Tuesday, 23 January 2018

Kiwanja Cha Kujenga Nyumba Kinauzwa Eneo la Mapinga Karibu na Bunju B


Kiwanja cha Kujenga Nyumba Kinauzwa , Kina Size ya 20 Kwa 20 Mita, Kipo Eneo la Mapinga Karibu na Bunju B, Kipo Karibu na Barabara ya Lami
Shilingi Mil 8. Maongezi yapo Kidogo

Piga simu 0714604974 Kwa Mawasiliano zaidi


Jeshi la Polisi lasema Nabii Tito anamatatizo ya akili


JESHI la Polisi mkoani Dodoma,  baada ya kumkamata na kumfanyia mahojiano Onesmo Machija (44) anayejiita ‘nabii’ Tito, kutokana na mahubiri ya kidini anayoyafanya, limesema mtu huyo ana  matatizo ya akili.

Akizungumza na wanahabari mjini Dodoma leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gillesi Muroto, amesema mnamo Juni 23, 2014, mtu huyo aliwahi kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya akili chini ya daktari aliyejulikana kwa jina moja la William ambapo aliporuhusiwa alitakiwa kurejea hospitalini hapo Julai 9 mwaka huohuo lakini hakurejea.

Kamanda Muroto aliendelea kusema kwamba baada ya hapo, Machija ambaye kanisa lake halijasajiliwa popote,  aliibukia mkoani Dodoma katika kijiji cha Nong’ona kilicho karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akifanya  mahubiri ya kidini yaliyodaiwa kuwa hayakuwa na maadili ya kidini.

Kwa msingi huo, alisema jeshi la polisi limempeleka Hospitali ya Rufaa ya Mirembe iliyoko mkoani Dodoma  kwa ajili ya kumpima tena matatizo hayo ya akili na baada ya majibu kutolewa,  Dkt. Dixon Philipo aliyemshughulikia alithibitisha kwamba bado ana matatizo hayo.

Pamoja na hayo, Muroto alisema jeshi la polisi mkoani humo  bado linaendelea kumshikilia kutokana na matendo yake aliyoyafanya ili kufanya uchunguzi zaidi.

Source:Global Publishers

Wenger kumsajili Aubameyang




Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuendelea kwa mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa timu ya Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang.

Aubameyang mshambuliaji huyo wa kimataifa wsa Gabon amehusishwa kujiunga na the Gunners na Wenger amesema kila kitu kinaendelea.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama anauhakika wa kunasa saini ya Aubameyang, Wenger amesema “Kuwe na uhakika kusiwe na uhakika, mi sijui.”

Wenger ameongea “Huwezi jua ni kwa jinsi gani dirisha la usajili litakavyo kamilika.”

“Hivi ni vitu ambavyo uwezekano wa kukamili upo lakini pia tuna mambo mengine tunayofikiria mbali na usajili huo na nafasi tunayo na muda bado haujakwisha.”

“Kwa kipindi hiki bado hatujakamilisha dili lolote kuhusu Aubameyang au mtu mwingine yeyote.”

 Alipoulizwa kama mchezaji wake, Olivier Giroud atakuwa sehemu ya dili la kumnasa Aubameyang kwa yeye kuelekea Dortmund, Wenger amesema kuwa mazungumzo hayajafikia katika hatua hiyo.

Timu hiyo imekamilisha mpango wa Alexis Sanchez kutua Manchester United huku Arsenal ikinufaika kwa kumnasa Henrikh Mkhitaryan.


Onyo alilotoa Jaji Mkuu kwa viongozi wa serikali na wanasiasa


Jaji Mkuu wa Tananzania, Profesa Ibrahimu Juma amewataka viongozi wa serikali na vyama vya siasa kuacha mara moja vitendo vya kuingilia mhimili wa Mahakama na kuvunja amri zake.

Jaji Profesa Juma ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya Sheria inayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao (Februari mosi), siku ambayo ndio itakayoashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu 2018 yatakayofanyika katika viwanja vya Mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.

"Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama tu, nawasihi viongozi wote wa serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria wabaki ndani ya maeneo yao ya Kikatiba na wajiepushe kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na Mamlaka ya Kikatiba ya Mahakama", alisema Jaji Profesa Juma.

Kwa upande mwingine, Jaji Profesa Juma ametoa rai kwa wananchi na wadau wote wa sheria kutembelea Mnazi Mmoja kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za Kisheria kutoka kwa Majaji, Mahakimu, Wasajili, Watendaji, Mawakili wa serikali na Mawakili wanaojitegemea ambao watakuwa tayari kuwasikiliza na kuwahudumia ipasavyo.

Tanzia:Nguli wa muziki wa Jazz Afrika Kusini Hugh Masekela afariki dunia


Mwanamuziki maarufu nchini Afrika Kusini, Hugh Masekela anayefahamika kama baba wa muziki wa Jazz amefariki dunia baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya saratani ya tezi dume.

