Sunday, 21 January 2018

Elimu juu ya Tetenasi (Tetanus)


Tetenasi  ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria wanaoitwa ( Clostridium tetani). Wadudu hawa wanapatikana katika mazingira yanayotuzunguka mfano; ardhi, misumari au vitu vyenye ncha, vinyesi vya baadhi ya wanyama nk.

Bacteria wa tetenasi wanaweza kuishi katika mazingira kwa miaka mingi. Pia wanapenda vidonda, ndio maana wanaingia mwilini kupitia vidonda au mikwaruzo. Dalili za Tetenasi zinatokea siku 4-14 baada ya kupata jeraha.

Tetenasi imegawanyika sehemu mbili.

Tetenasi inayotokea kwa watu wazima (adult)
Tetenasi ya watoto (neonates) 

Nani yupo hatarini kupata tetenasi? Kwa watu wazima (Adults)
Ikiwa umeumia na kupata jeraha  au kidonda sehemu ya mwili wako uko katika hatari ya kupata ugonjwa huu hatari wa tetenasi. 
Ikiwa umetobolewa na msumari una zaidi ya 32% kupata tetenasi.
Ikiwa umeungua, au watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, au watu wanaojiwekea tattoo, watu wenye magonjwa ya meno, wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu
Kisukari ni moja ya hali inayoweza kukusababishia tetenasi. 
Pia upasuaji (surgery) isiyo salama, mfano matumizi ya vyombo visivyo salama(unsterilized)

Kwa watoto.   

Kama mama mjamzito hatapata chanjo ya tetenasi , au kujifungulia nyumbani, yupo kwenye hatari ya kumsababishia mtoto mchanga kupata tetenasi.

Dalili za Tetenasi.

Kukakamaa kwa misuli, mdomo kushindwa kufunguka(lock-jaw) 
Kutokwa na jasho jingi, homa kali
Kushindwa kumeza kwasababu ya kukakamaa kwa misuli. 
Kutokwa na udenda(drooling). 
Kupata matatizo ya kupumua.

Kinga. 

Tafadhali nenda hospitalini au kituo cha afya mara baada ya kupata jeraha lolote ili kupata chanjo ya tetenasi.       
Kwa wafanyakazi wa afya, ni muhimu kupata chanjo ya tetenasi kwasababu ya mazingira hatarishi  ya kazi.       
Kwa mama mjamzito tafadhali hakikisha unapata chanjo zote za tetenasi  ili kujikinga na pia kumkinga mtoto. Pia unapoona dalili za uchungu hakikisha unawahi ukajifungulie kituo cha afya mapema.       
Epuka majeraha yasiyokua ya lazima, vaa viatu, weka vitu vyenye ncha kali mbali na watoto.       
Mpeleke mtoto atahiriwe hospitalini na sio kwa mtaani, kwasababu ya hatari kubwa iliyopo ya kupata tetenasi.

Kilimo Cha Maharage Ya Njano



Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.

Ekari moja ya maharage ya njano kwa maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo unalolimia.

Shamba la maharage kama unalima kwa kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi minne.

 Upandaji wa Maharage

1.Mbegu.
Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.

Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.

Kuna aina nyingi za maharage ambazo zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder) ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa wakulima ambazo huhimili

baadhi ya magonjwa na wadudu.
Inashauriwa kupanda maharage katika umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.

Kama mbegu moja moja katika kila shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo idadi yake ni nusu ya  maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 = ekari 2.471.

2. Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage huhitaji madini ya ‘phosphorous’ na ‘potassium’ ambayo hupatikana kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo na mabaki ya mimea.

Ni muhimu kufahamu udongo ambao unatarajia kupanda mimea yako ili  kutathmini viwango vya madini yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.

Zaidi ya yote ni vizuri kutumia mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye udongo.

3.Magugu.
Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea.

Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza kushambulia
mimea.

4.Wadudu na magonjwa.
Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea  ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika).

Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka.  Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza  kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu.

Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu.

5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda. Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa.

Kwa mfano asilimia 80 ya maharage yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.

Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.

Baada ya kukauka hadi kufikia angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena.

