Wednesday, 29 November 2017

Rais Kenyatta aahidi mambo haya



Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta ameapishwa kuongoza Kenya kwa muhula wa pili wa miaka mitano na wa mwisho katika sherehe zilizofana na ameahidi katika hotuba yake kuondoa viza na kukutana na wanasiasa kwa masilahi ya Kenya.

"Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatii, nitahifadhi, nitalinda na kutetea Katiba ya Kenya kwa kuzingatia sheria, na nitazingatia sheria zote; na kwamba nitalinda na kusimamia kikamilifu utaifa, uadilifu na heshima ya watu wa Kenya,” alisema Kenyatta huku akiwa ameshika Biblia kwa mkono wa kulia alipokuwa akila kiapo cha kuingia ikulu.

Biblia hiyo, kwa mujibu wa Mkuu wa sherehe Duncan Okello, ni ileile iliyotumiwa na rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta aliyoishika wakati wa uhuru Desemba 12, mwaka 1963.

Hatua ya Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kula kiapo ina maana Kenya imekamilisha shughuli za kupata viongozi ikiwa ni baada ya siku 123 tangu ulipofutwa uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.

Katika uchaguzi huo Kenyatta alipata ushindi wa asilimia 54 na kumwangusha mshindani wake Raila Odinga wa muungano wa Nasa aliyeshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 44. Hata hivyo Odinga alifungua kesi Mahakama ya Juu kupinga ushindi huo na baada ya kupeleka ushahidi uchaguzi huo kwa kura ya urais ulifutwa.

Uchaguzi wa marudio uliopangwa Oktoba 26 ulisusiwa na Odinga aliyedai hayakufanyika marekebisho katika mfumo ili uwe wa haki na wa kuaminika. Kujiondoa kwake kulimwacha Kenyatta akijinyakulia ushindi wa asilimia 98 huku asilimia 38 tu ya wapigakura 19.6 milioni waliojiandikisha wakishiriki.

Maelfu ya watu walihudhuria sherehe hizo wakiwemo wakuu wa nchi na watu mashuhuri wapatao 40. Wahudhuriaji, wengi wao wakiwa wafuasi wa chama tawala cha Jubilee, walishangilia kwa nguvu, waliimba na kucheza katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kasarani.


Kukutana na wanasiasa
Kwa kuwa uchaguzi huo umesababisha mgawanyiko mkubwa, mara baada ya kula kiapo cha utiifu, Kenyatta aliahidi mambo kadhaa likiwemo la kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa na kuwaelezea nia yake ya kuendeleza umoja.

Kenyatta alisema ana malengo ya kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya na akadokeza kwamba siasa zimetumiwa vibaya kutatiza ustawi wa taifa "badala ya ilivyo nchi za Asia." “Hakuna aliyewahi kula siasa," alisema.

Vile vile aliahidi “kutenda haki kwa watu wote kwa kuzingatia Katiba, kwa sheria, kuheshimu sheria bila woga, upendeleo, uswahiba wala inda.”

Kenyatta amewahimiza Wakenya kuishi kama majirani kwani hufaana sana na hutegemeana wakati wa shida.

Viza
Rais Kenyatta ametangaza mtu yeyote kutoka nchi ya Afrika anayekwenda Kenya kwa shughuli yoyote sasa atapewa viza akifika mpakani au akiwasili kwenye viwanja vya ndege nchini Kenya.

Rais alisema hataweka masharti kwamba lazima mataifa mengine yafanye hivyo lakini ameiga mfano wa Rwanda (yenyewe ni raia yeyote wa nchi yoyote) ambayo ilichukua hatua hiyo hivi karibuni.

Kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenyatta amesema atashirikiana na viongozi wa EAC kufufua moyo wa Jumuiya hiyo kwamba wananchi wa nchi wanachama watahesabiwa kama Wakenya; watahitajika tu kutumia kitambulisho.

Amesema wananchi kutoka nchi za EAC wanaweza kuingia au kutoka na kufanya kazi, kumiliki mali au hata kuoana bila kuwekewa masharti.


Sheria
Kuhusu mahakama alisema watazungumza na idara hiyo kuhusu kuharakishwa kwa kesi ambazo zimekwama miaka mingi na nyingi nyingine ambazo zinatumiwa kukwamisha miradi ya serikali.

"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna mtu yeyote kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako,” amesema.

"Naomba niwakumbushe kwamba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushinda, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kura, tuliheshimu uamuzi huo. Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo," amesema.

