Tuesday, 19 December 2017

Airtel yaja na ofa kabambe msimu huu Wa sikukuu



Kampuni ya Simu za Mkononi nchini Airtel imezidi kuonesha ukomavu wake katika kuwaletea wateja wake huduma bomba baada ya sasa kuja na kifurushi cha Smatika ambacho kinaanzia Sh 2,00 hadi Laki moja.
Vifurushi hivyo vimekuja mahususi kwa lengo la kukata kiu ya bando la intaneti kwa watumiaji wa Airtel huku wakiboresha vifurushi hivyo katika msimu huu wa Sikukuu ambapo kifurushi cha MB 50 kwa Sh 250 sasa kitakujia kwa Sh 2,00 ili kwenda sawa na vocha za 2,00 zilizopo lakini kikikupatia bando la MB 40 kwa siku.
Airtel pia imekuja na bando jipya kabisa la Sh 2,000 ambalo litakua na kifurushi chenye ujazo wa GB 3 kwa siku tatu kulinganisha na awali ambapo Sh 2,000 mteja alikuwa akipata kifurushi cha GB 1.3 kwa siku.
Akizungumzia lawama ambazo zimekuwa zikitolewa na wateja wa mtandao huo kuhusu kupunguzwa kwa vifurushi vya mtandao huo, Meneja Masoko Airtel, Aneth Muga alisema wateja wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu kuondolewa kwa vifurushi vya UNI lakini wamesahau kuwa vifurushi hivyo vilikuwa maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo.
“ Ndugu zangu wanahabari Airtel imeendelea kukata kiu ya watumiaji wa mtandao wetu, watu wengi wanalalamika kuwa tumepunguza vifurushi vyetu bila kuangalia kwa undani, mathalani kifurushi cha 250 kilikuwa kikimpatia mteja MB 50 lakini sasa tunatoa MB 40 kwa Sh 200.
“ Ukiangalia hapo huoni utofauti wowote lakini pia kuwa na kifurushi cha Sh 200 kunampa unafuu mteja ambaye ananunua vocha za Sh 200,” alisema Aneth.

Rais Magufuli amwaga Neema Ruvuma



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia wizara ya Nishati, ametoa kiasi cha shilingi bilioni 210 kwaajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Umeme unaojengwa mkoani Ruvuma.
Akiongea katika ziara yake ya siku tatu mkoani Ruvuma Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema Rais Magufuli ametoa fedha hizo kwa kushirikiana na wahisani wengine.
“Mheshimiwa Rais ndio ametoa fedha hizi bilioni 210 kwa kushirikiana na wahisani ambapo bilioni 104 ni kwaajili ya kusambaza umeme katika wilaya zote za mikoa ya Ruvuma na Songea”, amesema Waziri Kalemani.
Mradi huo wa umeme unatarajiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 32,000 katika vijiji 120 vya mikoa hiyo. Waziri ameongeza kuwa mradi huo utawawezesha wananchi kuingiza fedha nyingi kutokana na fursa zitakazojitokeza baada ya kukamilika.
Kalemani amewataka Wakandarasi kumaliza kwa wakati mradi huo kwani tayari wameshapewa fedha zao bila kucheleweshewa. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2018.

Mtulia Kurudi tena Kinondoni



Aliyekuwa Mbunge Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia ambaye amehamia CCM ametangaza nia ya kugombea tena ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Desemba 2 Mtulia amejiuzulu nafasi ya ubunge, huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishiwa mtu yeyote na amebaini Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani iliahidi kuyatekeleza.
Baada ya hatua hiyo, chama cha CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza kuwaomba radhi wapiga kura wa Kinondoni kwa Mtulia kujiuzulu uanachama kisha ubunge.
Lakini leo Jumanne Desemba 19, 2017 kupitia andiko lake alilolituma kwa vyombo vya habari, Mtulia amesema atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa ndani ya CCM ili agombee tena nafasi hiyo.
“Chama changu kikiridhia nitakwenda mbele ya Wanakinondoni kuomba ridhaa ya kuwatumikia katika nafasi ya ubunge kupitia CCM. Pia nawapa pole sana kwa maumivu mliyoyapata kutokana na uamuzi wangu wa kujiuzulu ubunge wa Kinondoni,” amesema Mtulia.
Hata hivyo, Mtulia amewahakikishia wakazi wa Kinondoni kuwa bado anawapenda na yupo tayari kutumikia tena kwa lengo la kuleta maendeleo ya jimbo hilo ambalo awali lilikuwa likishirikiliwa na CCM kwa kipindi cha muda mrefu.

