Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo `amewalilia’ watoto wa mitaani wanaoomba akisema wanafanya hivyo kwa kutumwa na wazazi au walezi wao.
Akihubiri katika misa takatifu ya watoto mashahidi leo Alhamisi Desemba 28, 2017 katika viwanja vya Msimbazi Center wilayani Ilala, Pengo amesema watoto wanateswa na wazazi ama walezi.
Misa hiyo ni sehemu ya kumbukumbu Mfalme Herode aliyemuru mauaji ya watoto wote wenye umri wa miaka miwili ili aweze kumuangamiza Yesu huko Bethrehem.
Akisimulia kisa kimoja, Pengo amesema “siku moja nilikuwa naendesha gari siku hizo nikiwa na nguvu,” amesema
“Nilisimama mbele ya mtoto mmoja aliyekuwa akiomba msaada katika mtaa mmoja wa jijini Dar es Salaam,” amesema .
“Nikamuuliza wewe umekaa hapa jua linakuwakia mchana kutwa, mvua ikija inakunyeshea, je ungependa nikakuandikishe shule ili uweze kuwa na maisha yako,” amesema Pengo.
Amesema baada ya kumuuliza kuhusu shule yule mtoto alitoweka na kutokomea kusikojulikana.
“Mtoto yule hakutaka kusikia neno linaloitwa shule, nikajiuliza huyu mtoto anataka kubaki hapa mtaani kuombaomba na adha zote hizi,”amesema.
Amesema alikuja kugundua baadaye kwamba wengine ni watoto yatima ambao wanalazimika kuomba ili wapate mahitaji yao.
Amesema watoto wengi wanaoomba mitaani wanafanya hivyo kwa kutumwa na wazazi wao ua walezi.
“Wanatumwa na wazazi wao kuomba lakini fedha zinazopatikana ni za wazazi wao na wasipopata wanalala na njaa, inasikitisha,” amesema.
Kardinali Pengo amesema wako baadhi ya wazazi ambao wanawapa ulemavu wa kudumu watoto wao ili wawe kivutio wakati wa kuomba.
“Kuna kesi moja ambayo mzazi alimvunja mkono mtoto wake akawa mlemavu ili awe kivutio wakati wa kuomba,”amesema.
Amesema wako wazazi ambao kwa makusudi wanawapa upofu watoto wao ili mradi wao wanufaike.
“Kwa hiyo akina Herode wako hadi leo, unaweza kujiuliza mwenyewe Herode na wazazi wa aina hii nani katili,” alisema
Amesema uovu dhidi ya watoto unafanywa hadi leo na akaishauri jamii ya watanzania kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini unyanyasaji dhidi ya watoto.
“Tusinyamaze kimya tunapobaini watoto wananyanyaswa,” amesema.
Katika misa hiyo, watoto wa kanisa hilo, Jimbo la Dar es Salaam walimkabidhi Askofu Pengo kiasi cha Sh1.8 milioni ili ziweze kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amewapongeza watoto hao kwa kuchanga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wenye mahitaji.
“Endeleeni hivyo hivyo kila mnachokifanya tangulizeni upendo wa Mungu kwa kuwajali wengine, msiwe wabinafsi,” amesema Nzigilwa.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment