Sunday, 21 January 2018

Waziri Mwakyembe amchangia Wastara

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe jana Januari 20, 2018 amemtembelea na kumjulia hali msanii wa filamu Wastara nyumbani kwake Tabata Sanene, Dar es Salaam.

Wastara kwa kipindi kirefu sasa amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu na yupo kwenye maandalizi ya safari kwenda India kwa matibabu zaidi.

Waziri Mwakyembe akiambatana na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu na Katibu Mtendaji wa BASATA alimtakia kheri Wastara na kumkabidhi mchango wa Shs. 1,000,000/= (milioni moja).

Aidha, Mwakyembe aliwasihi wasanii na Watanzania kwa ujumla kumchangia Wastara kwa hali na mali ili aweze kupata fedha za kumwezesha kwenda India kwa matibabu zaidi.

Yanga yamkingia kifua beki wake

Klabu ya soka ya Yanga imetoa sababu kwanini mlinzi wake mpya wa kimataifa Fiston 'Festo' Kayembe Kanku ameshindwa kujiunga na timu tangu asajiliwe Disemba 2017.

Akiongea leo Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika amesema mchezaji huyo raia wa DR Congo hajajiunga na timu kwasababu anashughulikia matatizo ya kifamilia.

“Kanku ana matatizo makubwa ya kifamilia ndiyo maana tumempa ruhusa ya kwenda kuyashughulikia, akimaliza atakuja kuanza kazi, na atacheza tu ligi bado ina mechi nyingi sana,”amesema Nyika.

Kwa upande mwingine Nyika ameongelea suala la uhamisho wa kimataifa (ITC), amabapo ameeleza kuwa ulikuwa unasumbua ila kwasasa wapo kwenye hatua za mwisho kuupata japo kuwa tayari mchezaji huyo ni mali ya Yanga.

Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara wanashika nafasi ya 5 kwenye msimamo wakiwa na alama 22 kwenye mechi 13 walizocheza huku kesho wakishuka dimbani kucheza na Ruvu Shooting.

Johari afunguka siri ya kifo cha Mama yake

MREMBO wa filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’ ameanika siri ya kifo cha mama yake kwa kueleza namna ambavyo alipigana kutetea kifo cha mama yake mzazi.

Johari alipata pigo hilo usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya Hindu Mandali, jijini Dar es Salaam baada ya mama yake kulazwa kwa ugonjwa wa kisukari kwa saa chache tangu afikishwe hospitalini hapo.

Kabla ya kupatwa na umauti huo, Johari alikuwa akiishi na mama yake mzazi, maeneo ya Gereji, Mabibo jijini Dar ambapo kwa zaidi ya miaka mitatu, msanii huyo alihangaika kutetea uhai wa mama yake, kwa nyakati tofauti.

Katika kipindi chote hicho, Johari alikuwa mzito sana kuelezea mateso aliyokuwa anayapitia mama yake, zaidi alikuwa akiwaelezea watu wake wa karibu sana. Akizungumza na Risasi Jumamosi, akiwa kwenye nyumba ya familia, Mburahati jijini Dar, Johari alisema kifo cha mama yake kimekuwa pigo kubwa kwake na kueleza namna alivyopambana kumpigania.

“Nimehangaika jamani. Nilikuwa silali, mchana na usiku nilikuwa nikipambana kuhakikisha naokoa maisha ya mama yangu. “Unajua alikuwa kuna wakati anakuwa na hali nzuri, kuna wakati ndio hivyo kikipanda, hali inakuwa mbaya sana. Kwa miaka zaidi ya mitatu nimekuwa nikipambana na afya ya mama yangu,” alisema Johari huku akilengwalengwa machozi.

Akizungumza kuhusu ratiba ya mazishi Jumatano iliyopita, muigizaji Salum Mchoma ‘Chiki’, ambaye alichaguliwa kuwa msemaji wa familia, alisema siku ya Alhamisi (juzi), mwili wa mama yake Johari ungefikishwa nyumbani hapo kisha ungepelekwa Msikitini wa Mbukusi, Mburahati baadaye kuzikwa katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar. Msiba huo ulihudhuriwa na waigizaji wengi akiwemo, Vincent Kigosi ‘Ray’, Ndambangwe Misayo ‘Thea’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Nuru Nassor ‘Nora’ na wengine wengi.


Waziri Mpina awasilisha majina ya Viongozi waliokaidi agizo la Serikali

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewasilisha majina ya viongozi wa halmashauri ambazo hazijaanza kutekeleza upigaji chapa mifugo na zile ambazo ziko chini ya asilimia 10 ya utekelezaji,

Kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ili zichukuliwe hatua.

