Thursday, 25 January 2018

Makonda Azindua Jengo La Upasuaji Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua jengo la upasuaji katika Hospitali ya Mwananyamala lililojengwa kwa msaada wa kampuni ya GSM.

Katika uzinduzi huo Makonda amesema kuwa Serikali itaandaa mpango wa kuwezesha wananchi kupata matibabu kwa kutumia kadi ya bima ya afya katika hospitali zote za umma.

Aidha amesema mwananchi mkoani Dar es Salaam ambaye hatakuwa na kadi hiyo hataweza kupata huduma.
Amesema lengo la mpango huo ni kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa matibabu hata wakati hawana fedha.

"Ni muhimu tuingie kwenye mfumo wa matibabu kwa kadi badala ya kuchangishana na kusumbua watu kwenye simu. Itafikia wakati mtu ambaye hana kadi hatatibiwa kwenye hospitali zetu," amesema.

Serikali inaendelea kuboresha mazingira na miundombinu ili kuwapatia wananchi huduma bora ya afya.

Makonda aliyefanikisha ujenzi wa jengo hilo kwa kutafuta wafadhili ameahidi mwaka huu ataanza ujenzi wa wodi za wagonjwa na hasa akina mama.

Akizungumzia jengo hilo jipya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dk Festo Bugange amesema kukamilika kwake kutapunguza msongamano wa akina mama waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu kufanyiwa upasuaji.
Dk Bugange amesema jengo hilo lina vyumba viwili vya upasuaji tofauti na kimoja kilichokuwepo awali. Amesema sasa watahudumia wagonjwa wengi zaidi na kwa muda mfupi.

Amesema Hospitali ya Mwananyamala inahudumia wagonjwa kati ya 1,800 na 2,000 kwa siku. Pia, inahudumia wajawazito kati ya 1,500 na 2,000 kwa mwezi.

"Asilimia 25 ya wajawazito wanaokuja Mwananyamala wanahitaji kufanyiwa upasuaji, kwa hiyo walikuwa wanasubiri kwa muda mrefu lakini sasa tuna vyumba vya upasuaji vitatu," amesema Dk Bugange.

Lava Lava – Kilio (Behind The Scene)

Lava Lava – Kilio (Behind The Scene)

Lava Lava – Kilio (Behind The Scene)


Wanaohusika na uteswaji wa Vijana kukamatwa



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Mwigulu Nchemba ameagiza kutafutwa na kukamatwa mara moja kwa watu wote wanaohusika na uteswaji wa vijana wanaopelekwa nje ya nchi kutafuta ajira.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa ya mateso wanayopata baadhi ya wananchi wa Tanzania wanaokwenda kufanya kazi tofauti tofauti nje ya nchi na kusema wameshafanya mawasiliano na Wizara zote zinazohusika na wameshakubaliana kila mmoja kuchukua hatua kulingana na wizara yake.

"Wale watu wanaoweka rehani vijana wetu, wamekuwa wakikimbia hapa na pale na ambao bado hawajakamatwa mpaka sasa waendelee kusakwa wote na wafikishwe katika mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwa vitendo hivyo vya kinyama na kuwapeleka vijana wetu katika vitendo vya kinyama na kusababisha majonzi kwa familia husika",alisema Dkt. Mwigulu.

Pamoja na hayo na Waziri Nchemba amesema matatizo wanayoyapata vijana hao kwa kisingizio cha kupatiwa kazi nje ya nchi mpaka sasa yamekuwa makubwa mno.

"Tumeona vijana wakiwa wamefungwa miguu vichwa chini na mikono yote huku wakitandikwa viboko kwa madai ya kwamba miongoni mwao kuna aliyewapeleka kuwapa kazi nzuri ya kufanya lakini kwa bahati mbaya wakifika huko wanawekwa rehani kwamba hawataondolewa pale walipo mpaka wale waliowapeleka wakiwa wameshamaliza kupeleka fedha za dawa za kulevya", alisisitiza Waziri Mwigulu Nchemba.

Mwalimu atiwa mbaroni kwa kumuua mtoto wa miezi 7




Mwalimu wa sekondari Stephen Wachira Wangara mwenye umri wa miaka 43, amefikishwa Mahakamani kwa kosa la kumuua mtoto wake wa miezi 7 kwa kumchinja na panga nchini Kenya.
Mashahidi watano wa tukio hilo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Jimbo la Kirinyaga, Maina Muriuki wamemweleza Jaji Lucy Gitari wa Mahakama Kuu ya Kerugoya, jinsi mtuhumiwa alivyoua mtoto wake,
Maina ameieleza Mahakama kuwa mwili wa mtoto huyo ulikuwa umewekwa ndani ya gunia ukiwa na damu, nje ya nyumba ya Wangara na pembeni ya mwili huo kuliwa na panga ambalo lilitumiwa kumuua mtoto huyo.
Shahidi mwingine Joseph Muriithi amesema wakati wa tukio hilo alikuwa shambani kwa Wangara akifanya kibarua na alimwona mtuhumiwa akiwa na madoa ya damu na muda mfupi baadaye alisikia kelele kutoka kwenye nyumba ya mwalimu huyo.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi March 1, 2018, ambapo itasikilizwa tena.
Wangara ambaye ni mtuhumiwa ni baba mwenye watoto wawili na mwalimu katika shule ya Sekondari ya Gituya.

Mtoto wa miaka 14 auawa kikatili



Mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Vikonge Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi mwenye miaka 14 ameuawa kikatili baada ya kubakwa kisha kuchomwa kisu ubavuni na kisha kunyofolewa sehemu za siri wakati akiwa anakwenda shuleni na mdogo wake aliyekuwa anasoma naye shule moja.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi Damas Nyanda alisema tukio hilo limetokea Januari 23,2018 majira ya saa moja na nusu asubuhi umbali wa kilometa moja na nusu kutoka katika shule ya msingi Vikonge ambapo marehemu huyo alitoka nyumbani kwao kwa lengo la kwenda shuleni kama kawaida yake huku akiwa na mdogo wake wa kiume (11) mwanafunzi wa darasa la nne shule ya Msingi Vikonge ambaye jina lake limehifadhiwa.

“Wakati wakiwa njiani alitokea mwendesha pikipiki mmoja ambae walikuwa hawamfahamu na kusimamisha pikipiki yake na kisha aliwaambia awape msaada wa usafiri wa kuwafikisha shuleni kwao na baada ya kuambiwa hivyo wanafunzi hao walikubali kupewa msaada wa pikipiki”, alieleza.
“Hata hivyo mara baada ya marehemu kuwa amepanda pikipiki hiyo mwendesha boda boda huyo alimzuia mdogo wa marehemu asipande kwenye pikipiki hiyo na kisha aliiondoa kwa kasi huku akiwa na marehemu na kumwacha kaka yake”, aliefafanua Kamanda wa polisi.
Alisema hali hiyo ilimfanya kaka yake aamue kuifuata pikipiki hiyo kwa nyuma na ndipo wakati akiwa njiani aliona pikipiki kama ile iliyokuwa imembeba dada yake ikiwa pembezoni mwa barabara kwenye kichaka hata hivyo aliendelea na safari yake ya kwenda shuleni.
“Kaka huyo wa marehemu kutokana na kuwa na umri mdogo baada ya kufika shuleni hakuweza kumtafuta dada yake na badala yake aliingia darasani na kuendelea na masomo kama kawaida na baada ya muda wa masomo ilipofikia majira ya saa nane na nusu mchana alianza safari ya kurejea nyumbani pasipo kumtafuta dada yake”,alisimulia Kamanda huyo.
Kamanda Nyanda alieleza baada ya kuwa amefika nyumbani kwao wazazi wake walishtuka kumwona akiwa peke yake ndipo aliwaeleza mazingira yote ya jinsi alivyo achana na dada yake wakati walipokuwa njiani na jinsi alivyoiona pikipiki iliyombeba dada yake ilivyokuwa kwenye kichaka.

Alisema baada ya kupata maelezo hayo, wazazi wa marehemu walipatwa na mashaka hivyo walimtaka mdogo wa marehemu awapeleke kwenye eneo aliloona pikipiki ikiwa kwenye kichaka.
“Wazazi wa marehemu waliokuwa wameongozana na majirani zao baada ya kufika kwenye eneo hilo walishtuka kuona majani yakiwa yamelala na walipoenda mbele kidogo waliuukuta mwili wa marehemu ukiwa amechomwa kisu sehemu ya ubavu wake wa kulia na sehemu za siri zikiwa zimenyofolewa”, alieleza Kamanda Nyanda.

Alisema jeshi la polisi mkoa wa Katavi linaendelea na msako wa kumtafuta mtu au watu waliohusika na mauaji hayo ya kikatili hadi sasa hakuna mtu wala watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kaimu mwalimu Mkuu wa Shule ya Vikonge Mwalimu Gadinendi Kaseka ameiambia Malunde1 blog kuwa mpaka walipomaliza masomo ya siku hiyo hawakuwa na taarifa juu ya kifo cha mwanafunzi huyo ila walipata taarifa hiyo siku hiyo hiyo majira ya saa kumi na mbili jioni baada ya mwili wa marehemu kupatikana.

Stand United yatamba kuiburuza Ndanda leo



 Stand United inaikaribisha Ndanda leo Alhamisi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

 Kivutio katika mchezo huo kitakuwa ni nahodha  wa Ndanda, Jacob Massawe kurejea katika uwanja huo kuikabili  timu yake ya zamani Stand United.

Kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal 'Bilo' amesema wako vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Hata hivyo Bilo alisema itakuwa mechi ngumu kwani zinakutana timu zenye pointi sawa hivyo kila mmoja atataka ushindi ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

"Tumefanya maandalizi yetu vizuri na tuko tayari kwa mchezo kuhakikisha tunavuna pointi zote tatu.

"Itakuwa mechi ngumu kwani Ndanda ina wachezaji wazuri na pia kama unavyojua wote tuna pointi sawa hivyo itakuwa ni vita ya kuwania ushindi" alisema Bilo.

Naye kocha wa Ndanda, Malale Hamsini alisema anajua ugumu wa kucheza ugenini lakini watapambana ili kuweza kupata ushindi.

"Hii ni mechi ya pili Kanda ya ziwa baada ya ile ya Mwadui kutoka sare wiki iliyopita sasa tunahitaji ushindi dhidi ya Stand United ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi," alisema Malale.

Hakimu akataa kujitoa kesi dhidi ya Sugu


 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite amekataa kujitoa kusikiliza kesi inayomkabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na mwenzake.

Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli wanayodaiwa kuitoa Desemba 30,2017.

Awali, leo Alhamisi Januari 25,2018 Sugu na Masonga waliwasilisha ombi mahakamani wakimkataa hakimu huyo wakitaka ajitoe kusikiliza kesi kwa maelezo kuwa hawana imani naye.

Hakimu Mteite amesema sababu zilizotolewa na akina Sugu hazipo kisheria na hazimfanyi kujitoa.

Baada ya hakimu kukataa kujitoa, mawakili Boniface Mwabukusi, Hekima Mwasipu na Sabina Yongo wanaowawakilisha washtakiwa walitangaza kujitoa katika shauri hilo.

Soma: Sugu, mwenzake wamkataa hakimu

Sugu na Masonga wameiomba Mahakama kuwapatia wiki mbili za kutafuta mawakili wengine.

Hakimu Mteite ameahirisha kesi hadi Februari 2,2018  na ameamuru washtakiwa kurejeshwa rumande.

TAKUKURU yaeleza haya baada ya kukamilisha upelelezi kesi ya Malinzi


 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF), Jamal Malinzi na wenzake umekamilika.

Mbali ya Malinzi, wengine ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Msiande Mwanga.

Wakili wa TAKUKURU, Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa, pia jalada la kesi hiyo wameshalifanyia kazi ambapo upelelezi wamekamilisha.

Swai amedai kuwa jalada la kesi hiyo watalirudisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kama alivyowaagiza walirudishe kwake ili alikague tena baada ya upelelezi wao kukamilika.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi February 8,2018 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418 na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

Waziri Kigwangalla atoa agizo kwa Jeshi la Polisi


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamisi Kigwangalla amesema anawajua vigogo wanne waliopanga mauaji ya muhamasishaji wa utalii ‘Wayne Lotter’ mwaka jana na kulitaka jeshi la polisi liwakamate watu hao ingawaje hajawataja hadharani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dodoma, Dkt. Kigwangalla amelitaka jeshi hilo lichukue hatua haraka za kuwakamata vigogo hao la sivyo ataenda moja kwa moja kutoa taarifa kwa Amiri jeshi Mkuu.

“Nawajua watu 4 waliopanga mauaji ya mhamasishaji wa utalii Wayne Lotter, watu hao ni vigogo na wanajulikana,“amesema Dkt. Kigwangalla.

Waziri Kigwangalla amesema ndani ya kipindi cha siku 100, Wizara yake imebaini mitandao 74 ya watu wanaojihusisha na ujangili ikiwa na washiriki 949 ambapo amedai baadhi ya washiriki hao tayari wameshafikisha Mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Kuhusu kifo cha Mwanaharakati Wayne Lotter soma zaidi kwa kubonyeza link hii “Mwili wa mwanaharakati wa tembo aliyeuawa kwa risasi kuagwa Dar“.

Mwanafunzi auawa baada ya kubakwa


MWANAFUNZI wa kike mwenye umri wa miaka 14 ameuawa kikatili baada ya kubakwa kwa zamu na mwendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ kisha akachomwa kisu ubavuni na sehemu zake za siri kunyofolewa wakati akienda shule akiwa amefuatana na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 11.

Mwanafunzi huyo alikuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Vikonge katika wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, sambamba na mdogo wake wa kiume ambaye alikuwa akisoma darasa la nne kwenye shule hiyo. Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema kuwa tukio hilo la kikatili lilitokea juzi Jumanne saa moja asubuhi umbali wa kilometa moja na nusu kutoka shuleni hapo.

“Asubuhi hiyo ya tukio, marehemu akiwa ameongozana na mdogo wake wa kiume huku wakielekea shuleni walikutana na mwendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ ambaye alikuwa hawamfahamu na kuwaambia kwamba atawapa lifti. Marehemu alipopanda mwendesha bodaboda alimzuia mdogo wake wa kiume asipande ambapo aliondoka akiendesha pikipiki hiyo kwa kasi isiyo ya kawaida huku kaka wa marehemu akiikimbilia bila mafaniko.

Aliongeza kuwa mdogo wa marehemu alipoamua kutembea kwa miguu kuelekea shuleni baada ya kuchoka kuifukuza pikipiki hiyo, ghafla aliiona pikipiki ile iliyombeba dada yake ikiwa imeegeshwa karibu na kichaka kando ya barabara inayoelekea shuleni kwao na akaipita.

Kamanda Nyanda alisema kaka huyo wa marehemu alienda shuleni hapo na kuhudhuria darasani kama kawaida hadi ilipofika saa nane na nusu alianza safari kuelekea nyumba pasipo kumtafuta dada yake.

“Kaka wa marehemu bila shaka kutokana na umri wake kuwa bado mdogo baada ya kufika shuleni hakushughulika kumtafuta dada yake, aliingia darasani na kuendelea na masomo kama kawaida na baada ya muda wa masomo yaani saa nane na nusu alianza safari ya kurejea nyumbani bila kumtafuta dada yake,” alieleza Kamanda Nyanda.

Aliongeza kuwa baada ya mtoto huyo kufika nyumbani wazazi wake walishtuka kumuona akiwa pekee yake ndipo walipomuhoji alikomuacha dada yake ndipo alipowasimulia kila kitu.

“Wazazi wa marehemu baada ya kupata maelezo hayo walipatwa na mashaka hivyo walimtaka mdogo wa marehemu awapeleke kwenye eneo alipoina pikipiki iliyombeba dada yake ikiwa imepakiwa karibu na kichaka. Mtoto huyo aliwaongoza wazazi wake ambao walikuwa wamefutana na majirani zao hadi kwenye eneo la tukio, walishtuka kuona kuwa kuna nyasi zilikuwa zimelala ndipo walipoona mwili wa marehemu ukiwa umechomwa kisu ubavuni huku sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa.

Mwalimu akamatwa kwa kutumia lugha ya matusi kwenye mtandao


JESHI  la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari  Mkolani, Deogratius Kisandu, akidaiwa kutumia lugha ya matusi, kejeli na kudhalilisha katika ukurasa wake wa Facebook.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema  Kisandu alikamatwa jana baada ya kuwapo taarifa kuhusu kuonekana ujumbe wa matusi na lugha zisizofaa  katika ukurasa  wake ya Facebook.

Alisema walimfuatilia mtuhumiwa na kumkamata akiwa na simu yake ambayo huitumia kupeleka na kuandika matusi hayo kinyume na Sheria Namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

“Polisi bado wanaendelea na  na mahojiano na upelelezi dhidi ya mtuhumiwa. Utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

“Taarifa zinaonyesha kuwa mtuhumiwa amewahi kushtakiwa kwa makosa kama hayo kipindi cha nyuma,” alisema Kamanda Msangi.

Kamanda   amewataka  vijana wanaotumia mitandao ya  jamii kuacha kwa sababu  ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema alipokea  malalamiko kutoka kwa wananchi siku mbili zilizopita kuhusu lugha ya kudhalilisha, matusi na kejeli  inayotumiwa na Kisandu ambaye pia ni mtumishi wa umma, katika  ukurasa wake wa Facebook.

“Tumetumia siku mbili mpaka kumpata Kisandu. Mwanzoni nilifikiri labda haya mambo yanafanywa na mtu ambaye si raia wa Tanzania lakini katika mahojiano amekiri yeye ni Mtanzania.

“Kwa kweli lugha anayoitumia ni ya kudhalilisha, matusi na kejeli na haifai kutumiwa kutokana na utamaduni wetu,” alisema.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa,   Lawi Odiero, alisema sheria ipo na inakataza matumizi mabaya ya mitandao na  kwa kuwa kesi hiyo ipo polisi  atatoa ushirikiano unaohitajika kusaidia uchunguzi.

Akukumiwa Kwa kumwingilia mwanaume kinyume cha maumbile


Mahakama ya Mkoa wa Mwera imemuhukumu mshtakiwa Simai Khamis Salum mwenye umri wa miaka 30 mkaazi wa Uzini wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kutiwa hatiani kwakosa lakumuingilia mwanamme mwenziwe kinyume na maumbile.
Imedaiwa Mahakamani hapo namuendesha mashtaka Rahima Kheir mbele ya hakimu Muhammed Ali Muhammed kwamba mnamo tarehe 2/3 /2015 huko Uzini bila ya ridhaa kwamakusudi amefanya kitendo hicho kwakijana mwenye umri wa miaka 20 jinalimehifadhiwa na kumsababishia maumivu makali huku akijua jambo hilo ni kosa kisheria.
Akisoma hukumu Hakimu Muhammed amesema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwa upande wa mashtaka na kumuona nimkosa wakosa hilo ndipo Mahakama hiyo ilipomtia hatiani kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka saba pamoja na kumlipa fidia mtendewa yashilingi Milioni mbili ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Mawakili wa Sugu wajiondoa kwenye Kesi


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya, Michael Mteite, amegoma kujitoa katika kusikiliza kesi inayowakabili Mbunge Joseph Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Mapema leo Alhamisi Januari 25,2018 Sugu na Masonga waliwasilisha ombi mahakamani wakimkataa hakimu huyo wakitaka ajitoe kusikiliza kesi kwa maelezo kuwa hawana imani naye.

Hakimu Mteite amesema sababu zilizotolewa na akina Sugu hazipo kisheria na hazimfanyi kujitoa.

Baada ya hakimu kukataa kujitoa, mawakili Boniface Mwabukusi, Hekima Mwasipu na Sabina Yongo wanaowawakilisha washtakiwa walitangaza kujitoa katika shauri hilo.

Sugu, mwenzake wamkataa hakimu Sugu na Masonga wameiomba Mahakama kuwapatia wiki mbili za kutafuta mawakili wengine.

Hakimu Mteite ameahirisha kesi hadi Februari 2,2018 na ameamuru washtakiwa kurejeshwa rumande.