6. Kilimo mchanganyiko.
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.

Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi weupe.

BIZARI: Kiungo Cha Mboga Chenye Faida Nyingi


Inawezekana katika maisha yako hujawahi kula mboga iliyowekwa kiungo kinachoitwa bizari, kama umewahi, inawezekana pia hujawahi kujua faida zake mwilini.

Bizari (Turmeric) ni kiungo cha mboga jamii ya mimea unaochimbwa kama mizizi, mfano wa tangawizi, lakini tangawizi yenyewe ina rangi ya njano na hujulikana pia kama ‘manjano’ kutokana na rangi yake.

Kiungo hiki kinatumiwa sana katika Bara la Asia na hasa India na China. Kutokana na umuhimu wake kiafya, vyakula vingi hupikwa kwa kuchanganya na kiungo hiki ambacho sasa kimeenea dunia nzima, ikiwemo Tanzania.

FAIDA ZA BIZARI KIAFYA
Bizari hutumika na watu wengi kama kiungo cha mboga cha kuongeza ladha katika mchuzi na pengine kuweka rangi, lakini kuna faida nyingi unazozipata unapotumia kiungo hiki kila mara katika mapishi yako.

Inaelezwa kuwa bizari ina virutubisho vyenye uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili, mara 8 zaidi ya Vitamin C na Vitamin E, ina uwezo wa kushusha kiwango cha lehemu (cholesterol) na kuzuia mtu kuzeeka kabla ya wakati.
Aidha, bizari huimarisha sehemu za magoti hivyo kukuepusha na matatizo ya miguu kuuma. Bizari pia hun’garisha ngozi na kuifanya kuwa yenye afya na huimarisha pia mfumo wa usagaji chakula (Digestion).

SUALA LA UBORA NI MUHIMU
Katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolijia tulionao sasa, bizari hutengenezwa viwandani na kuhifadhiwa kwa usafirishaji sehemu mbalimbali duniani na kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu. Katika hali kama hiyo, si ajabu kukuta bizari iliyoongezewa kemikali zingine za kuhifahdia chakula.

Bizari ya aina hiyo, tayari inakosa faida zilizoelezwa hapo juu, hivyo ni suala muhimu kuangalia ubora wa bizari unayoitumia na mahali inapotoka. Katika nchi yetu, Mungu ametujaalia ardhi yenye rutuba ambapo kiungo kama hiki kinalimwa na kupatikana kwa wingi na kwa uhalisia wake.

Katika suala la kujali ubora, pendelea zaidi kununua bizari kutoka sokoni ambayo imetengenezwa katika mazingira safi na salama na bila kuchanganywa na kitu kingine. Iwapo pia utanunua bizari iliyokwisha hifadhiwa, ni vyema ukasoma maelezo yake kuona kama haina vikorombwezo (additives) vingine.

 Ni ukweli ulio wazi kuwa ukitumia bizari iliyobora utapa faida nyingi kiafya, hivyo hakikisha katika upikaji wako wa kitoweo cha nyama, kama vile kuku, samaki, ngo’mbe unaweka bizari. Upikaji mzuri ni ule wa kuweka kiungo hicho mwisho baada ya mboga yako kuchemka na kuiva, kwani haitakiwi bizari kuchemka sana.
Kwa ujumla hizi ndizo faida utakazozipata ukiifanya bizari kuwa sehemu ya viungo katika mlo wako wa kila siku:


UTAIMARISHA KINGA YA MWILI WAKO
UTAIMARISHA AFYA YA MACHO
UTAIMARISHA SEHEMU ZA VIUNGIO VYA MWILI WAKO
UTAIMARISHA UTENDAJI KAZI WA INI
UTAIMARISHA CHEMBE HAI ZA MWILI
UTAIMARISHA MFUMO WA USAGAJI CHAKULA
UTAIMARISHA MFUMO WA DAMU MWILINI
UTASHUSHA KIWANGO CHA KOLESTRO MWILINI
UTAIMARISHA MFUMO WA UZALISHAJI MBEGU ZA UZAZI
UTAIMARISHA KIWANGO CHA SUKARI MWILINI.