Kuhusu Katiba amesema ndiyo iliyounda mihimili mitatu huru ya serikali na akata kila mmoja ufanye kazi yake. "Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa tunajua namna ya kuungana tena.”

Alisema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na lenye ustawi.

Ruto
Vilevile, Makamu wa Rais William Ruto aliapishwa katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na wakuu wa nchi za Afrika Mashariki; Hailemariam Desalegn (Ethiopia), Paul Kagame (Rwanda), Mohamed Abdullahi Mohamed (Somalia), Salva Kiir (Sudan Kusini), Ian Khama (Botswana) na Yoweri Museveni (Uganda).

Mwananchi:

Dar: Walimu 12, mkurugenzi wa shule wafikishwa mahakamani

Dar: Walimu 12, mkurugenzi wa shule wafikishwa mahakamani


Dar es Salaam. Walimu 12 na mkurugenzi wa Shule ya Msingi Mount Pleasant iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano, likiwemo la kuishi nchini kinyume cha sheria.

Waliosomewa mashtaka hayo ni Anna Ochwo; mhasibu, Josephine Nelson; Janeth Onzia; Upakmungu Nobert; Abitegeka Israel; Hajara Umavu; Sibibuka Emmanuel; Stedia Chalikunda; Evelyn Rikoba; Mkamwagi Flavia; Byamugisha Fambe; meneja, Margaret Apophia na mkurugenzi, Julius Nelson.

Mwendesha mashtaka wa Uhamiaji, Gerald Maridai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa amedai washtakiwa hao isipokuwa mkurugenzi wa shule hiyo walijihusisha na kazi bila kibali halali.

Novemba 24,2017 washtakiwa wanadaiwa wakiwa raia wa Uganda walikutwa wakifanya kazi bila kuwa na leseni au vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo. Pia, wanadaiwa kuingia nchini bila ya kuwa na hati za utambulisho.

Mshtakiwa Apophia anadaiwa akiwa raia wa Uganda alishindwa kufuata masharti ya hati ya kuishi nchini ambayo imemkataza kujihusisha na shughuli zozote.

Nelson, raia wa Tanzania ambaye ni mkurugenzi wa shule hiyo, anadaiwa kuajiri wahamiaji wasiofuata sheria za uhamiaji.

Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa waliyakana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.

Hakimu Mwambapa alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye atasaini bondi ya Sh3 milioni.

Washtakiwa saba walikamilisha masharti na kuachiwa kwa dhamana, huku wengine wakipelekwa rumande. Kesi itatajwa Desemba 12,2017.

Mwananchi:


Rais Mnangagwa atangaza msamaha kwa walioficha fedha ughaibuni




Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza msamaha wa miezi mitatu kwa watu binafsi na kampuni mbalimbali ambazo zimeficha fedha za umma kinyume cha sheria nje ya nchi hiyo kuzisalimisha.

Kupitia taarifa, amesema kwamba serikali itawakamata na kuwafungulia mashtaka wale watakaokataa kufanya hivyo kabla ya msamaha huo kumalizika Februari.

"Vitendo kama hivi ni uhalifu wa hali ya juu wa kiuchumi dhidi ya watu wa Zimbabwe," Bw Mnangagwa amesema.

Tangu aapishwe Ijumaa wiki iliyopita, Mnangagwa ameahidi kukabiliana na rushwa.

"Fedha nyingi na mali ya umma vimefichwa nje ya nchi na watu binafsi na mashirika," amesema.

"Wale waliohusika wanahamasishwa kutumia fursa hii a miezi mitatu kurejesha fedha hizo na mali ili kuepuka uchungu na aibu ya kutembelewa na mkono mrefu wa sheria," ameongeza.

Mtangulizi wake, Robert Mugabe, aliondoka madarakani wiki iliyopita baada ya jeshi kuingilia kati.
Alikuwa ameongoza nchi hiyo kwa miaka 37 tangu uhuru.

Peter Crouch asaini mkataba mpya Stoke



Mshambuliaji wa klabu ya Stoke Peter Crouch ametia saini mkataba mwingine wa mwaka mmoja katika klabu hiyo, hatua itakayomuweka katika klabu hiyo hadi 2019.

Crouch, 36, ambaye amechezea England mechi 42, ndiye mfungaji mabao bora wa klabu hiyo ambapo amewafungia mabao manne msimu huu.

Hii ni licha ya kwamba mechi tisa ambazo amewachezea Ligi ya Premia msimu huu ameingia kama nguvu mpya.

