Saturday, 20 January 2018

Nafasi za kazi leo Jan 20

Kocha Mpya wa Simba apagawishwa na Okwi

KIKOSI cha Simba,  Alhamisi kilijitanua kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao Simba ilikuwa ikihitaji zaidi matokeo ya ushindi ili ijihakikishie nafasi yake ya kukaa kileleni, ilifanikiwa kupata bao la mapema dakika ya tatu lililofungwa na Shiza Kichuya. Beki wa kati wa timu hiyo,

Asante Kwasi, aliongeza bao la pili dakika ya 24 baada ya kukwepa mtego wa kuotea aliowekewa na mabeki wa Singida United.

Mara baada ya Kwasi kufunga bao hilo, kocha mpya wa Simba, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa, alinyanyuka kwenye kiti chake akiwa jukwaani na kuanza kushangilia pamoja na ofisa habari wa timu hiyo, Haji Manara huku akiwapungia mkono mashabiki wa timu hiyo.

Dakika ya 65 wakati Emmanuel Okwi wa Simba anajiandaa kuingia kuchukua nafasi Mzamiru Yasin, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimshangilia kwa nguvu jambo ambalo lilimhamasisha straika huyo na kuipatia Simba bao la tatu dakika ya 75.

Okwi aliongeza bao la nne dakika ya 82 ambapo kwa mara nyingine, Mfaransa, Lechantre aliinuka kwenye kiti na kushangilia kwa nguvu. Katika mchezo huo, Simba ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili ambapo ilianza kumtoa Mwinyi Kazimoto dakika ya 22 na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla kabla ya dakika ya 65 kutoka Mzamiru na kuingia Okwi.

Kwa upande wa Singida United, dakika ya 59 ilimtoa Kiggy Makasi na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Chuku. Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 29 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27. Mtibwa Sugar ni ya tatu ina pointi 24, Singida inakamata nafasi ya nne na pointi 23, huku Yanga ikiwa ya tano na pointi 22.

Wafanyabiashara waifungukia Serikali

Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango

Wafanyabiashara nchini wameiomba Serikali kuacha kufanyakazi kwa kukurupuka ikiwamo kuwaadhibu kwa makosa ya wengine badala yake iwe kitu kimoja na sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwa Taifa.

Wito huo ulitolewa jana na makamu mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte kwenye mkutano baina yao na Serikali ulifanyika katika ukumbi wa Hazina mjini hapa na kuhudhuriwa na wabunge na baadhi ya mawaziri.

Shamte alisema katika baadhi ya maeneo, Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kukurupuka na kujikuta ikiwaumiza wafanyabiashara ikiwamo masuala ya kodi.

Makamu mwenyekiti huyo alisema sekta binafsi inaumizwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa kukurupuka hasa wa kuwaadhibu watu wasiohusika kwa kosa la mtu mmoja.

“Wakati mwingine watu wanaumizwa sana kwa ajili ya maamuzi haya, kodi na kufunga biashara za watu ilhali kosa linakuwa la mtu mmoja. Kwa nini hamuondoi kasoro hiyo?” alihoji Shamte wazo ambalo liliungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wake, Godfrey Simbeye.

Akijibu hoja hiyo, waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango alikiri kuwapo kwa uamuzi wa kushtukiza serikalini na kusema wakati mwingine inalazimika kufanya hivyo.

Dk Mpango alisema wakati mwingine kuna madhara kwa watu kukurupuka na kufanya vitu visivyokuwepo na kusema ndani ya Serikali, kuna baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wanafanya vitu ama kwa kukurupuka au kutokujua.

“Nakiri kweli ndani ya Serikali kuna watu ambao wanafanya mambo ya ovyo na kuisababishia Serikali hasara kubwa, lakini kuna wakati tunafanya hivyo kwa sababu inabidi tufanye hivyo kwa masilahi ya nchi,” alisema Dk Mpango.

Hata hivyo, aliwatupia lawama baadhi ya wafanyabiashara akisema wamekuwa na tabia ya kukwepa kodi jambo ambalo ni kinyume na Serikali.

Sababu ya Engine kumchukua Wolper

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Engine ambaye hivi karibuni kulikuwa na tetesi za kumng'oa Jackline Wolper na kumuweka ndani, ameweka wazi sababu za kuamua kumtumia msanii huyo kwenye kazi yake.

Akizungumza kwenye Friday Night Live Engine amesema Wolper ni miongoni mwa wanawake wachache Tanzania wanaojitambua, na ndio sababu iliyomfanya asifikirie mara mbili kumfuata.

“Wolper ni mwanamke jasiri, mwanamke anayejitambua , anajituma yuko fit kila idara, na ndio maana nikamfuata”, amesema Engine.

Msanii huyo ambaye ameachia kazi yake mpya, amewaomba watanzania kufuatilia kazi zake kwani alishafanya kazi nyingi siku za nyuma lakini hazikuwahi kufanya vizuri.

Waziri Mkuu aagiza kiongozi huyu akamatwe

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA) Mhandisi Gantala Said.

