Sunday, 4 February 2018

Panya wawapa Wakulima wakati mgumu Morogoro



Wakulima wa Kata ya Kiberege Wilayani Kilombero mkoani Morogoro, wamejikuta katika wakati mgumu, baada ya mazao yao kuvamiwa na panya waharibifu, na kusababisha uharibifu mkubwa katika  mazao ya mpunga na mahindi ambayo wameyapanda katika msimu huu.

Wakulima wa kata hiyo wamesema tatizo hilo limeanza kwa muda mrefu, na cha kushangaza licha ya mvua kunyesha bado panya hao wameendelea na uharibifu, hali ambayo inawapa mashaka juu ya hali ya chakula itakavyokuwa msimu huu.

Aidha wakulima hao kutoka katika vijiji vya Nyamwezi na Misufini, wamedai ndiyo  mara ya kwanza kuwanaona panya hao wakiharibu mazao yao.

Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Kiberege amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na ameeleza kuwa Serikali ya Wilaya hiyo imeanza kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo.

Lulu Diva apokonywa kila kitu na Mpenziwe?



IMEVUJA! Ukiachana na habari ya kudaiwa kupangishiwa nyumba na kununuliwa gari mpya aina ya Jeep na kigogo, imebainika kuwa msanii huyo amepokonywa kila kitu alichokuwa amepewa na mpenzi wake wa zamani aitwaye Joho.

Hivi karibuni, Lulu Diva aliripotiwa kuwa amepangiwa nyumba na kupewa gari jipya ambapo aliibuka sosi mwingine na kudai kuwa Lulu si mkweli, aliyenunua gari hilo ni mpenzi wake Joho ambaye alikuwa akiishi naye kinyumba kwa takriban miaka mitatu kiasi cha kufikia hatua ya kutolewa mahari ambayo ilirudishwa hivi karibuni na hata hivyo gari hilo amepokonywa hayuko nalo tena.

Akipiga stori na Risasi Jumamosi kwa sharti la kutotajwa jina sosi huyo alisema kuwa anawajua vilivyo Lulu na Joho kwa sababu Joho ni rafiki yake hivyo anachokisema yeye ana uhakika nacho kwamba Lulu hajanunuliwa gari bali ni lile lile alilopewa na Joho.

“Hivi mnajua kuwa huyo Lulu ni muongo mbona gari analosema amepewa na kigogo ni la rafiki yangu Joho alimnunulia na walikuwa wakiishi pamoja ila kwa sasa ameachana naye na ninavyojua amechukua vitu vyake.

“Hii yote ilikuja baada ya jamaa kumshtukia kuwa Lulu anatembea na msanii mwenzake, Rich Mavoko,” alisema sosi huyo.

Sababu ya Ndege kuanguka yajulikana Z'bar

Hitilafu ya mfumo wa umeme imetajwa kuwa chanzo kikuu cha ajali ya ndege ambayo ilisababisha vifo vya watu wawili juzi visiwani Zanzibar.

Ajali hiyo ilitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume majira ya saa 7:00 mchana, wakati ndege hiyo ikijaribu kuruka.

Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) cha Dar es Salaam, Dk. Bwire Rufunjo, alisema jana kuwa uchunguzi zaidi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea hata hivyo.

Dk. Rufunjo alisema katika hatua za awali wamebaini chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu katika mfumo wa umeme wa ndege kusabisha moto uliozaa mlipuko kutokana na ndege kuwa na mafuta mengi.

Alisema ndege hiyo yenye usajili wa 5H-TDF yenye uwezo wa kubeba abiria wanne ni mali ya NIT na ilikuwa Zanzibar kwa ajili ya matengenezo.

“Wakati ikiwa katika matengenezo, marubani wetu walikuwa wakiifanyia majaribio ili kuweza kufanya kazi yake ambayo ilikuwa kwa ajili ya ufundishaji wa wanafunzi wetu wanaochukua mafunzo ya urubani,”alisema mkuu huyo wa chuo.

Alisema waliofariki katika ajali hiyo ni Injinia Edger Mcha (26) na rubani Dominic Bomani (64) ambao ni wafanyakazi wa NIT.