"Bado ana mchango muhimu wa kutekeleza kwetu," meneja Mark Hughes amesema.

Crouch alijiunga na Stoke kutoka Tottenham mwaka 2011 kwa uhamisho wa £10m uliovunja rekodi ya klabu hiyo wakati huo.

Awali, alikuwa amechezea Liverpool, Portsmouth, QPR, Southampton na Aston Villa.

Mapema mwezi huu, aliweka rekodi Ligi ya Premia kwa kuingia mara nyingi zaidi kama nguvu mpya - mara 143 baada ya kuingia kama nguvu mpya dhidi ya Brighton.

Oktoba, alitambuliwa pia kama mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwa kichwa Ligi ya Premia, mabao 51.

Kilimanjaro Stars yaanza kujifua




Timu ya Taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars imeendelea na kambi ya maandalizi kuelekea kwenye michuano ya kombe la CECAFA Challenge.

Kilimanjaro Stars chini ya kocha Ammy Ninje imefanya mazoezi mbalimbali katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam leo Novemba 28, 2017.

Timu hiyo inajiandaa kucheza Kombe la CECAFA Challange 2017 huko Kenya kuanzia Desemba 3 hadi 17 mwaka huu.

Wachezaji walioitwa na kocha Ninje kutoka vilabu mbalimbali vya ligi kuu soka nchini wamesharipoti kambini baada ya ligi kusimama kwa muda kupisha michuano hiyo.

Rais Macron awataka waafrika kupambana na ugaidi




Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewataka wananchi barani Afrika kupambana na ugaidi.

Kwa mujibu wa habari,Macron ameyazungumza hayo wakati akihutubia wanafunzi katika mji mkuu wa Ougadougu, Burkina Faso.

Rais Macron amesema kuwa ni dhahiri Burkina Faso na Ufaransa zimeandamwa na ugaidi na hivyo ni vyema kupambana.

Macron vilevile ameimsifu rais wa zamani Francois Hollande kwa kutuma jesho mali mnamo mwaka 2013 kupambana na wapiganaji mkoani Sahel.

Katika hotuba yake Macron amesema pia bara la Afrika linasumbuliwa na mizozo ya kisiasa na ni wazi kuwa hatotoa funzo ya jinsi uchaguzi unapaswa kufanyika.Hilo ni jambo kila mtu anapashwa kufahamu.

Shirika hili la ndege kutobeba wanyama katika safari zake kuelekea Ujerumani



Ndege za Turkish Airlines zimetangaza kuwa hazitokubali mnyama wa aina yoyote katika safari zake za kuelekea Ujerumani.

Kwa mujibu wa habari,Turkish Airlines imetoa tangazo hilo baada ya uamuzi kutoka katika serikali ya Ujerumani.

Ripoti zinaonyesha kuwa ndege za mizigo na abiria hazitokubali wanyama kuelekea Ujerumani.

Abiria wote wanaoelekea Ujerumani wameombwa kufuata sheria hiyo mpaka hapo serikali ya Ujerumani itakapotoa tangazo jingine.

Korea Kaskazini yarusha kombora Kubwa zaidi



Taifa la Korea Kaskazini limefanyia majaribio kombora lake la masafa marefu lililoruka juu zaidi na kombora hilo tayari limeonekana kuhatarisha usalama duniani kulingana na waziri wa maswala ya ulinzi nchini Marekani James Mattis.

Jaribio hilo la kombora mapema siku ya Jumatano lilianguka katika maji ya Japan.
Liliruka kwa urefu wa kilomita 4,500 na kusafiri umbali wa kilomita 960 kulingana na jeshi la Korea Kusini.

Ni jaribio la hivi karibuni ambalo limezua hali ya wasiwasi, Mara ya mwisho kwa taifa hilo kulifanyia jaribio kombora lake ni mwezi Septemba, Wakati huo, kombora lake la mwisho lilikuwa la sita la nguvu za kinyuklia mwezi huo.

Korea Kaskazini imeendeleza mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa utengenezaji wa makombora licha ya shutuma kutoka kwa jamii ya kimataifa.



Tuesday, 28 November 2017

Mwendokasi wageuka shule kwa nchi za Afrika



 Dar es Salaam. Tangu kuanza rasmi Mei 10, 2016 kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, zaidi ya nchi tano za Afrika zimetuma viongozi wake kujifunza namna ya uendeshaji wake.

Mfumo huo wa usafiri unalenga kupunguza foleni katika barabara, tangu uzinduliwe na Rais John Magufuli nchi za Ethiopia, Malawi, Uganda na Kenya zimetuma viongozi kuja kujifunza.

