Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Johansen Kahatano amesema kuanzia mwakani wataandaa mkakati wa mabasi kufanya kazi saa 24 na kupandisha nauli wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Kahatano amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 alipozungumza na waandishi wa habari eneo la Ubungo kuhusu hali ya usafiri.
Amesema kumekuwa na changamoto ya usafiri takriban kila mwisho wa mwaka na kusababisha kero kwa abiria.
“Tumeliona hilo na sisi Sumatra tumeandaa mpango ambao tunafikiri unaweza ukawa suluhisho la adha ya usafiri hapa Ubungo; kwanza tunafikiria kuruhusu mabasi kufanya kazi saa 24 wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka,” amesema.
Amesema pia wataweka nauli kubwa wakati wa msimu wa sikukuu ili abiria wasafiri kipindi ambacho nauli itakuwa ndogo.
Kahatano amesema mpango huo utaanza kufanyiwa kazi mwakani kwa kukaa na wadau wa usafiri na wananchi kuujadili.
Akizungumzia hali ya usafiri kituoni Ubungo amesema iko shwari kulinganisha na jana ambapo abiria walikuwa wengi na mabasi yalikuwa machache.
“Tumejitahidi kusaidia kupunguza adha hii kwa leo baada ya kuruhusu watu wenye magari yenye uwezo wa kupakia abiria kuja na kupatiwa vibali hapa Ubungo,” amesema.
No comments:
Post a Comment