WAZIRI wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameitaka Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) kubadilisha mfumo wa utendaji ikiwa ni pamoja na kutoingia mikataba inayoweza kuisababishia serikali hasara, badala yake kuangalia wabia wanaoweza kuisaidia kujipanua na kupata faida kubwa zaidi.
Waziri Mwijage, aliyasema hayo juzi wakati akiizindua bodi mpya ya Wakurugenzi ya TFC, na kuongeza kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli, haiko tayari kuona taasisi zake za umma zikiingizwa katika mikataba mibovu na isiyokuwa na tija.
Pia aliagiza kwamba, baada ya kuizindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Egid Mbofu na wajumbe wake, waanze kazi mara moja na moja ya majukumu yao ya awali ni kuangalia ama kuipitia upya miokataba ambayo awalo iliingiwa na TFC.
Alisema TFC ikifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kujielekeza kwenye kazi zenye faida kubwa, itaweza kusaidia kasi ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini, na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya Taifa la uchumi wa kati na wa Viwanda.
"Tunatambua sekta ya kilimo ni nguzo muhimu kwa ajili ya uchumi wa TANZANIA, lakini haiwezi kuleta mafanikio makubwa kwa jamii, ikiwa TFC haitaweza kupewa uwezo na kuwafikia wakulima wengi zaidi", alisema Waziri Mwijage
No comments:
Post a Comment