Pia, ugeni kutoka Rwanda jana uliongeza idadi ya viongozi wanaoendelea kuja mahsusi kwa ajili ya mradi huo huku kukiwa na taarifa za ujio mwingine Desemba kutoka nchini Senegal.

Akielezea utekelezaji wa mradi huo kwa wageni hao, mtendaji mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Lwakatare kuwa wanatarajia kuongeza mabasi kutoka 140 yaliyopo sasa hadi 305 katika awamu ya kwanza ya mfumo huo itakapokamilika Juni mwakani.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Lwakatare, inasema wageni hao sita kutoka Serikali ya Rwanda wana ziara ya siku tano kujifunza namna wakala huo unavyotoa huduma.

Lwakatare alisema ongezeko la mabasi kutasaidia kuongeza idadi ya abiria kutoka 200,000 wanaohudumiwa sasa kwa siku hadi kati ya 400,000 na 500,000. “Licha ya hilo, tutaongeza njia za mlisho kutoka mbili zilizopo sasa hadi tisa zitakazokuwa zikienda Masaki, Sinza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na maeneo mengine ambayo yapo jirani ili kupanua huduma ya usafiri kwa maeneo yaliyomo ndani ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi,” alisema.

Kuhusu athari zilizotokana na mvua iliyonyesha Oktoba 26, Lwakatare alisema mabasi 20 yaliharibika zaidi lakini yameshatengezwa na yanatoa huduma.

Alisema Dart imejipanga kuhakikisha mitaro yote inayozunguka karakana ya Jangwani inasafishwa, ili kuepuka eneo hilo kukumbwa tena na mafuriko.

Naye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Kigali, Rwagatore Etienne alisema wamechagua kutembelea wakala huo kwa sababu ndiyo mradi uliofanikiwa barani Afrika na upo karibu na Rwanda.

Katika msafara huo, Etienne ameambatana na wataalamu washauri ambao waliopewa kazi ya usanifu wa Jiji la Kigali ili liweze kuwa na mfumo wa mabasi yaendayo haraka. 


Siku ya kuzaliwa Rais Mugabe kuwa siku ya Taifa Zimbabwe




Serikali ya Zimbabwe imetangaza siku kuu mpya ya kukumbuka mchango wa Robert Mugabe ambaye aliondolewa madarakani wiki iliyopita.

Gazeti la serikali la Herald limesema sikukuu hiyo itakuwa ikiadhimishwa siku ya kuzaliwa kwa Bw Mugabe kila mwaka.

Uamuzi wa kusherehekea Siku ya Taifa ya Vijana ya Robert Gabriel Mugabe kila 21 Februari ulifanywa rasmi kupitia tangazo rasmi kwenye gazeti la serikali.

Tangazo hilo lilichapishwa Ijumaa – siku ambayo Rais Emmerson Mnangagwa aliapishwa kuwa rais, na kufikisha kikomo uongozi wa Mugabe wa miaka 37.

Serikali ya Bw Mugabe ilikuwa imeamua kutangaza siku ya kuzaliwa kwake kuwa sikukuu ya taifa mwezi Agosti, baada ya kampeni kutoka kwa mrengo wa vijana katika chama cha Zanu-PF.

Bw Mugabe aliondolewa mamlakani wiki iliyopita kutokana na shinikizo kutoka kwa wanajeshi waliokuwa wamechukua udhibiti wa serikali wiki iliyotangulia.

Credit:BBC

Masogange Marufuku kumtangaza Mwanaye



MREMBO aliyejipatia jina kubwa kutokana na kazi yake ya kuuza nyago kwenye video za wanamuziki Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ amesema kuwa, kwa upande wake ni marufuku kumuweka mtoto wake kwenye mitandao ya kijamii.

Masogange aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, ni bora yeye akiwa anatukanwa na kuambiwa maneno machafu kuliko mwanaye kwa sababu kwenye mitandao watu hawaangalii kama ni mtoto, bali wao ni kutukana tu.

“Siwezi kumnadi mwanangu, ni jambo ambalo nimejiwekea, kama atapenda mambo ya mtandaoni, akija kuwa mkubwa, atajiachia mwenyewe,” alisema Masogange ambaye mtoto mwanaye huyo wa kike ana umri miaka nane sasa.

Amuua Mke wake kisa nauli ya Bodaboda



KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA, MOHAMED MPINGA.