Mpina alibainisha hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa upigaji chapa mifugo nchini, mjini Dodoma.

Alisema kwa tathmini iliyofanyika hadi sasa jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa na asilimia 59.3 wamepigwa chapa huku asilimia 40.7 wakiwa hawajapigwa chapa na zoezi hilo linatarajiwa kukamilishwa Januari 31, mwaka huu.

“Halmashauri 100 zimepiga chapa zaidi ya asilimia 50, halmashauri 54 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi 50, halmashauri 14 zimepiga chini ya asilimia 10 na Halmashauri 9 hazijaanza kupiga chapa,” alisema Mpina.

Alizitaja halmashauri ambazo hazijaanza kabisa ni Tandahimba, Nanyumbu, Mafia, Newala, miji ya Newala, Nanyamba na Masasi na manispaa za Kigamboni na Ilemela.

Kwa upande wa punda, Mpina alisema jumla ya punda ni 572,353 na watapigwa chapa.

Alibainisha kuwa sababu za kutokamilika kwa zoezi ni uwapo wa changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wafugaji kukataliwa kupigiwa chapa mifugo yao kwa kisingizio kuwa ni wavamizi au wahamiaji haramu.

“Mfano katika wilaya za Kibiti, morogoro, Rufiji, Sumbawanga, Tanganyika na Kibondo wamekumbana na changamoto hii,”alisema Mpina

Aidha alitaja changamoto nyingine kuwa ni wafugaji kuhamisha ng’ombe katika kipindi hichi cha kilimo na hivyo kutoshiriki, baadhi ya ng’ombe kuendelea kuwa katika maeneo ya hifadhi na Mapori Tengefu mfano kwa mkoa wa Kigoma na Ruvuma.

“Pia baadhi ya wafugaji kuendelea kugoma kupiga chapa mifugo yao kutokana na imani potofu na wengine kuficha idadi ya mifugo kwa mfano mkoa wa Manyara,”alisema

Mpina alisema kuwakatalia wafugaji kupiga chapa kwa kisingizio cha uhamiaji haramu haikubaliki kwa kuwa wilaya zote zilipewa jukumu la kuhakiki mifugo yao na kuwasilisha taarifa Wizarani.

“Hakuna halmashauri hata moja iliyoleta taarifa za wahamiaji haramu, pia zoezi lisihusishwe na migogoro ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi, mifugo yote ipigwe chapa isipokuwa ile ya kutoka nchi jirani,”alisema

Kadhalika, Mpina alisema wafugaji watakaoshindwa kufanya hivyo ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji namba 12 ya mwaka 2010 ibara ya 4 kifungu cha 26.

Rais wa Z'bar atembelea eneo ambalo kutahifadhiwa Mafuta

RAIS wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia pamoja na ujenzi wa bandari itakayotumika kusafirishia na kuingiza maliasili hizo.

Akiwa katika eneo hilo lililoko Mangapwani na Bumbwini lenye ukubwa wa hekta 399.25 juzi, Dk. Shein alipata maelezo kuhusu hatua zinazoendelea katika mradi huo.

Katibu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Ali Halil Mirza, alisema hatua inayoendelea hivi sasa ni upembuzi yakinifu unaotekelezwa na Benki ya Dunia ambao utakamilika miezi sita ijayo.

Mirza alisema kukamilika kwa upembuzi huo yakinifu ndiko kutaleta mapendekezo ya kulisanifu eneo hilo kwa ajili ya bandari na majengo mengine ya utawala na shughuli nyingine zinazoenda sambamba na mradi huo.

Alisema miongoni mwa sababu ya kutengwa eneo hilo kwa shughuli hizo ni kutokana na kuwa na kina kirefu cha maji ya bahari ambacho kitarahisisha kujengwa kwa bandari hiyo muhimu ambayo itatumika kwa ajili ya kusafirishia gesi asilia na mafuta ndani na nje ya nchi.

Alisema miongoni mwa faida kubwa za mradi huo baada ya kukamilika kwake ni pamoja na kuondoa kabisa uhaba wa mafuta nchini na kuipatia Serikali pato kubwa.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, akiwa na ujumbe wake alipata fursa ya  kulikagua eneo la Kampuni ya Salama International linalojengwa maalum kwa ajili ya kusafisha mafuta na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Abdallah Said Abdallah.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa eneo hilo ambalo ni kwa ajili ya kusafisha mafuta limefikia asilimia 65 za ujenzi.Mkurugenzi huyo alieleza kuwa matenki ya uwezo wa kuhifadhi lita milioni 24 kwa wakati mmoja yanajengwa kwa ajili ya kuhifadhia diseli, petroli, mafuta ya taa pamoja na mafuta ya kulainisha mitambo.