Hugh Masekela amefariki dunia baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya saratani ya tezi dume.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Afrika Kusini.  Masekela amabaye hadi kifo chake kinamkuta alikuwa na umri wa miaka 78.

Katika kipindi chake cha zaidi ya miongo mitano kwenye fani hiyo ya muziki alijijengea umaarufu kimataifa kutokana na utunzi wa nyimbo zake za muziki  wa Jazz ukiwemo wimbo  uliotumika katika harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo.

Hugh Masekela alitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini ikiwa ni mara ya kwanza fainali hizo kufanyika barani Afrika.

Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi siku ya Sheria nchini



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria itakayofanyika Februari Mosi mwaka huu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kuhusu maonyesho ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yenye maudhui ya ‘Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili’.

“Kila mwaka Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria ambayo huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama, kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi na Rais Magufuli katika viwanja vya Mahakama vilivyopo jijini Dar es Salaam,” amesema Jaji Mkuu Juma.

Jaji Mkuu amesema kuwa kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau muhimu katika Sekta ya Sheria watatumia siku tano kuanzia tarehe 27 hadi 31 Januari mwaka huu kwa ajili ya kufanya maonyesho yatakayotoa elimu kwa wananchi watakaopata nafasi ya kuhudhuria katika viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyopo jijini humo.

Maonyesho hayo yatatanguliwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria yatakayofanyika Januari, 28 mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yatakayoanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Rais Mstaafu Kikwete atazindua rasmi Wiki ya Sheria.

Aliongeza kuwa Wiki ya Sheria inatoa nafasi nzuri kwa wananchi kuzifahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wa sekta ya sheria ili kufanikisha maboresho endelevu ya Mahakama.

Wadau wengine watakaoshiriki katika wiki ya sharia pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Mafunzo ya Uanansheria kwa Vitendo Tanzania, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Watumishi wa serikali wapewa masaa 72

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe limetoa masaa 72 kwa watendaji 37 kutoka katika kata 15 wawe wamewasilisha kiasi cha milioni 73 walichokusanya kama mapato vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Watendaji hao wanadaiwa kukusanya fedha hizo katika kipindi cha robo mwaka kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na kubaki nazo majumbani mwao bila kuwasilisha kwa mweka hazina wa halmashauri.



Akisoma azimio la kikao cha Baraza hilo ambalo limekutana mjini Vwawa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erick Ambakisye alisema uamuzi huo unafuatia kitendo cha watendaji hao kutowasilisha fedha za makusanyo katika kipindi kilichowekwa kisheria na kusababisha halmashauri kukosa mapato hayo ya Sh. 73,777,736.29 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Mwenyekiti huyo alisema sambamba na hilo baraza limechukua hatua ya kuwaonya kwa barua kwa mara ya pili watendaji wa kata 15 za Wasa, Magamba, Ipunga, Nyimbili, Myovizi, Itaka, Mlangali, Halungu, Isansa, Kilimampimbi, Nambinzo, Bara, Ruanda, Iyula na Shiwinga huku wengine 16 wakiwa wakishindwa kutumia mashine za kielektroniki katika kukusanya mapato ya halmashauri na kutakiwa kujieleza na kuwasilisha fedha walizokusanya ifikapo tarehe hiyo saa 4.00 asubuhi.

Aidha mwenyekiti huyo alisema ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato halmashauri yake iliweka mkataba na watendaji hao wenye lengo kukusanya asilimia 50 ya lengo la makusanyo katika kipindi cha kila robo na kutoa zawadi ya Sh. 500000 kwa kata ya kwanza itakayokusanya vizuri, Sh. 300000 (kata ya pili) na Sh.200000 (kwa kata ya tatu) na kutoa ngao ya kufanya vibaya kwa kata tatu zilizofanya vibaya.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo akizungumza wakati akitoa salamu za serikali alisema wilaya ina fursa ya vyanzo vingi vya mapato lakini watendaji wamekuwa hawakusanyi ipasavyo kutokana na kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa upande mwingine Mbozi alisema hatua kali lazima zichukuliwe kwa watendaji wanaoshindwa kukusanya mapato na kwamba ofisi yake itasimama imara kusaidia katika kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato inayostahili.

Atiwa mbaroni kwa kuiba jeneza


Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Boniface mkazi wa Mwananyamala kwa Msisiri anashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kuiba masanduku ya kuzikia (majeneza) mawili na kuyaficha nyuma ya choo cha mkazi mwengine wa mtaa huo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni Jumanne Muliro, amesema tukio hilo limetokea kati ya ofisi mbili za kuuza masanduku hayo ambapo moja ndiyo iliyoibiwa majeneza hayo, ambayo moja ni la mtu mzima na moja likiwa la mtoto mdogo

“Kuna work shop mbili ambazo zinajishusisha na kutengeneza masanduku, zipo kwenye sehemu moja, asubuhi mtu kaingia kwenye work shop yake akakuta masanduku mawili hayapo akaanza kufuatilia, baada ya muda akajua yapo kwenye workshop nyingine, kwa hiyo kilichofanyika ni ufuatiliaji na askari wakafanikiwa kuyapata, ni suala ambalo linachunguzwa kujua kama wanadaiana au ni wizi umefanyika, ndipo sheria ifuate”, amesema Kamanda Muliro.

Mmiliki wa masanduku hayo Bi. Judith Carlos amesema masanduku hayo aligundua yapo kwa jirani yake baada ya kumuahidi mtu atampa elfu 50 iwapo atamsaidia kujua nani kayachukua, na ndipo baadaye akaambiwa mahali yalipo.

ANC yaendelea kumjadili Jacob Zuma


 Chama tawala cha African National Congress kimethibitisha kwamba mazungumzo yanaendelea kuona namna Rais Jacob Zuma atakavyoondoka ofisini bila shaka ikiashiria mwanzo wa mwisho wa kashfa zilizodumu miaka tisa ya utawala wake.

Zuma amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu tangu alipoachia uaongozi wa ANC kwa makamu wake Cyril Ramaphosa.

 Kashfa

Halmashauri kuu “ilijadili suala hili...kutakuwa na majadiliano kati ya maofisa, Rais Zuma na kwa chama Ramaphosa," alisema Katibu Mkuu Ace Magashule.

"Hakuna muda uliowekwa...Hatufanyi kazi kwa mtindo huo, tunashikiana, tunajadili,” aliongeza Magashule kwamba hakuna uamuzi wa mwisho uliowekwa kuhusu kuondoka kwa Zuma.

Urais wa Zuma ulikumbwa na kashfa za rushwa na ulichafuliwa na kudorora kwa uchumi hali iliyochangia chama kukosa kuungwa mkono kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2019.

Wafuasi wa Ramaphosa wanafanya kampeni atawazwe sasa kama rais na ajaribu kufufua uchumi kabla ya uchaguzi mkuu ambao ANC inaweza kupoteza udhibiti wake kwa mara ya kwanza tangu ulipokomeshwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Audio | Nutty Neithan X Wyre X J’bryte X Ketchup X Gabiro – AYAWA Remix | Mp3 Download

Audio | Nutty Neithan X Wyre X J’bryte X Ketchup X Gabiro – AYAWA Remix | Mp3 Download

Audio | Nutty Neithan X Wyre X J’bryte X Ketchup X Gabiro – AYAWA Remix | Mp3 Download

DOWNLOAD Mp3

Mtoto amuua Mama yake kwa kumkata mapanga


KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA, MPONJOLI LOTSON.

MJANE mkazi wa kijiji cha Kamhanga, wilaya na mkoa wa Geita amefariki dunia baada ya kukatwakatwa na panga kichwani na mwanaye usiku na kisha mtoto huyo kutoroka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, jana na kumtaja marehemu kuwa ni Kabula Karume (73).

Mtuhumiwa anayedaiwa kutoroka baada ya kutekeleza  ukatili huo ni Dotto Lukenze na chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana na upelelezi unaendelea.

Kamanda Mponjoli alisema kuwa taarifa za awali za kikachero zinaonyesha mtuhumiwa ana rekodi ya kuwahi kutuhumiwa kwa mauaji katika matukio mengine na uhalifu mbalimbali.

Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa kabla ya mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye ni mtoto wa marehemu alikuwa akimshinikiza mama yake kuuza mali zikiwamo ng'ombe na mashamba, hatua ilikuwa ikipingwa na marehemu.

Mponjoli alisema siku ya mauaji Januari 16, mwaka huu saa tatu usiku marehemu alikuwa akiota moto na watoto wake wengine na ghafla ndipo mtuhumiwa alipotokea na kuanza kumshambulia.

Alisema katika kutekeleza mauaji hayo mtuhumiwa alitumia kitu chenye ncha kali kumkatakata kichwani marehemu huku waliokuwapo wakijaribu kupiga kelele za kuomba msaada bila mafanikio.

Watu hao ndiyo walimtambua mtuhumiwa kabla hajakimbia, alisema Mponjoli.

Chanjo saratani kutolewa bure


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuanzia Aprili, mwaka huu, itaanza kutoa bure chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi (human papillon virus) kwa wasichana wa kuanzia umri wa miaka 14.

Hatua hiyo inatokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kuonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na  wagonjwa wapya wa saratani ya mlango wa kizazi 51 kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Naibu Waziri wa wizara hiyo Dk. Faustine Ndugulile, alisema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni ya uchunguzi wa mabadiliko ya awali ya saratani hiyo na ya matiti, uliofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.