Saturday, 20 January 2018

VIDEO: Mtulia Uso Kwa Uso Na Meneja

Aliyekuwa meneja wa kampeni wa Maulid Mtulia kwenye uchaguzi wa 2015 Kinondoni,  Rajabu Salim Jumaa amerejesha fomu ya kuombea kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwania nafasi hiyo.

Jumaa ambaye amerejesha fomu hizo leo Januari 20, 2018 katika ofisi ya uchaguzi  wa jimbo la Kinondoni iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, amesema hatua ya Chadema kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo ni kudhoofisha upinzani.

Mwaka 2015 mgombea wa CUF Mtulia alishinda ubunge wa jimbo hilo lakini alijivua uanachama wa CUF na kuhamia CCM na hivyo kupoteza sifa ya ubunge. Hata hivyo Mtulia amepitishwa na chama hicho tawala kugombea ubunge katika jimbo hilo, leo anatarajia kurejesha fomu za NEC.

Jumaa ambaye yupo CUF upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, amesema hatua ya Chadema kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo ni kudhoofisha upinzani.

"Chadema wanakuja kupoteza nguvu na kuja kugawa kura za wapinzani. CUF ililipata jimbo la Kinondoni kukiwa na ushirikiano wa Ukawa na siyo mtu mmoja.

Chama kilichoshirikiana katika mchakato huo bado kipo na kimemsimamisha mgombea iweje leo Chadema wamesimamisha mgombea," amehoji.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI......... USISAHAU KUSUBSCRIBE

Mawaziri Wakutana Dar Kuanza Kutekeleza Ujenzi wa Reli

Mawaziri wa Miundombinu na Uchukuzi kutoka Tanzania na Rwanda wamekutana leo jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maelekezo ya Marais wa nchi hizo mbili yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu na makubaliano ya Ujenzi wa Reli ya kisasa ya yenye urefu wa kilomita 572 itakayoanzia Isaka mpaka Kigali Rwanda.Katika mazungumzo yao, mawaziri hao wameridhia kwa pamoja rasimu ya kujenga reli ya kisasa kwa lengo la kuendeleza uhusiano wa nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji, kuunganisha miundombinu, kukuza za uchumi na kutoa huduma bora kwa wakazi ws ukanda huu.

Kata hatua nyingine, Mawaziri Dk Augustine Mahiga na Waziri wa Fedha Philip Mpango ambao ni miongoni wa Viongozi waliohudhuria mazungumzo hayo wamesema ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa baina ya Tanznaia na Rwanda itakuwa ni kiungo muhimu cha kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizo.

Nitashinda Ubunge Asubuhi Mapema - Mgombea CHADEMA

Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Elvis Mosi, amesema atashinda ubunge wa jimbo hilo mapema asubuhi kutokana na mgombea aliyepitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Godwin Mollel, kutokuwa na nguvu ya kushinda kwani amekosa sifa za kuwa kiongozi kwa madai kuwa ni mtu mwenye tamaa na asiyekuwa na msimamo.

Mgombea huyo amesema chama chake kimemuamini na kumpitisha baada ya kumpima na kuona anao uwezo wa kukabiliana na Dk. Mollel na kwamba ushindi wake utapatikana asubuhi.

“Mgombea wa CCM hawezi kamwe kushindana na mimi yaani ni ardhi na mbingu na sifa ya kumshinda tunayo, kwanza ni mtu aliye na tamaa na asiyekuwa na msimamo wananchi hawawezi kumchagua mtu wa namna hiyo kwani walimuamini lakini amewasaliti,” amesema.

Naibu Waziri Aagiza Kutoa Vikwazo Vyuo Vya Ufundi

Naibu waziri wa elimu sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameviagiza vyuo vya ufundi kote nchini kuondoa vikwazo na kutoa upendeleo maalum kwa wanafunzi wa kike wenye sifa wanaojiunga na elimu ya ufundi kwakuwa  idadi kubwa wanafunzi wa kike wanaichukia elimu ya ufundi kutokana na vikwazo vilivyopo kwenye vyuo hivyo dhidi yao.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza na wahitimu wa fani mbalimbali za ufundi kwenye chuo cha ufundi Arusha ATC.