Alieleza kuwa kuanzia mwezi ujao wataendelea na shughuli za ujenzi zilizobaki, shughuli ambazo zilianza mwaka 2015.

Alisema hadi walipofikia wameshatumia dola za Marekani milioni tano (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 10) ikiwa ni awamu ya kwanza.

Alisema watakuwa wakisafisha tani 600 ambazo zitatumika Zanzibar kwa asilimia 70 na kiasi kilichobaki kitauzwa nje ya nchi.

Akiwa katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya uhifadhi wa mazingira katika mchakato wa usafishaji wa mafuta mara mradi huo utakapokamilika.

MAGAZETI YA LEO 21/1/2018

 

































Elimu juu ya Tetenasi (Tetanus)


Tetenasi  ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria wanaoitwa ( Clostridium tetani). Wadudu hawa wanapatikana katika mazingira yanayotuzunguka mfano; ardhi, misumari au vitu vyenye ncha, vinyesi vya baadhi ya wanyama nk.

Bacteria wa tetenasi wanaweza kuishi katika mazingira kwa miaka mingi. Pia wanapenda vidonda, ndio maana wanaingia mwilini kupitia vidonda au mikwaruzo. Dalili za Tetenasi zinatokea siku 4-14 baada ya kupata jeraha.

Tetenasi imegawanyika sehemu mbili.

Tetenasi inayotokea kwa watu wazima (adult)
Tetenasi ya watoto (neonates) 

Nani yupo hatarini kupata tetenasi? Kwa watu wazima (Adults)
Ikiwa umeumia na kupata jeraha  au kidonda sehemu ya mwili wako uko katika hatari ya kupata ugonjwa huu hatari wa tetenasi. 
Ikiwa umetobolewa na msumari una zaidi ya 32% kupata tetenasi.
Ikiwa umeungua, au watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, au watu wanaojiwekea tattoo, watu wenye magonjwa ya meno, wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu
Kisukari ni moja ya hali inayoweza kukusababishia tetenasi. 
Pia upasuaji (surgery) isiyo salama, mfano matumizi ya vyombo visivyo salama(unsterilized)

Kwa watoto.   

Kama mama mjamzito hatapata chanjo ya tetenasi , au kujifungulia nyumbani, yupo kwenye hatari ya kumsababishia mtoto mchanga kupata tetenasi.

Dalili za Tetenasi.

Kukakamaa kwa misuli, mdomo kushindwa kufunguka(lock-jaw) 
Kutokwa na jasho jingi, homa kali
Kushindwa kumeza kwasababu ya kukakamaa kwa misuli. 
Kutokwa na udenda(drooling). 
Kupata matatizo ya kupumua.

Kinga. 

Tafadhali nenda hospitalini au kituo cha afya mara baada ya kupata jeraha lolote ili kupata chanjo ya tetenasi.       
Kwa wafanyakazi wa afya, ni muhimu kupata chanjo ya tetenasi kwasababu ya mazingira hatarishi  ya kazi.       
Kwa mama mjamzito tafadhali hakikisha unapata chanjo zote za tetenasi  ili kujikinga na pia kumkinga mtoto. Pia unapoona dalili za uchungu hakikisha unawahi ukajifungulie kituo cha afya mapema.       
Epuka majeraha yasiyokua ya lazima, vaa viatu, weka vitu vyenye ncha kali mbali na watoto.       
Mpeleke mtoto atahiriwe hospitalini na sio kwa mtaani, kwasababu ya hatari kubwa iliyopo ya kupata tetenasi.

Kilimo Cha Maharage Ya Njano



Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.

Ekari moja ya maharage ya njano kwa maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo unalolimia.

Shamba la maharage kama unalima kwa kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi minne.

 Upandaji wa Maharage

1.Mbegu.
Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.

Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.

Kuna aina nyingi za maharage ambazo zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder) ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa wakulima ambazo huhimili

baadhi ya magonjwa na wadudu.
Inashauriwa kupanda maharage katika umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.

Kama mbegu moja moja katika kila shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo idadi yake ni nusu ya  maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 = ekari 2.471.

2. Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage huhitaji madini ya ‘phosphorous’ na ‘potassium’ ambayo hupatikana kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo na mabaki ya mimea.

