Monday, 25 December 2017

Misingi ya Uvumilivu kwenye Ndoa



Ni wazi kuwa migogoro kwenye uhusiano wowote ule ipo, hasa pale wenza hao wasipopeana nafasi ya kusikilizana.
Kila siku narejea hii hoja kuwa, hata kwenye uhusiano wa mapenzi lazima kutakuwepo na mikwaruzano ya hapa na pale jambo la msingi ni namna ya kushughulikia misuguano hiyo bila kuibua chuki na hatimaye kuvunja uhusiano.
Hata katika uhusiano wa kawaida, mikwaruzano na misuguano ni kama kukanyaga bomu, bila kuchukua tahadhari na kutegua bomu lenyewe, ukiondoa mguu mtu bomu hilo linalipuka na kuharibu kila kitu.
Uvumilivu ndio jibu kubwa kwa wenza endapo itatokea kukwaruzana au kutoelewana.
Endapo mwenza wako amekuudhi na kukupandisha hasira jambo la msingi kabisa ni kuhakikisha unadhibiti hasira hizo. Jaribu kuelewa kwanza tatizo kabla hasira hazijakuathiri na kukutawala.
Kumbuka kuwa hasira hasara na siku zote mtu mwenye hasira huzungumza na kufanya mambo ambayo baadaye hujikuta akijilaumu. Lakini pia watalamu wa masula ya mahusiano wanasema ya kwamba siku zote epuka kuchukua maamuzi ukiwa na hasira.
Unapotokea msuguano katika mapenzi epuka kuwa mzungumzaji na mlalamishi, kuwa mtulivu na tanguliza busara mbele kabla ya kutamka chochote kinywani kwako.
Huo ndio msingi wa uvumilivu.
Katika hili, vitabu vingi vya uhusiano vinashauri kuwa endapo mwenza anaona hali na mazingira ya mazungumzo hairidhishi kutokana na ugomvi wenyewe ni bora kuahirisha mazungumzo hayo na kupanga muda mwingine wakati wote wawili wakiwa wametulia.

Sunday, 24 December 2017

Jeshi la Polisi Lawaonya Wavunjifu Wa amani



Jeshi la Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam, limewaonya na kuwatahadharisha watu wenye tabia za uhalifu kutovunja sheria katika siku hizi za sikuu, kwani limekaa macho na kujipanga kuwadhibiti.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam Lazaro Mambosasa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, ambapo amesema kwamba hapo kesho jiji litazingirwa na askari wa kutosha kuhakikisha wakazi wake wanakuwa salama dhidi ya vitendo viovu.
"Kwanza nimepiga marufuku disco toto kwa ajili ya usalama, lakini pia kwenye fukwe polisi watakuwepo kuangalia usalama, wale wanaovizia mikoba na vitu vingine niwaambie tu hawatakuwa salama, kwani askari wetu wamejipanga kukabiliana nao, kutakuwa na ulinzi wa kutosha, askari wa jeshi la polisi, tumeomba ushirikiano kutoka kwa askari wa makampuni binafsi, walinzi shirikishi, hivyo hawataweza kwenda hatua tatu bila kudakwa", amesema Mambosasa.
Sambamba na hilo Kamanda Mambo sasa amewataka wananchi kusherehekea sikukuu hizo kwa amani wakiwa majumbani kwao na familia zao, ili kuhakikisha watoto wanakuwa salama, huku akiwaonya wale watumia vyombo vya moto kuwa makini na kufuata sheria za barabara.
"Tunaelekeza watu watii sheria, tunajua watu wakishakunywa wanapoteza ufahamu, wito ni kwamba watii sheria za barabarani na washerehekee na familia zao majumbani mwao, ili watoto waendelee kuwa salama, wasiwaache wenyewe", amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema ulinzi huo mkubwa na wa hali juu utaendelea mpaka sikukuu za mwaka mpya, ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea siku za sikukuu.

Sherehe za Mapinduzi Kugharimu 1.2 bilioni



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itatumia zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12 mwakani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 ofisini kwake Vuga mjini Unguja alipotoa taarifa ya maandalizi ya sherehe hizo.
Amesema fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya siku ya kilele, ufunguzi wa miradi 49 ya maendeleo ya kiuchumi, miradi ya maji, majengo ya shule, umeme na barabara.
Waziri amesema miradi 33 itazinduliwa baada ya kukamilika na 16 itawekwa mawe ya msingi. Miradi hiyo ni ya taasisi za umma, jamii na ya wawekezaji.
Waziri Mohamed amesema Serikali imepiga hatua katika kufanikisha huduma za kijamii na maendeleo sambamba na lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yatazinduliwa Desemba 30,2017 kwa kufanya usafi wa mazingira.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Idriss Muslim Hijja amesema miradi iliyopendekezwa kuingizwa katika maadhimisho imefuatiliwa na kutolewa taarifa kwa sekretarieti ya halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa.
Amesema katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi, viongozi wa kitaifa wa Serikali zote mbili wamejumuishwa wakiwemo marais, mawaziri na wastaafu wa pande zote mbili.
Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Januari 12,2018 katika Uwanja wa Amani mjini Unguja ambako Rais Ali Mohammed Shein atakuwa mgeni ra

Mabasi ya Kwenda Mikoani Kufanya kazi masaa 24



Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Johansen Kahatano amesema kuanzia mwakani wataandaa mkakati wa mabasi kufanya kazi saa 24 na kupandisha nauli wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Kahatano amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 alipozungumza na waandishi wa habari eneo la Ubungo kuhusu hali ya usafiri.
Amesema kumekuwa na changamoto ya usafiri takriban kila mwisho wa mwaka na kusababisha kero kwa abiria.
“Tumeliona hilo na sisi Sumatra tumeandaa mpango ambao tunafikiri unaweza ukawa suluhisho la adha ya usafiri hapa Ubungo; kwanza tunafikiria kuruhusu mabasi kufanya kazi saa 24 wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka,” amesema.
Amesema pia wataweka nauli kubwa wakati wa msimu wa sikukuu ili abiria wasafiri kipindi ambacho nauli itakuwa ndogo.
Kahatano amesema mpango huo utaanza kufanyiwa kazi mwakani kwa kukaa na wadau wa usafiri na wananchi kuujadili.
Akizungumzia hali ya usafiri kituoni Ubungo amesema iko shwari kulinganisha na jana ambapo abiria walikuwa wengi na mabasi yalikuwa machache.
“Tumejitahidi kusaidia kupunguza adha hii kwa leo baada ya kuruhusu watu wenye magari yenye uwezo wa kupakia abiria kuja na kupatiwa vibali hapa Ubungo,” amesema.

VIDEO:Mtoto wa Babu SEYA afunguka kauli ya Magufuli, Lowasa



Mtoto wa Babu Seya aitwaye, Mbangu Nguza amesema kuwa wao kama familia wanamshukuru Rais Dk John Magufuli kutokana na kuwaachia kwa msamaha Baba yake, Nguza Viking 'Babu Seya' na mdogo wake Papii Kocha waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela katika gereza la Ukonga, siku ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu.
Pia amefunguka kuhusiana na kauli ya aliyekuwa mgombea wa Urais wa UKAWA, Edward Lowasa ambaye aliahidi kuwaachia huru endapo angeshinda urais mwaka 2015.
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI....USISAHAU KUSUBSCRIBE