Mambo ya kukumbukwa aliyoyafanya Rais Magufuli Mwaka 2017



RAIS Dk. John Magufuli amefanya mambo mengi ndani ya mwaka huu, lakini haya 10 yatazidi kukumbukwa na Watanzania.
BABU SEYA, PAPII KOCHA
Tukio la kuachiwa kwa wanamuziki Nguza Mbangu Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) lilitangazwa na Rais Magufuli wakati wa maadhimisho ya uhuru, Desemba 9, mwaka huu.
Rais alipotangaza msamaha kwa wanamuziki hao maarufu kuliamsha nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Familia hiyo ilianza kutumikia kifungo cha maisha jela tangu Juni mwaka 2004 kwa kosa la kuwalati wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, jijini Dar es Salaam.
RELI YA KISASA
Tukio la ujenzi wa reli ya kisasa lilikuwa la kipekee kwa nchi yetu kwani Rais Magufuli alizindua rasmi ujenzi wake akasema itasafiri kwa mwendo wa kilomita 160 kwa saa.
Rais alisema Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo imeweza kujenga mradi wa reli kama hiyo kwa fedha zake za ndani.
Ujenzi wake umeanzia Dar es Salaam kwenda Morogoro na utagharimu dola za Marekani bilioni 1.29 na shughuli za ujenzi wa reli hiyo zinaendelea.
TANESCO, WIZARA ZIVUNJWE
Mwaka huu pia, Rais Magufuli alitembelea mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo na kuagiza majengo ya makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Maji yavunjwe.
Alitoa maagizo hayo kutokana na majengo hayo kujengwa ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro.
Majengo ya wizara tayari yamevunjwa na Tanesco inaendelea na mchakato wa ubomoaji.
MABWENI YA UDSM
Jambo jingine ambalo Rais Magufuli atakumbukwa nalo kwa mwaka huu, ni uzinduzi wa majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 na yalijengwa chini ya mwaka mmoja na kugharimu sh. bilioni 10.
Hivi karibuni majengo hayo yaliripotiwa kuwa na nyufa, lakini Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) uliwatoa hofu wanafunzi kuwa hayana tatizo.
KUVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI
Oktoba mwaka huu, Rais Magufuli alivunja Baraza la Mawaziri na kufanya mabadiliko kadhaa.
Katika mabadiliko hayo, aliongeza wizara na mawaziri kutoka 19 hadi 21. Nafasi za manaibu mawaziri ziliongezwa kutoka 16 hadi 21.
Lengo la mabadiliko hayo ilielezwa ni kuleta ufanisi wa kiutendaji serikalini.
DAWA ZA KULEVYA
Alipoingia madarakani alitangaza kiama cha wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na vigogo kadhaa walikamatwa kujihusisha nazo.
Februari mwaka huu, rais alimteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Baada ya uteuzi huo, Sianga alimhakikishia rais kuwa atapambana na dawa hizo hadi ushindi upatikane.
Agosti, mwaka huu, Rais Magufuli alimteua pia Luteni Kanali Frederick Felix Milanzi kuwa Kamishna wa Operesheni wa mamlaka hiyo ili kukoleza vizuri moto wa kukabiliana na dawa hizo nchini.
BANDARINI
Mwaka huu rais alifanya pia ziara ya kushtukiza bandarini na kukuta tena madudu mengine, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake bandarini hapo.
Safari hii alikuta magari 50 yaliyoagizwa nchini na watu wasiojulikana kwa jina la Ofisi ya Rais.
Rais Magufuli alisema magari hayo siri yake ni kubwa kwani yamekaa bandarini tangu Juni mwaka 2015 na yaliletwa pamoja na magari ya serikali.
Akahoji,“inakuwaje rais nipate taarifa za magari kufichwa lakini waziri, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) msijue?”
MADENI YA WALIMU
Desemba mwaka huu, rais alirejesha matumani ya walimu ambao kwa muda mrefu wanasumbukia madai yao bila ufumbuzi.
Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Desemba 14, mwaka huu, mjini Dodoma, aliahidi kulipa takriban sh. bilioni 25 za madeni ya walimu.
“Ninawaahidi walimu wenzangu, mara baada ya uhakiki kuisha wale walimu ambao wanadai malipo halali watalipwa,”alisema.
Alisema kabla hajawa rais alikuwa mwalimu hivyo anazifahamu vizuri shida za walimu hivyo walimu wajisikie wana mwakilishi mzuri.
MADINI
Rais Magufuli aliunda tume mbili kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na wawekezaji tangu walipoanza uzalishaji wa dhahabu nchini.
Ripoti ya kamati ya kwanza ilipotoka ikiongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibaini kasoro za usimamiaji, hivyo rais alimfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kuvunja Bodi ya Uwakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Ripoti ya kamati ya pili iliongozwa na Profesa Nehemia Ossoro ilibaini usafirishaji wa mchanga umepotezea taifa fedha nyingi.
Profesa Ossoro alisema fedha zilizopotea tangu mwaka 1998 ni kati ya sh. trilioni 132 hadi trilioni 380.
BOMBA LA MAFUTA
Mwaka huu ulikuwa pia na tukio la aina yake. Ni uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Bomba litapita mikoa nane, wilaya 24 na vijiji 124 na wakandarasi watatu kutoka nje wanasimamia mradi huo na kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa wananchi wa pande hizo mbili.

Wananchi washerehekea kuuawa kwa Fisi 15



MAMIA ya wakazi wa Kijiji cha Buzanaki kata ya Nyamarimbe katika mkoa wa Geita, wamesherehekea kuuawa kwa fisi 15 hadi jana, katika matukio tofauti wiki moja baada ya mtoto wa miaka sita kuliwa na wanyama hao na wengine watatu kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Yusufu, Martha Musa na Simon Balele walidai marehemu alikamatwa na fisi saa moja jioni Desemba akiwa na watoto wengine wanne ambao baada ya tukio walikimbia na kutoa taarifa.
Desemba 2 mabaki ya mwili wa mtoto Yusufu yalipatikana kijijini hapo yakiwa yamebakia utumbo na mfupa mmoja wa paja ambavyo ndivyo vilivyozikwa kwa heshima ya familia.
Kutokana na tukio hilo, wanakijiji chini ya Mwenyekiti wa Kijiji Robert Maholosha, Ofisa Mtendaji, Rose Paul walitangaza msako wa fisi ulioongozwa na kuratibiwa na Musese Kabulizina ambaye ni ofisa wanyamapori wilaya ya Geita.
Hadi jana fisi 15 walikuwa wameuawa katika matukio tofauti katika kijiji cha Buzanaki fisi 6 na katika kijiji cha Idoselo fisi 9 wameuawa ambako nako wanakijiji watatu walijeruhiwa.
Kwa mujibu wa ofisi ya wanyamapori wilaya ya Geita mwaka 2010 hadi 2014 watu saba waliuawa na fisi huku mwaka 2017 ameuawa mtoto mmoja na wengine watatu kujeruhiwa.
Hata hivyo, tukio la Mei 7 mwaka 2012 lililotokea katika kijiji cha Luezera ndilo lililotisha zaidi kwani baada ya fisi kumkamata mtoto mwenye umri wa miaka 8 saa moja jioni wakati akitoka dukani kununua mafuta ya taa na kutoweka naye kuliibuka sintofahamu kubwa.
Katika tukio hilo, wanakijiji kadhaa walihamasishanana kuwaua watu watatu kwa marungu, mapanga na fimbo wakiwatuhumukuwafuga fisi hao kwa ajili ya ushirikina.
Katika tukio hilo pia wanakijiji hao waliteketeza nyumba 5 za familia tofauti kwa moto huku mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 akijinyonga kwa kuhofia naye kuuawa kwa kipigo na wananchi baada ya kutuhumiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa.
Hata hivyo, Musese Kabulizina, Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ameionya jamii kutoyahusisha matukio ya fisi na imani za kishirikina na badala yake anasema kuwapo kwa fisi wengi katika makazi ya watu ni matokeo ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa wanyamapori wakiwamo fisi kuanza kuvamia makazi ya binadamu kusaka mahitaji kikiwamo chakula.

