Thursday, 28 December 2017

Waziri ashiriki ujenzi Wa shule




Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, ameshiriki kazi ya ujenzi wa Shule ya Msingi Chambasi wilayani Kisarawe, ikiwa ni kuamsha ari ya wananchi kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa ujenzi huo, Dk. Ndugulile alisema kuwa kwa kipindi kirefu dhana ya wananchi kujitolea katika kufanya kazi za maendeleo imepungua kwa kiasi kikubwa na kuiachia Serikali ikitoa kila kitu kutekeleza miradi ya maendeleo hata kama inawezekana kazi hizo kutekelezwa na wananchi.
Alisema kipindi cha sasa cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, wananchi hawana budi kujitoa katika kufanya shughuli za maendeleo katika maeneno hayo ili kuisaidia Serikali na kujisaidia wao wenyewe kujiletea maendeleo.
“Msisubiri kila kitu kifanywe na Serikali, vingine mnaweza kufanya wenyewe, hongereni sana, ninyi ni mfano wa kuigwa kwa vijiji vingine katika hili,” alisema Dk. Ndugulile.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chambasi, Fodia Tungaraza, alisema mradi huo wa ujenzi wa shule umeibuliwa na wananchi wenyewe mara baada ya watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda kijiji cha jirani kuifuata Shule ya Msingi Msimbu, takribani kilomita sita, hivyo kuhatarisha maisha na usalama wa wanafunzi hao.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msimbu, Hussein Mkambara, ambaye pia anasimamia Shule ya Chambasi hadi itakapopata usajili, ameishukuru Serikali kwa kuona na kuwaunga mkono katika jiitihada za kujikwamua katika changamoto waliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu.
Dk. Ndugulile alifanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kwa kushiriki ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Chambasi, kuvitembelea vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na biashara, viwanda vidogo vidogo vinavyowezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na mahakama inayohusika na mashauri ya watoto.

No comments:

Post a Comment