Saturday, 16 December 2017

Waziri Jafo Azuia shule ya Ihunge kuwa Chuo Kikuu



Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,TAMISEMI Selemani Jafo amewasisitiza viongozi wa mkoa wa Kagera kutokubadilisha malengo ya shule ya Ihungo kwa kuigeuza kuwa chuo kikuu baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Jafo ameyasema hayo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo inayojengwa upya baada ya hapo awali kukumbwa na tetemeko la ardhi.
Shule ya Ihungo inajengwa kisasa na itakapokamilika itakuwa shule ya kipekee kwa kuwa na miundombinu ya kisasa hapa nchini.
Amesema Majengo ya shule hiyo kwasasa yanaweza kuwatamanisha baadhi ya viongozi kutaka kubadilisha shule hiyo hapo baadae kuwa chuo kikuu kitu ambacho amezuia jambo hilo.
Amesema amezuia ili vijana wa kidato cha tano na sita ili waweze kupata nafasi kusoma katika shule hiyo yenye mazingira mazuri.
Baada ya ukaguzi wa shule hiyo,Waziri Jafo alielekea na ukaguzi wa shule nyingine ya Nyakato inayojengwa na Suma JKT na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi.

Tani 9 za dawa ya meno Aloe zaangamizwa Zanzibar



Wafanyakazi kutoka Bodi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wameangamiza Tani tisa za Dawa ya meno aina ya Aloe zilizoharibika katika jaa la Kibele Wilaya ya Kati Unguja
Dawa hizo ziliingizwa nchini na Kampuni ya Bacelona Interprises Limited zikiwa zimeharibika baada ya kontena lilikuwa na dawa hizo kuinga maji wakati wa kusafirishwa kuja Zanzibar .
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Chakula Dawa Zanzibar Mwadini Ahmadi Mwadini alisema walibaini kuwa dawa hizo zimeharibika wakati wa kuzitoa bandarini na kumshauri mmiliki wa dawa hizo kuzirejesha zilikotoka au kuziangamiza na alikubali ziangamizwe ili kujiepusha na gharama nyengine.
Mwadini alisema Bodi inaendelea kufanya ukaguzi kwa bidhaa zinazoingizwa bandarini na maduka mbali mbali ili kuhakikisha zinakuwa salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapoagiza Bidhaa na kujenga ushirikiano wa karibu na Bodi yake kwa kutowa taarifa wanapoona bidhaa zao zinamashaka kuuzwa kutokana na kuharibika au kupitwa na muda wake wa matumizi.
Aidha aliwaomba wananchi wanaponunua bidhaa madukani na kuzigundua kuwa hitilafu watowe taarifa katika Bodi ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa kwa usala wao.
“Kama mukigundua kunafanyika udanganyifu kwa bidhaa mnazonunua kama kuharibika au kupitwa na wakati musisite kutoa taarifa kwetu, tupo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi.” alisema Mkaguzi Mkuu.
Nae mtoa mzigo Bandarini aliesimamia kontena hilo Omar Kombo Sharif alisema mzigo huo uliingia Zanzibar mnamo mwezi wa nane na baada ya kubainika umeharibika walitoa taarifa kwa mmiliki na walikubaliana uzuiliwe kwa ajili ya kuuangamiza.
Wakati huo huo Mkuu wa Uchunguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar Mohamed Shadhil alisema wamekamata Nyama ya ngombe kilo 180 iliyokuwa inasafirishwa kinyume na taratibu zilizowekwa na Bodi hiyo.
Alisema bidhaa hiyo imekamatwa wakati inasafirishwa kutoka machinjioni kwa kutumia Baskeli pamoja na vespa bila ya kuwa na kibali cha daktari na nikinyume cha utaratibu. Bidhaa za nyama zinatakiwa kusafirishwa kwa kutumia gari kwa ajili ya usalama wa watumiaji.
Nyama hiyo wameamua kuifukia baada ya kufanyika uchunguzi na kuwaita wamiliki ambao walikubali kuwa wamefanya kosa licha ya kulalamika kuwa utaratibu wa kusafiri bidhaa hiyo kwa kutumia baskeli na vespa umekuwapo kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa uchunguzi aliwataka wananchi wanaochinja nyama kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia vyombo vinavyotakiwa vyakuchukulia bidhaa hiyo ili kuepuka usumbufu na hasara katika biashara zao.

Waziri Lukuvi ampiga STOP mkurugenzi mkuu NHC



Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesimamishwa kazi.
Taarifa ya kusimamishwa kazi kiongozi huyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 16,2017 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akieleza uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Mchechu aliteuliwa kuliongoza shirika hilo Machi Mosi, 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CBA.
Taarifa ya Dk Abbasi imesema Lukuvi amechukua uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.
Mbali na Mchechu, Lukuvi ameitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Mikoa na Utawala, Raymond Mndolwa.
"Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika imesisitiza kuwa uamuzi huo unapaswa kutekelezwa kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watendaji hao," amesema.
Desemba 13, wakati Rais John Magufuli akizindua nyumba 300 za shirika hilo alieleza hujuma zinazofanywa na viongozi wa NHC, akiwemo Mchechu na Bodi ya wakurugenzi.
"Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako. Unanunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandikia kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako, mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya," alisema Rais Magufuli.
Katika hotuba yake, Rais alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi kwa maelezo kuwa wapo wanaotaka nafasi yake na kutumia wajumbe wa bodi na wanasiasa kumchafua.
"Wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu," alisema Rais.

Salam Za JK Kikwete baada ya Zanzibar Heroes kufuzu Fainali challenge cup



Baada ya timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ kufuzu kucheza fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge Cup 2017, Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Dr. Jakaya Kikwete ‘JK’ ametuma salam za pongezi kwa timu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa twitter JK ameandika: “Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu.”
Zanzibar waliifunga 2-1 timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwenye mchezo wa nufu fainali, ikumbukwe Uganda ndio walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo walilolitwaa mwaka 2015. Mwaka huohuo Uganda waliifunga Zanzibar 4-0 katika mchezo wa hatua ya makundi.
Mchezo wa fainali utachezwa Jumapili December 17, 2017 kati ya wenyeji Kenya dhidi ya Zanzibar.

Zitto Kabwe aiombea uanachama Zanzibar heroes



Mbunge wa Kigoma mjini Mh. Zitto Kabwe ambaye ni mdau mkubwa wa michezo hususani soka amekiombea aunachama wa FIFA chama cha soka cha Zanzibar ZFA.
Hatua hiyo imekuja baaada ya timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kutinga hatua ya fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge 2017 inayoendelea nchini Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook Zitto amefunguka ya moyoni akitaka ZFA iwe mwanachama wa shirikisho la soka la kimataifa FIFA pamoja na lile la Africa CAF angalau kwa miaka mitano na inaweza kupiga hatua ambazo TFF imeshindwa.
“Kama hatutaki Zanzibar kuwa Mwanachama wa FIFA kama ilivyo Scotland. Tuseme kwa miaka 5 ijayo kuanzia mwaka huu ZFA ndio mwanachama FIFA na CAF ili TFF ipate muda wa kujipanga. Ndani ya hiyo miaka 5 nawaambia Zanzibar itakwenda AFCON na hata Kombe la Dunia. #MsemaKweliMpenziWaMungu”, ameandika Zitto Kabwe.
Zitto ametoa mfano kuwa Zanzibar ingepata uanachama kamili wa FIFA kama ilivyo kwa nchi za Scotland pamoja na Wales ambazo pia ni nchi dada za taifa la Uingereza lakini zinatambuliwa na FIFA kama mataifa wanachama huku Uingereza ikitambulika kama England

Mwaijage Ameitaka kampuni ya mbolea kubadili mfumo



WAZIRI wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameitaka Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) kubadilisha mfumo wa utendaji ikiwa ni pamoja na kutoingia mikataba inayoweza kuisababishia serikali hasara, badala yake kuangalia wabia wanaoweza kuisaidia kujipanua na kupata faida kubwa zaidi.
Waziri Mwijage, aliyasema hayo juzi wakati akiizindua bodi mpya ya Wakurugenzi ya TFC, na kuongeza kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli, haiko tayari kuona taasisi zake za umma zikiingizwa katika mikataba mibovu na isiyokuwa na tija.
Pia aliagiza kwamba, baada ya kuizindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Egid Mbofu na wajumbe wake, waanze kazi mara moja na moja ya majukumu yao ya awali ni kuangalia ama kuipitia upya miokataba ambayo awalo iliingiwa na TFC.
Alisema TFC ikifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kujielekeza kwenye kazi zenye faida kubwa, itaweza kusaidia kasi ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini, na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya Taifa la uchumi wa kati na wa Viwanda.
"Tunatambua sekta ya kilimo ni nguzo muhimu kwa ajili ya uchumi wa TANZANIA, lakini haiwezi kuleta mafanikio makubwa kwa jamii, ikiwa TFC haitaweza kupewa uwezo na kuwafikia wakulima wengi zaidi", alisema Waziri Mwijage

Ramsey Noah asema pengo la kanumba haliwezi kuzibikka



NGULI wa filamu za Nigeria, Ramsey Noah amesema japokuwa miaka mingi imepita tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa msanii mahiri wa filamu za Kibongo, Steven Kanumba, bado pengo lake haliwezi kuzibika katika ulimwengu wa tasnia ya filamu.
Akizungumza katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam alikoenda kuzuru kaburi la marehemu Steven Kanumba leo Jumamosi, Desemba 16, 2017, Ramsey, alisema Kanumba aliondoka kipindi ambacho nyota yake ya mafanikio ndiyo kwanza ilikuwa imeanza kung’ara na kwamba, kila anapomkumbuka na mambo waliyoyafanya pamoja, huwa haamini kama hatamuona tena maishani mwake.
Ramsey alizuru hapa nchini kuhudhuria Tamasha la Kutambua Fursa kwa vijana lilioandaliwa chini ya Kampuni ya Sahara, tamasha hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), juzi Alhamisi.
Katika kuzuru kaburi hilo aliongozana na mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa, mdogo wa marehemu, Seth Bosco, wasanii wa filamu na mashabiki wa marehemu Kanumba.
Ramsey ndiye msanii wa kwanza mkubwa nchini Nigeria kufanya filamu na Mtanzania ambapo walifanya Moses na Devil’s Kingdom jambo ambalo liliunganisha Bongo Movie na Nollywood hivyo kutengeneza uhusiano imara kati ya nchi hizi mbili katika tasnia ya filamu.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 baada ya kutokea mzozo kati yake na aliyekuwa mpenzi wake, muigizazi Elizabeth Michael ‘Lulu’. Mwanadada huyo kwa sasa anatumiankifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na ya kumuua Kanumba bila kukusudia.

Kituo kimetakiwa kuwa kitovu Cha kuwaandaa na kuwanoa viongozi na taasisi nyengine


Arusha. Kituo cha maendeleo na ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Denmark (MS-TCDC) kilichopo Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha, kimetakiwa kuwa kitovu cha kuwaandaa na kuwanoa kikamilifu viongozi wa Serikali na taasisi nyingine barani Afrika.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hayo kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kituo hicho kinachotoa mafunzo ya uongozi, utawala bora, demokrasia na masuala ya kijamii.
Mghwira aliyewahi kuwa mwalimu na mjumbe wa bodi ya kituo hicho, amesema jana Ijumaa Desemba 15,2017 kuwa kituo kina manufaa mengi, utajiri wa maarifa, elimu na fursa pana ya kujifunza.
“Niwatie moyo watumishi kwa kadri inavyowezekana waje kusoma, binafsi baada ya kufundisha kisha nikaingia kwenye uongozi imenisaidia,” amesema.
Mghwira amesema, “Moja ya mambo ya kuangalia kwenye majadiliano ni kuhakikisha kituo kinafanya kazi na nini kifanyike miaka 50 ijayo, sekta hii ya uongozi ifanyiwe kazi kikamilifu watu waandaliwe na wanolewe kuwa viongozi.”
Amesema kituoni hapo alifundisha masomo ya uongozi na utawala, haki za binadamu katika uongozi, haki za mama na mtoto.
Mkuu huyo wa mkoa amesema baada ya Taifa kuingia kwenye mkataba mpya wa kimataifa wa mtoto mjadala uliokwenda kwenye asasi za kiraia na kusaidia kupatikana sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na Balozi wa Denmark Tanzanua, Einar Hebogard Jensen wito umetolewa kwa Serikali kushirikiana na kituo hicho kuendelea kuwajengea uwezo viongozi.
Macrine Rumanyika, mratibu wa muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama Mkoa wa Arusha amesema alijifunza mafunzo ya afya ya jamii na katika kufanya kazi alikabiliwa na changamoto zilizomsukuma kwenda kusoma MS-TCDC.
“Nilihitaji elimu ya maendeleo, hivyo tangu mwaka 1996 nimekuwa mwanafunzi hapa katika kozi fupi na ndefu na baadaye nikiwa hapa nilipata shahada ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MS TCDC, Emmanuel Munisi amesema wadau waliofanya kazi katika kituo hicho walikutakana kujadili na kutafakari miaka 50 iliyomalizika na mingine 50 ijayo.

Libya, badala ya kuwa mkimbizi unageuka kuwa ‘mtumwa’



Maelfu ya watu kutoka nchi kadhaa za Kiafrika, wengi vijana, wanazipa mgongo nchi zao na kutafuta bahati zao Ulaya. Hali ngumu za maisha katika nchi zao, umskini na migogoro na vita imewasukuma kutafuta hata njia za hatari na zisizokuwa za kisheria kufika Ulaya. Kuna waliofaulu na kutambuliwa rasmi kuwa wakimbizi walipofika Ulaya, lakini kuna wengi waliozama katika Bahari ya Mediterenia. Kuna wengi ambao wamepata masaibu makubwa hata kabla ya kutia mguu Ulaya.
Nchi ya Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011, imegeuka kuwa “mchafukoge”, haina serikali iliyo imara na makundi tafauti ya kijeshi yamekuwa yakikabana roho. Hali hiyo ya fujo imewarahisishia watu kutoka nchi kadhaa za Kifrika kukusanyika katika miji iliyo kwenye mwambao wa Libya katika Bahari ya Mediterenia wakitamani waivuke bahari hiyo ili wafike Ulaya. Sasa Libya imekuwa ni kituo kukubwa kinachotumiwa na walanguzi wa biashara ya wanadamu kuwakusanya wateja wao wanaowaahidi kwamba watawafikisha “Mtoni” (yaani Ulaya). Makundi ya kijeshi katika nchi hiyo hushirikiana na walanguzi hao kuwakabidhi wakimbizi wa kutoka nchi mbalimbali za Afrika chini ya Jangwa la Sahara katika masoko na watu hao kuuzwa kama “watumwa”.
Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ni kwamba hivi sasa wanaishi Libya hadi Waafrika milioni moja wakitokea nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara, zile za Ukanda wa Sahel, Somalia, Eritrea na Sudan. Maelfu yao wamezuiliwa katika kambi, tena chini ya hali ya kutisha isiyokuwa ya kiutu. Libya ilisaidiwa na Umoja wa Ulaya kwa kupatiwa boti za doria kulinda mipaka yake ya bahari na pia kuziokoa boti zinazobeba wakimbizi na ambazo ziko katika hatari ya kuzama. Msaada huo umewezesha kupungua idadi ya watu wa kutoka nchi chini ya Jangwa la Sahara kuivuka bahari kutoka watu 11,500 Julai na kufikia 6,300 Septemba mwaka huu. Hiyo ina maana kwamba idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa nguvu katika makambi ya Libya imeongezeka.
Malalamiko ya serikali za nchi za Afrika na pia mashirika ya kutetea hali za binadamu yalizidi pale televisheni ya Kimarekani, CNN, ilipotangaza na kuthibitisha hapo Novemba 14 kuweko Libya kambi za minada ambapo wakimbizi kutoka nchi za Kiafrika huuzwa kama watumwa. Jambo hilo, licha ya kwamba limeiaibisha Libya, lakini limetoa sura kwamba kuna serikali za nchi nyingine za Kiafrika zisizojali nini kinawasibu Waafrika wenzio huko Libya. Lakini, ilipojulikana kashfa hiyo, angalau serikali ya Rwanda ilitangaza kwamba itakuwa tayari kuwachukua Waafrika 30,000 wanaoshikiliwa katika kambi hizo.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Rwanda ilisema mwezi uliopita: “ Kama ilivyo dunia iliyobaki, Rwanda nayo pia imeshtushwa na picha zilizochapishwa na zinazoonyesha maafa yaliyoko huko ambapo Waafrika- wakiwamo wanawake na watoto- waliokamatwa walipokua njiani kwenda kutafuta himaya ya ukimbizi Ulaya wanashikiliwa. Kutokana na falsafa ya kisiasa ya Rwanda na kutokana na historia yetu wenyewe, sisi hatuwezi kunyamaza kimya wakati watu wanafanyiwa uovu wa kinyama wa kuuzwa kwa mnada kama vile wao ni wanyama wa mifugo.” Tangazo hilo la serikali ya Kigali liliendelea kusema: “Huenda Rwanda haiwezi kusema kwamba kila mtu anakaribishwa, lakini mlango wetu uko wazi.”