Kaimu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dkt. Masud Senzia amesema chuo hicho kimetekeleza kwa vitendo adhima ya serikali ya viwanda kwani kimeanza kufanya majaribio ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.

Mkurugenzi wa elimu ya ufundi Thomas Katebalirwe akaelza mikakati ya serikali katika kuboresha elimu ya ufundi.

Man Fongo Amvaa Sholo Mwamba

Msanii wa miondoko ya singeli Man Fongo amesema hawezi kukaa na kumzungumzia Sholo Mwamba kwa madai yeye ni mfa maji ndiyo maana haishi kutapa tapa kila uchao kumtaja.

 Man Fongo ameeleza hayo baada ya masaa machache kupita tokea kuonekana kwa 'video' ya Sholo iliyorushwa na EATV katika kipindi cha 'FRIDAY NIGHT LIVE' (FNL) usiku wa kuamkia leo, ikiwa imemuonyesha akimlaumu msanii mwenzake kuwa hana kipaji cha kuendelea kufanya muziki mzuri ndani ya mwaka 2018 huku akimtaka arejee katika fani yake ya awali ya 'DJ'.

"Mimi kwa sasa siwezi kumzungumzia mtu yeyote kwa maana naangalia muziki wangu kwa sababu ndiyo unaonifanya nieleweke kwa wadau wangu, pia unasababisha familia yangu ipate kula. Kwa hiyo mtu akitaka kutoka kwa kutumia kiki na kupitia mgongo wangu nakuwa bado simuelewi. Hivyo siwezi kumtumikia Sholo Mwamba 'eti aniambie mimi nirudi katika fani yangu ya 'DJ' wakati yeye hayupo katika 'manegement' yangu na yeye ni msanii kama mimi", alisema Man Fongo wakati alipofanyiwa mahojiano maalum.

Pamoja na hayo, Man Fongo ameendelea kwa kusema "ninachopenda kumshauri Sholo Mwamba ni kwamba atoe ngoma mpya ili aweze kusikilizwa na raia anachokifanya, apambanie muziki wake aweze kufika mbali na asiangalie muziki wangu mimi", alisisitiza Man Fongo.

Kwa upande mwingine Man Fongo amesema mwaka 2018 amejiandaa vizuri katika ufanyaji kazi wake na wala haiwezi kuwa kama alivyosema mpinzani wake huyo ambae kwa muda mrefu wamekuwa wakitoleana mapovu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

"Kazi mpya nimeangusha juzi tu na mpaka sasa ninapo kwambia inafanya vizuri hivyo Sholo Mwamba ni mfa maji tu kama mtu ambae anatapa tapa yaani mfa maji haishi kutapa tapa. Kwa hiyo ameona bora apate kiki kwa mgongo wangu ili aweze kutoka", alisema Man Fongo.

Viongozi CCM Moshi Waaswa Kubadilika

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa chama hicho Manispaa ya Moshi, kuacha kutembea na watu mifukoni na kutengeneza kofia za ubaguzi ndani ya chama kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikikigharimu chama wakati wa uchaguzi.

Polepole amesema chama hicho kimekuwa kikijikuta katika wakati mgumu wakati wa uchaguzi kutokana na baadhi ya viongozi ndani ya chama kupenda ubinafsi na kuweka mbele uheshimiwa badala ya utumishi.

Ametoa rai hiyo leo Jumamosi wakati akizungumza  kwenye kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Manispaa ya Moshi kilichofanyika mjini Moshi katika ukumbi ulioko kwenye ofisi za chama hicho mkoa ambapo amesema sasa ni wakati wa kujiimarisha ili kuweza kushika hatamu kila ngazi.

Amesema kumekuwepo na baadhi ya viongozi ndani ya chama ambao wamekuwa wakitengeneza makundi ya walionacho na wasio nacho wakati wa uchaguzi hali ambayo imekuwa ikikifanya  chama kushindwa kila mwaka wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali likiwemo jimbo la Moshi Mjini.