 Alisema hatua hiyo ya chanjo inalenga kukinga kirusi kinachoeneza saratani ya mlango wa kizazi ambayo Tanzania inaongoza kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Aidha, alisema katika awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo hiyo mwaka huu wamepanga kuwafikia wasichana wa kuanzia miaka 14 wapatao 616,734. "Hawa 616,734 ndio tumepanga kuwapatia chanjo mwaka huu na katika mwaka ujao tutawafikia wasichana wa kuanzia miaka tisa hadi 14 na mwaka utakaofuata tutawapa chanjo wale wenye umri wa kuanzia miaka tisa," alisema Dk. Ndugulile. Alisema chanjo hiyo itasaidia kuwalinda wasichana ambao wako katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha saratani ya matiti na mlango wa kizazi. "Saratani ya mlango wa kizazi moja ya sababu ambazo zinachangia ni wasichana kushiriki ngono katika umri mdogo, kuwa na wenza wengi lakini pia kubeba mimba nyingi kunaweza kusababisha mtu kupata maambukizi," alisema.

Hata hivyo, aliwataka kinamama kupima afya zao mara kwa mara na wanapobainika kuwa na maambukizi, wanatakiwa kuwaona wataalamu ili kupatiwa matibabu. "Saratani hii inatibika kabisa kama mtu atapata vipimo vya afya yake kila mara, lakini watu wengi wamekuwa wakija katika hospitali wakiwa wamechelewa sana hali ambayo saratani inakuwa imesambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile mifupa, ini na damu na kuwa vigumu kutibika,"alisema  Dk. Ndugulile aliwaagiza wakuu wa mikoa wote kuhakikisha kuwa wasimamia upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa yao ili kufikia malengo ya serikali iliyojipangia hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imefikia kimama milioni tatu.

Aliongeza pamoja na juhudi hizo pia serikali kwa sasa inaboresha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ambayo ni taasisi pekee nchini katika kukabiliana na tatizo la saratani, kwa kuweka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kutoa huduma za matibabu ambazo zilikuwa zinatolewa nje ya nchi.

 "Katika mwaka 2016 Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ilipokea wanawake 1,934 wa saratani ya mlango wa kizazi. Takwimu hizi zimekuwa zikongezeka si tu kwamba kujua ukubwa wa tatizo na hii itatusaidia kuona jinsi gani jamii imeamka na kuhamasika kufahamu athari za saratani na kuanza kuchukua hatua," alisema.

Wawili wafariki dunia, wanane wajeruhiwa ajali ya Mabas


WATU wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa vibaya katika ajali ya mabasi mawili yakugongana uso kwa uso katika kijiji cha Kamanga, Sengerema mkoani Mwanza saa nne asubuhi jana.

Akizungumzia ajali hiyo, shuhuda aliyekuwa katika pikipiki na kunusurika kugongwa na mabasi hayo, Philipo Budeba, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi yote mawili.

“Mimi nilikuwa naendesha pikipiki, mbele yangu kulikuwa na basi la Mkombozi Trans lenye namba T540 DLF na nyuma kulikuwa na Basi la Walawi Express  lenye namba T167 CSN yote yalikuwa na mwendokasi," alisema Budeba.

"Dereva wa Mkombozi ndiye aliyetaka kupita gari lingine, lakini ilishindikana na kusababisha magari hayo kuvaana... mimi nilijirusha kwenye kilima cha pembeni mwa barabara."

Naye abiria wa Mkombozi Trans iliyokuwa ikitokea Kanyara Buchosa, Sengerema, Fransisco Kansola alisema tabia ya madereva kushindwa kuchukua tahadhari na kujali kuwahi abiria ndiyo chanzo cha ajali hiyo.

Walawi Express lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Nemba wilayani Biharamulo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema dereva wa basi la Walawi, Frank Kimboka ni miongoni mwa majeruhi wanane wa ajali hiyo baada ya kujeruhiwa miguu yote.

“Waliofariki ni dereva wa basi la Mkombozi Trans aliyefahamika kwa jina la Simon Mdalesalamu na mwanamke aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 20," alisema Kamanda Msangi.

Majeruhi watatu wametajwa kuwa ni Frank Mushi aliyevunjika miguu yote miwili, Isaack Hamisi (22) mkazi wa Nyasaka wilayani Ilemela na Mwinyi Ismail (50) aliyevunjika miguu yote miwili, alisema Kamanda Msangi.

"Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi hayo.”

Aidha, ajali hiyo ilitokea wakati mkoa wa Mwanza ukizindua maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, yenye kaulimbiu inayosema ‘Zuia ajali, tii sheria, okoa maisha'.

Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu.