Rais John Magufuli amewasilisha fomu ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasilisha fomu leo Alhamisi Desemba 28,2017 ikiwa ni siku moja baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwataka viongozi kuziwasilisha, ameipongeza sekretarieti kwa kazi inazofanya.
Pia, amemtaka Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo Desemba 31,2017.
“Ikifika Desemba 31, ambayo ni siku ya mwisho kwa mujibu wa sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema,” amesisitiza Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu.
Jaji mstaafu Nsekela amemshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo.
Amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma si ombi.
No comments:
Post a Comment