ndege hiyo iliruka na kusafiri salama hadi Dar es Salaam.

Matukio ya ndege kugonga mtu ni nadra kutokea duniani kwa mujibu wa utafiti wa Nipashe, lakini ajali inayokaribiana na ya Mwanza ni ile iliyotokea katika jimbo la California, Marekani Aprili 3, 2016.

Katika ajali hiyo, mtu mmoja alifariki baada ya ndege ndogo kuangukia gari lililokuwa barabarani.

Mashuhuda, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), walisema ndege hiyo ilionekana kama ilikuwa na matatizo ya injini na ikalazimika kutua kwa dharura kwenye barabara ya magari.

Rubani wa ndege hiyo aliyetajwa kuwa Dennis Hogge, alishindwa kuidhibiti na ikateleza na kugonga gari lililokuwa na watu wanne lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara hiyo, ili dereva azungumze kwa simu.

Mtu mmoja alifariki dunia hapo hapo huku wengine watatu wakipelekwa hospitalini. Mtu aliyefariki dunia, Antoinette Isbelle (38), kutoka mji wa San Diego alikuwa ameketi nyuma katika gari hilo lililogongwa.

Katika hali ya kushangaza, haikuwa mara ya kwanza kwa ndege hiyo kutua kwenye barabara hiyo ya San Diego.

Mwaka 2000 mmiliki wa kwanza wa ndege hiyo alipatwa na hitilafu ya kimitambo na akalazimika kutua ndege aina ya Lancair 1V, kwenye barabara hiyo hiyo, BBC iliripoti.

Hata hivyo, tukio hilo halikusababisha maafa wala uharibifu wa ndege hiyo.

Arsenal na Liverpool zaingia vitani

Liverpool na Arsenal zimeingia vitani kuwania saini ya mchezaji wa AS Monaco, Thomas Lemar mwishoni wa msimu huu.

Taarifa zinaweka wazi kwamba makocha wa timu hizo mbili, Jurgen Klopp na Arsene Wenger wote wana fedha za kufanya usajili wakati dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa na kwamba, kila mmoja ametenga Pauni 90 milioni kuinasa huduma ya staa huyo wa Ufaransa.

Liverpool na Arsenal zote zimeondokewa na mastaa wake wa maana katika dirisha hili la usajili, ambapo Philippe Coutinho ameachana na wababe hao wa Anfield akitimkia Barcelona, wakati Alexis Sanchez aliondoka Emirates kwenda Manchester United. Kuna mastaa wengi wanaosakwa na makocha hao, lakini vita inaripotiwa kwamba, itakuwa kali kwelikweli kwa Lemar.

Hata hivyo, Arsenal na Liverpool si wao tu watakaoitaka huduma ya Lemar baada ya Manchester City nao kutajwa kwenye vita kutokana na kumkosa Sanchez, huku matajiri wa Paris, PSG wakimweka kwenye mipango yao ya msimu ujao Mfaransa huyo.

Wenger alikaribia kumnasa Lemar katika dirisha lililopita baada ya kukubali kulipa Pauni 92 milioni, lakini staa huyo mwenyewe aligoma kuihama Monaco katika dakika za mwisho na kubaki katika timu hiyo ya huko kwenye Ligue 1.

Chin Bees bifuni na Mganda


Chin Bees.

MSANII wa Bongo Fleva, Chin Bees amejikuta akiingia kwenye bifu zito na msanii wa Muziki wa Uganda, Fik Fameica kwa kumuibia ‘beat’ la wimbo wake wa Pepeta.

Akizungumza na Full Shangwe, Chin Bees amesema kuwa ameshtushwa na kitendo cha msanii huyo kutumia beat lake na kuuita Mafia bila kuzungumza naye.

Fik Fameica

Inaumiza sana kuona msanii anatumia beat lako bila kukushirikisha kwa chochote. Huyo msanii wala simjui na sijaongea naye ila tumewasilisha malalamiko yetu Cosota ili hatua stahiki zichukuliwe.

Full Shangwe ilimtafuta Fik Fameica kwa njia ya WhatsApp na kumsomea mashtaka yake lakini hakujibu chochote zaidi ya kutuma wimbo wake wa Mafia.

BREAKING NEWS: Nabii Tito akamatwa na polisi Dodoma


IGP Sirro akizungumza na Nabii Tito mjini Dodoma leo.

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma inadaiwa limemtia mbaroni mkazi mmoja wa mkoani humo anayejitangaza kama nabii, Tito Machija, ambaye amekuwa akionekana mitandaoni akifanya mambo yasiyoendana na maadili ya dini na injili anayodai kuihubiri.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro,  amezungumza na ‘mhubiri binafsi’ huyo licha ya jeshi hilo kutotoa taarifa rasmi ya kilichojiri na utaratibu unaoendelea iwapo ni kumhoji au kumfikisha mahakamani.

Nabii huyo ambaye video zake zimesambaa akihamasisha kuoa mke zaidi ya mmoja, ikiwa ni pamoja na kutembea na wafanyakazi wa ndani,  anatumia pombe kunasa waumini na anadai hataki nyimbo za injili kwenye ‘ibada’ zake, ambazo nyingi hufanyikia baa.

Aidha ameonekana akicheza nyimbo za Bongo Fleva akiwa ‘madhabahuni’ badala ya kwaya na huku akieleza kuwa wafadhili wake wanatumia pombe,  hivyo na yeye lazima waumini wake watumie pombe ambazo amezifanyia upako.