"Kushindwa kwa CCM  katika majimbo mengi Kilimanjaro hasa hili la Moshi Mjini, kulisababishwa na viongozi, kutembea na majina yao mifukoni na kuweka uheshimiwa mbele badala ya utumishi,  hali hii ilijenga makundi, sasa ni lazima  tubadilike," amesema Polepole

VIDEO: CHADEMA Watoa Kauli Nzito Uchaguzi Kinondoni


Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Salum Mwalimu amefanikiwa kurudisha fomu ya kugombea Ubunge jimbo la Kinondoni huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha muda mfupi.

TAZAMA FULL VIDEO HAPO CHINI.......USISAHAU KUSUBSCRIBE

Mkurugenzi wa Maji Musoma atumbuliwa

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe , ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Musoma, Gantala Said (pichani kushoto) ambaye anachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Mradi wa Maji Bunda na akizivunja Bodi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira za Mikoa ya Arusha na Mara (Musoma) baada ya kujiridhisha kuwa utendaji wao siyo mzuri.

Kamwele amefikia uamuzi huo leo baada kubaini kuwa kumekuwepo na uzembe wa utekelezaji wa miradi ya serikali ya maji kwa baadhi ya watendaji katika idara hizo.

“Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majliwa mkoani Mara, imebainika kuwa kumekuwepo na matatizo ya huyo Mkurugenzi Gantala ambaye Waziri Mkuu ameagiza Mkurugenzi huyu watendaji wengine wachunguzwe na TAKUKURU.

“Hivyo kuanzia leo Januari 20, 2017 ninatengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Musoma, Gantala Said na nafasi yake itakaimiwa na Eng. Robert Petro Mponya wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUASA), ninamuagiza aisaidie Musoma ili waweze kufanya kazi inayotakiwa,” alisema Kamwele.

Wolper awafunda mabinti

Msanii wa filamu bongo ambaye sasa amegeukia ujasiriamli, Jackline Wolper, amewapa somo mabinti na kuwafunda juu ya kujishughulisha ili kujipatia kipato chao, na hatimaye waweze kuheshimika.

Akizungumza kwenye Friday Night Live ya East Africa Television, Jackline Wolper amesema ni wakati sasa mabinti kuacha kutegemea pesa wanazopewa na wanaume, na badala yake wajishughulishe ili kutengeneza pesa yako mwenyewe.

“Wadogo zangu wa kike 2018 mi ntaendelea kuwatia hasira, na kuendelea kuwaambia kwamba hela ya mwanaume sio ya kwako, ukishachukua hela ya mwanaume fanya kitu chako, iwe hela yako, usikubali kunyanyasika, kwa hela ya mtu, kwa hiyo wadogo zangu nitaendelea kuwaisipire ili mfanye kazi ili utambe na hela yako, usitambe kwa hela ya kuhongwa”, amesema Wolper.

Hivi sasa Wolper anamiliki biashara yake ya mavazi ambayo ana buni na kushona mwenyewe, ambayo aliwahi kusikika akisema inamuingizia pesa nyingi ingawa watu wengi wakimdharau kwa kumuita 'fundi cherehani'.


Waziri Mkuu ataka Watumishi Na Madiwani kushirikiana

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri na Mji wa Bunda pamoja na Madiwani washirikiane katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Pia amewaagiza watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya na mji wa Bunda wafanye kazi kwa bidii na wawahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya na wa Halmashauri Mji wa Bunda, katika ukumbi wa Halmashauri ya Bunda.

“Watumishi wa umma  acheni kukaa sana maofisini tengeni muda wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na shirikianneni nao katika kutatua kero zinazowakabili. Madiwani na watumishi lazima mshirikiane ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema watumishi na madiwani wakishirikiana katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo, wilaya itafanikiwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi  na wajiepushe na vitendo vya rushwa, wizi , ufisadi na uzembe kwa sababu vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa maji wa Bunda na baadae alizindua kikundi cha Ushirika cha Igembe Sabo na kukagua skimu ya umwagiliaji wa zao la mpunga ya Nyatwali wilayani Bunda.

Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake wilayani Bunda kwa kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Stendi Mpya katika mji mdogo wa Bunda.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU