Wednesday, 24 January 2018

Dully Sykes `kuufikisha mtandao wa simu Mahakamani



MKONGWE kwenye Muziki wa Bongo Fleva, Anthony Wayson ‘Dully Sykes’ ameeleza kuwa anatarajia kuuburuza mahakamani mtandao maarufu wa simu za mkononi Bongo kwa madai kwamba umeshindwa kulinda nyaraka zake muhimu.

Akipiga stori na Risasi Vibes, Dully alisema kuwa, mtandao huo umesababisha matapeli kutumia laini yake ya simu kufanya utapeli kwa watu wake mbalimbali.

“Kuna mtu ame-renew laini yangu, akapewa ushirikiano mkubwa na kampuni hiyo ya simu, aka-hack’ facebook yangu kisha akawaomba watu pesa na picha za utupu kwa wanawake, lazima niushtaki mtandao huu kwani unahusika,” alisema Dully Sykes.

Aslay afunguka Idadi ya ngoma alizotoa tangu kuondoka Yamoto Band




Mwanamuziki Aslay amefunnguka idadi ya nyimbo alizotoa tangu kuondoka Yamoto Band.

Muimbaji huyo ameiambia Power Breakfast ya Clouds Fm kuwa hadi sasa ametoa nyimbo zipatazo 16 na kufanya hivyo kwa kipindi kifupi kimemsaidia katika show zake.

“Imenisadia kwa namna moja au nyingine kwenye show zangu, nikienda kufanya show nafanya nikiwa na nyimbo zangu mimi kama mimi na show inakamilika, nina nyimbo 16 sasa hivi,” amesema Aslay.

Kwa sasa Aslay anafanya vizuri na wimbo ‘Subal kheir’ alioshirikiana na Nandy ambao awali uliimbwa na Culture Group kutoka visiwani Zanzibar.

Nafasi za kazi leo Jan 24

Vurugu za Kidini zasababisha Wanafunzi kuchomana visu Kenya



Mamia ya wanafunzi nchini Kenya katika shule ya Sekondari ya Jamhuri jijini Nairobi wapo katika hali mbaya ya kiafya baada ya usiku wa jana kutokea vurugu ya kidini kwenye shule hiyo.

Taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya zinaeleza kuwa wanafunzi hao walikuwa wakizozana kati ya Waislamu na Wakristo.

Kwenye mzozo huo Wanafunzi wa dini ya Kiislamu walikuwa wanawalazimisha wenzao wakristo kubadilisha dini (Kuslimu) na ndipo vurugu zilipoanzia.

Taarifa za awali zinaelezakuwa vurugu hizo zimetokea usiku wa kuamkia leo na mamia ya Wanafunzi wamejeruhiwa kwa kuchomwa visu huku vitanda na madawati yakivunjwa kwenye vurugu hizo.

Hata hivyo tayari Jeshi la Polisi jijini Nairobi limefika shuleni hapo asubuhi hii kufuatilia tukio hilo ili kutoa taarifa rasmi idadi ya wanafunzi waliojeruhiwa.

Source:Bongo 5


Thierry Henry bifuni na mashabiki wa Arsenal


Thierry Henry kwa sasa amepachikwa majina mengi ya kejeli na mashabiki wa Arsenal kutokana na madai ya kumshawishi Alexis Sanchez kujiunga na Manchester United.

Wengine wamekuwa wakimuita nyoka msaliti na mengine mengi. Kocha huyo msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji na mchezaji wa zamani wa Arsenal amekana kuwa hakuwahi kumshauri Sanchez kufanya maamuzi hayo.

Henry ametoa taarifa hiyo kupitia mtandao wake wa Twitter, ameandika, “Ninajua sihitaji kuelezea hili kwa mashabiki wengi wa Arsenal lakini kinyume na uvumi hakuna muda wowote nilimwambia Alexis Sanchez aondoke Arsenal. Sikujua kwamba angeenda kusajiliwa na Man Utd mpaka nilipoona kwenye habari kama wengine.”

Baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na Man United, Alexis Sanchez alithibitisha kwa kuandika ujumbe kuwa alipokea ushauri wa kuondoka Arsenal na kujiunga na Manchester kutoka kwa Henry.

“Nakumbuka leo, mazungumzo niliyokuwa nayo na Henry, mchezaji wa kihistoria wa Arsenal, ambaye alibadilisha klabu kwa sababu hiyo hiyo na leo ni wakati wangu,” aliandika Sanchez.

Bushoke afunguka kuhusu Q Chief


Msanii Bushoke ambaye aliwahi kufanya vizuri katika tasnia ya muziki wa Bongofleva katika kipindi cha nyuma amefunguka na kukana taarifa za yeye kugombana na Q-chief na kudai wanaweza kutofautiana lakini siyo kuzinguana kabisa.

Bushoke ameeleza hayo kupitia kipindi cha eNewz kutoka EATV baada ya kuwepo fununu kuwa wakongwe hao kwa sasa ni kama paka na panya licha ya kuwa karibu hapo awali na hata kurekodi wimbo mmoja studioni lakini mpaka sasa kazi hizo zimefungiwa studio.

"Some times' tunaweza kutofautiana lakini siyo kivile kwa hiyo namshukuru Mwenyezi Mungu yaani tupo karibu hata huko kutofautiana inawezekana mmoja wetu siku ameamka vibaya kwa hiyo ndio vitu hivyo lakini kugombana hatujawahi", alisema Bushoke.


Rais wa TFF aguswa na msiba wa Kocha wa Mwadui


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Jumanne Ntambi na wachezaji wa Mwadui kwa kuondokewa na kocha wao usiku wa kuamkia leo huku akiwataka wafiwa wawe na moyo wa subira

Rais Karia amesema hayo katika salamu zake zilizotolewa rasmi na Shirikisho hilo huku akisema ameshtushwa kupata taarifa hizo kwani marehemu Ntambi alikuwa na mchango mkubwa katika soka la Tanzania.

"Kifo cha Kocha Ntambi kimenishtua sana na kwa niaba ya Shirikisho natoa pole kwa wafiwa, nawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu kwao kumpoteza mpendwa wao. Hakika alikuwa kocha aliyejitahidi kuibua vipaji na amekuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu ambao bado alikuwa anautumikia mpaka kifo chake," alisema Rais Karia.

Enzi za uhai wake Jumanne Ntambi aliwahi kufundisha timu za Kahama United ya Shinyanga, Mlale JKT ya Ruvuma, Panone ya Kilimanjaro, timu ya mkoa wa Shinyanga Igembe Nsabo na mpaka mauti yanamkuta alikuwa akiifundisha Mwadui ya Shinyanga akiwa kocha msaidizi.

Serikali yatakiwa kupiga marufuku mifuko ya plastiki


Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeiagiza Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kutoka nje ya nchi ili kulinusuru Taifa na madhara yanayotokana na mifuko hiyo.

Maagizo hayo yalitolewa baada ya kamati hiyo jana kukutana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Akizungumza jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Sadiq Murad alisema walipata maelezo kutoka serikalini kuwa uzalishaji katika viwanda 41 vya plastiki nchini ulikuwa ni tani 73 katika mwaka 2016.

Hata hivyo, alisema mifuko iliyoingia nchini kupitia bandarini na mipakani ilikuwa tani 1,375.

“Kamati ilishauri ipigwe marufuku mifuko ya plastiki kutoka nje ya nchi na iwekwe tahadhari katika mipaka yetu,” alisema.

Alisema kamati inaitaka Serikali kufanya uhakiki wa uzalishaji katika viwanda vya nchini ambavyo vimepunguza uzalishaji ili waweze kukaa chini na kuzalisha mifuko ambayo itakayokidhi mahitaji na vigezo.

“Na hii itakuwa ni ya muda kuzalisha mifuko hiyo kwa masharti ya vigezo baadaye Tanzania isiwe na uzalishaji wa mifuko hii tena inayoharibu mazingira,” alisema.

Murad alisema zipo nchi nyingine kama Kenya, Rwanda, Uganda na Zanzibar ambazo zimepiga marufuku uzalishaji na uingizaji wa mifuko hiyo na kutafuta mifuko mingine inayotengenezwa na nguo, karatasi na majani.

Alisema mfano mzuri ni Zanzibar ambayo imepiga marufuku mifuko hiyo tangu mwaka 2016 na mtu anapoingia na mifuko hiyo bandarini hunyang’anywa na kupewa mingine.

“Tueleweke kabisa sisi kama kamati hatutaki kiwanda chochote kifungwe, tunataka uzalishaji kwa kufuata masharti na vigezo. Tunaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda lakini vigezo na masharti lazima yazingatiwe,” alisema.

Akizungumzia agizo hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema hawaja japelekewa rasmi hayo mapendekezo. Hata hivyo alisema watapiga marufuku mifuko yote ya ndani na nje. “Wenye viwanda wajiandae maana yake dhamira ya Serikali wanaijua tangu mwaka 2016,” alisema

Aliyekua kipa wa Yanga azikwa Burundi


 Kipa wa zamani wa Yanga, Ismail Suma enzi za uhai wake.

KIPA wa zamani wa Yanga, Ismail Suma amezikwa nchini Burundi baada ya kukosa msaada wa kiuchumi kumrejesha nchini.

Habari za awali zilizopatikana Jumanne asubuhi zilisema kwamba Suma alifia kwa rafiki yake alipokuwa amekwenda kumsalimia.

Baada ya kutokea tatizo hilo, wadau wakaanza kupambana kusaka fedha za kurejesha mwili Tanzania lakini jioni, zikatumwa picha kwenye mitandao ya Burundi kwamba ameshazikwa kulekule.

Habari zinasema kwamba alizikwa kidini na idadi ndogo ya watu kwavile alikuwa hafahamiki.

Akifanyiwa maombi kabla ya kuzikwa.

Sanchez aimwagia sifa Man United



Mshambuliaji Alex­ies Sanchez.

MANCHESTER United, juzi, ilimsajili mshambuliaji Alex­ies Sanchez ambapo kwenye mahojiano yake ya kwanza amesema kuwa amejiunga na timu kubwa dun­iani.

Sanchez amejiunga na Manches­ter United baada ya staa wa timu hiyo Henrikh Mkhitaryan ku­jiunga na Arsenal.

Sanchez alikubali ku­saini mkataba wa miaka minne kuitumikia timu hiyo ya United ambayo in­afundishwa na kocha Jose Mourinho.

“Ninafuraha kubwa k u j i u n g a na timu kubwa duniani, hakika ni jambo jema kupata nafasi ya kucheza kwenye uwanja huu mkubwa na wenye his­toria.

“Lakini nikiri kuwa ninafuraha kubwa sana kufanya kazi chini ya kocha Jose Mourinho hili lilikuwa jambo gumu kukataa.

Sanchez ndiye mchezaji atakayekuwa ak­ilipwa ghali zaidi kwenye Ligi Kuu ya England kwa sasa akiwa anachukua jumla ya pauni 600,000 kwa wiki.

“Kuanzia nilipokuwa mdogo nilikuwa nase­ma kuwa nataka kuona siku moja naichezea United na siyo kwamba nasema hivyo kwa kuwa sasa nipo hapa, leo nasema kuwa ndo­to imetimia.

“Naamini nikiwa kwenye klabu hii nina uhakika wa kupata kombe lol­ote, nataka kuwa hapa na kushin­da kila kitu.

“Nataka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya, naamini ni jambo linalowezekana,” alisema Sanchez.

Sanchez alipewa jezi namba saba kwenye timu hiyo, jezi ambayo pia alikuwa akiivaa alipokuwa akiitumikia Arsenal.

Jezi hiyo ina historia nzuri kwenye kikosi cha United ikiwa iliwahi kuvaliwa na mas­taa George Best, Eric Cantona, David Beckham na Cristiano Ronaldo.

“Waliponiambia kuwa jezi hii ilivaliwa na Cristiano, Cantona, David Beckham nilikaa nikaamini kuwa ni rahisi kupata Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu Eng­land.

Hiki ndicho alichokerwa Vanessa kwa Jux



Malkia wa Bongo Fleva anayefanya vizuri ndani na nje ya nchi, Vanessa Mdee amefunguka na kuweka bayana kwamba alikuwa anakerwa na tabia ya mpenzi wake Jux ya ku-follow wanawake ambao hawaendani nae katika mitandao ya kijamii.

Vanessa ametoa siri hiyo ambayo ilikuwa inamtafuna katika moyo wake kwa kipindi kirefu kupitia kipindi cha 'Planet Bongo ya East Afrika Radio' wakati alipokuwa akifanya mapitio ya albamu yake 'Money Monday', na kusema wimbo wa unfollow ni jambo la kweli ambalo yeye mwenyewe amelipitia katika mahusiano yake na lilikuwa linamkera kupita kiasi.

"Wimbo huu ni stori ya ukweli kabisa ambapo mpenzi wangu alikuwa ananikera na tabia ya ku-follow wasichana wengine katika 'Instagram' ambao nilikuwa siwataki, siwapendi halafu hatuendani nao. Nikawa namuuliza unawa-follow wa kazi gani ? lakini sikuwa napata majibu sahihi", alisema Vanessa.

Pamoja na hayo, Vanessa amedai ameandika wimbo huo kutoka na shida wanazipitia jinsia ya kike (wasichana na wanawake) wanayoipata kwa wapenzi wao pindi wanapotumia mitandao ya kijamii.


TBA yavunjiwa Mkataba na Serikali


Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Josephat Kandege.

SERIKALI imevunja mkataba na Wakala wa Majengo TBA baada ya kutoa taarifa za uongo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu ujenzi wa majengo ya Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Butiama na halmashauri mpya Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Wiki iliyopita kuwa wakala huyo wa majengo alipewa onyo na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako baada ya kusuasua kuanza mradi wa Ujenzi wa Madarasa, Ofisi za Chuo Kikuu cha Muhimbili Kampasi ya Mloganzila huku wakiwa wamepewa fedha na Serikali tayari.

CCM, Chadema kuzindua kampeni siku moja


Vyama vya CCM na Chadema vinatarajia kuzindua kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni Jumamosi Januari 27,2018.

Wakati CCM ikisema itazindua kampeni katika viwanja vya Biafra; Chadema haijaweka wazi eneo la uzinduzi.

Uchaguzi katika jimbo hilo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya CUF, Maulid Mtulia kujivua uanachama wa chama hicho akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye alijiunga na CCM.

Mtulia amepitishwa na CCM kuwania tena ubunge jimboni humo ambako atachuana na Salum Mwalimu wa Chadema ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar.

CCM imeanza kwa kumtambulisha Mtulia katika vikao vya ndani na kwenye kata mbalimbali.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba amesema kampeni zitaanza saa sita  mchana.

Amewaomba wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara.

Naye Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema amesema watazindua kampeni Kinondoni Jumamosi, ikiwa ni siku moja baada ya uzinduzi kufanyika katika jimbo la Siha.

“Jimbo la Siha kampeni zitafanyika uwanja wa Ngarenairobi na Kinondoni bado hatujajua ni wapi ila tutawaeleza. Kampeni hizi zitahudhuriwa na viongozi wakuu na ndiyo maana tumetofautisha siku ya uzinduzi,” amesema.

Uchaguzi katika jimbo la Siha unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema, Dk Godwin Mollel kujivua uanachama na kujiunga na CCM ambayo imempitisha kuwania tena nafasi hiyo.