DAKTARI wa magonjwa ya ndani ya watu wazima,katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari Itigi,DK.Kazaura Joseph amesema kumekuwa na ongezeko la ugonjwa wa homa ya ini katika Hospitali hiyo ambapo kati ya watu 100,watu wanane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo.
Daktari huyo aliyasema hayo wakati akiongea na kituo hiki alipokuwa akielezea madhara ya ugonjwa wa homa ya ini kwa binadamu katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari,Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida.
Aidha mtaalamu huyo aliweka bayana pia kwamba maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa zaidi ya mara kumi ya maambukizi ya VVU na kwamba kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi hayo, shirika la afya duniani lilitenga julai,28 ya kila mwaka kuwa siku ya homa ya ini duniani(World Hepatitis Day). Kwa mujibu wa Dk.Kazaura sababu zinazochangia kuongeza idadi ya watu wenye maambukizi hayo ni pamoja na njia za maambukizi yake ni rahisi sana ikiwemo kujamiiana,elimu ndogo kwa jamii na imani potofu kuhusu ugonjwa huo.
Kuhusu madhara yanayoweza kuwapata wagonjwa wa ugonjwa huo,daktari huyo aliyataja kuwa ni pamoja na ini kunyauka na kushindwa kufanya kazi,kupata saratani ya ini na kuharibika kwa viungo vingine kama figo.Hata hivyo Dk.Kazaura alisisitiza pia kwamba ili kukabiliana na ugonjwa huo alishauri elimu iendelee kutolewa kwa jamii kuhusu homa ya ini,kuendelea kutoa huduma za upimaji wa homa ya ini bure na kutoa chanjo ya homa ya ini kwa watu wote ambao hawajaambukizwa.
Kutokana na ongezeko hilo Daktari huyo wa magonjwa ya ndani ya watu wazima alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wanaopatwa na ugonjwa huo kuwahi kwenda haraka kwenye huduma za afya ili wapate matibabu.Ushauri mwingine ni jamii kuacha imani potofu kuwa ini linasababishwa na imani za kishirikina na kuongeza kuwa homa ya ini ikifikia kwenye hatua za saratani ya ini hakuna tiba lakini kuna matibabu ya kupunguza kasi ya ugonjwa huo.
Kuhusu watu ambao hawajui hali zao kama wameambukizwa au la,Dk.Kazaura aliwataka watu hao kwenda kwenye vituo vya afya ili kupima homa ya ini na kupatiwa matibabu. Homa ya ini iligunduliwa na Dk.Barack Blumberg mnamo mwaka 1963 na kwamba mwaka 1969 Dk.Brack na wenzake waligundua chanzo cha homa ya ini inayosababishwa na Hepatitis B virus.
No comments:
Post a Comment