MWANAMKE mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Minza Paul (25) amefariki dunia mkoani Mbeya kwa kucharazwa bakora na mumewe hadi mauti yalipomfika.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga aliwaambia waandishi wa habari katika taarifa yake ya jana kuwa mbali na Minza, mwanaume mmoja pia alifariki dunia katika tukio tofauti.

Katika taarifa yake hiyo, Kamanda Mpinga alisema kuwa tukio la kwanza linalohusiana na kuuawa kwa Minza, lilitokea juzi katika kijiji cha Ipwizi, Kata ya Mjele wilayani Mbeya ambapo inadaiwa majira ya saa 4:06 usiku mumewe aliyemtaja kwa jina la Shilondi Mwakwenge, alianza kumshambulia kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo kilikuwa ni Shilondi kurejea nyumbani usiku akiwa amelewa huku akiwa amekodi bodaboda, na alipofika nyumbani alimwamuru mkewe huyo kumlipa dereva wa pikipiki.

Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, marehemu Minza alidai hana fedha za kumlipa dereva wa bodaboda na ndipo ugomvi ulipoibuka baina yake na mumewe ambaye alianza kumcharaza bakora mpaka alipopoteza maisha.

Kamanda Mpinga alisema kuwa baada ya kusababisha mauaji hayo, Shilondi alikimbia na hajulikani alipo na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Ifisi wakati Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa.

Katika tukio lingine, Kamanda Mpina alisema mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Florian Kagombe (46), mkazi wa kijiji cha Itumbi wilayani Chunya aliuawa na walinzi wa Kampuni ya Itumbi Reaching Plant inayojishughulisha na uchenjuaji wa dhahabu baada ya kudhaniwa kuwa ni mwizi.

Taarifa hiyo iliwataja waliofanya mauaji hayo kuwa ni Imani Kayuni (36) na Kelvin Ngonyani (32) wote walinzi wa Kampuni ya Panic Security Group ambao wanadaiwa kumshambulia Kagombe kwa kumpiga na vitu vibutu mpaka kupelekea umauti.

Inadaiwa kuwa watuhumiwa walipomkuta Kagombe katika eneo la kampuni hiyo majira ya saa 2:00 usiku mwishoni mwa wiki, walimshuku kuwa ni mhalifu hivyo wakamshambulia na kisha wakamwachia akiwa taabani.

Hata hivyo ainadaiwa marehemu alipoteza maisha majira ya saa 9:00 alasiri juzi kijijini hapo na kwamba mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Watuhumiwa wawili hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, taarifa ilisema.

Aidha, Kamanda Mpinga alitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa wa mauaji ya Minza kutoa kwa jeshi hilo, ili kufanikisha kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

Magunia 150 ya majani ya chai yateketeza



MAJANI ya chai magunia 150 ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu yaliyoingizwa nchini kwa njia za panya kupitia mipaka ya Holili na Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro yameteketezwa kwa moto kuepusha kusambazwa kwa walaji.

Uteketezaji wa chai hiyo uliratibiwa na kutekelezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Taarifa zilizoifikia Nipashe na kuthibitishwa na Mkaguzi wa TFDA, Edward Mamlawa, zimeeleza kuwa utafiti uliofanywa na wataalamu wa vyakula ulibaini kwamba majani hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

“Ni kweli tumeyateketeza majani ya chai yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 10, kwa sababu kama yangeingia sokoni yangeleta madhara makubwa kwa afya za binadamu. Tumeifanya kazi hiyo kwa ushirikiano na TRA,” alisema Mamlawa.

Wilaya ya Rombo, ina njia za panya zaidi ya 360 zilizopo kwenye mipaka ya Holili na Tarakea inayozitenganisha nchi za Tanzania na Kenya.

Kutokana na hasara iliyopatikana kuteketezwa kwa bidhaa hizo, Mkaguzi huyo alishauri   wafanyabiashara wafuate sheria za uingizwaji wa bidhaa za chakula nchini ili kuepuka hasara na kulinda afya za walaji.

Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, aliwataka wafanyabiashara na walipa kodi kuacha kutumia njia za magendo kuvusha bidhaa kutoka nje ya nchini na badala yake watumie njia halali na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Meneja Msaidizi anayeshughulikia Idara ya forodha mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kitundu, akizungumzia bidhaa hizo alisema biashara kati ya nchini ya Kenya na Tanzania ni nzuri na kwamba changamoto kubwa ni uwepo wa njia za panya ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara wasio waadilifu kuingiza bidhaa mbalimbali ambazo hazijafanyiwa ukaguzi.