Mwanamke Amfungia mumewe Ndani na Kisha Kumchoma moto - Mtwara



Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail (29) kwa tuhuma za kumuua mume wake baada ya kumfungia ndani na kisha kuichoma nyumba kwa petroli.
Taarifa hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Lucas Mkondya, ambapo amesema kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, baada ya mwanamke huyo kugundua kuwa aliyekuwa mume wake anaishi na mke mwingine, na kuamua kumvizia nyumbani kwake kisha kuichoma moto na kusababisha kifo chake.
"Ni kweli Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja ayefahamika kwa jina la Zuhura Ismail kwa tuhuma za kuichoma nyumba aliyokuwa anaishi mume wake na mwanamke mwingine, kutokana na wivu wa kimapenzi baada ya Zuhura kugundua kuwa mumewe anaishi na mke mwingine, na kuamua kwenda kuchoma nyumba hiyo moto na kuwasababishia majeraha makubwa, ambapo mumewe alipelekwa hospitali lakini kutokana na majereha hayo makubwa alifariki dunia, lakini mwanamke aliyekuwa nae anaendelea vizuri", amesema Kamanda Mkondya.
Aidha Kamanda Mkondya amesema mara baada ya tukio hilo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail alitoroka na kwenda kusikojulikana, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na pindi atakapopatikana watatoa taarifa.

Rose Muhando Awafungukia wanaomsema kuhusu kujiunga CCM



Msanii wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Rose Muhando ameamua kufunguka ya moyoni baada ya kupokea maoni mengi ya watu wakimponda kuhusu maamuzi yake ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Rose Muhando amesema wanaomponda na kumkebehi anawachukulia ni watu wa kawaida kwani hawezi kujifunza kwa watu walioshindwa huku akidai ameshazoea kusemwa.
“Watu wengine hawaelewagi nini wanachoongea, wanaongea ili waonekane nao wanaongea. Mimi ni mtu ambaye ninayejitambua sawa eehhh!! mimi hata sijali, nimeshazoea kutukanwa kwahiyo hata sihangaikagi na maneno yao. Mimi ni funzi kwa walioshindwa na nimeondoka kwa walioshinda, walioshindwa wana maneno mengi kutokana na nilishaimba uoga wako ndio umasikini wako, Mimi siwezi kuishi kwa uoga kwenye nchi yangu kwani ni maamuzi yangu na sijavunja sheria ya nchi na ningeogopa zaidi kama ingekuwa ni dhambi.”amesema Rose Muhando kwenye mahojiano yake na E-Gospel ya Radio E-FM.
Mapema mwezi huu kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma, Rose Muhando alialikwa kutumbuiza kwenye mkutano huo na kabla ya kukaribishwa Jukwaani, Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema Rose na Kundi lake wamekuja na maombi mawili likiwemo la kujiunga CCM na kutumbuiza huku akisema kuwa vyote vimekubaliwa.
Awali Rose Muhando hakuwa kwenye upande wowote wa vyama vya kisiasa na amesema kujiunga CCM au Chama chochote ni maamuzi yake na sio dhambi wala kosa kisheria.

RC Gambo ashiliki Kwenye Ujenzi Wa Hospitali ya Wilaya



Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la Njiro kontena. Shughuli ambayo ilihidhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza na wananchi hao Gambo alisema “Nina furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya watu wetu wa Arusha,kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi na tunatekeleza kwa vitendo.”
Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya mkoa ya Mount Meru kuelemewa.
 Vile vile Gambo anasema kwa sasa mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.
“Jiji la Arusha mapato yake ya ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli?? Gambo alihoji.
Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500 hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.
Naye mkurugenzi wa Jiji la Arusha Athuman Kihamia alimshukuru Mhe Gambo kwa kuweza kulipigania eneo hilo mpaka limeweza kurudi kwenye mikono ya wananchi.
“Kwakweli kama sio jitihada zako eneo hili lilishaondoka mikononi mwetu hivyo kwa niaba ya wananchi wa Arusha ninakushukuru sana, pia nikuahidi tutazingatia ushauri wako wa kulitumia eneo hili vizuri kwa kujenga majengo ya ghorofa kuanzia tano ili kulitumia eneo hili vizuri” alisema Kihamia. Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika June mwaka 2018 ambapo zaidi ya wakazi laki 4 watapata huduma ya afya karibu na

Rais Mnangagwa amteua mkuu wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ya kumng’oa Mugabe



Jenerali wa Jeshi la Wananchi Zimbabwe ambaye aliongoza mapinduzi yaliyopelekea Robert Mugabe kung’olewa madarakani, ameteuliwa kuwa naibu kiongozi wa chama tawala cha ZANU-PF.
Constantino Chiwenga ameteuliwa na Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambapo hivi karibuni alistaafu kama mkuu wa jeshi, na kuenea kwa tetesi kuwa atapewa wadhifa wa kwenye serikali ya mpya ya Rais Mnangagwa.
Uteuzi huo unaonekana kama hatua ya kuelekea kutajwa kuwa makamu wa Rais baada ya makamu wa Makamu wa sasa wa Zanu PF, Kembo Mohadi ambaye alikuwa waziri usalama chini ya Robert Mugabe kuonekana kuelemewa.

JPM, Mahalia Walivyoitikisa Bandari Dar Mwaka 2017



Kama kuna mashirika au taasisi za Serikali ambazo zilikuwa na wakati mgumu kwa mwaka huu unaomalizika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) huwezi kuiweka kando.
Ugumu wake haukutokana tu na ziara za kushtukiza zilizofanywa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, bali yale ambayo viongozi hao wakuu wa nchi waliyabaini; wizi, upigaji dili na ubadhirifu wa mali za umma.
Waliibua zaidi ya matukio matano kwa nyakati tofauti bandarini hapo jambo lililoashiria kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo nyeti kwa uchumi wa nchi.
Mara zote walizofanya ziara, kama si kubaini udanganyifu wa taarifa za uingizwaji mizigo, basi walikumbana na ukwepaji kodi wa bidhaa na mizigo iliyoingizwa nchini.
Miongoni mwa mambo waliyoyabaini ni kuwapo kwa vichwa 13 vya treni visivyo na mwenyewe, magari 53 aina ya Suzuki ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubebea wagonjwa yaliyohusishwa na Ofisi ya Rais, na malori zaidi ya 50 ya Jeshi la Polisi ambayo yaliingizwa tangu mwaka 2015 bila kuwa na nyaraka zinazoeleweka.
Magari yaingizwa kwa jina la Ikulu
Novemba 26, Rais Magufuli alifanya ziara bandarini hapo kuwaaga mabaharia wa meli ya Peace Arc kutoka China waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa wiki moja, lakini baada ya hafla hiyo fupi, alitembelea eneo la maegesho ya magari hayo yanayodaiwa kuingizwa na Ofisi ya Rais.
Akionekana kama wakili anayewabana mashahidi wa upande mwingine, Rais aliuliza maswali kutoka kwa waziri mmoja hadi mwingine, mtumishi mmoja wa Serikali hadi mwingine akitaka kujua aliyeyaagiza, sababu za taarifa kutotolewa kwa takribani miaka miwili, wahusika kutowafuatilia. Waliowekwa katika hali ngumu ni Dk Philip Mpango, ambaye ni waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Valentino Mlowola (Mkurugenzi Mkuu Takukuru), Simon Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi), George Mnyitafu (Kaimu Kamishna wa Forodha wa TRA) na Deusdedit Kakoko ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Wengi walionekana kupata taarifa za magari hayo wakati wa ziara hiyo, kiasi cha kumfanya Rais aonekane kutoridhishwa na utendaji wao wa kutofuatilia vizuri kazi zao na kufanya magari mengine kukaa bandarini kwa takriban miaka 10 wakati sheria inaruhusu siku 21.