Agizo la Waziri Mkuu limekuja kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Wilayani Bunda mkoani Mara zinazomkabili Mkuregenzi huyo. Waziri Mkuu yupo Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.

Mhandisi Gantala Said ameshindwa kueleza sababu zilizosababisha mradi wa maji mjini Bunda kutokamilika pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi kwaajili ya kutekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.

Majaliwa amesema Mkurugenzi huyo amekuwa akimlipa mkandarasi fedha kabla ya kufanya kazi ambapo hadi sasa tayari mkandarasi wa mradi huo ameshalipwa zaidi ya Sh. bilioni saba na mradi haujakamilika huku wananchi wakiendelea kutumia maji ambayo siyo salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Malima ameagiza kufungwa kwa ofisi za MUWASA na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchungi utakapokamilika.

Wastara: "Sitozikwa na wasanii pekee"



Msanii Wastara Juma

Msanii wa filamu nchini Wastara Juma amesema hatokuja kumladhimisha mtu yeyote katika tasnia ya 'bongo movie' kuwa yeye hana pesa ya kujitibia ugonjwa wake unaomsumbua kwa madai hata siku ikitokea akifa hawezi kuzikwa na hao pekee yao.

Wastara ametoa kauli hiyo kwenye kipindi cha 'FRIDAY NIGHT LIVE' (FNL) kinachorushwa na EATV tinga namba moja kwa vijana, baaada ya kuwepo kwa baadhi ya watu kutomuamini kwa kile kinachomsumbua huku wengine wakidiriki hata kujaribu kumwambia anatafuta kiki kupitia tatizo hilo linalomsumbua la mguu wake.

"Yani hapa mtu anaweza akaniumiza kwa maneno au vitendo kwa sababu yeye anaamini kwa mawazo yake na kichwa chake kwamba, mimi nimekaa kitandani siumwi au pengine nimejiona nimepotea katika ulimwengu hivyo natafuta kiki yaani nijifunue nguo niupige picha mguu wangu uliyochanika kisha niuweke kwenye gazeti ama kwenye runinga (Tv) ?", alihoji Wastara.

Hata hivyo Wastara amesema hawezi kubadilisha fikra za watu wanavyofikilia kwa kuwa hayo ndiyo maisha yao ya kutoamini jambo lolote lile.

"Na kama kuna wasanii ambao wanaamini mimi siumwi siwezi kumladhimisha hata siku moja na ambaye atasema hatokuja kumtembelea Wastara kwa sababu haumwi au hana shida pesa, mimi siwezi kumfanya aniamini kwamba sina pesa. Sitoweza kufanya hicho kitu kwa sababu maelezo ninayoyaeleza katika runinga ndiyo yaleyale hayotokuja kubadilika. Kwa hiyo ninachoongea hapa ni ukweli hautokuja kubadilika miaka yote hata nikifa", alisisitiza Wastara.

Pamoja na hayo Wastara aliendelea kwa kusema "wapo watu wa kweli wanaoamini na wengine wasioamini ambao huwezi kuwafanya waniamini. Watanzania wanaoniamini mimi wanatosha kwa sababu mwisho wa siku sitokuja kujizika mwenyewe au kuzikwa na wasanii pekee yake", alisema Wastara.


Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Yawaandikiia Barua Wabunge Kutaka Miamala Yao

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewaandikia barua baadhi ya wabunge, ikiwataka kuwasilisha taarifa za miamala ya benki za kuanzia Januari hadi Desemba 2017.

Sekretarieti hiyo imetaka taarifa hizo ziwe zimeifikia ndani ya siku 30 kuanzia Januari 15, 2018.

Barua hiyo  inawataka wabunge hao  kutekeleza agizo hilo ili kuthibitisha taarifa zilizomo kwenye tamko lake  alilowasilisha.

Ofisa mmoja wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha kuwepo kwa barua hizo, akisema si wote walioandikiwa barua za kutakiwa kutoa taarifa hizo.

Hata hivyo, alisema wabunge walioandikiwa ni wale ambao fomu zao zinaonyesha haja ya uhakiki zaidi wa taarifa zao.

Rais wa John Pombe Magufuli ndiye alikuwa wa kwanza kuwasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam Desemba 28, 2017.

Baada ya kuwasilisha fomu hiyo, Rais aliipongeza sekretarieti hiyo kwa kazi inazofanya na kumtaka Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu, Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye angeshindwa kuwasilisha tamko la kabla ya Desemba31, 2017.

Kauli hiyo ya Rais iliwaamsha viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wengine wa Serikali kufurika kwenye ofisi hiyo kuwasilisha matamko yao ya mali walizonazo.

Chadema kugombea Kinondoni na Siha

 Wakati naibu katibu mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu akichukua fomu ya kuwania ubunge wa Kinondoni, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameeleza sababu zilizowafanya kurejea katika uchaguzi wa Februari 17.

Mwalimu na mwenzake wa Siha, Elvis Mosi walipitishwa na Kamati Kuu ya Chadema jana kugombea ubunge wa majimbo hayo huku Mbowe akisema, “hiki ni chama cha siasa si zege inayoendeshwa na matamanio na ushawishi wa wananchi.”

Chadema na vyama vinavyounda Ukawa- NLD, CUF, NCCR Mageuzi- pamoja na Chaumma na ACT Wazalendo vilisusia uchaguzi mdogo wa ubunge wa Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini uliofanyika Januari 13 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoridhishwa na mazingira ya uchaguzi wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba 26.

Vyama hivyo viliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha uchaguzi huo ili kutoka fursa ya kukutana na kufanya tathmini ya mazingira ya uchaguzi huo jambo ambalo tume hiyo ililipinga ikisema inasimamia sheria.

Jana, Mbowe alisema walipotangaza kutoshiriki uchaguzi wa Januari 13 walitoa sababu za kutoridhishwa na uchaguzi wa madiwani wa kata 43. “Hatukusema kwamba hatutashiriki kabisa uchaguzi hapana, tulitoa sababu kuwa hatukuridhishwa na uchaguzi wa zile kata 43. Bila shaka mmeona wenyewe hata uchaguzi ulivyokuwa, kama haukuwepo na hata vyama vingine vilivyoshiriki kama havikuwepo vile,” alisema mbunge huyo wa Hai.

“Kilio chetu kimesikika ndani na nje ya nchi, kimesikika kwa wananchi na kwa hatua hiyohiyo tumeona hatutawatendea haki wananchi wa Kinondoni na Siha ambao wamewekewa wagombea ambao hawawataki na hilo kila mtu analijua.”

Mgombea wa CCM aliyepitishwa kugombea Jimbo la Kinondoni ni Maulid Mtulia, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CUF kabla ya kuhamia chama tawala kwa madai ya kuunga mkono utendaji kazi wa Rais John Magufuli. Katika Jimbo la Siha, chama tawala kimemuweka Dk Mollel aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, lakini akakihama chama hicho na kujiunga CCM kwa madai ya kuunga mkono utendaji kazi wa Rais Magufuli.

Mbowe alisema, “Tunarudi katika uchaguzi, vyombo vinavyopaswa kusimamia haki vifanye hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vingine vyote, hatutaidai tena haki kwa kupiga magoti hivyo watekeleze majukumu yao ipasavyo.”

Alipoulizwa ilikuwaje wakampitisha Mwalimu ambaye hakushiriki kura za maoni, Mbowe alisema utaratibu wa kura ya maoni ndani ya Chadema haupo kikatiba, wanaamini maridhiano ndiyo njia sahihi ya kutokukigawa chama.

“...Unajua unapofanya kura za maoni unaweza kuwa na makundi mawili na adui yako akayatumia makundi hayo kufanikisha kumpata mtu ambaye ni dhaifu, kwa hiyo Kamati Kuu imeyaona hayo na ililiona hilo Kinondoni ndiyo maana ikamteua Mwalimu,” alisema Mbowe

Vuguvugu laisukuma

Wakati Mbowe akitoa sababu hizo, baadhi ya watu waliojitokeza kuomba kuteuliwa kugombea ubunge wa Kinondoni walisema vuguvugu la kuanzisha mchakato wa kuchukua fomu limesaidia chama hicho kushiriki uchaguzi huo mdogo.

Vuguvugu hilo lilitokana na Chadema Wilaya ya Kinondoni kutoa ruhusa kwa wanachama wao kutangaza nia ya kugombea jimbo hilo kisha mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa uliofanyika Januari 16.

Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki, mkurugenzi wa mambo ya nje na itifaki wa Chadema, John Mrema alinukuliwa akisema msimamo wa Ukawa wa kutoshiriki uchaguzi wa majimbo ya Siha na Kinondoni haujabadilika na kwamba wameunda kamati ndogo inayofanya utafiti kuhusu mchakato huo.

Alisema hata mchakato wa kuchukua fomu uliokuwa unafanywa na ngazi hiyo ya wilaya haukuwa na baraka za ngazi za juu.

Pamoja na hayo, mchakato wa kura za maoni Kinondoni uliendelea kwa wanachama saba ambao ni David Assey, Nicholus Agrey, Rose Moshi, Mustafa Muro, Ray Kimbitor, Juma Uloleulole na Mozah Ally kupigiwa kura.

Katika mchakato huo wa kura za maoni, Kimbitor aliibuka kidedea kwa kuwabwaga wenzake na baada ya kumalizika viongozi wa wilaya walisema wanayapeleka majina hayo yote saba katika kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichoketi jana ili kupata baraka na kusubiri uteuzi wa mgombea mmoja kutoka katika chombo hicho cha uamuzi.

Akizungumzia uamuzi huo wa Kamati Kuu, Kimbitor ambaye pia ni Diwani wa Hananasif alisema shida yao ni kuona Chadema inashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na kuna dalili za chama hicho kuibuka mshindi kutokana na misingi bora iliyojiwekea.

“Kila mtu anajua kulikuwa na sintofahamu Chadema kushiriki au kutoshiriki. Ndiyo maana sisi tulianzisha lile vuguvugu la kuchukua fomu ndani ya chama na hatimaye limezaa matunda kwa chama kuingia katika uchaguzi huu,” alisema Kimbitor.

Katibu wa Chadema Mkoa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema Kamati Kuu ilipelekewa majina tisa na jina la Mwalimu lilirudi baada ya kupendekezwa na alisisitiza mchakato uliofanywa na ngazi ya wilaya haukuwa na baraka ya juu.

“Kesho (leo) tutatoa ratiba za kampeni baada ya mchakato huu kukamilika. Nawaomba wana-Chadema na Ukawa wawe watulivu kila kitu kitakwenda sawa na mgombea wao yupo makini,” alisema Kilewo.

Kwa upande wake, Mwalimu ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 aligombea Jimbo la Kikwajuni na kushindwa na mgombea wa CCM, Hamad Yussuf Masauni aliishukuru Chadema kwa imani naye na kumpa nafasi hiyo.

“Naingia katika kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya wakazi wa Kinondoni kuwa mbunge wa Kinondoni. Siendi kuwa mbunge wa Chadema au Ukawa, nitakuwa mbunge wa watu wa Kinondoni,” alisema Mwalimu na kuongeza.

“...Naomba wakazi wa Kinondoni watupime, watuchuje na watutathmini wagombea na baadaye waamue nani anakidhi vigezo na anatosha kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitatu iliyobakia.”

Alisema Kinondoni ni taswira na sura ya nchi na imebeba vitu vingi kuliko kawaida na ana imani ya wakazi wa jimbo hilo watawapima vizuri kabla ya kufanya uamuzi wa kuwachagua na atahakikisha anasimamia vyema masilahi ya Taifa.

Amber Lulu afunguka historia ya kusikitisha ya maisha yake

Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye alipata umaarufu kwa kupiga picha za utupu na kuweka mitandaoni, Amber Lulu, amesimulia historia ya maisha yake ambayo imemfanya abadilike na kuwa alivyo sasa.

Akizungumza kwenye Backstage ya Bongo Fleva Top 20 ya East Africa Radio, Amber Lulu amesema maisha yake ya nyuma yalikuwa yenye mahangaiko ya maisha akiwa na umri mdogo, huku akilazimika kujitafutia hadi pesa ya shule.

Amber Lulu amesema wakati yupo mdogo akisoma mama yake alikuwa na tatizo na lililomfanya ashindwe kutimiza majukumu mengi ya kifamilia, hivyo akaamua kujiingiza kwenye masuala mbali mbali ya kujitafutia riziki ili aweze gharama za kumudu maisha.

FAHAMU KWA UNDANI UGONJWA WA PUMU (ASTHMA)


LEO tutaangalia ugonjwa wa pumu au kitaalamu huitwa asthma. Ugonjwa wa pumu huathiri njia za hewa ambazo huingiza na kutoa hewa katika mapafu. Mtu mwenye ugonjwa huu kuta zake za ndani za njia ya hewa hupata maumivu ambayo kitaalamu huitwa inflammation na kuvimba.

Maumivu katika njia za hewa huzifanya njia hizo za hewa kujihami kwa kusinyaa na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachopita kwenda kwenye mapafu. Hali hii husababisha mgonjwa kutoa mlio kama wa filimbi au mluzi wakati wa kupumua. Ugonjwa wa pumu unaweza kudhibitiwa kama vile ugonjwa wa kisukari na moyo unavyoweza kudhibitiwa.

AINA ZA PUMU
Kuna aina kuu mbili za pumu. Aina ya kwanza ni ile inayoanza mapema kitaalamu huitwa early onset asthma na aina ya pili ni ile inayochelewa kuanza yaani late onset asthma. Tuchambue kwa kifupi aina hizo za pumu. Pumu inayoanza mapema (early onset asthma) Aina hii ya pumu huanza kumkumba mtu akiwa mtoto ambapo miili yao hutengeneza kingamwili (antibodies) za IgE. Wagonjwa wa aina hii ya pumu hutambuliwa kwa vipimo maalum vya ngozi ambapo huonyesha kuathirika kwa asilimia kubwa ya vipimo hivyo vinapofanywa. Pia wagonjwa hawa huwa na matatizo mengine ya mzio (allergic disorders) kama mafua na ukurutu (eczema).

Pumu inayochelewa kuanza (late onset asthma) Aina hii ya pumu,tofauti na iliyopita, humkumba mtu akiwa mkubwa. Hakuna ushahidi wowote unaohusisha maradhi haya na mizio (allergens) vinavyotokana na mazingira na uwezo wa kusababisha aina hii ya pumu. Haifahamiki hasa ni sababu zipi zinazofanya njia za hewa kupata maumivu na hivyo kusababisha mtu kupata ugonjwa huu wa pumu. Vyanzo mbalimbali vinaonyesha kuwa ni kutokana na mseto wa vitu kama tumbaku, maradhi na baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio.