Gazeti la New Times la huko Kigali liliripoti baadaye kwamba serikali ya Rwanda na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kwamba nchi hiyo itachukuwa wakimbizi 30,000 na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Louise Mushukiwabo, aliandika katika mtandao wa Twitter kuhusu Waafrika wanaouzwa huko Libya: ” Rwanda ni nchi ndogo, lakini tutatafuta nafasi kwa ajili yenu.” Inasemakana Rwanda pia inafanya mazungumzo na Israel ili kuwachukua Wasudan na Waeritrea waliokwama huko Israel walipokuwa njiani kwenda Ulaya kutafuta ukimbizi. Moussa Faki Mahamat, mkuu wa Kamisheni ya AU, ameipongeza hatua ya Rwanda na akazitaka nchi wanachama wa AU, sekta ya kibinafsi na raia wa Kiafrika kuwaunga mkono ndugu zao wanaosononeka na kuteseka huko Libya.
Mwezi uliopita huko Abidjan, Ivory Coast, ulifanyika mkutano wa kilele wa kawaida baina ya Umoja wa Ulaya na Afrika ambao ulijishughulisha sana na siasa ya uhamiaji pamoja na kashfa hii ya kuuzwa na kununuliwa watumwa huko Libya. Pia, serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa iliahidiwa kusaidiwa ili iondokane na kambi hizo. Kutokana na malalamiko kutoka mashirika ya kiraia, siku chache zilizopita nchi zaidi za Kiafrika zimeondosha mabalozi wao kutoka Libya na zimeutaka Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague zilishughulikie suala hilo la unyama na uhalifu unaofanywa Libya.
Habari ya kuweko makambi ya utumwa nchini Libya si mpya, ila sasa malalamiko yaliotolewa ni makali zaidi, na mbinu zinazotumiwa na hao walanguzi wa biashara ya wanadamu ni za kikatili zaidi. Pia, licha ya nchi za Ulaya kulalamika juu ya kuweko kambi hizo, lakini nchi hizohizo zinafunga kabisa milango kwa wakimbizi. Nchi hizo za Ulaya zinataka hata wale wanaoomba ukimbizi ambao tayari wameshakanyaga ardhi ya Ulaya warejeshwe makwao. Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Uhamiaji (IOM), limetaja juu ya kuweko masoko ya watumwa huko Libya na limesema kwamba mustakbali wa watu hao haujulikani, si leo wala si kesho. Wengi wao wako karibu na maeneo ya Kusini kabisa ya Ulaya. IOM ilisema isitarajiwe kwamba hali ya mambo itabadilika.
Kwa mujibu wa mashahidi walioshuhudia minada hiyo ya kuuzwa binadamu huko Libya ni kwamba katika masoko hayo watu huuzwa na kununuliwa, halafu hupelekwa kufanya kazi ngumu. Watu wanaofanya biashara ya magendo ya binadamu humuuza kila mkimbizi kwa dola 200 hadi 500. Pia, hulazimihswa kuwapigia simu jamaa zao ili watume fedha zitakazowezesha wajikomboe. Pale familia zao wanaposikia sauti zao zikilia ndani ya simu, baadhi ya wakati fedha hutumwa. Hivyo ndivyo walanguzi wa biashara hii inayoshamiri wanavyotajirika. Wakimbizi ambao hawana bahati ya kutumiwa fedha za ukombozi na jamaa zao hunyimwa chakula hadi wanakufa. Kwa mujibu wa IOM hayo ni maelezo ya watu walioko sasa Niger na ambao wamerejea kutoka Libya.
Libya iliyosambaratika, ambapo haijulikani serikali gani inayoshika hatamu ni taabu kuinusuru. Nchini humo hakuna sheria, kila mtu anafanya anavyotaka ni shida kukomesha uuzaji na ununuzi wa binadamu, licha ya kuweko malalamiko mengi duniani.
Mara nyingi wanasiasa hujifanya “hamnazo”, hujitoa kimasomaso, bila ya kujali kama wanasiasa hao ni Waafrika au Wazungu, hulipuuza tatizo hasa ambalo liko machoni mwao. Viongozi wa Ulaya na Afrika wanatambua kuwapo Waafrika wanaokimbilia Ulaya ni kutokana na hali ngumu ya maisha katika nchi wanakotokea.
Karibu tutaingia mwaka 2018. Mambo hayaonyeshi yatabadilika, watu zaidi watarajiwe watajaribu kwa kila njia kuingia Ulaya kuliko miaka iliopita. Watajaribu kuivuka Bahari ya Mediterenia kwa kutumia boti za mbao zilizo mbovu na kongwe. Kwa wengi wao bahari hiyo itakuwa kaburi lao. Baada ya baridi ya sasa kupungua kidogo Ulaya, msimu wa kuangamia Waafrika wengi katika bahari hiyo utaanza. Inanihuzunisha.
Source: Mwananchi

TANESCO yaboresha mfumo Wa malipo




Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeboresha mfumo wa malipo ya ankara na kuanzia sasa wateja wa mita za kawaida na wanaoomba kuunganishiwa umeme watalazimika kufanya malipo kwa mfumo wa kielektroniki.
Evaristo Winyasi, kaimu meneja wa Tehama, utafiti na utengenezaji mifumo wa Tanesco amesema mfumo huo umeanza Desemba 14,2017 kwa mikoa minne ya shirika hilo iliyopo Dar es Salaam na Pwani.
Amesema lengo la mfumo huo ni kutekeleza kwa vitendo matakwa ya sheria iliyopitishwa na Bunge, hivyo shirika limejiunga na mfumo huo ili kuhudumia wateja kwa kutumia benki na mitandao ya simu.
“Tumeshaungana na mfumo wa malipo ya Serikali wa GPG katika benki za NMB, CRDB na NBC. Kila benki imetoa njia zote za malipo ikiwemo ATM na simu,” alisema Winyasi jana Ijumaa Desemba 15,2017.
Amesema wateja wa Tanesco watafanya malipo kwa kutumia mitandao ya simu ikiwemo Airtel Money, M-Pesa na Tigo Pesa.
Winyasi amesema mteja hawezi kukamilisha malipo pasipo kufika ofisi za malipo na kupewa deni analodaiwa likiwa limeambatana na kumbukumbu namba ambayo itatumika kulipia kwa mfumo wa kielektroniki.
Meneja Masoko wa Tanesco, Mussa Chowo amesema madhumuni ya kujiunga na mfumo huo wa Serikali ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya shirika.
Chowo amesema mfumo huo hautawahusu wateja wa mita za Luku. Amesema wataendelea kupokea malipo kwa wateja watakaolipia kwenye ofisi, huku wakipewa maelekezo na ukomo.
“Wiki tatu kutoka sasa; Januari (2018) kwa mikoa ya Dar es Salaam tutasitisha malipo kwenye ofisi na wateja watayafanya kupitia benki na mitandao ya simu,” amesema.

Ramsey Noah Atua BONGO azungumza na wanafunzi UDSM



Mwigizaji na mtayarishaji wa filamu wa Nigeria, Ramsey Nouh amewataka vijana wa Tanzania kuwa na shauku ya mafanikio na kutokubali kurudishwa nyuma katika juhudi za kujikwamua.
Nouah ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi wa uhamasishaji na kuwajengea uwezo vijana, kutambua na kusimamia ndoto zao unaoratibiwa na kampuni ya mafuta ya Sahara Group ukilenga kuwafikia zaidi ya vijana 10 milioni.
Nouah ambaye pia ni balozi wa Sahara Group amesema hakuna mafanikio ambayo yanaweza kufikiwa bila kupitia changamoto hivyo ni muhimu kwa vijana kukabiliana nazo bila kuyumbishwa.
Akijitolea mfano amesema mafanikio aliyoyapata hakuja kwa urahisi kwani alipigana na kusimamia alichokuwa akiamini.
“Imani yangu ilikuwa kwenye filamu, nilikuwa na shauku ya kufanya vizuri kwenye tasnia hiyo, sikujali changamoto nilizokutana nazo. Nilisimama na kufanya kazi kwa juhudi zaidi hadi pale watu walipoanza kunielewa,”
Sambamba na Ramsey, wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na vijana hao ni mjasiriamali Jokate Mwegelo na mshindi wa Big Brother Africa mwaka 2014 Idris Sultan.
Kwa upande wake Jokate aliwataka vijana kuwa wabunifu na kutumia mawazo katika kuleta mabadiliko na maendeleo kwenye jamii.
“Ni nadra sana ukafanikiwa kwa kuiga kitu cha mwingine. Tujaribu kuwa na ubunifu, nilipomaliza chuo nilipata ufaulu mzuri ulioniwezesha kuendelea kubaki kufundisha chuoni lakini sikutaka nikafungua kampuni ya urembo, wengi walinishangaa wakaniona kama nimechanganyikiwa. Hilo halikunipa shida kwa sababu kichwani mwangu nilijua nini nataka,

maji maji yaibomoa ngome ya lipuli FC


Klabu ya Majimaji imefanikiwa kuipata saini ya mshambuliaji Waziri Ramadhan kutoka Lipuli FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Meneja Mkuu wa Majimaji, Geofrey Mvula alisema kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Peter Mhina alihitaji kufanya usajili wa mshambuliaji pekee ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.
"Tumefunga usajili kwa mchezaji huyo pekee na hawa wengine tutaendelea nao kwani tumeona wako vizuri.”
Mvula alisema Ramadhan amefanyiwa uhamisho kutoka Lipuli lakini alikuwa na mkataba na wanapaluhengo nao.

Kumbe Zari na Kajala hawapiki chungu kimoja,,,



Baada ya kuenea taarifa kwa muda mrefu kuwa hawapikiki chungu kimoja, staa wa filamu Bongo, Kajala Masanja amedhihirisha msemo huo baada ya kumkimbia ukumbini mjasiriamali maarufu Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.
Kwa mujibu wa chanzo kilichokuwepo eneo la tukio hilo lililojiri katika Ukumbi Cardinal Rugambwa Hall maeneo ya Oysterbay hivi karibuni, Kajala alikuwa mmoja kati ya mastaa waalikwa katika sherehe ya harusi na alipofika ukumbini alikaa siti ya nyuma.
“Hatukuwa tukijua kama Kajala naye amealikwa. Aliingia ukumbini na kusalimiana na mastaa wenzake kadhaa kisha akaenda kuketi siti ya nyuma kabisa akifuatilia sherehe inavyoenda,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kiliendelea kupenyeza ubuyu kuwa, wakati shangwe zikiendelea ukumbini hapo ilifika muda wa kufungua shampeni ambapo mastaa kibao walienda mbele akiwemo msanii wa Bongo Fleva pamoja na mzazi mwenziye, Zari na baada ya muda MC alimuita Kajala naye ajumuike nao.
“Hapo ndipo Kajala akaona isiwe tabu, akainama na kupitia mlango wa nyuma kisha akaondoka zake na kuwaacha na mshangao,” kilimaliza chanzo.
Akizungumzi ishu hiyo Kajala alisema “Ni kweli nilikwenda kwenye hiyo harusi na nikaitwa mbele lakini niliamua kuondoka zangu kwa sababu sikutaka kuonana na baadhi ya watu (Zari).”