Ni muhimu kufahamu udongo ambao unatarajia kupanda mimea yako ili  kutathmini viwango vya madini yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.

Zaidi ya yote ni vizuri kutumia mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye udongo.

3.Magugu.
Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea.

Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza kushambulia
mimea.

4.Wadudu na magonjwa.
Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea  ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika).

Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka.  Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza  kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu.

Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu.

5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda. Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa.

Kwa mfano asilimia 80 ya maharage yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.

Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.

Baada ya kukauka hadi kufikia angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena.

6. Kilimo mchanganyiko.
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.

Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi weupe.

BIZARI: Kiungo Cha Mboga Chenye Faida Nyingi


Inawezekana katika maisha yako hujawahi kula mboga iliyowekwa kiungo kinachoitwa bizari, kama umewahi, inawezekana pia hujawahi kujua faida zake mwilini.

Bizari (Turmeric) ni kiungo cha mboga jamii ya mimea unaochimbwa kama mizizi, mfano wa tangawizi, lakini tangawizi yenyewe ina rangi ya njano na hujulikana pia kama ‘manjano’ kutokana na rangi yake.

Kiungo hiki kinatumiwa sana katika Bara la Asia na hasa India na China. Kutokana na umuhimu wake kiafya, vyakula vingi hupikwa kwa kuchanganya na kiungo hiki ambacho sasa kimeenea dunia nzima, ikiwemo Tanzania.

FAIDA ZA BIZARI KIAFYA
Bizari hutumika na watu wengi kama kiungo cha mboga cha kuongeza ladha katika mchuzi na pengine kuweka rangi, lakini kuna faida nyingi unazozipata unapotumia kiungo hiki kila mara katika mapishi yako.

Inaelezwa kuwa bizari ina virutubisho vyenye uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili, mara 8 zaidi ya Vitamin C na Vitamin E, ina uwezo wa kushusha kiwango cha lehemu (cholesterol) na kuzuia mtu kuzeeka kabla ya wakati.
Aidha, bizari huimarisha sehemu za magoti hivyo kukuepusha na matatizo ya miguu kuuma. Bizari pia hun’garisha ngozi na kuifanya kuwa yenye afya na huimarisha pia mfumo wa usagaji chakula (Digestion).

SUALA LA UBORA NI MUHIMU
Katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolijia tulionao sasa, bizari hutengenezwa viwandani na kuhifadhiwa kwa usafirishaji sehemu mbalimbali duniani na kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu. Katika hali kama hiyo, si ajabu kukuta bizari iliyoongezewa kemikali zingine za kuhifahdia chakula.

Bizari ya aina hiyo, tayari inakosa faida zilizoelezwa hapo juu, hivyo ni suala muhimu kuangalia ubora wa bizari unayoitumia na mahali inapotoka. Katika nchi yetu, Mungu ametujaalia ardhi yenye rutuba ambapo kiungo kama hiki kinalimwa na kupatikana kwa wingi na kwa uhalisia wake.

Katika suala la kujali ubora, pendelea zaidi kununua bizari kutoka sokoni ambayo imetengenezwa katika mazingira safi na salama na bila kuchanganywa na kitu kingine. Iwapo pia utanunua bizari iliyokwisha hifadhiwa, ni vyema ukasoma maelezo yake kuona kama haina vikorombwezo (additives) vingine.

 Ni ukweli ulio wazi kuwa ukitumia bizari iliyobora utapa faida nyingi kiafya, hivyo hakikisha katika upikaji wako wa kitoweo cha nyama, kama vile kuku, samaki, ngo’mbe unaweka bizari. Upikaji mzuri ni ule wa kuweka kiungo hicho mwisho baada ya mboga yako kuchemka na kuiva, kwani haitakiwi bizari kuchemka sana.
Kwa ujumla hizi ndizo faida utakazozipata ukiifanya bizari kuwa sehemu ya viungo katika mlo wako wa kila siku:


UTAIMARISHA KINGA YA MWILI WAKO
UTAIMARISHA AFYA YA MACHO
UTAIMARISHA SEHEMU ZA VIUNGIO VYA MWILI WAKO
UTAIMARISHA UTENDAJI KAZI WA INI
UTAIMARISHA CHEMBE HAI ZA MWILI
UTAIMARISHA MFUMO WA USAGAJI CHAKULA
UTAIMARISHA MFUMO WA DAMU MWILINI
UTASHUSHA KIWANGO CHA KOLESTRO MWILINI
UTAIMARISHA MFUMO WA UZALISHAJI MBEGU ZA UZAZI
UTAIMARISHA KIWANGO CHA SUKARI MWILINI.