Daktari bingwa wa uchunguzi katika Hospital Kuu ya Mnazi Mmoja, Dk. Msafiri Marijani, alisema vifo vya watu hao vilisababishwa na kukosa hewa safi wakati ajali ilipotokea.

“Marubani hao walikosa msaada kwa muda mrefu tangu ndege hiyo ianguke na kulipuka,” alisema.

Serikali ya Zanzibar imesema kuwa imepokea kwa mshtuko mkubwa vifo vya marubani hao kutokana na ajali hiyo na uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

 

Mama Mobeto amfungukia Diamond

KUFUATIA skendo nzito inayofukuta ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kudaiwa kutoka kimapenzi na warembo, Wema Isaac Sepetu na Tunda Sebastian, mama mzazi wa mwanamitindo Hamisa Mobeto, Shufaa Lutigunga ‘amemtapika’ jamaa huyo kuwa vitu vyote vinavyoendelea kwenye mitandao ya kijamii havihusiani na mwanaye.

Akizungumza na gazeti hili, mama Mobeto alisema kuwa, kwa sasa, kwa upande wao, yeye na mwanaye Mobeto hawataki malumbano na kuwekana kwenye mitandao wa kijamii ndiyo maana hawataki kusikia habari zinazomhusu Diamond.

Alisema kuwa, muda huo  wa malumbano hawana kwa sababu mwanaye anaendelea na maisha yake mengine kabisa ya kutafuta maendeleo na jinsi gani ya kuwalea watoto wake na si kumtegemea mwanaume huyo.

“Jamani sisi mambo hayo ya kwenye mitandao muda huo hatuna tena. Hata mtoto wangu (Mobeto) ameshayasahau mambo hayo na badala yake yupo bize na mambo yake mengine kabisa,” alisema mama Mobeto.

Mama Mobeto aliendelea kueleza kuwa, mtoto wake yuko kwenye mchakato mkubwa wa kufungua biashara yake ya lipstiki hivyo muda wa kufuatilia chochote kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii hana.

“Michakato yetu sisi zaidi ni kutafuta pesa na si vingine. Muda wa kuchokonoana kwenye mitandao hatuna kwa sababu tukifanya hivyo hatuwezi kupiga hatua hata siku moja, lakini kama kuna watu wanaweza kufanya hivyo, wafanye kwani sisi tulishajivua siku nyingi sana na wala hatutaki kumsikia huyo Diamond na mambo yake,” alisema mama Mobeto.

Saturday, 3 February 2018

Nchemba awataka wanaotoa vitambulisho wawe makini

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wanaosimamia usajili wa wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho wa Taifa kuwa makini.

Akizungumza leo Februari 3, 2018 katika uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa wakazi wa Tabora,  Mwigulu amesema umakini huo utasaidia vitambulisho hivyo kutotolewa kwa watu wasiostahili.

Amesema miaka ya nyuma wakati utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo haujaanza, baadhi ya raia wa kigeni walikuwa wakitumia mwanya huo kunufaika na huduma za jamii kama elimu.

“Watu hao walipomaliza masomo walirejea katika nchi zao na kuzinufaisha kwa namna moja au nyingine wakati wametumia pesa za watanzania. Mnapaswa kuwa makini ili kubaini wageni,” amesema Mwigulu.

Amesema kila mwananchi anatakiwa kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuhakikisha hakuna mgeni anayepenya na kupata kitambulisho hicho.

“Uandikishaji na utoaji wa vitambulisho hivi ni bure. Wananchi hawapaswi kutozwa fedha yoyote,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Andrew Massawe amesema lengo ni kuhakikisha mpaka Desemba, 2018 utoaji wa vitambulisho hivyo uwe umefanyika nchi nzima.