“I’m sorry jamani, haya mengine ni frustration zangu. Nisameheni sana,” alisema Rais Magufuli baada ya kueleza udhaifu wa utendaji wa vigogo hao wa kutochukua hatua.
Rais, ambaye alisema ana taarifa za magari hayo na mtu aliyeyaagiza, alitoa siku saba kwa mawaziri na wakuu hao wa taasisi wawe wamempa taarifa kamili ya suala hilo.
Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli aliwahoji mawaziri na viongozi hao wa taasisi ambao kila mmoja alipewa kipaza sauti ili majibu yake yasikike.
Alianza kwa kumhoji Kakoko kuhusu uhalali wa magari hayo kukaa bandarini kwa muda mrefu na aliyeyaagiza.
Rais Magufuli: Nataka kujua haya magari ni ya nani?
Kakoko: Haya magari yameingia wakati hujaingia madarakani, ila yameingizwa na Ofisi ya Rais. Jina la aliyeyaagiza ni la Kichina au Kihindi hivi, lakini anwani ya mwingizaji ni Ofisi ya Rais ingawa na lenyewe limeandikwa vibaya vibaya na hata maneno yana utofauti. Magari yapo 50.
Rais: Kwa hiyo yameagizwa na ofisi yangu? Kuna mtu yeyote wa ofisi yangu ambaye aliagiza?
Kakoko: Hili jina si la mtu wa ofisini kwako na anuani si ya ofisi yako, bali ni lile jina la mwanzo tu.
Rais: Lakini wanasema yameagizwa na Ofisi ya Rais?
Kakoko: Ndivyo nyaraka zinavyoonyesha.
Rais: Mmeshafanya juhudi gani kama tangu mwaka 2015 Rais ameagiza magari kwa jina la Kichina na hayajachukuliwa na yamekaa hapa kwa jina la Kichina mpaka leo. Ulifanyaje? Ulimjulisha waziri? Na yeye anasema ndiyo amepata taarifa leo.
Kakoko: Utaratibu wetu baada ya siku 21 huwa unahama kwetu. Kimsingi yanakuwa yamehamia TRA.
Rais: Kamishna wa TRA yupo hapa hebu tueleze kuhusu haya magari ya Rais.
Mnyitafu: Rais ni kweli magari haya yaliingia mwaka 2015 Juni na taratibu zetu za kiforodha ilitakiwa tuyatangaze baada ya siku 21 ili yaweze kuuzwa.
Rais: Mliyatangaza?
Mnyitafu: Bado baada ya kushauriana na uongozi…
Rais: Mlishauriana na uongozi gani? Nataka jibu ndiyo maana nimewaita viongozi wote hapa.
Mnyitafu: Uongozi wa mamlaka wa wakati huo, tukashauriana, lakini sikuwepo wakati huo.
Rais: Nani ulimhusisha kwenye uongozi ule taja tu majina.
Mnyitafu: Sikuwepo.
Rais: Ulijuaje kama walishauriana wakati hukuwepo?
Mnyitafu: Nilivyouliza kwa wenzangu ambao…
Rais: Nani jina lake?
Mnyitafu: Maofisa ambao wapo bandarini.
Rais: Ulimuuliza nani, taja jina lake?
Mnyitafu: Meneja wa bandari ambaye yupo sasa hivi. Hata hivyo yeye ni mgeni anasema aliambiwa.
Rais: Nataka uwe muwazi, wewe si msomi bwana? Mimi mpaka kuja hapa nina taarifa nyingi ndiyo maana nataka uwe wazi ili nijue. Si umemuona mwenzako amesema wazi ofisi yangu ndiyo ilihusika mwaka 2015?
Mnyitafu: Sisi tunaangalia mtu wa kwanza aliyeagiza ambapo inasomeka kama imeagizwa na Ofisi ya Rais.
Rais: Ameshakuja mteja yeyote kufuata magari haya hapa?
Mnyitafu: Hajaja mteja yeyote kuchukua magari haya.
Rais: Ina maana hamjafanya upelelezi wowote kutambua kwamba haya magari ni ya nani?
Mnyitafu: Tuliamini kwamba ni ya Ofisi ya Rais.
