Saturday, 16 December 2017

Waziri Lukuvi ampiga STOP mkurugenzi mkuu NHC



Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesimamishwa kazi.
Taarifa ya kusimamishwa kazi kiongozi huyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 16,2017 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akieleza uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Mchechu aliteuliwa kuliongoza shirika hilo Machi Mosi, 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CBA.
Taarifa ya Dk Abbasi imesema Lukuvi amechukua uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.
Mbali na Mchechu, Lukuvi ameitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Mikoa na Utawala, Raymond Mndolwa.
"Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika imesisitiza kuwa uamuzi huo unapaswa kutekelezwa kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watendaji hao," amesema.
Desemba 13, wakati Rais John Magufuli akizindua nyumba 300 za shirika hilo alieleza hujuma zinazofanywa na viongozi wa NHC, akiwemo Mchechu na Bodi ya wakurugenzi.
"Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako. Unanunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandikia kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako, mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya," alisema Rais Magufuli.
Katika hotuba yake, Rais alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi kwa maelezo kuwa wapo wanaotaka nafasi yake na kutumia wajumbe wa bodi na wanasiasa kumchafua.
"Wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu," alisema Rais.

Salam Za JK Kikwete baada ya Zanzibar Heroes kufuzu Fainali challenge cup



Baada ya timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ kufuzu kucheza fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge Cup 2017, Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Dr. Jakaya Kikwete ‘JK’ ametuma salam za pongezi kwa timu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa twitter JK ameandika: “Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu.”
Zanzibar waliifunga 2-1 timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwenye mchezo wa nufu fainali, ikumbukwe Uganda ndio walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo walilolitwaa mwaka 2015. Mwaka huohuo Uganda waliifunga Zanzibar 4-0 katika mchezo wa hatua ya makundi.
Mchezo wa fainali utachezwa Jumapili December 17, 2017 kati ya wenyeji Kenya dhidi ya Zanzibar.

Zitto Kabwe aiombea uanachama Zanzibar heroes



Mbunge wa Kigoma mjini Mh. Zitto Kabwe ambaye ni mdau mkubwa wa michezo hususani soka amekiombea aunachama wa FIFA chama cha soka cha Zanzibar ZFA.
Hatua hiyo imekuja baaada ya timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kutinga hatua ya fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge 2017 inayoendelea nchini Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook Zitto amefunguka ya moyoni akitaka ZFA iwe mwanachama wa shirikisho la soka la kimataifa FIFA pamoja na lile la Africa CAF angalau kwa miaka mitano na inaweza kupiga hatua ambazo TFF imeshindwa.
“Kama hatutaki Zanzibar kuwa Mwanachama wa FIFA kama ilivyo Scotland. Tuseme kwa miaka 5 ijayo kuanzia mwaka huu ZFA ndio mwanachama FIFA na CAF ili TFF ipate muda wa kujipanga. Ndani ya hiyo miaka 5 nawaambia Zanzibar itakwenda AFCON na hata Kombe la Dunia. #MsemaKweliMpenziWaMungu”, ameandika Zitto Kabwe.
Zitto ametoa mfano kuwa Zanzibar ingepata uanachama kamili wa FIFA kama ilivyo kwa nchi za Scotland pamoja na Wales ambazo pia ni nchi dada za taifa la Uingereza lakini zinatambuliwa na FIFA kama mataifa wanachama huku Uingereza ikitambulika kama England

Mwaijage Ameitaka kampuni ya mbolea kubadili mfumo



WAZIRI wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameitaka Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) kubadilisha mfumo wa utendaji ikiwa ni pamoja na kutoingia mikataba inayoweza kuisababishia serikali hasara, badala yake kuangalia wabia wanaoweza kuisaidia kujipanua na kupata faida kubwa zaidi.
Waziri Mwijage, aliyasema hayo juzi wakati akiizindua bodi mpya ya Wakurugenzi ya TFC, na kuongeza kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli, haiko tayari kuona taasisi zake za umma zikiingizwa katika mikataba mibovu na isiyokuwa na tija.
Pia aliagiza kwamba, baada ya kuizindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Egid Mbofu na wajumbe wake, waanze kazi mara moja na moja ya majukumu yao ya awali ni kuangalia ama kuipitia upya miokataba ambayo awalo iliingiwa na TFC.
Alisema TFC ikifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kujielekeza kwenye kazi zenye faida kubwa, itaweza kusaidia kasi ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini, na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya Taifa la uchumi wa kati na wa Viwanda.
"Tunatambua sekta ya kilimo ni nguzo muhimu kwa ajili ya uchumi wa TANZANIA, lakini haiwezi kuleta mafanikio makubwa kwa jamii, ikiwa TFC haitaweza kupewa uwezo na kuwafikia wakulima wengi zaidi", alisema Waziri Mwijage

Ramsey Noah asema pengo la kanumba haliwezi kuzibikka



NGULI wa filamu za Nigeria, Ramsey Noah amesema japokuwa miaka mingi imepita tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa msanii mahiri wa filamu za Kibongo, Steven Kanumba, bado pengo lake haliwezi kuzibika katika ulimwengu wa tasnia ya filamu.
Akizungumza katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam alikoenda kuzuru kaburi la marehemu Steven Kanumba leo Jumamosi, Desemba 16, 2017, Ramsey, alisema Kanumba aliondoka kipindi ambacho nyota yake ya mafanikio ndiyo kwanza ilikuwa imeanza kung’ara na kwamba, kila anapomkumbuka na mambo waliyoyafanya pamoja, huwa haamini kama hatamuona tena maishani mwake.
Ramsey alizuru hapa nchini kuhudhuria Tamasha la Kutambua Fursa kwa vijana lilioandaliwa chini ya Kampuni ya Sahara, tamasha hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), juzi Alhamisi.
Katika kuzuru kaburi hilo aliongozana na mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa, mdogo wa marehemu, Seth Bosco, wasanii wa filamu na mashabiki wa marehemu Kanumba.
Ramsey ndiye msanii wa kwanza mkubwa nchini Nigeria kufanya filamu na Mtanzania ambapo walifanya Moses na Devil’s Kingdom jambo ambalo liliunganisha Bongo Movie na Nollywood hivyo kutengeneza uhusiano imara kati ya nchi hizi mbili katika tasnia ya filamu.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 baada ya kutokea mzozo kati yake na aliyekuwa mpenzi wake, muigizazi Elizabeth Michael ‘Lulu’. Mwanadada huyo kwa sasa anatumiankifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na ya kumuua Kanumba bila kukusudia.

Kituo kimetakiwa kuwa kitovu Cha kuwaandaa na kuwanoa viongozi na taasisi nyengine


Arusha. Kituo cha maendeleo na ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Denmark (MS-TCDC) kilichopo Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha, kimetakiwa kuwa kitovu cha kuwaandaa na kuwanoa kikamilifu viongozi wa Serikali na taasisi nyingine barani Afrika.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hayo kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kituo hicho kinachotoa mafunzo ya uongozi, utawala bora, demokrasia na masuala ya kijamii.
Mghwira aliyewahi kuwa mwalimu na mjumbe wa bodi ya kituo hicho, amesema jana Ijumaa Desemba 15,2017 kuwa kituo kina manufaa mengi, utajiri wa maarifa, elimu na fursa pana ya kujifunza.
“Niwatie moyo watumishi kwa kadri inavyowezekana waje kusoma, binafsi baada ya kufundisha kisha nikaingia kwenye uongozi imenisaidia,” amesema.
Mghwira amesema, “Moja ya mambo ya kuangalia kwenye majadiliano ni kuhakikisha kituo kinafanya kazi na nini kifanyike miaka 50 ijayo, sekta hii ya uongozi ifanyiwe kazi kikamilifu watu waandaliwe na wanolewe kuwa viongozi.”
Amesema kituoni hapo alifundisha masomo ya uongozi na utawala, haki za binadamu katika uongozi, haki za mama na mtoto.
Mkuu huyo wa mkoa amesema baada ya Taifa kuingia kwenye mkataba mpya wa kimataifa wa mtoto mjadala uliokwenda kwenye asasi za kiraia na kusaidia kupatikana sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na Balozi wa Denmark Tanzanua, Einar Hebogard Jensen wito umetolewa kwa Serikali kushirikiana na kituo hicho kuendelea kuwajengea uwezo viongozi.
Macrine Rumanyika, mratibu wa muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama Mkoa wa Arusha amesema alijifunza mafunzo ya afya ya jamii na katika kufanya kazi alikabiliwa na changamoto zilizomsukuma kwenda kusoma MS-TCDC.
“Nilihitaji elimu ya maendeleo, hivyo tangu mwaka 1996 nimekuwa mwanafunzi hapa katika kozi fupi na ndefu na baadaye nikiwa hapa nilipata shahada ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MS TCDC, Emmanuel Munisi amesema wadau waliofanya kazi katika kituo hicho walikutakana kujadili na kutafakari miaka 50 iliyomalizika na mingine 50 ijayo.

Libya, badala ya kuwa mkimbizi unageuka kuwa ‘mtumwa’



Maelfu ya watu kutoka nchi kadhaa za Kiafrika, wengi vijana, wanazipa mgongo nchi zao na kutafuta bahati zao Ulaya. Hali ngumu za maisha katika nchi zao, umskini na migogoro na vita imewasukuma kutafuta hata njia za hatari na zisizokuwa za kisheria kufika Ulaya. Kuna waliofaulu na kutambuliwa rasmi kuwa wakimbizi walipofika Ulaya, lakini kuna wengi waliozama katika Bahari ya Mediterenia. Kuna wengi ambao wamepata masaibu makubwa hata kabla ya kutia mguu Ulaya.
Nchi ya Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011, imegeuka kuwa “mchafukoge”, haina serikali iliyo imara na makundi tafauti ya kijeshi yamekuwa yakikabana roho. Hali hiyo ya fujo imewarahisishia watu kutoka nchi kadhaa za Kifrika kukusanyika katika miji iliyo kwenye mwambao wa Libya katika Bahari ya Mediterenia wakitamani waivuke bahari hiyo ili wafike Ulaya. Sasa Libya imekuwa ni kituo kukubwa kinachotumiwa na walanguzi wa biashara ya wanadamu kuwakusanya wateja wao wanaowaahidi kwamba watawafikisha “Mtoni” (yaani Ulaya). Makundi ya kijeshi katika nchi hiyo hushirikiana na walanguzi hao kuwakabidhi wakimbizi wa kutoka nchi mbalimbali za Afrika chini ya Jangwa la Sahara katika masoko na watu hao kuuzwa kama “watumwa”.
Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ni kwamba hivi sasa wanaishi Libya hadi Waafrika milioni moja wakitokea nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara, zile za Ukanda wa Sahel, Somalia, Eritrea na Sudan. Maelfu yao wamezuiliwa katika kambi, tena chini ya hali ya kutisha isiyokuwa ya kiutu. Libya ilisaidiwa na Umoja wa Ulaya kwa kupatiwa boti za doria kulinda mipaka yake ya bahari na pia kuziokoa boti zinazobeba wakimbizi na ambazo ziko katika hatari ya kuzama. Msaada huo umewezesha kupungua idadi ya watu wa kutoka nchi chini ya Jangwa la Sahara kuivuka bahari kutoka watu 11,500 Julai na kufikia 6,300 Septemba mwaka huu. Hiyo ina maana kwamba idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa nguvu katika makambi ya Libya imeongezeka.
Malalamiko ya serikali za nchi za Afrika na pia mashirika ya kutetea hali za binadamu yalizidi pale televisheni ya Kimarekani, CNN, ilipotangaza na kuthibitisha hapo Novemba 14 kuweko Libya kambi za minada ambapo wakimbizi kutoka nchi za Kiafrika huuzwa kama watumwa. Jambo hilo, licha ya kwamba limeiaibisha Libya, lakini limetoa sura kwamba kuna serikali za nchi nyingine za Kiafrika zisizojali nini kinawasibu Waafrika wenzio huko Libya. Lakini, ilipojulikana kashfa hiyo, angalau serikali ya Rwanda ilitangaza kwamba itakuwa tayari kuwachukua Waafrika 30,000 wanaoshikiliwa katika kambi hizo.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Rwanda ilisema mwezi uliopita: “ Kama ilivyo dunia iliyobaki, Rwanda nayo pia imeshtushwa na picha zilizochapishwa na zinazoonyesha maafa yaliyoko huko ambapo Waafrika- wakiwamo wanawake na watoto- waliokamatwa walipokua njiani kwenda kutafuta himaya ya ukimbizi Ulaya wanashikiliwa. Kutokana na falsafa ya kisiasa ya Rwanda na kutokana na historia yetu wenyewe, sisi hatuwezi kunyamaza kimya wakati watu wanafanyiwa uovu wa kinyama wa kuuzwa kwa mnada kama vile wao ni wanyama wa mifugo.” Tangazo hilo la serikali ya Kigali liliendelea kusema: “Huenda Rwanda haiwezi kusema kwamba kila mtu anakaribishwa, lakini mlango wetu uko wazi.”
Gazeti la New Times la huko Kigali liliripoti baadaye kwamba serikali ya Rwanda na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kwamba nchi hiyo itachukuwa wakimbizi 30,000 na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Louise Mushukiwabo, aliandika katika mtandao wa Twitter kuhusu Waafrika wanaouzwa huko Libya: ” Rwanda ni nchi ndogo, lakini tutatafuta nafasi kwa ajili yenu.” Inasemakana Rwanda pia inafanya mazungumzo na Israel ili kuwachukua Wasudan na Waeritrea waliokwama huko Israel walipokuwa njiani kwenda Ulaya kutafuta ukimbizi. Moussa Faki Mahamat, mkuu wa Kamisheni ya AU, ameipongeza hatua ya Rwanda na akazitaka nchi wanachama wa AU, sekta ya kibinafsi na raia wa Kiafrika kuwaunga mkono ndugu zao wanaosononeka na kuteseka huko Libya.
Mwezi uliopita huko Abidjan, Ivory Coast, ulifanyika mkutano wa kilele wa kawaida baina ya Umoja wa Ulaya na Afrika ambao ulijishughulisha sana na siasa ya uhamiaji pamoja na kashfa hii ya kuuzwa na kununuliwa watumwa huko Libya. Pia, serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa iliahidiwa kusaidiwa ili iondokane na kambi hizo. Kutokana na malalamiko kutoka mashirika ya kiraia, siku chache zilizopita nchi zaidi za Kiafrika zimeondosha mabalozi wao kutoka Libya na zimeutaka Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague zilishughulikie suala hilo la unyama na uhalifu unaofanywa Libya.
Habari ya kuweko makambi ya utumwa nchini Libya si mpya, ila sasa malalamiko yaliotolewa ni makali zaidi, na mbinu zinazotumiwa na hao walanguzi wa biashara ya wanadamu ni za kikatili zaidi. Pia, licha ya nchi za Ulaya kulalamika juu ya kuweko kambi hizo, lakini nchi hizohizo zinafunga kabisa milango kwa wakimbizi. Nchi hizo za Ulaya zinataka hata wale wanaoomba ukimbizi ambao tayari wameshakanyaga ardhi ya Ulaya warejeshwe makwao. Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Uhamiaji (IOM), limetaja juu ya kuweko masoko ya watumwa huko Libya na limesema kwamba mustakbali wa watu hao haujulikani, si leo wala si kesho. Wengi wao wako karibu na maeneo ya Kusini kabisa ya Ulaya. IOM ilisema isitarajiwe kwamba hali ya mambo itabadilika.
Kwa mujibu wa mashahidi walioshuhudia minada hiyo ya kuuzwa binadamu huko Libya ni kwamba katika masoko hayo watu huuzwa na kununuliwa, halafu hupelekwa kufanya kazi ngumu. Watu wanaofanya biashara ya magendo ya binadamu humuuza kila mkimbizi kwa dola 200 hadi 500. Pia, hulazimihswa kuwapigia simu jamaa zao ili watume fedha zitakazowezesha wajikomboe. Pale familia zao wanaposikia sauti zao zikilia ndani ya simu, baadhi ya wakati fedha hutumwa. Hivyo ndivyo walanguzi wa biashara hii inayoshamiri wanavyotajirika. Wakimbizi ambao hawana bahati ya kutumiwa fedha za ukombozi na jamaa zao hunyimwa chakula hadi wanakufa. Kwa mujibu wa IOM hayo ni maelezo ya watu walioko sasa Niger na ambao wamerejea kutoka Libya.
Libya iliyosambaratika, ambapo haijulikani serikali gani inayoshika hatamu ni taabu kuinusuru. Nchini humo hakuna sheria, kila mtu anafanya anavyotaka ni shida kukomesha uuzaji na ununuzi wa binadamu, licha ya kuweko malalamiko mengi duniani.
Mara nyingi wanasiasa hujifanya “hamnazo”, hujitoa kimasomaso, bila ya kujali kama wanasiasa hao ni Waafrika au Wazungu, hulipuuza tatizo hasa ambalo liko machoni mwao. Viongozi wa Ulaya na Afrika wanatambua kuwapo Waafrika wanaokimbilia Ulaya ni kutokana na hali ngumu ya maisha katika nchi wanakotokea.
Karibu tutaingia mwaka 2018. Mambo hayaonyeshi yatabadilika, watu zaidi watarajiwe watajaribu kwa kila njia kuingia Ulaya kuliko miaka iliopita. Watajaribu kuivuka Bahari ya Mediterenia kwa kutumia boti za mbao zilizo mbovu na kongwe. Kwa wengi wao bahari hiyo itakuwa kaburi lao. Baada ya baridi ya sasa kupungua kidogo Ulaya, msimu wa kuangamia Waafrika wengi katika bahari hiyo utaanza. Inanihuzunisha.
Source: Mwananchi

TANESCO yaboresha mfumo Wa malipo




Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeboresha mfumo wa malipo ya ankara na kuanzia sasa wateja wa mita za kawaida na wanaoomba kuunganishiwa umeme watalazimika kufanya malipo kwa mfumo wa kielektroniki.
Evaristo Winyasi, kaimu meneja wa Tehama, utafiti na utengenezaji mifumo wa Tanesco amesema mfumo huo umeanza Desemba 14,2017 kwa mikoa minne ya shirika hilo iliyopo Dar es Salaam na Pwani.
Amesema lengo la mfumo huo ni kutekeleza kwa vitendo matakwa ya sheria iliyopitishwa na Bunge, hivyo shirika limejiunga na mfumo huo ili kuhudumia wateja kwa kutumia benki na mitandao ya simu.
“Tumeshaungana na mfumo wa malipo ya Serikali wa GPG katika benki za NMB, CRDB na NBC. Kila benki imetoa njia zote za malipo ikiwemo ATM na simu,” alisema Winyasi jana Ijumaa Desemba 15,2017.
Amesema wateja wa Tanesco watafanya malipo kwa kutumia mitandao ya simu ikiwemo Airtel Money, M-Pesa na Tigo Pesa.
Winyasi amesema mteja hawezi kukamilisha malipo pasipo kufika ofisi za malipo na kupewa deni analodaiwa likiwa limeambatana na kumbukumbu namba ambayo itatumika kulipia kwa mfumo wa kielektroniki.
Meneja Masoko wa Tanesco, Mussa Chowo amesema madhumuni ya kujiunga na mfumo huo wa Serikali ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya shirika.
Chowo amesema mfumo huo hautawahusu wateja wa mita za Luku. Amesema wataendelea kupokea malipo kwa wateja watakaolipia kwenye ofisi, huku wakipewa maelekezo na ukomo.
“Wiki tatu kutoka sasa; Januari (2018) kwa mikoa ya Dar es Salaam tutasitisha malipo kwenye ofisi na wateja watayafanya kupitia benki na mitandao ya simu,” amesema.

Ramsey Noah Atua BONGO azungumza na wanafunzi UDSM



Mwigizaji na mtayarishaji wa filamu wa Nigeria, Ramsey Nouh amewataka vijana wa Tanzania kuwa na shauku ya mafanikio na kutokubali kurudishwa nyuma katika juhudi za kujikwamua.
Nouah ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi wa uhamasishaji na kuwajengea uwezo vijana, kutambua na kusimamia ndoto zao unaoratibiwa na kampuni ya mafuta ya Sahara Group ukilenga kuwafikia zaidi ya vijana 10 milioni.
Nouah ambaye pia ni balozi wa Sahara Group amesema hakuna mafanikio ambayo yanaweza kufikiwa bila kupitia changamoto hivyo ni muhimu kwa vijana kukabiliana nazo bila kuyumbishwa.
Akijitolea mfano amesema mafanikio aliyoyapata hakuja kwa urahisi kwani alipigana na kusimamia alichokuwa akiamini.
“Imani yangu ilikuwa kwenye filamu, nilikuwa na shauku ya kufanya vizuri kwenye tasnia hiyo, sikujali changamoto nilizokutana nazo. Nilisimama na kufanya kazi kwa juhudi zaidi hadi pale watu walipoanza kunielewa,”
Sambamba na Ramsey, wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na vijana hao ni mjasiriamali Jokate Mwegelo na mshindi wa Big Brother Africa mwaka 2014 Idris Sultan.
Kwa upande wake Jokate aliwataka vijana kuwa wabunifu na kutumia mawazo katika kuleta mabadiliko na maendeleo kwenye jamii.
“Ni nadra sana ukafanikiwa kwa kuiga kitu cha mwingine. Tujaribu kuwa na ubunifu, nilipomaliza chuo nilipata ufaulu mzuri ulioniwezesha kuendelea kubaki kufundisha chuoni lakini sikutaka nikafungua kampuni ya urembo, wengi walinishangaa wakaniona kama nimechanganyikiwa. Hilo halikunipa shida kwa sababu kichwani mwangu nilijua nini nataka,

maji maji yaibomoa ngome ya lipuli FC


Klabu ya Majimaji imefanikiwa kuipata saini ya mshambuliaji Waziri Ramadhan kutoka Lipuli FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Meneja Mkuu wa Majimaji, Geofrey Mvula alisema kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Peter Mhina alihitaji kufanya usajili wa mshambuliaji pekee ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.
"Tumefunga usajili kwa mchezaji huyo pekee na hawa wengine tutaendelea nao kwani tumeona wako vizuri.”
Mvula alisema Ramadhan amefanyiwa uhamisho kutoka Lipuli lakini alikuwa na mkataba na wanapaluhengo nao.

Kumbe Zari na Kajala hawapiki chungu kimoja,,,



Baada ya kuenea taarifa kwa muda mrefu kuwa hawapikiki chungu kimoja, staa wa filamu Bongo, Kajala Masanja amedhihirisha msemo huo baada ya kumkimbia ukumbini mjasiriamali maarufu Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.
Kwa mujibu wa chanzo kilichokuwepo eneo la tukio hilo lililojiri katika Ukumbi Cardinal Rugambwa Hall maeneo ya Oysterbay hivi karibuni, Kajala alikuwa mmoja kati ya mastaa waalikwa katika sherehe ya harusi na alipofika ukumbini alikaa siti ya nyuma.
“Hatukuwa tukijua kama Kajala naye amealikwa. Aliingia ukumbini na kusalimiana na mastaa wenzake kadhaa kisha akaenda kuketi siti ya nyuma kabisa akifuatilia sherehe inavyoenda,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kiliendelea kupenyeza ubuyu kuwa, wakati shangwe zikiendelea ukumbini hapo ilifika muda wa kufungua shampeni ambapo mastaa kibao walienda mbele akiwemo msanii wa Bongo Fleva pamoja na mzazi mwenziye, Zari na baada ya muda MC alimuita Kajala naye ajumuike nao.
“Hapo ndipo Kajala akaona isiwe tabu, akainama na kupitia mlango wa nyuma kisha akaondoka zake na kuwaacha na mshangao,” kilimaliza chanzo.
Akizungumzi ishu hiyo Kajala alisema “Ni kweli nilikwenda kwenye hiyo harusi na nikaitwa mbele lakini niliamua kuondoka zangu kwa sababu sikutaka kuonana na baadhi ya watu (Zari).”

Mwarubaini ni mti Wenye kutibu maradhi mbali mbali,,



KATIKA karne hii ya sayansi na teknolojia, Mwenyezi Mungu amewajaalia baadhi ya wanadamu (Madaktari) kuwapa taaluma (elimu) ya kufahamu maradhi yanayosumbuwa wanaadamu wenzao kwa kutumia vifaa mbalimbali ikiwemo vya kisasa na dawa katika kuwatibu.Hata
hivyo uwezo wa aina hii ulikuwepo hata kabla ya kuja sayansi na teknolojia ambapo binadamu wa awali alitumia tiba za asili kwa kujitibu na maradhi ya aina mbalimbali.Hivi sasa toka kuwepo sayansi na teknolojia, asilimia kubwa ya watu wanadharau kutumia dawa za asili na
badala yake wameelemea sana katika matibabu ya dawa za kemikali.Kwa mtazamo, takribani miti yote iliyopo duniani ni dawa hivyo ni vizuri kwa jamii kuelimishwa ili kuweza kujuwa ni jinsi gani wataweza kuitumia miti hiyo kwa kuitibu miili yao.Kutokana na hali hiyo na matibabu
hayo, inaonekana wazi kuwa mti wa Muarubaini ama wengine huita Mtunda, ni mjarabu kwakutibu maradhi mbalimbali na hivyo upo umuhimu wa kila mtu kuupanda katika makaazi yake na pia kwa kupitia Wizara ya kilimo kutenga eneo maalum kwa ajili ya kupanda miti ya
aina hii.Mti wa Mwarubaini ambao kwa kiingereza unajulikana kama ‘Neem’ , ulianza kugunduliwa kama tiba ya maradhi zaidi ya miaka 4.000 iliyopita.Mti huu hutibu maradhi ya aina mbalimbali kwa kuanzia mizizi, magome, mbegu na majani yake.Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
baraza la tiba asilia Zanzibar Mayasa Salum Ali, alisema mti wa Mwarubaini unapatikana au unaota zaidi katika nchi za joto kote Ulimwenguni.Mwenyekiti huyo ambae pia ni mtaalam wa fani hiyo alisema kwa upande wa watu wa India, kwao mti huu unasifa sana katika matibabu yao na unajulikana kama duka la dawa la kijiji.Aidha alifahamisha kuwa wanauthamini kama dawa kutokana na matibabu yake
kwani unatibu maradhi ya aina mbalimbali ambayo humuandama mwanadamu na hata wanyama na mimea ya shambani.Hata hivyo kwa upande wa wataalamu wa India kutokana na umuhimu wa dawa hizi za asili, wamefakiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kupitia mti huu ili kurahisisha matumizi ya watu kwa kupitia tiba ya mwarubaini.Bidhaa hizo ni pamoja na dawa za kumeza, dawa za mswaki, sabuni, vipodozi
vya aina mbalimbali kama vile krimu, mafuta ya kujipaka ‘lotion’ , majani ya chai na vitu vingine vingi.China nayo haipo nyuma katika kutumia dawa za mti huu kwani nao wameweza kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali ili kurahisisha matumizi.Kwa upande wa Zanzibar,
sehemu ndogo sana ambayo inatumia mti huu kama ni dawa ya malaria na sehemu hiyo ni kwa wale watu wazima wanaoishi vijijini. Wao kidogo wanatumia mti huu kama ni dawa ya kutibu malaria sugu huku ikiwa mti wa Mwarubaini unatibu maradhi ya aina mbalimbali.Watu wengi husikia wakisema kuwa Mwarubaini ni dawa ambayo inatibu maradhi arobaini (40) kumbe sivyo ilivyo kwani mti huu unatibu zaidi ya
maradhi arubaini lakini tu jamii haijui na haina utaalam wa kufahamu kwa maradhi mengi yanayotibiwa kwa kutumia mti huo.Hivyo upo umuhimu kwa upande wa wataalamu wa tiba asilia kutoa elimu hiyo kwa jamii ili kuweza kujuwa kutumia mti huo ili kuweza kuondokana na maradhi ya aina mbalimbali.Kutokana na ufahamu huo mdogo kwa Wazanzibari katika tiba zinazopatikana kutokana na Mwarubaini, wengi
wanapoumwa na maradhi ya aina mbalimbali na hata malaria hukimbilia hospitali kupata dawa za vidonge au sindano vitu ambavyo hutokana na mchanganyiko wa kemikali mbalimbali ambazo zinauwezo wa kusababisha madhara makubwa kwa mwili wa mwanadamu.Miongoni mwa dawa ambazo zina madhara yanayoweza kumpata mwanadamu ambayo husababisha na vidonge au sindano
hizo ni pamoja na Fansida au Chloroquine ambapo utafiti unaonesha kuwa baadhi ya wagonjwa waliotumia dawa hizo wameathirika aidha kwa kuwashwa na mwili na wengine wameathirika na macho kwa kutumia Fansida.Ili kuondokana na athari kama hizo, Mwenyekiti huyo amewashauri Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kutumia dawa za asili ili kuondokana na matatizo kama hayo.Hata hivyo Mwenyekiti
huyo alifahamisha kuwa katika baadhi ya maradhi badala ya kutumia pesa nyingi kwa kununua dawa za kemikali ambazo bei zake zinapanda siku hadi siku ukilinganisha na dawa za asili ambazo bei zake ni nafuu.Hata hivyo aliwashauri wagonjwa kufuata ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia dawa hizo ili kuzidi kuboresha afya na kujiepusha na matatizo yasiyo ya lazima.Majani ya mti wa Mwarubaini
yanatumika kwa kutibu maradhi mbalimbali kama vile homa za watoto, suruwa na kwa upande wa watu wazima hutibu malaria, muwasho, maradhi ya moyo, Ukimwi, mkanda wa jeshi na maradhi ya buba.Mengne ni maradhi ya ganzi ya mwili, kisukari na mtu ambae anaupungufu
wa kinga mwilini, mapele sugu yalioshindikana kutibika hospitali na maradhi mengine.Dk. Mayasa pia alifahamisha majani hayo yanauwezo wa kuuwa hata kwa upande wa wadudu wa shambani ambao wanakula mazao.Mbegu za Mwarubaini zinatengenezwa mafuta ambayo
mafuta hayo yanajulikana kwa jina la (Neem oil) ambayo yanauwezo wa kutibu maradhi ya aina mbalimbali kama vile kuondoa chunusi, mapele, fangasi na mabaka mwilini.Pia mafuta hayo huuwa wadudu mbalimbali ambao wanatambaa na kuruka nyumbani na hata vijidudu
(bacteria), sisimizi na wadudu wengine.Mizizi na magome ya mwarubaini huuwa wadudu wa aina mbalimbali kama vile funza, maradhi ambayo huwapata wanawake kama vile vikanga na maradhi mengine mengi ambayo ni maradhi sugu na yameshindwa kutibiwa basi
Mwarubaini huyatibu.“Kwani hata wanyama tunaofuga nyumbani mfano ng’ombe na wengine ambao hugandwa na kupe na wadudu wengine, mnyama huyo ukimkogeshea maji hayo uliosaga magome ya mti huo huondoa wadudu wote”, alifahamisha dk. Mayasa.Mtaalamu huyo alifahamisha kuwa dawa za mti huo hazina madhara kama zilivyo dawa nyengine za kemikali lakini kwa ushauri unatakiwa kumuona
Daktari mwanzo alio karibu nawe kabla ya kuanza kutumia.Alifahamisha kuwa dawa za kemikali zinatibu haraka kuliko dawa za asili lakini dawa za asili ni bora zaidi kuliko dawa za kemikali kwani zinatibu kidogo kidogo na zikitibu zimetibu na hazina maradhi yanayosababishwa na dawa hizo.

Figo kushindwa kufanya. kazi ( RENAL/KIDNEY FAILURE )



Figo ni miongoni mwa viungo muhimu sana katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana kama yale ya maharage, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu za chini.
Kazi za figo
Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu kadhaa katika damu na hivyo kusaidia katika kuhifadhi na kuthibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Katika kutekeleza hayo, figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.
Kazi nyingine za mafigo ni
Kurekebisha na kuthibiti kiasi cha vitu mbalimbali katika damu pamoja na kiasi cha maji katika mwili.
Husaidia kutengeneza kiasili cha erythropoietin ambacho ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
Husaidia uzalishaji wa vitamini D
Husaidia pia katika kuthibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure)
Utengenezaji wa mkojo
Kwa kawaida damu inayozunguka mwilini hatimaye huingia kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa, kutoa uchafu pamoja na sumu nyingine zisizohitajika mwilini. Kitendo hiki cha utengenezaji mkojo hufanyika katika hatua kuu zifuatazo;
Hatua ya kwanza ni uchujaji. Damu kutoka nje huingia ndani ya mafigo na kupita kwenye glomeruli, lenye umbo kama chekeche/chujio ambalo limeundwa na mishipa mingi midogo ya damu iliyojizungusha pamoja. Vitu mbali mbali, maji pamoja na sumu zilizo katika damu inayopita kwenye vimishipa hivi na kisha kuingia katika mirija mingine mikubwa kwa ajili ya uchujaji zaidi.
Mirija inayofuata huendelea kuchuja damu na kunyonya baadhi ya vitu vilivyo chujwa kimakosa kuvirudisha mwilini, mpaka kiasi sahihi cha uchafu kinachotakiwa kuchujwa kinapokuwa kimefikiwa.
Mara baada ya mkojo kutengenezwa na kutolewa kwenye figo, husafiri kuingia kwenye kibofu cha mkojo kwa kupita kwenye mirija ijulikanayo kama ureta. Kutoka kwenye kibofu, mkojo hutolewa nje ya mwili kupitia kwenye mrija waurethra.
Figo kushindwa kufanya kazi (Renal Failure/ Kidney Failure)
Kushindwa kufanya kazi kwa figo hutokea iwapo sehemu ya figo au figo lote litapoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kutoka katika damu na kutengeneza mkojo. Kitendo hiki husababisha kusanyiko la uchafu pamoja na sumu kadhaa katika damu ambazo ni hatari kwa afya ya mhusika.
Aina za figo kushindwa kufanya kazi
Figo kushindwa kufanya kazi kumeganyika katika makundi yafuatayo
Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) au Acute Kidney Failure (AKF).
Figo kushindwa kufanya kazi kwa kiasi (Mild renal/kidney insufficiency)
Tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi (Chronic renal failure)
Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF)
Hii ni hali inayotokea kwa ghafla, na kudumu kwa saa chache mpaka siku chini ya 14, na kusababisha ongezeko la kiwango cha creatinine na urea katika damu. Hali hii huwapata karibu asilimia 5% ya wagonjwa waliolazwa hospitali kwa sababu ya matatizo mbalimbali. Aidha hali hii hutokea zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale wanaohitaji uangalizi wa kipekee, yaani waliolazwa ICU.
Katika makala hii tutatumia zaidi kifupisho cha ARF.
Visababishi na aina za ARF
Visababishi (au aina) vya ARF vinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu:
Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure)
Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure)
Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)
Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal
causes/failure)
Aina hii hutokea kwa takribani asilimia 60 mpaka 70 ya ARF zote. Katika kundi hili, figo hukosa damu ya kutosha kwa ajili ya kuchuja na hatimaye hushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Mambo yanayoweza kusababisha prerenal failure ni pamoja na:
Upungufu wa maji mwili unaosababishwa na kutapika kupita kiasi, kuharisha, au kupoteza damu kupita kiasi (kwa sababu ya ajali au kuumia)
Kuvurugika kwa mtiririko wa damu inayoingia kwenye figo kwa sababu ya:
Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa upasuaji mkubwa, kuumia au kuungua sehemu kubwa ya mwili, au maambukizi katika mfumo wa damu (sepsis) yanayoweza kufanya mishipa ya damu kutanuka na kushusha shinikizo la damu
Kuziba au kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu kwenye figo
Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) au shambulio la moyo (heart attack) linalosababisha kushuka kwashinikizo la damu
Ini kushindwa kufanya kazi (liver failure) kunakoweza kusababisha mabadiliko katika mfumo wa homoni zinazoathiri shinikizo la damu pamoja na mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.
Mwanzoni kabisa mwa pre-renal failure huwa hakuna athari yoyote inayotokea kwenye figo, na mara nyingi, figo laweza kurudi katika hali yake ya kawaida iwapo chanzo cha tatizo kitagunduliwa na kushughulikiwa ipasavyo.
Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure)
Mambo yanayosababisha madhara katika figo husababaisha karibu asilimia 25 mpaka 40 ya vyanzo vyote vya ARF. Visababishi vilivyo katika kundi hili hujumuisha vile vinavyoathiri uchujaji, mtiririko wa damu ndani ya figo na seli za figo zinazoshughulika na uchujaji na ufyonzaji wa chumvi na maji.
Visababishi hivyo ni pamoja na:
Magonjwa katika mishipa ya damu
Kuwepo kwa damu iliyoganda ndani ya mishipa ya damu inayopita katika figo
Ajali/Kuharibika kwa tishu na seli za figo
Magonjwa ya mzio katika glomeruli na figo kwa ujumla (glomerulonephritis). Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi (infection) ya bacteria jamii ya streptococci.
Magonjwa ya mzio katika nyama za figo (acute interstitial nepthritis). Mambo yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile Aspirin, Ibuprofen (Brufen), baadhi ya antibiotics, na baadhi ya dawa za kutoa maji mwilini (antidiuretics); magonjwa kama vile saratani ya damu (leukemia), lupus na lymphoma. Magonjwa ya mzio katika nyama za figo husababisha madhara katika seli zinazohusika na uchujaji na ufynzaji wa chumvi na maji.
Magonjwa ya ukosefu wa damu katika mirija ya figo (acute tubular necrosis) ambayo hufanya seli na tishu za mirija hii kufa na hivyo mirija kushindwa kufyonza chumvi na maji kuyarudisha mwilini. Mambo yanayosababisha hali hii ni pamoja na shock (upungufu wa damu kuingia kwenye figo), matumizi ya madawa kama vile baadhi ya antibiotiki, sumu, dawa zinazotumika viwandani na kwenye x-rays na baadhi ya madawa yanayotumika kutibu saratani.
Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)
Mambo yanayosababisha hali hii huchangia kati ya silimia 5 mpaka 10 ya vyanzo vyote vya ARF. Postrenal failure wakati mwingine huitwa pia obstructive renal failure kwa sababu husababishwa na mambo yanayozuia utoaji wa mkojo nje ya figo.
Kuziba kwa ureta moja ama zote mbili kunaweza kusababishwa na:
Vijiwe figo (renal stones)
Saratani ya viungo vya njia ya mkojo au viungo vilivyo karibu na njia ya mkojo kiasi cha kuzuia mkojo kutoka nje ya figo
Matumizi ya baadhi ya madawa
Kuziba kwa njia ya mkojo katika eneo la kibofu cha mkojo kunaweza kutokana na:
Kijiwe kibofu (bladder stone)
Kuvimba kwa tezi dume (hii ni kwa wanaume)
Kuwepo kwa damu iliyoganda katika kibofu
Saratani ya kibofu cha mkojo
Matatizo ya mfumo wa fahamu yanayoathiri utendaji kazi wa kibofu cha mkojo
Tafsiri nyingine ya ARF
Wagonjwa wa ARF wanaweza kupata mkojo kidogo sana au wasipate kabisa., au wanaweza kuwa na ongezeko la creatinine kwa kasi ya kutisha au kwa kasi ndogo sana. Hali hizi zinaweza pia kutumika kutoa tafsiri nyingine ya maana ya ARF.
Mtu anayetoa kiasi cha mkojo chini ya 400mL kwa siku hujulikana kama ana oliguria, na huchukuliwa kuwa ana hali mbaya ya kutoweza kupona.
Mtu anayetoa mkojo chini ya 100mLkwa siku husemwa ana Anuria, ambayo kama imetokea ghafla, huashiria kuwepo kwa tatizo la kuziba kwa mirija inayotoa mkojo kwenye figo zote mbili, na mara niyingi hali hii ni ya hatari zaidi. Tafsiri hii husaidia sana katika kuamua aina ya matibabu na muda wa kumpatia mgonjwa matibabu ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kumpata.
Dalili za ARF
Katika hatua za mwanzo mwanzo, baadhi ya waathirika wanaweza wasioneshe dalili zozote za tatizo hili. Dalili ni kama
Kupungua kwa uzalishaji mkojo
Kuvimba mwili
Kupoteza umakini
kuchanganyikiwa
Uchovu
Kulegea mwili
Kichefuchefu na kutapika
Kuharisha
Maumivu ya tumbo
Kuhisi ladha ya chuma na uchachu mdomoni
Na katika hatua za mwisho kabisa, mgonjwa anaweza kupata degedege na hatimaye kupoteza fahamu (coma).
Vipimo na uchunguzi
Kama ilivyoainishwa hapo juu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wasiwe na dalili zozote za tatizo hili. Hata wale wenye kuonesha dalili, zinaweza zisiwe mahsusi (non-specific). Uchunguzi wa mwili unaweza usioneshe tatizo lolote lile, au kukawa na dalili chache sana ambazo zinaweza zisimsaidie sana daktari kufikia uamuzi.
Baadhi ya vipimo vinavyoweza kugundua uwepo wa ARF ni pamoja na Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu. Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika damu.
Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes)
Uchunguzi wa damu (Full Blood Picture): Husaidia kuonesha uwepo wa maambukizi ya bacteria na/au upungufu wa damu mwilini (anaemia)
Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24
Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.
Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo
Renal biopsy.
Matibabu ya ARF
Matibabu ya ARF hutegemea kwanza chanzo chake na pili ukubwa wa tatizo. Kujua chanzo cha tatizo husaidia kufahamu ni aina gani ya matibabu yanayohitajika wakati kufahamu ukubwa wa tatizo huathiri uchaguzi wa aina ya matibabu na hata hitaji la kufanya dialysis. Hata hivyo inashauriwa sana kumpeleka mgonjwa kwa daktari bingwa wa magonjwa ya figo (nephrologist) kwa matibabu zaidi.
Kulingana na chanzo cha ARF, baadhi ya matibabu yanayoweza kufanyika, hutolewa yakiwa na lengo la:
Kurekebisha kiasi cha upotevu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa i.v fluids pamoja kurekebisha kiasi cha madini (electrolytes) kilichopotea
Kupunguza au kuzuia ongezeko la maji kwa wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kabisa kutoa maji nje ya mwili
Kuongeza uwezo wa moyo kufanya kazi vizuri au kuongeza shinikizo la damu husaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenda kwenye figo
Kurekebisha kiasi cha madini mwilini kitendo ambacho husaidia mwili kufanya kazi zake vema
Dialysis
Iwapo pamoja na matibabu hayo, figo za mgonjwa zinaendelea kudorora, mgonjwa hana budi kufanyiwa dialysis. Dialysis ni kitendo cha kutoa uchafu na maji yasiyohitajika katika damu. Kitendo hiki hufanywa kwa kupitia mishipa ya damu iliyo chini ya ngozi (hemodialysis) au kwa kupitia tumboni (peritoneal dialysis). Katika hemodialysis mirija hii huunganiswa kwenye mashine ambayo hufanya kazi kama figo. Damu kutoka kwa mgonjwa huingia katika mashine kisha huchujwa ili kuondoa sumu, uchafu pamoja na maji yasiyohitajika kabla ya kurejeshwa tena mwilini.
Kitendo hiki hufanyika angalau mara mbili mpaka tatu kwa wiki, na kwa kiasi fulani ni ghali na si watu wote wa kipato cha chini wanaoweza kumudu gharama zake.
Katika peritoneal dialysis, uchafu pamoja na maji kutoka katika mzunguko wa damu huingia katika nafasi inayotenganisha tumbo na utando wake (peritoneal space), huchujwa kwenye utando huo kisha hutolewa kupitia sindano maalum (catheter ) iliyowekwa juu ya ngozi na kuingia ndani ya tumbo (peritoneal cavity).
Matarajio
Wagonjwa wengi wenye ARF hupona bila hata kuhitaji dialysis mara tu chanzo cha tatizo kinapogundulika na kushughuikiwa mapema. Hata hivyo wakati mwingine, pamoja na matibabu, baadhi ya figo hushindwa kurudia kufanya kazi kwa ufanisi wake wa awali. Watu kama hawa hawa wanahitaji kufuatiliwa kwa ukaribu na umakini mkubwa.
Kinga ya ARF
Inashauriwa
kufanya uchunguzi wa figo walau mara moja kila mwaka. Hii husaidia kuchunguza utendaji wa figo na hivyo kuepuka madhara kabla hayajatokea.
Kunywa maji kwa wingi ili kuyafanya mafigo yatende kazi zake kwa ufanisi.
Kuepuka matumizi ya vitu ama madawa yanayoweza kuathiri nyama, seli au tishu za figo. Ni vema kutumia dawa pale tu unaposhauriwa na daktari.
Watu wenye hatari ya kupata tatizo sugu la kushindwa kufanya kazi kwa figo (Chronic Renal Failure) wanashauriwa kufanya vipimo na cuhunguzi mara kwa mara
Muone mtaalamu wa afya mara tu uonapo dalili za kuwepo kwa shida katika kukojoa au uonapo damu katika mkojo.