Ametaja faida za vitambulisho hivyo kuwa ni kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na wananchi kutambulika haraka wanapokwenda kupata huduma mbalimbali, zikiwemo afya na elimu

Wanaofanya udanganyifu kwenye asasi za kiraia waonywa

Asasi za kiraia zimetakiwa kufuata taratibu kabla ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi ili kukwepa udanganyifu, ikiwa ni pamoja na kuwachangisha fedha na kutokomea kusikujulikana.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 3, 2018  na ofisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Temeke, John Bwana wakati akizindua  mradi wa kuwajengea wanawake uwezo kuhusu ujasiriamali ili  kujiinua kiuchumi ulioandaliwa na asasi ya Iwapoa.

Amesema kuna lundo la asasi za kiraia zinazotoa mafunzo kiholela na kuwatapeli wanawake kwa kuwachangisha michango na kutokomea na fedha zao.

“Iwapoa mmefanya jambo la maana kufuata taratibu za kuonana na mamlaka husika na kupata wataalamu kutoka katika kata mtakazofanya kampeni hii ya kupunguza umasikini kwa kuwajengea wanawake uwezo,|” amesema na kuongeza,

“Nawaunga mkono na ninatoa rai kwa asasi nyingine zisizofuata utaratibu zifanye hivyo mara moja kwa sababu tunazifuatilia na tukizibaini tutazizuia kufanya kazi zake katika maeneo yetu.”

Mratibu wa  mradi huo kutoka Iwapoa,  Yusuph Kutegwa amesema mradi huo utatekelezwa katika kata sita za Manispaa ya Temeke.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Buza, Keko, Chamazi, Vituka, Azimio na Charambe.

Amesema utawafikia wanawake 150 kutoka katika maeneo hayo waliyoyachagua kutokana na kuwa na wingi wa watu, wakiwamo wanawake wasiokuwa na shughuli za kudumu.

“Ili kuwapatia masoko na mitaji tutawaunganisha katika vikundi vya watu watano watano, ili iwe rahisi kuwapa ujuzi kwa pamoja, ”amesema Kutegwa.

Nduda, Mbonde njiani kurejea dimbani

Mlinda mlango namba mbili wa Simba, Said Mohammed 'Nduda' wiki ijayo anatarajia kujiunga na wenzake tayari kuanza mazoezi baada ya kuwa nje kwa miezi mitano, kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti Oktoba mwaka jana nchini India.

Nduda aliyesajiliwa na klabu ya  Simba Julai mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, hajacheza mechi yoyote msimu huu kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata Agosti mwaka jana mazoezini akiwa visiwani Zanzibar wakati Simba inajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Agosti 23, mwaka jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kwa sasa mlinda mlango huyo ameanza programu za mazoezi yake binafsi tangu mwanzoni mwa mwaka huu, akijifua ufukweni kwa mazoezi.

Wakati huo huo, beki wa kati wa Simba, Salim Mbonde anaendelea na mazoezi ya gym baada ya kuwa nje kwa zaidi ya miezi mitatu kufuatia kuumia Oktoba 15, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya timu yake ya zamani, Mtibwa Sugar uliomalizika kwa sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam.

Kiongozi mwengine wa Upinzani akamatwa Kenya

Mbunge mwingine nchini Kenya, amekamatwa kuhusiana na mzozo unaozunguka kujiapisha kwa aliyekuwa waziri mkuu Raia Odinga kwa kile anachokitaja kama rais wa watu wa Kenya.

Mbunge wa Makadara jijini Nairobi George Aladwa alikamatwa asubuhi ya Jumamosi nyumbani kwake na maafisa wa idara ya upelelezi na kupelekwa hadi makao makuu ya idara hiyo kwa mahojiano zaidi.

Aladwa ambaye amewahi kuwa meya wa jiji la Nairobi, alikuwa katika mstari wa mbele katika mipango ya sherehe hizo ambayo haikuwa na idhini ya serikali.

Aladwa sasa ni mbunge wa pili kukamatwa kuhusiana na hafla hiyo ambayo pia imeshutumiwa na jamii ya kimataifa.

Mbunge mwingine wa Nairobi Tom Kajwang alikamatwa na kufikishwa mahakamani na hatimaye kuachiliwa kwa dhamana.