Kuna vitu katika mazingira ambavyo vinaweza kusababisha mtu kushambuliwa na pumu. Vitu vinavyosababisha mzio ni kama vumbi, mende, chavua (pollen) kutoka kwenye miti na majani, viwasho (irritants) kama moshi wa sigara, uchafuzi wa hewa, harufu kali kutoka kwenye rangi au kitu chochote kitoacho harufu, au msongo wa mawazo na maradhi yatokanayo na virusi au manyoya au magamba ya wanyama.
Mtu anaweza kupata pumu kutokana na kuwa na mzio na madawa kama aspirin, ugonjwa wa kucheua, viwasho au vizio vitokanavyo na kemikali au kuwa na magonjwa ya njia ya hewa n.k Mtu anaweza kupata ugonjwa wa pumu kama anaishi katika miji mikubwa na kukumbana na vitu ambavyo kwake
humsababishia mzio, au kuvuta hewa iliyo na moshi, kemikali zitokanazo na kilimo,dawa za kutengeneza nywele, rangi, vyuma, plastiki au vifaa vya elektroniki. Mtoto anaweza kuwa na pumu kwa kurithi kwa mmoja wa wazazi wake mwenye pumu au baada ya kuathirika na maradhi ya mfumo wa hewa kama kikohozi na mafua wakati wa utoto au kutokana na kuwa na unene wa kupita kiasi (obesity), kuwa na ugonjwa wa kucheua na kiungulia (Gastro esophageal reflux disease).

DALILI ZA PUMU Baadhi ya dalili za kawaida za ugonjwa wa pumu ni kama zifuatazo: Mgonjwa kushikwa na kikohozi: Mara nyingi kikohozi cha pumu huwa kikali nyakati za usiku au alfajiri na hivyo kumfanya mgonjwa kutolala vizuri usiku. Mgonjwa kutoa sauti ya mfano wa mtu anayepiga mluzi au filimbi wakati wa kupumua, kifua kubana ambapo mgonjwa husikia kama kitu kinakandamiza kifuani au wakati mwingine husikia kama mtu amemkalia kifuani. Dalili nyingine ni mgonjwa kukosa hewa na kujikuta kama hawawezi kupumua kwa hewa inayoingia na kutoka kwenye mapafu. Kutokana na hilo mgonjwa huyo atakuwa anapumua harakaharaka. Dalili hizo zinaweza kuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha. Wengine hupata dalili hizo mara moja tu kwa mwezi, wengine kila wiki na wengine hupata dalili kila siku.

UCHUNGUZI Mgonjwa ni lazima afanyiwe kipimo kwa kuangalia jinsi mapafu yanavyofanya kazi. Kipimo hicho hujulikana kitaalamu spirometry na hutumika kwa watu kuanzia miaka
mitano na kuendelea na hutathmini kiasi cha hewa mtu awezacho kukitoa baada ya kuvuta hewa kwa nguvu na kwa haraka. Kipimo hiki cah spirometry pia hutumika kutathmini jinsi mgonjwa wa pumu anavyoendelea, kupata nafuu au tatizo kuongezeka. Mgonjwa pia anaweza kufanyiwa kipimo cha mzio (Allergy Test). Kipimo cha ugonjwa wa kucheua na kiungulia pia hufanyiwa mgonjwa.

Mgonjwa pia ni lazima apimwe mapafu kwa X-ray ili kuona iwapo kuna kitu chochote kilichoziba njia ya hewa au kama kuna maradhi yoyote katika mapafu au moyo. TIBA Kuna aina mbili za matibabu ya pumu, moja ni ile ya dharura ili kutoa msaada au nafuu ya haraka. Dawa hizi ni zile zinazosaidia kutanua njia za hewa ambazo zimesinyaa yaani bronchopdilators ambazo pia husaidia kuilainisha misuli ya njia za hewa iliyosinyaa ili iweze kutanuka na kuruhusu hewa ya kutosha kuingia kwenye mapafu. Aina nyingine ya dawa ni zile za muda mrefu. Aina hizi za dawa hutumiwa mara kwa mara kwa kipindi kirefu kuzuia dalili za pumu na mashambulizi. Watu wenye pumu isiyoisha wanahitaji matumizi ya dawa ya muda mrefu.Kotikosteroidi za kuvuta (inhaled corticosteroids) ni nzuri kwa aina hii ya pumu.

TIBA KWA WATOTO Watoto wenye pumu kama ilivyo kwa watu wazima wanapaswa kumwona daktari wale walio na umri mdogo wanahitaji uangalizi wa wazazi/ walezi ili kudhibiti pumu. Watu wazima wanaweza kutakiwa kupunguza au kuongeza matumizi ya dawa za pumu kutokana na maradhi mengine waliyonayo. Madawa kama ya kutibu shinikizo la juu la damu, ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona (glaucoma),aspirini na dawa za maumivu (non steroidal anti inflammatory drugs) huingiliana na utendaji wa dawa za pumu au zenyewe kusababisha pumu, hivyo matumizi yake yanahitaji ushauri wa daktari.

Wajawazito wenye pumu wanahitaji ushauri wa karibu wa daktari kwa kuwa ikiwa pumu itasababisha kusinyaa kwa njia ya hewa basi wanaweza kusababisha upungufu wa hewa ya oksijeni kwa mtoto hali ambayo ni hatari kwa mtoto tumboni. Dawa nyingi za pumu hazina madhara kwa mtoto aliye tumboni, hivyo ni muhimu kuendelea na matibabu wakati wa mimba kwa ushauri wa daktari kuliko kuacha.

KINGA Njia pekee ya kujikinga na pumu ni kuepuka mzio au vitu vinavyoweza kusababisha ugonjwa huo kwa kusafisha nyumba kila wiki kupunguza vumbi, kuwaepusha watoto na baridi au kukumbatia paka au wanyama, kuepuka kufanya mazoezi kwenye baridi, kuepuka moshi wa sigara, kudhibiti ugonjwa wa kucheua na kiungulia na kadhalika.

DALILI ZA MIMBA KUTUNGA NJE YA MJI WA UZAZI


HILI ni tatizo ambalo linawaathiri wanawake wengi. Kwa kawaida, mimba zinazotungwa nje ya mfuko wa uzazi hazina uwezo wa kukua kuwa mtoto kamili. Mimba hizi ni hatari kwa afya ya mjamzito kwa vile humfanya kupoteza damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo asipowahi kutibiwa. Katika mfumo wa uzazi wa mwanamke, kuna sehemu nyingi ambazo kila moja ina umuhimu wake.

Ikiwa sehemu mojawapo itapata hitilafu, husababisha athari katika mfumo wa uzazi. Miongoni mwa sehemu muhimu ni ovari ambayo ndiyo sehemu mayai ya uzazi yanapotengenezwa. Mayai haya husafiri kupitia mirija ya fallopian.

Kazi za mirija ya fallopian ni kusafirisha mayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji (ovari) mpaka kwenye mfuko wa uzazi (uterus). Utungisho wa yai la kike (ovum) na mbegu ya kiume (sperm) hufanyika kwenye mirija hii.

Mara baada ya utungisho, misuli inayozunguka mirija ya fallopian ikishirikiana na vinyweleo vilivyopo ndani ya mirija hii husukuma kiinitete au yai lililorutubishwa na kulipeleka kwenye uterus. Yai lililorutubishwa au
kiinitete, lifikapo kwenye uterus hujipachika katika mojawapo ya kuta zake kwa ajili ya kuendelea kurutubishwa, kukua taratibu na hatimaye kufanya mtoto.

RIPOTI MAALUM: NI KWELI KUNA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU KIUME -3


MSOMAJI,bado naendelea kukufungua ufahamu kuhusu suala la tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Wiki iliyopita tuliona jinsi wataalamu walivyoelezea mishipa ya damu inavyosababisha ukosefu wa nguvu za kiume kama ina hitilafu. Tuliona pia jinsi moyo ukiwa na hitilafu unavyosababisha mwanaume kukosa nguvu hizo za kufanya tendo la ndoa, endelea sehemu hii ya tatu ambayo inajikita zaidi na virutubisho katika mwili vinavyosaidia kumpa nguvu yule ambaye hana nguvu za kiume.
Endelea: Toleo lililopita tuliona kuwa upungufu wa nguvu za kiume unasababishwa na mambo mengi kama vile mishipa ya damu kuwa na kasoro lakini leo tutafafanua kuhusu ukosefu wa virutubisho muhimu mwilini na jinsi ya kuongeza nguvu za kiume bila kutumia dawa za viwandani.

Ni jambo muhimu kama mtu atazingatia kula vizuri na kufanya mazoezi ili kuthibiti nguvu za kiume. Mazoezi yapo ya aina nyingi, kwa wale wenye umri mkubwa wanaweza kufanya mazoezi ya kutembea kwa mwendo wa kasi kwa dakika 35 au saa nzima kila siku. Wakati mwingine pia wanaweza kufanya mazoezi ya kukimbia kwa zaidi ya dakika 30, kuogelea au mazoezi ya kufanyia kwenye vyumba maalum vya mazoezi(gym), kufanya jogging mkiwa katika makundi au mmoja mmoja.

Mazoezi ni tiba ya vitu vingi mwilini ikiwa ni pamoja kuondoa presha na kwa wale wenye matatizo ya nguvu za kiume. Ili kuongeza nguvu za kiume si lazima kutumia dawa kali kama viagra au vilevi vikali. Dawa na pombe hukupa nguvu zinazodumu na kuisha kwa muda mfupi, lakini hukuletea madhara makubwa yatakayoathiri mwili kwa muda mrefu zaidi.

Ili kupata suluhisho la uhakika la nguvu za kiume Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai anasema ni vizuri kuzingatia vyakula vinavyoweza kukuongezea stamina na kujenga mwili wako vizuri na kukupa uwezo wa kufanya mapenzi vizuri zaidi bila kutumia dawa; vyakula ni suluhisho maridhawa kwa kila kitu maishani mwako. Anasema mwili wako una maarifa ya kujirekebisha pasipo kuhitaji dawa au vilevi, unachotakiwa kuzingatia ni chakula bora tu.

Sehemu za viungo vya uzazi kwa mwanaume kutokuwa na kiwango cha kutosha cha homoni ya Testosterone, kupungukiwa protini na hivyo kukosa amino asidi mwilini na kusababisha ukosefu wa nguvu za kiume. Leo napenda tuangalie vyakula ambavyo vinasaidia kuongeza na kuboresha nguvu za kiume na kusaidia kwa kiasi kikubwa kudumisha mapenzi na kulinda uhusiano na ndoa, hivyo hii ni dawa nzuri ya asili ya kurejesha nguvu za kiume.

Matunda ambayo husaidia kuondoa tatizo hilo ni haya yafuatayo:
BLUEBERRY Blueberry ni matunda yanayosaidia sana kuongeza nguvu za kiume, wengi hupendelea kuyaita ‘viagra’ asilia kutokana na kazi nzuri inayoifanya mwilini ya kuongeza nguvu za kiume. Kama tulivyoona wiki iliyopita kuwa mishipa ya damu ni muhimu, Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai anasema, blueberries ina virutubishi vinavyoimarisha mishipa ya damu na kusaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini, niwakumbushe tu kuwa damu ndiyo kila kitu katika nguvu za kiume.

Anasema blueberries zina nyuzinyuzi (fiber) ambazo husaidia kuondoa kolesteroli (Cholestrol) mwilini kabla hazijanganda kwenye mishipa ya damu. Kuwa na mzunguko mzuri wa damu husaidia mwanaume kuwa na nguvu za kiume hivyo kuhimili kufanya mpenzi wa muda mrefu zaidi. “Kuna matunda yanayoitwa mtini (figs); ni matunda yenye kiwango kikubwa cha amino asidi, ambayo ni kiungo kikubwa katika kuzalisha homoni mwilini. Homoni ndiyo kishawishi cha nguvu za kiume mwilini. Kukosa amino asidi huweza kusababisha kukosa hamu ya mapenzi au kupungukiwa na nguvu za kiume,” anasema Mandai.

CHAZA/KOMBE (RAW OYSTERS)
Anaongeza kusema chaza wana kiwango kikubwa
cha madini ya zinc. Madini za zinc hutumika katika utengenezaji wa homoni ya testosterone, na mbegu za kiume. Uwingi wa uzalishwaji wa testosterone mwilini huathiri pia hamu ya mapenzi na nguvu za kiume ikiwa kidogo huondoa hamu, ikiwa nyingi humfanya mtu kuwa na hamu na nguvu zaidi. Kupungukiwa kwa madini ya zinc husababisha kupungua kwa nguvu za kiume, udhaifu na kushuka kwa kiwango cha uwezo wa kufanya ngono.
KARANGA
Mtaalamu huyo anasema, karanga ni chanzo kikubwa cha kujenga protini mwilini kwani huwa na kiwango kikubwa cha amino asidi ambayo husaidia kuweka vizuri mfumo wa damu, hivyo kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha nguvu za kiume.

VITUNGUU SAUMU Anaongeza kuwa kitunguu saumu kina allicin, kiambato kinachosaidia mzunguko mzuri wa
damu kwenye viungo vya uzazi. Kuwa na mzunguko mzuri wa damu kwenye uume ni sababu kubwa ya kuongeza stamina ya kufanya mapenzi.

NDIZI Anasisitiza kuwa ndizi ni chanzo kikubwa cha vitamin B ambayo husaidia sana katika kuongeza stamina na nguvu mwilini hasa wakati wa kufanya kazi nzito. Ndizi ina kimeng’enyo cha Bromelain ambacho huongeza nguvu za kiume na ashki ya mapenzi (libido).
CHOCOLATE
Kuhusu chocolate mtaalamu huyo anasema inasaidia kuongeza stamina kwenye kufanya kwa sababu ina viambato vya phenylethylamine na alkaloid. Anasema Phenylethylamine ni kiambato kinachofanya mtu kujisikia vizuri, hasa wakati wa kufanya mapenzi na alkaloid huongeza stamina na nguvu za kiume.

Haishauriwi kutumia dawa kama Viagra kuongeza nguvu za kiume badala yake watu wanatakiwa kutumia njia asilia katika kutatua matatizo hayo ya kiafya. Mwili una njia zake za kurekebisha kila kitu. Ukiona kuna tatizo mwilini, inaashiria kuna upungufu ambao unatakiwa kurekebishwa.

Kutumia madawa makali hudhoofisha mwili na hivyo kuupunguzia uwezo wa kufanya kazi kama inavyotakiwa. Ni vizuri kama utamuona daktari kama ukiona hakuna kinachowezekana kabla hujaanza kutumia dawa za viwandani.

Mara nyingi njia asilia ya kutumia vyakula hutumia muda mrefu sana kuleta mabadiliko, lakini matokeo yake hudumu zaidi kuliko kutumia madawa makali ambayo hutibua mfumo wa kawaida wa ufanyaji kazi wa mwili wako.

Ni vizuri kula kwa kiasi kabla ya kufanya mapenzi, hasa wakati wa usiku kabla ya kwenda kulala. Ni vizuri ukajaribu kubadilisha chakula unachokula, fanya mazoezi mara kwa mara ili kupata mwili wenye nguvu. Itaendelea wiki ijayo.
Na Elvan Stambuli

VYAKULA VINAVYOSAIDIA KUONDOA MAUMIVU WAKATI WA HEDHI


WIKI iliyopita tuliona jinsi matunda yanavyosaidia kutibu maradhi mbalimbali mwilini, leo tutaangalia aina mbalimbali za matunda yanayoweza kutibu matatizo mbalimbali yanayowahusu wanawake wakati wa siku zao (menstruation period). Miongoni mwa matunda hayo ni papai bichi lakini lililokomaa ambalo lina uwezo wa kulainisha misuli ya njia ya uzazi hivyo kufanya kipindi cha hedhi kutokuwa na maumivu.

Katika suala hili, ili wanawake kujiepusha na kupatwa na matatizo ya maumivu, kutokwa damu kwa wingi kusiko kawaida, kuchelewa kuona siku zao, wanashauriwa kuzingatia suala la lishe. Wanapaswa kujua vyakula gani wale na vipi wasile ili kujiwekea kinga ya kudumu dhidi ya tatizo hili.

LISHE YA KUDHIBITI MATATIZO YA HEDHI
Matatizo mbalimbali yanayohusiana na hedhi, yanaweza kudhibitiwa na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa kutibu mfumo mzima wa mwili, ili kuondoa sumu iliyojilimbikiza katika mwili wa mgonjwa kwa kipindi cha muda mrefu, sumu ambayo imegeuka na kuwa chanzo cha matatizo yanayojitokeza wakati wa hedhi.

Mfumo mzima wa mwili unapokuwa umezingirwa na sumu (toxins), ndiyo huwa chanzo cha matatizo mbalimbali, yakiwemo hayo yanayojitokeza kwa wanawake wakati wa hedhi na dawa pekee katika hili ni kwanza, kuondoa sumu hizo mwilini kwa njia ya lishe.

Ili kuondoa sumu hizo mwilini, mgonjwa anatakiwa kuanza mpango maalum wa kula matunda na mbogamboga pekee, kutwa mara tatu kwa muda wa siku tano mfululizo. Katika siku hizo, anachokuwa anakula ni matunda, juisi za matunda kama machungwa, mananasi, zabibu, tufaa, papai bichi, karoti, parachichi, nyanya, mboga mbalimbali pamoja na maji, kila wakati wa kula unapowadia, maji hayo mtu anywe nusu saa baada ya mlo.

Hii ina maana kwamba mlo wa mtu huyu, katika kipindi cha siku hizo tano, utakuwa vyakula vilivyotajwa hapo juu, kuanzia asubuhi, mchana na jioni, katika kipindi hicho, matunda, juisi na mbogamboga atakazokuwa anakula zitakuwa zinafanya kitu kinachoitwa kitaalamu ‘detoxification’, yaani uondoshaji wa sumu mwilini kwa njia ya asili
aliyotuumba nayo Mungu. Hata hivyo, kwa wale wanawake ambao ni wembamba sana, ambao pengine katika kipindi cha funga hiyo ya matunda wanaweza kupoteza uzito sana, wanaweza kunywa glasi ya maziwa freshi sambamba na mlo wao wa matunda. Hii ni kwa sababu ya kuepuka kupoteza uzito kuliko kawaida.

UFUATE MLO KAMILI Baada ya kumaliza siku tano za kula na kunywa juisi na matunda, mtu mwenye kufanya zoezi hili atatakiwa kuzingatia ulaji wa mlo kamili utakaotilia maanani matunda, mboga za majani, vyakula vya nafaka kama ugali wa mahindi, mtama, ulezi n.k. Nafaka zinazoshauriwa ni zile ambazo hazijakobolewa na kuondolewa viini lishe (wholegrain).

Waepuke kula vyakula vitokanavyo na unga mweupe, ikiwemo mikate myeupe, sukari, vitu vitamu (confectioneries), vyakula vya kwenye makopo. Aidha, mtu huyu anashauriwa kuepuka kunywa chai iliyowekwa majani mengi au kahawa iliyowekwa kahawa nyingi

. UVUTAJI SIGARA UKOME Kwa wale akina mama wenye matatizo wakati wa siku zao na ambao wameamua kuingia katika mpango huu wa kusafisha mwili, hawana budi kuachana kabisa na uvutaji sigara kama ni wavutaji ili kufanikisha zoezi hilo. Kwa ujumla uvutaji sigara ni mbaya kwa afya ya binadamu.

Makala hii imeandaliwa na Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai, kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0754391743 au 0717 961 795. Usikose pia kusoma makala zangu za Afya Yako kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda kila Jumatatu uelimike.