Rais: Labda niulize swali jingine. Magari ya polisi yalikuja lini na haya pia yalikuja kipindi gani?
Mnyitafu: Yamekuja mwaka 2015 mwezi Juni.
Rais: Ndiyo maana nauliza magari ya polisi yalikuja mwezi wa sita na haya ya mtu ambaye hajulikani yamekuja Juni huyu hajayachukua? Polisi magari yenu yapo mangapi?
IGP Sirro: Yapo 55.
Rais: Sirro, haya magari 50 ambayo ni ambulance yanawahusu ninyi?
IGP Sirro: Hapana kwa kweli hatuyatambui na hatujui chochote kuhusu magari haya.
Rais: Nani mwingine anayefahamu kuhusu haya magari? Waziri pia hujui chochote.
Profesa Mbarawa: Mimi sijui. Nimepata taarifa leo asubuhi.
Rais: Kwa hiyo tangu mwaka 2015 Juni aliyekuwa mkurugenzi wa pale TPA mpaka ameondoka ndugu (Madeni) Kipande hakutoa taarifa na aliyeingia naye hakutoa taarifa na wewe waziri watu wako wa TRA waliokuwepo na walioko mpaka sasa hivi hawajaeleza kuwa kuna magari hamsini na kitu ambayo yamekaa hapo kwa miaka miwili, ambayo hayana mwenyewe, yameandikwa hapa president’s office wala hata mimi sijaulizwa. Mtu wa PCB, hebu njoo hapa wewe unafahamu kuhusu hili kwa sababu wewe ndiyo mtumiaji na mpelelezi mzuri. Unafahamu chochote kuhusu haya magari?
Mlowola: Kwa sasa sijui chochote mheshimiwa Rais. Ndiyo kwanza nimepata taarifa hii.
Rais: Na wewe ndiyo umepata taarifa hii leo kwa hiyo mtu wako wa PCB anayekaa bandarini naye hajui? Sheria za TRA zinasemaje Mheshimiwa Waziri? Gari linaweza likakaa humu hata miaka 30 mnatunza tu?
Waziri Mpango: Hapana mheshimiwa Rais. Sheria zinaweka ukomo wa muda na baada ya hapo inabidi zinadiwe.
Rais: Sasa kwa nini haya hayajanadiwa wala hayajatangazwa mnada kuanzia mwaka 2015?
Waziri Mpango: Kwa kweli kama nilivyosema sijui labda kamishna wa customs (ushuru) anisaidie kwa idhini yako.
Rais: Kamishna wa customs (ushuru) kwa nini hayajanadiwa au ulipewa rushwa kusudi usinadi ili kusudi siku tutakapokuwa tunatoa magari ya Serikali na haya yatoke?
Kamishna wa Forodha: Hapana mheshimiwa kama nilivyosema kwamba haya magari yaliandikwa ofisi ya Rais na siyo ofisi ya Rais tu kwa Serikali.
Rais: Kwa nini hukuandika barua kuuliza ofisi ya Rais, na Rais yupo.
Mnyitafu: Mheshimiwa tumeunda kikosi kazi kwa sababu ya kupitia magari haya pamoja na mengine. Mengi ambayo yapo bandarini ni matatizo kama haya
Rais: Kwa hiyo yako magari mengi yaliyoandikwa Ofisi ya Rais
Mnyitafu: Hapana, magari ambayo yamepitiliza muda wa kukaa bandarini lakini hayajauzwa.
Rais: Magari ya polisi yamebaki mangapi?
Mnyitafu: Ninayoyafahamu yapo 32 yapo 28 na mengine manne.
Rais: Wewe unayafahamu mangapi?
Kakoko: Yapo ya awamu tatu, ambayo hayajachukuliwa, yaliyochukuliwa zamani, lakini hayo ambayo wamesema wanagawiwa ya awamu tatu yapo kadri 53.
Jina la Waziri Mkuu latumika
Novemba 29 ikiwa ni siku tatu baada ya ziara ya Rais, Waziri Mkuu Majaliwa naye alifika bandarini hapo na kubaini uwapo wa matrela 44 yaliyotaka kutolewa bandarini kwa jina lake.
Tukio hilo lilisababisha kutimuliwa kazi kwa maofisa kadhaa akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Lazaro Twange.
Pia, Majaliwa alimuagiza IGP Sirro kumkamata wakala wa kampuni ya Wallmark anayefahamika kwa jina la Samwel na mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Bahman kutoka kampuni ya NAS kwa tuhuma za kutaka kutoa bandarini magari makubwa 44 ‘semi trailers’ kutoka katika kampuni ya Serini ya Uturuki bila kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
Pia, aliitaka TPA kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha kutoka kwa viongozi wa juu serikalini.
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Waziri Majaliwa alisema Bahman wa kampuni ya NAS alitaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa matrela hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kampuni ya Serin ya Uturuki.
“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka, ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana hajafanya hivyo,” alisema.
Alieleza kuwa kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria; na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Alisema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhoofisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini.
Vichwa vya treni vyakosa mwenyewe
Julai 2, Rais Magufuli alishikwa na mshangao baada kukuta vichwa 13 vya treni vikiwa vimeshushwa bandarini lakini havijulikani ni vya nani. Alikumbana na hali hiyo alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
“Kuna vichwa 13 vya treni vilishushwa hapa lakini havina mwenyewe. Inawezekana vipi vichwa vya treni vinafika hapa bandarini, vinashushwa lakini mwenyewe hajulikani! Ni kwa sababu hakuna ‘coordination’, huo ni mchezo mchafu. Vyombo vya dola vianze kuwachunguza hao,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliendelea kuhoji, kwa nini wahusika hawakuuliza ni vya nani tangu awali ila baada ya meli kuondoka ndipo waulize! “Siku nyingine si watakuja kushusha hata na vifaru au makontena ya sumu,?” alihoji.
Kutoka na hilo, Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano iliiagiza TPA na TRA kuandaa taarifa kuhusu vichwa hivyo.
Sakata la makinikia
Machi 23, Rais Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo akifuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini.
Katika ziara hiyo alikuta makontena 20 ya mchanga wenye madini ambayo yalizuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2.
Kutokana na hali hiyo, alimwagiza aliyekuwa IGP, Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga huo unashikiliwa popote ulipo mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
Siku mbili baadaye, TPA ilizuia makontena 262 yenye mchanga huo yaliyokuwa kwenye bandari hiyo. Makontena hayo yalikuwa na lakiri (seal) za TRA. Kuzuiwa kwake ndio ukawa mwanzo wa Rais kuunda tume kuchunguza biashara ya madini ambako matokeo yake yalisababisha vigogo kadhaa kung’olewa katika nyadhifa zao sambamba na kubadilishwa kwa sheria za madini.

Leicester City pungufu yaiduwaza Manchester United



Klabu ya Manchester United jana Jumamosi usiku imeduwazwa kwa kulazimishwa sare ya goli 2-2 na klabu ya Leicester City waliocheza pungufu uwanjani, kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka England.
Manchester United walionekana kuutawala mchezo huo kuanzia kipindi cha kwanza na ingawaje hadi mapumziko timu zote mbili zilikuwa zimeshafungana goli 1-1, magoli kutoka kwa Jamie Vardy na Juan Mata.
Kipindi cha pili United walianza kuuwasha moto na kufanikiwa kupata goli la pili kupitia kwa Mata kunako dakika ya 60 na watu wengi walijua mchezo ulikuwa umeisha baada ya beki wa Leicester City, Daniel Amartey kulimwa kadi nyekundu.
Leicester wakiwa pungufu walipambana mpaka dakika nne za nyongeza walipofanikiwa kusawazisha goli la pili na kuwaduwaza mashabiki wa Man United.
Kwa matokeo hayo Manchester United bado wamepunguzwa pointi katika mbio za kuusaka ubingwa wa EPL dhidi ya vinara wa Ligi hiyo, Manchester City. Tazama msimamo wa ligi hiyo.

Wagonjwa Wa Homa ya Ini Waongezeka Itigi



DAKTARI wa magonjwa ya ndani ya watu wazima,katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari Itigi,DK.Kazaura Joseph amesema kumekuwa na ongezeko la ugonjwa wa homa ya ini katika Hospitali hiyo ambapo kati ya watu 100,watu wanane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo.
Daktari huyo aliyasema hayo wakati akiongea na kituo hiki alipokuwa akielezea madhara ya ugonjwa wa homa ya ini kwa binadamu katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari,Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida.
Aidha mtaalamu huyo aliweka bayana pia kwamba maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa zaidi ya mara kumi ya maambukizi ya VVU na kwamba kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi hayo, shirika la afya duniani lilitenga julai,28 ya kila mwaka kuwa siku ya homa ya ini duniani(World Hepatitis Day). Kwa mujibu wa Dk.Kazaura sababu zinazochangia kuongeza idadi ya watu wenye maambukizi hayo ni pamoja na njia za maambukizi yake ni rahisi sana ikiwemo kujamiiana,elimu ndogo kwa jamii na imani potofu kuhusu ugonjwa huo.
Kuhusu madhara yanayoweza kuwapata wagonjwa wa ugonjwa huo,daktari huyo aliyataja kuwa ni pamoja na ini kunyauka na kushindwa kufanya kazi,kupata saratani ya ini na kuharibika kwa viungo vingine kama figo.Hata hivyo Dk.Kazaura alisisitiza pia kwamba ili kukabiliana na ugonjwa huo alishauri elimu iendelee kutolewa kwa jamii kuhusu homa ya ini,kuendelea kutoa huduma za upimaji wa homa ya ini bure na kutoa chanjo ya homa ya ini kwa watu wote ambao hawajaambukizwa.
Kutokana na ongezeko hilo Daktari huyo wa magonjwa ya ndani ya watu wazima alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wanaopatwa na ugonjwa huo kuwahi kwenda haraka kwenye huduma za afya ili wapate matibabu.Ushauri mwingine ni jamii kuacha imani potofu kuwa ini linasababishwa na imani za kishirikina na kuongeza kuwa homa ya ini ikifikia kwenye hatua za saratani ya ini hakuna tiba lakini kuna matibabu ya kupunguza kasi ya ugonjwa huo.
Kuhusu watu ambao hawajui hali zao kama wameambukizwa au la,Dk.Kazaura aliwataka watu hao kwenda kwenye vituo vya afya ili kupima homa ya ini na kupatiwa matibabu. Homa ya ini iligunduliwa na Dk.Barack Blumberg mnamo mwaka 1963 na kwamba mwaka 1969 Dk.Brack na wenzake waligundua chanzo cha homa ya ini inayosababishwa na Hepatitis B virus.

Yanya Sc Waanza kazi kombe la Azam Sports Federation Leo



MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wanaanza kampemni yao ya kuwania Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kumenyana na Reha FC ya Daraja la Pili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Yanga itamkosa kocha wake, Mzambia George Lwandamina ambaye ataendelea kuwa kwao, Lusaka kwa muda mrefu kufuatia kufiwa na mtoto wake wa tatu jana, Mofya Lwandamina ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumanne.
Ikumbukwe Lwandamina aliondoka Dar es Salaam wiki iliyopita kwenda nyumbani kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya mwanawe wa kike, Nasanta Lwandamina aliyehitimu Stashahada ya Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha NRDC.
Wakati anajiandaa kurejea nyumbani baada ya hafla ya binti yake kuhitimu masomo NRDC, Lwandamina anakutwa na msiba na mwanawe.
Yanga wanaingia kwenye michuano ya ASFC siku mbili tu baada ya, mahasimu wao, Simba SC kuvuliwa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Warriors juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za leo, Burkina ya Morogoro wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Coastal Union ya Tanga watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Shupavu na Real Moja Moja wakati Villa Squad watacheza na Mtibwa Sugar ya Morogoro.