Mwanaharakati mwingine wa upinzani wakili Miguna miguna pia alikamatwa siku ya Ijumaa na angali anazuliwa na polisi licha ya mahakama kuruhusu kuachiliwa kwake kwa dhamana.

Bwana Aladwa alikamatwa siku ya Ijumaa usiku katika nyumba yake iliopo Buruburu kulingana na kiranja wa walio wachache bungeni Junet Mohamed.

Bwana Mohammed ambaye pia mbunge wa Suna Mashariki alisema kuwa bwana Aladwa kwa sasa anazuiliwa katika makao makuu ya ujasusi.

Polisi hawajatoa tamko lolote kuhusiana na kukamatwa kwa Aladwa

Msanii Radio azikwa kwao Uganda

Msanii Radio wa nchini Uganda ambaye alifariki Februari 1, amezikwa leo kijijini kwao Nakawuka nchini Uganda, na kuhdhuriwa na maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali za nchi hiyo na wasanii wa nchi jirani.

Hapo jana Ijumaa ya Februari 2, wananchi wa Uganda na mashabiki wa muziki walipata fursa ya kufanya ibada ya mwisho ya kumuombea marehemu kanisani, na kisha baadaye mwili wake kupelekwa kwenye uwanja wa michezo wa Airstip, ambapo walikesha nao huku kukipigwa show ya nguvu kutoka kwa wasanii mbali mbali wa nchini Uganda.

Kabla ya mazishi hayo kuliibuka mvutano mkubwa wa nguo ya kuvalishwa marehemu, huku Lilian Mbabazi ambaye ni mama wa watoto wake wawili ambaye mwenyewe alimtambulisha kama mke wake akitaka marehemu azikwe na suti aliyovaa kwenye tamasha la 'Nakudata' ambayo ndio ngoma iliyompa umaarufu na kumfanya atoboe kwenye game, na mwanamke wake mzungu ambaye amezaa naye mtoto mmoja akisema marehemu alitaka akifa azikwe na nguo za jeshi kwani alipenda kuitwa mwanajeshi, na hatimaye akavalishwa gwanda za jeshi.

Asubuhi ya leo mwili huo ulipelekwa kijijni kwao Nakawuka na kuwekwa kwenye makazi yake ya milele, ambapo kwenye tukio hilo watu walionekana kuwa wengi na baadhi wakizimia.

Miongoni mwa wasanii waliohudhuria mazishi hayo ni msanii na mbunge Jaguar wa Kenya, wasanii mbali mbali wa Uganda na viongozi wa serikali.

Diwani Dar Aja Na Mpango Kunusuru Wananchi Wake



Diwani wa kata ya Salanga jijini Dar es salaam Harun Mdoe amekuwa na mpango mkakati wa mda mfupi na mrefu kuhusiana na barabara ambayo kwa sasa imekua kero kwa wananchi wa eneo hilo.

Mdoe amesema hayo leo alipotembelea barabara hiyo ambayo inaunganisha Matangini, Michungwani, King'ongo, Matosa, Kata ya Goba pia kuelekea Bagamoyo ambapo kwa mkakapi wa mda mfupi wamekuwa wakiweka vifusi ambavyo vinasaidia angalau kupitika kwa urahisi.

Kutokana na kero hiyo pia amewataka wananchi wanaoishi maeneo hayo kuacha mara moja tabia ya kumwaga maji barabarani ambayo yanasababisha uharibifu na wataoendelea kufanya hivyo watachukuliwa hatua za sheria.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Michungwani Ismaili Kipungula amesema kuwa kuna shida kubwa katika barabara hiyo ambayo inaunganisha mitaa mitatu.

"hii barabara imekuwa ni tatizo kwamba imeoza na sio kuharibika tumejaribu kuhangaika kama mtaa tukishirikiana na wananchi pamoja  Diwani wetu kama mnavyoona hizi ni jitihada za wananchi wenyewe lakini barabara bado sio nzuri hivyo tunaiomba Serikali waiangalie hii barabara pia wenzetu wa Tarura ambao wamekubali kutengeza wafanya haraka kwani ilifika hatua tulika mawasiliano" amesema Kipungula

Aidha kwa upanda wake mkazi na mtumiaji wa barabara hiyo Upendo Mbise amesema kuwa kina mama wamekuwa wakijifungulia njiani kutokana na adha na ubovu ulipo mimi mwenyewe nikiwa kama shahidi juzi mama mmoja alijifungulia njiani hali ambayo ni hatari pia inaweza kupelekea hata kifo


Mkuu wa shule aingia matatani kwa kuchangisha michango



Sumbawanga. Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza mkuu wa shule ya sekondari Muhama manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuchukuliwa hatua kwa tuhuma za kuwatoza wanafunzi michango ya Sh5,000 kama gharama ya kuwapatiwa fomu za maelezo ya kujiunga na shule hiyo.

Wangabo ametoa agizo hilo jana Februari 2, 2018 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Malangali baada ya baadhi ya wananchi kufichua jambo hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Sadock Kalinga amesema wazazi wamekuwa wakichangishwa kiasi hicho cha fedha ili wapatiwe fomu hizo.

“Tulilazimika kutoa fedha hizi na kupewa stakabadhi kwa kuwa tuliambiwa mwanachi ambaye hatotoa fedha  hawezi kupewa fomu hizo na hivyo kukosa sifa ya kujiunga katika shule hii,” amesema Kalinga.

Baada ya kupokea malalamiko hayo na kuonyeshwa risiti iliyotolewa kama ushahidi, Wangabo amemhoji Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu kuhusu uhalali wa mchango huo ambapo naye alikana kufahamu jambo hilo.

Alimuagiza mkurugenzi huyo kumchukulia hatua mkuu huyo wa shule kwa kuwa kitendo alichokifanya si sahihi kwa sababu Serikali imepiga marufuku michango shuleni.

“Ni marufuku kwa mwalimu yeyote kujihusisha na michango katika mkoa huu. Walimu kazi yao ni kufundisha na sio kuchangisha. Nakuagiza mkurugenzi kuchukua hatua katika hili na ninataka nipate taarifa’,” amesema.

Mwananchi:

Tume yaundwa kufuatilia korosho zenye kokoto

Serikali mkoani Lindi imeunda timu ya kuchunguza matukio ya baadhi ya wakulima kuchanganya mchanga na korosho kwa nia ya kuongeza uzito wakati wa kupima kwenye mizani, ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika kufanya hhujuma hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi amewaambia waandishi wa habari mjini Lindi kuwa, korosho iliyochanganywa na mchanga kugundulika kwenye ghala la Buko mjini humo na korosho nyingine iliyochanganywa na kokoto za lami iligundulika nchini Vietnam baada ya kusafirishwa kutoka Tanzania, ambapo mwenye korosho hizo alidai alizinunua wilayani Liwale mkoani humo.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuchafua taswira ya Tanzania kibiashara, imemlazimu kukutana na viongozi wa mkoa kujadili suala hilo na hatimaye kuunda timu ya uchunguzi wa matukio hayo ili hatua zichukuliwe haraka.

Pamoja na uchunguzi unaoendelea, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Ushirika cha Pangatena wilayani Lindi wanashikiliwa kwa uchunguzi na kusimamishwa kwa bodi ya chama hicho baada ya kubainika korosho walizofikisha kwenye ghala kuu la BUCCO zina viroba vya mchanganyiko wa korosho na mchangaTume

Rais Trump awasiliana na viongozi wa Japan na Korea Kusini

Rais wa Marekani Donald Trump amewapigia simu viongozi wa Japan na Korea Kusini siku chache kabla ya michezo ya Olimpiki kuanza nchini Korea Kusini.

Kwa mujibu wa habari,Trump amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe.

Viongozi hao wawili wamezungumzia mfumo wa ulinzi wa makombora wa Japan na vilevile uhamisho wa ngome ya Marekani katika kisiwa cha Okinawa.

Japan na Korea Kusini zimekuwa zikijitahidi kuidhibiti Korea Kaskazini kutofanya majaribio ya makombora ya nyuklia.

Korea Kaskazini ilirusha kombora la nyuklia mnamo mwezi Novemba mwaka jana.