Arusha. Kituo cha maendeleo na ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Denmark (MS-TCDC) kilichopo Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha, kimetakiwa kuwa kitovu cha kuwaandaa na kuwanoa kikamilifu viongozi wa Serikali na taasisi nyingine barani Afrika.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hayo kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kituo hicho kinachotoa mafunzo ya uongozi, utawala bora, demokrasia na masuala ya kijamii.
Mghwira aliyewahi kuwa mwalimu na mjumbe wa bodi ya kituo hicho, amesema jana Ijumaa Desemba 15,2017 kuwa kituo kina manufaa mengi, utajiri wa maarifa, elimu na fursa pana ya kujifunza.
“Niwatie moyo watumishi kwa kadri inavyowezekana waje kusoma, binafsi baada ya kufundisha kisha nikaingia kwenye uongozi imenisaidia,” amesema.
Mghwira amesema, “Moja ya mambo ya kuangalia kwenye majadiliano ni kuhakikisha kituo kinafanya kazi na nini kifanyike miaka 50 ijayo, sekta hii ya uongozi ifanyiwe kazi kikamilifu watu waandaliwe na wanolewe kuwa viongozi.”
Amesema kituoni hapo alifundisha masomo ya uongozi na utawala, haki za binadamu katika uongozi, haki za mama na mtoto.
Mkuu huyo wa mkoa amesema baada ya Taifa kuingia kwenye mkataba mpya wa kimataifa wa mtoto mjadala uliokwenda kwenye asasi za kiraia na kusaidia kupatikana sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na Balozi wa Denmark Tanzanua, Einar Hebogard Jensen wito umetolewa kwa Serikali kushirikiana na kituo hicho kuendelea kuwajengea uwezo viongozi.
Macrine Rumanyika, mratibu wa muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama Mkoa wa Arusha amesema alijifunza mafunzo ya afya ya jamii na katika kufanya kazi alikabiliwa na changamoto zilizomsukuma kwenda kusoma MS-TCDC.
“Nilihitaji elimu ya maendeleo, hivyo tangu mwaka 1996 nimekuwa mwanafunzi hapa katika kozi fupi na ndefu na baadaye nikiwa hapa nilipata shahada ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MS TCDC, Emmanuel Munisi amesema wadau waliofanya kazi katika kituo hicho walikutakana kujadili na kutafakari miaka 50 iliyomalizika na mingine 50 ijayo.
No comments:
Post a Comment