Saturday, 20 January 2018

VIDEO: Mtulia Uso Kwa Uso Na Meneja

Aliyekuwa meneja wa kampeni wa Maulid Mtulia kwenye uchaguzi wa 2015 Kinondoni,  Rajabu Salim Jumaa amerejesha fomu ya kuombea kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwania nafasi hiyo.

Jumaa ambaye amerejesha fomu hizo leo Januari 20, 2018 katika ofisi ya uchaguzi  wa jimbo la Kinondoni iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, amesema hatua ya Chadema kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo ni kudhoofisha upinzani.

Mwaka 2015 mgombea wa CUF Mtulia alishinda ubunge wa jimbo hilo lakini alijivua uanachama wa CUF na kuhamia CCM na hivyo kupoteza sifa ya ubunge. Hata hivyo Mtulia amepitishwa na chama hicho tawala kugombea ubunge katika jimbo hilo, leo anatarajia kurejesha fomu za NEC.

Jumaa ambaye yupo CUF upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, amesema hatua ya Chadema kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo ni kudhoofisha upinzani.

"Chadema wanakuja kupoteza nguvu na kuja kugawa kura za wapinzani. CUF ililipata jimbo la Kinondoni kukiwa na ushirikiano wa Ukawa na siyo mtu mmoja.

Chama kilichoshirikiana katika mchakato huo bado kipo na kimemsimamisha mgombea iweje leo Chadema wamesimamisha mgombea," amehoji.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI......... USISAHAU KUSUBSCRIBE

Mawaziri Wakutana Dar Kuanza Kutekeleza Ujenzi wa Reli

Mawaziri wa Miundombinu na Uchukuzi kutoka Tanzania na Rwanda wamekutana leo jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maelekezo ya Marais wa nchi hizo mbili yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu na makubaliano ya Ujenzi wa Reli ya kisasa ya yenye urefu wa kilomita 572 itakayoanzia Isaka mpaka Kigali Rwanda.Katika mazungumzo yao, mawaziri hao wameridhia kwa pamoja rasimu ya kujenga reli ya kisasa kwa lengo la kuendeleza uhusiano wa nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji, kuunganisha miundombinu, kukuza za uchumi na kutoa huduma bora kwa wakazi ws ukanda huu.

Kata hatua nyingine, Mawaziri Dk Augustine Mahiga na Waziri wa Fedha Philip Mpango ambao ni miongoni wa Viongozi waliohudhuria mazungumzo hayo wamesema ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa baina ya Tanznaia na Rwanda itakuwa ni kiungo muhimu cha kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizo.

Nitashinda Ubunge Asubuhi Mapema - Mgombea CHADEMA

Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Elvis Mosi, amesema atashinda ubunge wa jimbo hilo mapema asubuhi kutokana na mgombea aliyepitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Godwin Mollel, kutokuwa na nguvu ya kushinda kwani amekosa sifa za kuwa kiongozi kwa madai kuwa ni mtu mwenye tamaa na asiyekuwa na msimamo.

Mgombea huyo amesema chama chake kimemuamini na kumpitisha baada ya kumpima na kuona anao uwezo wa kukabiliana na Dk. Mollel na kwamba ushindi wake utapatikana asubuhi.

“Mgombea wa CCM hawezi kamwe kushindana na mimi yaani ni ardhi na mbingu na sifa ya kumshinda tunayo, kwanza ni mtu aliye na tamaa na asiyekuwa na msimamo wananchi hawawezi kumchagua mtu wa namna hiyo kwani walimuamini lakini amewasaliti,” amesema.

Naibu Waziri Aagiza Kutoa Vikwazo Vyuo Vya Ufundi

Naibu waziri wa elimu sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameviagiza vyuo vya ufundi kote nchini kuondoa vikwazo na kutoa upendeleo maalum kwa wanafunzi wa kike wenye sifa wanaojiunga na elimu ya ufundi kwakuwa  idadi kubwa wanafunzi wa kike wanaichukia elimu ya ufundi kutokana na vikwazo vilivyopo kwenye vyuo hivyo dhidi yao.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza na wahitimu wa fani mbalimbali za ufundi kwenye chuo cha ufundi Arusha ATC.

Kaimu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dkt. Masud Senzia amesema chuo hicho kimetekeleza kwa vitendo adhima ya serikali ya viwanda kwani kimeanza kufanya majaribio ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.

Mkurugenzi wa elimu ya ufundi Thomas Katebalirwe akaelza mikakati ya serikali katika kuboresha elimu ya ufundi.