Thursday, 28 December 2017

Pretyy Kind aingizwa mjini na muhuni


Kisura wa filamu Bongo, Suzan Michael ‘Pretty Kind’ amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuibiwa hela kiasi cha shilingi milioni moja alizokuwa ameweka kwenye gari lake pamoja na kadi ya benki, baada ya kumpa mtu funguo ili asogeze gari lake ambalo lilikuwa limeziba njia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, ishu hiyo ilijiri siku chache zilizopita, ambapo msanii huyo alikuwa studio moja maeneo ya Sinza, ndipo kijana mmoja ambaye si mwenyeji wa studio hiyo akamuomba funguo akamsogezee gari yake ambayo ilikuwa imezuia njia, akampa. Baadaye wakati anaondoka, mrembo huyo alibaini kuwa amelizwa fedha hizo.

Kutokana na sekeseke hilo Pretty alipotafutwa alisema; “Nimekoma kuwapa watu hovyo gari langu, maana bora kaiba hivyo tu, angeiba gari sijui ingekuwaje, nilimuweka ndani mtu wa studio amuonyeshe huyo mwizi alipo, eti anadai ni mtoto wa mkubwa hawezi kupatikana, nimeumia sana,”alisema bishosti huyo ambaye amefungua jalada la kesi Kituo cha Polisi Kijitonyama KJN/RB/12224 WIZI.



OMG kufunga mwaka na kolabo ya Kimataifa


Kundi la muziki la OMG limesema linatarajia kuachia kolabo kubwa na msanii mkubwa kutoka Afrika.

Member wa kundi hilo Young Lunya ameiambia The Playlist ya Times Fm kuwa pia katika kolabo hiyo kuna msanii mwingine kutoka nje ya Afrika.

“Na kabla mwaka hajaisha kuna zawadi moja kubwa sana naona tuiachie, kuna kolabo kubwa sana tumefanya na msanii wa Afrika ila kuna mmoja ni nje ya Afrika,” amesema.

Kwa upande wake Con Boi amezungumzia utendaji kazi wao kwa mwaka huu, 2017 kwa kusema; “Mwaka huu hatukuachia kazi nyingi lakini tunafanya kazi, zipo zinafanyika, 2018 utakuwa ni mwaka wa ku-release, tutaachia sana nyimbo kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa 12 ni mauaji kutoka OMG,”.




Wasomi waeleza athari za kurudia uchaguzi


Utashi wa kisiasa wa wabunge kuvihama vyama vyao umetajwa kulisababishia Taifa hasara kutokana na Serikali kutumia fedha nyingi kugharamia chaguzi za marudio.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili wamesema hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo wananchi wataanza kuchagua chama badala ya mtu.

Wamesema katika utaratibu huo, ikiwa mbunge atahamia chama kingine, chama chake cha awali kitapitisha mtu mwingine kuchukua nafasi yake, bila kulazimika kuingia kwenye uchaguzi.

Hivi karibuni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alieleza jinsi ofisi yake ilivyookoa Sh156 bilioni ambazo zingetumika iwapo Serikali ingeshindwa kesi na kurudia uchaguzi katika majimbo 52.

Hiyo inamaanisha kwamba kwa wastani, Sh3 bilioni hutumika kugharamia uchaguzi wa ubunge katika jimbo moja.

Hivi karibuni wabunge wawili wa upinzani, Dk Godwin Mollel wa Siha (Chadema) na Maulid Mtulia wa Kinondoni (CUF) walijivua uanachama wa vyama vyao na kujiunga CCM sawa na Lazaro Nyalandu ambaye alijiuzulu uanachama wa CCM na ubunge wa Singida Kaskazini na kuhamia Chadema.

Mbali na majimbo hayo ambako utafanyika uchaguzi unaotokana na utashi wa wanasiasa, majimbo ya Longido na Songea Mjini yatafanya uchaguzi kutokana na sababu zisizoepukika.

“Nadhani umefikia wakati wa wananchi kuchagua chama, mfano mbunge akihama chama chake, chama hicho kipitishe mtu mwingine kuwa mbunge wa jimbo husika bila NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kuitisha uchaguzi mwingine,” alisema Dk Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema.

Kwa kurejea wastani wa jimbo moja kugharimu Sh3 bilioni, majimbo hayo matatu yatatumia kiasi cha Sh9 bilioni. Gazeti hili limechambua kiasi hicho cha fedha na kubaini kuwa kinaweza kutumika kununua magari manne ya kubebea wagonjwa, kujenga zahanati tano, madarasa 400 na mashine mbili za CT-Scan kwa pamoja.

Magari moja la kubebea wagonjwa linagharimu Sh300 milioni, hivyo Sh1.2 bilioni za sehemu hiyo ya fedha zingeweza kutumika kununua magari manne na kuwezesha mikoa minne nchini kupata magari hayo.

Pia, zahanati moja yenye vifaa vyote muhimu, ujenzi wake unagharimu kati ya Sh600 milioni na Sh700 milioni. Hivyo, Sh3 bilioni zingeweza kutumika kujenga zahanati tano.

Pia fedha hizo zingeweza kujenga vyumba 400 vya madarasa kwa kutumia Sh3 bilioni. Ujenzi wa chumba kimoja cha darasa ni Sh7.5milioni.

Kipimo maarufu cha CT-Scan kinauzwa kwa wastani wa Sh900 milioni hivyo Sh1.8 bilioni zingeweza kutumika kununua mashine hizo mbili.

Wanasiasa, wasomi walonga

Katika ufafanuzi wake Dk Mashinji alisema, “Tukiwa na mfumo wa watu kuchagua chama tutaepuka gharama za chaguzi ndogo na hili wimbi la watu kuhama halitakuwa na athari zozote kwa maendeleo ya nchi. Unajua kinachoendelea sasa ni athari za demokrasia ambayo tumeichagua wenyewe.”

Alisema mgombea ubunge hubebwa na ajenda na ilani ya chama chake si yake binafsi, hivyo ikitokea akahama, chama alichokikimbia ndicho kinapaswa kuteua mtu mwingine kuwa mbunge, si uchaguzi kurudiwa.

“Huu utaratibu ndio unaotumika hata Afrika Kusini. Wananchi wanapaswa kuchagua chama si mtu.”

Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ngemela Lubinga alifafanua jambo hilo kwa kina na kusisitiza, “Kama wanataka kuondoa gharama ya uchaguzi wapeleke muswada bungeni maana suala la uchaguzi halipo kwa matakwa ya kikundi au matakwa binafsi, ni sheria na kanuni tulizojiwekea.”

“Kwamba ili tutekeleze demokrasia Tanzania yafuatayo yatatekelezwa, moja wapo ni ikiwa mbunge, diwani au mwenyekiti wa kijiji akifa au akijiuzulu lazima uchaguzi ufanyike.”

Alisema ikiwa wananchi watahoji jambo hilo na kupelekwa bungeni linaweza kubadilishwa na kwamba utaratibu huo ndio utekelezaji wa demokrasia.

Dk Charles Kitima wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) alisema jimbo likiwa wazi, uchaguzi unapaswa kufanyika ila kinachopaswa kujadiliwa ni baadhi ya wabunge kuwa kigeugeu na kujiuzulu ubunge na kujivua uanachama wakati waliomba kura wakiahidi kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema inasikitisha kuona gharama kubwa inatumika kurudia uchaguzi uliotokana na watu kujiuzulu wakati bado kukiwa na uhitaji wa dawa hospitalini, ajira kwa vijana, ujenzi wa barabara na shughuli nyingine nyingi za maendeleo.

“Kwa hiyo hili liwe fundisho kwa wananchi wakati wanapochagua wawatafakari wagombea, wasiwapigie kura vigeugeu,” alisema Dk Kitima.

Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Dk Jimson Sanga wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI). Alisema ni bora Serikali ingesitisha uchaguzi kwenye majimbo ambayo wabunge wake wanajiuzulu ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha ambazo zingetumika kwenye kazi nyingine za maendeleo ya wananchi.


Alisema haiingii akilini mbunge kujiuzulu kwa madai ya kuunga mkono sera na utendaji kazi mzuri wa Rais John Magufuli wakati uamuzi wake wa kuhama unapingana na sera ya kubana matumizi.

“Sasa kama wanaunga mkono kazi nzuri za Rais kwa nini wasipande majukwaani kuhubiri sera hizo badala ya kujiuzulu? Ni bora wangefukuzwa na vyama vyao kwa kuunga mkono jitihada za Rais jambo ambalo lingekuwa na namna nyingine ya kujadilika,” alisema Dk Sanga.

Alisema kazi ya mbunge kwenye jimbo ni kuwawakilisha wananchi na inapotokea Serikali inatekeleza sera za wananchi hao haimaanishi kuwa mbunge anatakiwa kuwasaliti na kuachia madaraka.

Aliongeza kuwa ipo miradi mingi ya maendeleo inayohitaji fedha nyingi ambazo badala ya kupelekwa huko, zitapaswa kutumika kwenye uchaguzi, hilo si jambo sahihi.

Katibu Mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi aliungana na Dk Mashinji na kusisitiza, “Iweje mbunge uhame kwa madai ya kuridhishwa na juhudi anazozifanya Rais Magufuli. Kwa nini juhudi hizo usiziige kwa kuliletea maendeleo jimbo lako.”

“Katika majimbo yao hakuna maji, umeme, huduma za afya ni duni lakini wanakimbia wananchi waliowachagua na kwenda kumuunga mkono Rais. Kwanini wasishirikiane na Rais kuwaletea wananchi maendeleo.”





Kardinali Pengo alilia wimbi la watoto wa mitaani


Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo `amewalilia’ watoto wa mitaani wanaoomba akisema wanafanya hivyo kwa kutumwa na wazazi au walezi wao.

Akihubiri katika misa takatifu ya watoto mashahidi leo Alhamisi Desemba 28, 2017 katika viwanja vya Msimbazi Center wilayani Ilala, Pengo amesema watoto wanateswa na wazazi ama walezi.

Misa hiyo ni sehemu ya kumbukumbu Mfalme Herode aliyemuru mauaji ya watoto wote wenye umri wa miaka miwili ili aweze kumuangamiza Yesu huko Bethrehem.

Akisimulia kisa kimoja, Pengo amesema “siku moja nilikuwa naendesha gari siku hizo nikiwa na nguvu,” amesema

“Nilisimama mbele ya mtoto mmoja aliyekuwa akiomba msaada katika mtaa mmoja wa jijini Dar es Salaam,” amesema .

 “Nikamuuliza wewe umekaa hapa jua linakuwakia mchana kutwa, mvua ikija inakunyeshea, je ungependa nikakuandikishe shule ili uweze kuwa na maisha yako,” amesema Pengo.

Amesema  baada ya kumuuliza kuhusu shule yule mtoto alitoweka na kutokomea kusikojulikana.

“Mtoto yule hakutaka kusikia neno linaloitwa shule, nikajiuliza huyu mtoto anataka kubaki hapa mtaani kuombaomba na adha zote hizi,”amesema.

Amesema  alikuja kugundua baadaye kwamba wengine ni watoto yatima ambao wanalazimika kuomba ili wapate mahitaji yao.

Amesema  watoto wengi wanaoomba mitaani wanafanya hivyo kwa kutumwa na wazazi wao ua walezi.

“Wanatumwa na wazazi wao kuomba lakini fedha zinazopatikana ni za wazazi wao na wasipopata wanalala na njaa,  inasikitisha,” amesema.

Kardinali Pengo amesema wako baadhi ya wazazi ambao wanawapa ulemavu wa kudumu watoto wao ili wawe kivutio wakati wa kuomba.

“Kuna kesi moja ambayo mzazi alimvunja mkono mtoto wake akawa mlemavu ili awe kivutio wakati wa kuomba,”amesema.

Amesema  wako wazazi ambao kwa makusudi wanawapa upofu watoto wao ili mradi wao wanufaike.

“Kwa hiyo akina Herode wako hadi leo, unaweza kujiuliza mwenyewe Herode na wazazi wa aina hii nani katili,” alisema

Amesema  uovu dhidi ya watoto unafanywa hadi leo na akaishauri jamii ya watanzania kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini unyanyasaji dhidi ya watoto.

“Tusinyamaze kimya tunapobaini watoto wananyanyaswa,” amesema.


Katika misa hiyo, watoto wa kanisa hilo, Jimbo la Dar es Salaam walimkabidhi Askofu Pengo kiasi cha Sh1.8 milioni ili ziweze kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amewapongeza watoto hao kwa kuchanga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wenye mahitaji.

“Endeleeni hivyo hivyo kila mnachokifanya tangulizeni upendo wa Mungu kwa kuwajali wengine, msiwe wabinafsi,” amesema  Nzigilwa.

Mwananchi.

Timu ya watu 50 kumkabidhi Nchi Weah


Wakati wananchi wa Liberia wakiendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi wa duru ya pili ya urais uliofanyika Desemba 26,2017 Rais anayemaliza muda wake Ellen Johnson Sirleaf ametangaza timu ya wataalamu watakaofanikisha mchakato wa kukabidhi madaraka.

Ikijulikana “Timu ya pamoja ya kukabidhi madaraka ya Rais” ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kufanikisha hatua zote za ubadilishanaji madaraka kutoka yule anayemaliza muda wake kwenda kwa Rais ajaye.

Kulingana na waraka wa Rais, timu hiyo itaongozwa na marais wawili, anayemaliza muda wake na yule anayesubiri kuingia madarakani.

Iwapo wawili hao watakosekana waziri wa masuala ya nchi ndiye atakayeiongoza.

Pia, itakuwa na wajumbe wengine wanaofikia 50 ambao miongoni mwao ni mawaziri wanaohusika na Mambo ya Nchi na Masuala ya Rais;  Sheria; Mambo ya Nje; Fedha na Mipango; Mambo ya Ndani; na Ulinzi wa Taifa


Rais Sirleaf anamaliza kipindi chake cha uongozi ambapo sasa anatarajiwa kumkabidhi madaraka mwanandinga wa zamani wa Taifa hilo na Klabu ya AC Milan, George Opong Weah ambaye amefanikiwa kumshinda mpinzani wake ambaye pia ni Makamu wa sasa wa Rais.



JPM awaonya viongozi wa umma



Rais John Magufuli amewasilisha fomu ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu leo Alhamisi Desemba 28,2017 ikiwa ni siku moja baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwataka viongozi kuziwasilisha, ameipongeza sekretarieti kwa kazi inazofanya.

Pia, amemtaka Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo Desemba 31,2017.

“Ikifika Desemba 31, ambayo ni siku ya mwisho kwa mujibu wa sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema,” amesisitiza Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu.

Jaji mstaafu Nsekela amemshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo.

Amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma si ombi.


Waziri atoa ogizo kwa TANESCO kuhusu Spea za akiba



Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa shirika la umeme nchini TANESCO mkoa wa Kagera kuhakikisha linanunua Spea za akiba ili kuepuka usumbufu kwa wananchi kukosa umeme mara kwa mara.

Dkt. Kalemani ametoa agizo hilo leo wakati akiendelea na ziara yake mkoani Kagera ya kukagua miradi mbalimbali ya umeme.

"Lazima tuwe na Spea sasa hivi sio lazima tusubiri mpaka tatizo litokee ni bora muanze kuagiza mapema Spea ambazo mnahisi hazipo ili linapotokea tatizo la umeme muweze kukabiliana nalo," amesema Dkt. Kalemani.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani yupo mkoani Kagera katika majukumu yake ya kazi ya kukagua miradi ya umeme mkoani hum

VIDEO: Taarifa Rasmi Ya TFF Kufuta Ndondo Cup



Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na kufuta Ndondo Cup.

Kupitia msemaji wake Alfred Lucas amesema kuwa "kuna upotoshaji unaofanywa kwa makusudi kuwa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzani (TFF), Wallace Karia kafuta mashindano ya Ndondo Cup taarifa hizi sio sahihi alichokisema Rais Karia ni kuwa TFF inaandaa kanuni ili mashindano yote ya aina hiyo yakidhi vigezo katika utaratibu mzuri na watapata vibali kupitia FA wilaya na mikoa baada ya kutimiza vigezo  vitakavyowekwa wakati yale yenye sura ya kitaifa yatapata kibali kutoka TFF" Alfred Lucas.

Aidha kupitia mkutano, Timu ya Soka ya Mbao FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara Leo imesaini mkataba wenye thamani ya Sh 100M na Kampuni ya Hawaii ambao ni watengenezaji wa maziwa ya CowBell.

Akizungumza na wandishi wa habari wakati wa kutiliana saini mkataba huo, Meneja Masoko wa CowBell Elisaria Ndeta amesema wameamua kuendeleza udhamini wao kwenye Timu hiyo kutokana na kuridhishwa na kiwango chao pamoja na umoja uliopo.

" Udhamini huu ni wa Sh 100Milioni ambapo Million 70 italipwa Cash na 30Milioni itatumika kwenye vifaa vya michezo, tunaamini Mbao itaendeleza ushirikiano mzuri na udhamini huu utawasaidia kufanya vizuri" Alisema Ndeta.

Pia Mbao Fc kupitia Mwenyekiti wake wametambulisha jezi yao mpya ambayo itatumika msimu huu.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI........USISAHU KUSUBSCRIBE



Pretty Kind afunguka kufanyishwa ngono



Msanii wa muziki na filamu Suzan Michael maarufu kama 'Pretty Kind', ambaye alishawahi kupelekwa nchini India na marafiki na kwenda kufanyishwa biashara ya ngongo, atoa siri ya watu wengi waliopo huko na hofu yao ya kurudi nyumbani.
Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Pretty Kind amesema maisha wanayoishi wasichana wanaotoka huku na kwenda kule ni magumu, kiasi kwamba wanahofia hata kurudi nyumbani kwni hawana kitu chochote wala fedha.
Pretty Kind ameendelea kueleza kuwa maisha ya biashara ya ngono yanawapa wakati mgumu kwani kuna muda wanashindwa hata kula pamoja na kupatwa na misuko suko mingine, lakini wanaona aibu kuja kuzikabili familia zao baada ya kuziacha kwa muda mrefu.
"Unajua mi nilivyochukulia mara ya kwanza yatakuwa ni maisha kama tunavyoishi bongo, nilienda kule niliitwa na msichana mwenzangu akaniambia nitapata kazi ya hela nyingi, nilipofika nikashangaa, watu niliowakuta kule maisha magumu, wanatamani kurudi nyumbani lakini wanaona aibu, anatrudije nyumbani hana kitu cha maana, na familia inajua yuko nje, na kwanza muda mwengine unakuwa ushanyang'anywa passport unalipa madeni ya watu", amesema msichana huyo ambaye kwa sasa amegeukia bongo fleva.
Pretty Kind hivi sasa ana kazi mpya ya bongo fleva inayoitwa 'Vidudu washa' aliyomshirikisha Gigy Money, baada ya kujaribu kwenye filamu nakuona h

Lukuvi ametoa onyo kwa Vishoka Wa Ardhi



Serikali imekemea baadhi ya wawekezaji wanaotumia vibaya jina la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwatoa wananchi katika maeneo yao kwa kisingizio cha kupewa kibali na wizara hiyo wakati sio kweli.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Ardhi William Lukuvi ambapo amewaonya baadhi ya wawekezaji ambao wameonekana kushirikiana na baadhi ya watumishi wa serikali katika kunyang'anya haki za wananchi kitendo ambacho amesema kwa utawala wa serikali hii ya awamu ya tano hakina nafasi.
Ameongeza kwamba, kwa sasa serikali inaendelea na zoezi la kurudisha ardhi ya wananchi mikononi mwao bila ya gharama yeyote na kwa yale maeneo ambayo yatabainika kuwa na ukiukwaji wa umiliki watayarudisha kwa wenyewe ili kuendelezwa.
Mh. Lukuvi amesema zoezi la utambuzi wa umiliki wa maeneo na urasimishaji ni endelevu kwa mikoa yote nchini lengo ni kujua maeneo yanayomilikiwa kihalali na kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imeonekana bado ni changamoto kwa maeneo mengi mijini na vijijini.

Dk Tulia azindua Mradi Wa maji Kata ya ilemi mbeya



Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt.Tulia Ackson amewataka wananchi kuheshimu na kuitunza miradi mbalimbali inayoibuliwa na wadau bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa.
Dkt.Tulia ameyasema hayo wakati akizindua mradi wa maji katika kata ya Ilemi Jijini Mbeya, mradi ulioibuliwa na chama cha mapinduzi CCM na kujengwa kwa nguvu za wananchi kutokana na eneo hilo kukabiliwa na kero ya uhaba wa maji kwa muda mrefu.
“Ni vizuri tukaitunza na kuiheshimu miradi mbalimbali inayotolewa na wadau wetu na tukaachana na itikadi zetu za kisiasa na kuacha kuhujumu miundombinu hiyo kwa kuwa lengo la miradi ni kuwanufaisha watanzania wote bila kubagua.”,amesema Dkt.Tulia
Kata ya Ilemi Jijini Mbeya inadaiwa kukabiliwa na kero ya uhaba wa maji kwa muda mrefu huku wadau mbalimbali wakionyesha jitihada ya kutatua kero ya maji katika eneo hilo.

Waziri ashiriki ujenzi Wa shule




Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, ameshiriki kazi ya ujenzi wa Shule ya Msingi Chambasi wilayani Kisarawe, ikiwa ni kuamsha ari ya wananchi kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa ujenzi huo, Dk. Ndugulile alisema kuwa kwa kipindi kirefu dhana ya wananchi kujitolea katika kufanya kazi za maendeleo imepungua kwa kiasi kikubwa na kuiachia Serikali ikitoa kila kitu kutekeleza miradi ya maendeleo hata kama inawezekana kazi hizo kutekelezwa na wananchi.
Alisema kipindi cha sasa cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, wananchi hawana budi kujitoa katika kufanya shughuli za maendeleo katika maeneno hayo ili kuisaidia Serikali na kujisaidia wao wenyewe kujiletea maendeleo.
“Msisubiri kila kitu kifanywe na Serikali, vingine mnaweza kufanya wenyewe, hongereni sana, ninyi ni mfano wa kuigwa kwa vijiji vingine katika hili,” alisema Dk. Ndugulile.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chambasi, Fodia Tungaraza, alisema mradi huo wa ujenzi wa shule umeibuliwa na wananchi wenyewe mara baada ya watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda kijiji cha jirani kuifuata Shule ya Msingi Msimbu, takribani kilomita sita, hivyo kuhatarisha maisha na usalama wa wanafunzi hao.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msimbu, Hussein Mkambara, ambaye pia anasimamia Shule ya Chambasi hadi itakapopata usajili, ameishukuru Serikali kwa kuona na kuwaunga mkono katika jiitihada za kujikwamua katika changamoto waliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu.
Dk. Ndugulile alifanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kwa kushiriki ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Chambasi, kuvitembelea vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na biashara, viwanda vidogo vidogo vinavyowezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na mahakama inayohusika na mashauri ya watoto.

BASATA yaikana kamati ya Miss Tanzania




Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limekanusha taarifa iliyotolewa na waandaaji wa shindano la Miss Tanzania ya LINO Agency, kwamba Baraza hilo ni moja ya chanzo cha kukwamisha shindano hilo kufanyika.
Kweye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, BASATA imesema ilitoa kibali cha muda kwa kampuni hiyo kuweza kushughulikia matatizo yake, pamoja na kuratibu safari ya Miss Tanzania 2017 aliyeshiriki mashindano ya Miss World mwaka huu.
Taarifa hiyo imeendelea kwa kutoa wito kwa makampuni yanayoandaa mashindano ya sanaa kuongeza weledi, na kuzingatia sheria, ili kuepuka matatizo kama hayo.