MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wanaanza kampemni yao ya kuwania Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kumenyana na Reha FC ya Daraja la Pili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Yanga itamkosa kocha wake, Mzambia George Lwandamina ambaye ataendelea kuwa kwao, Lusaka kwa muda mrefu kufuatia kufiwa na mtoto wake wa tatu jana, Mofya Lwandamina ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumanne.
Ikumbukwe Lwandamina aliondoka Dar es Salaam wiki iliyopita kwenda nyumbani kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya mwanawe wa kike, Nasanta Lwandamina aliyehitimu Stashahada ya Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha NRDC.
Wakati anajiandaa kurejea nyumbani baada ya hafla ya binti yake kuhitimu masomo NRDC, Lwandamina anakutwa na msiba na mwanawe.
Yanga wanaingia kwenye michuano ya ASFC siku mbili tu baada ya, mahasimu wao, Simba SC kuvuliwa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Warriors juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za leo, Burkina ya Morogoro wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Coastal Union ya Tanga watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Shupavu na Real Moja Moja wakati Villa Squad watacheza na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
No comments:
Post a Comment