Watupwa Jela kwa kutumia vibaya madaraka


MAOFISA watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wamehukumiwa kifungo kwenda jela mwaka mmoja na nusu kwa kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.
Waliopata adhabu hiyo walikuwa wajumbe wa bodi ya zabuni ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Kabla ya kuhukumiwa kwenda jela, watumuhiwa hao walikuwa wamepewa adhabu hiyo au kulipa faini ya Sh. milioni 1. 5.
Watumishi hao ni Ramadhani Zongo aliyekuwa ofisa maendeleo ya jamii (amestaafu), Stephen Mayani (ofisa ugavi), Maduhu Magili (mhandisi wa maji), Joachim Leba (ofisa utumishi) na Leonard Batigashaga (ofisa biashara).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya mkoa wa Simiyu, John Mkwabi.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Simiyu, Polycarp Mtega, aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 30 ya 2016 chini ya kifungu cha 31 cha sheria ya makosa ya rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mtega alidai kuwa washtakiwa wote wanatuhumiwa kwa kosa la kubadilisha maamuzi ya timu ya tathmini ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa bwawa katika halmashauri hiyo kinyume cha kifungu cha 75 cha sheria ya manunuzi namba 07 ya mwaka 2011.
Alidai kuwa maofisa hao kwa kujua kuwa wanatenda kinyume cha sheria, walitumia madaraka yao vibaya, kubadilisha mkandarasi aliyepitishwa na timu hiyo katika ujenzi wa bwawa la umwagiliaji lililoko katika Kijiji cha Ikungulyambeshi kwa Sh. bilioni 1.8.
Alisema Mei 7, 2012 maofisa hao wakiwa chini ya Mwenyekiti wa bodi ya zabuni ya halmashauri ambaye ni makamu mwenyekiti pamoja na wajumbe walimbadilisha mkandarasi GAT Engineering Co.Ltd aliyepitishwa na timu ya tathmini, badala yake kumpatia Jossam & Company Ltd kinyume cha utaratibu.
Aliongeza mkandarasi aliyepitishwa na maofisa hao kampuni yake ilikuwa na uwezo wa daraja la tano (v), wakati tangazo la zabuni lilihitaji mkandarasi mwenye darasa la nne hadi moja (1V-1) ambaye alikuwa GAT Engineering Co.Ltd.
Baada ya maelezo hayo, mwendesha mashtaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuacha kutumia madaraka yao vibaya.
Kwa upande wao washtakiwa hao waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia kifungo kutokana na kosa hilo kuwa la kwanza, huku wengine wakidai wana umri mkubwa na wanategemewa na familia zao.
Baada ya utetezi huo, kila mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu au kulipa faini Sh. milioni 1.7. Hata hivyo, wote walipelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa.

CHADEMA yaikosoa CCM



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekosoa kitendo cha CCM kuweka mgombea wake kwenye nafasi ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki wakati haikutakiwa kufanywa hivyo, na kusema kwamba kitendo hicho kitasababisha mgogoro wa kidiplomasia.
Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka kwa chama hiko, imesema CCM imekiuka utaratibu wa Bunge hilo la kumtafuta Spika la kuliongoza kwa kumuweka mtu wao kwenye kinyang'anyiro, wakati kiutaratibu ilitakiwa Spika wa awamu hii atoke nchi ya Rwanda kulingana na mzunguko ambao ulikuwa unafuatwa, na kwamba kitendo hicho kinaweza kuleta migogoro itakayoathiri Jumuiya hiyo kama kipindi cha Idi Amin.
"Awamu hii Spika alipaswa kutoka Rwanda, lakini Tanzania kwa kuwa CCM imezoea kutokuheshimu sheria na kanuni zilizopo imemteua mbunge wake Adam Kimbisa kugombea nafasi ya Spika kinyume kabisa na kanuni za Bunge hilo, na huu ukiwa ni mwendelezo wa utamaduni wao wa kutokuheshimu sheria na kanuni, kitendo ambacho kinatishia ustawi na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki", imeandika Taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa .."CHADEMA tunalaani kitendo hiki, CCM wajue kuwa watabeba lawama zote kama kutakuwa na mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki ambayo unaweza kupelekea mgogoro wa kidiplomasia katika Jumuiya nzima kutokana na tabia yao ya kutoheshimu taratibu zilizowekwa. Ttunataka kanuni za EAC ziheshimiwe, kwani tunakumbuka matendo ya Idd Amin mwaka 1977 yalivyovunja Jumuiya hii, hatutaki

yajirudie kamwe".

BREAKING : Sadifa Apata dhamana



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma iemwachia kwa dhamana aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis (Mbunge) anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa UVCCM Taifa.
Sadifa ameachiwa leo Desemba 19, 2017 baada ya mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa mashtaka ambao waliliwasilisha mahakamani hapo kuweka zuio la kupewa dhamana.
Mtuhumiwa huyo ametakiwa kudhaminiwa na watu watatu pamoja na kusaini bondi ya Tsh. Milioni 1, huku akipewa masharti ya kutosafiri nje ya nchi.

JPM Atoa Onyo Kwa Viongozi Wa Serikali


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wa Serikali na hasa anaowateua kuwaheshimu na kuzingatia maagizo yanayotolewa na viongozi wa chama hicho, vinginevyo atawachukulia hatua.
Dk Magufuli aliitoa kauli hiyo jana mara mbili alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa chama hicho asubuhi na akairudia tena alipokuwa anaufunga usiku.
Katika mkutano huo uliofanyika siku nzima na kuonyeshwa muda wote moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa mkutano huo kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kupigiwa kura zote 1,828 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
“Viongozi wa Serikali wanapaswa kutambua kwamba viongozi wa CCM ndio hasa wanaostahili. Kiongozi wa Serikali wa cheo chochote anawajibika kwa viongozi wa CCM,” alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo.
“Viongozi wa Serikali katika ngazi yoyote watambue kuwa waajiri wetu wakuu ni CCM, mimi bila CCM nisingekuwa Rais, CCM ndiyo kimejadili jina langu. Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM na wenye ilani hiyo ni hawa hapa (wajumbe) nendeni mkawasikilize,” alisema.
Dk Magufuli alionya asijitokeze kiongozi yeyote wa Serikali wa kusema hayajui (mambo) ya CCM.
“Kama mimi Rais niliyewateua ninayajua ya CCM asitokee mtu yoyote akasema hayajui mambo ya chama changu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kauli hiyo isiwavimbishe kichwa viongozi wa CCM na kufanya mambo kinyume wakitegemea uongozi wao ndani ya chama hicho tawala.
“Nataka viongozi wa CCM kuheshimu viongozi wa Serikali na viongozi wa Serikali kuheshimu sana sana sana viongozi wa chama,” alisisitiza.
Achaguliwa kwa kura zote
Katika mkutano huo, Magufuli alichaguliwa kwa kupata kura zote 1,828, huku makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula akichaguliwa kwa kura 1,827. Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akichaguliwa kwa kura 1,819.
Viongozi hao watatu walichaguliwa kwa kupata asilimia 100 ya kura zilizopigwa.
Mkutano huo pia uliwachagua wajumbe 30 wa Halmashauri Kuu (NEC) kati yao 15 kutoka Tanzania Bara na 15 wa Zanzibar.
Miongoni mwa waliochaguliwa ni Stephen Wasira, Jerry Silaa, Dk Fenela Mukangara, Angel Akilimali, Jackson Msome, Dk Ibrahim Msengi, Theresia Mtewele, Mwantumu Zodo, Ernest Sungura, Deougratius Ruta, Burton Kihaka, William Sarakikya, Richard Charles, Anna Msuya na Charles Shanda.
Baadhi ya wajumbe wa Zanzibar ni, Nasri Omary Juma, Pereira Ame Silima, Faidha Juma, Sophia Mziray na Amina Omary.
Mbunge wa upinzani atathminiwa
Akifungua mkutano huo jana asubuhi, Magufuli alisema kuna watu wengi wanataka kurejea katika chama hicho ila wanawafanyia tathmini wasije kupokea mamluki.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa CCM jana, Rais Magufuli alisema hicho ni kimbunga na wataisoma namba.
Alisema katika hamahama hiyo kuna mbunge wa upinzani ambaye amemuomba sana kuhamia CCM akiwa na madiwani wanane.
Kauli ya Rais Magufuli imekuja kukiwa na presha upande wa upinzani baada ya wabunge wawili kuhamia CCM wakiachia majimbo yao.
Wabunge hao walioachia nafasi zao ni aliyekuwa wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia na Dk Godwin Mollel wa Siha (Chadema).
Licha ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo wa majimbo matatu, kuna majimbo matano ambayo yapo wazi yakiwemo mawili ya Kinondoni na Siha ambayo wabunge wao walijiuzulu hivi karibuni. Uchaguzi wa Januari 13 mwakani utahusisha majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido.
Akizungumzia uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 43 Novemba 26, Rais Magufuli alisema CCM ilishinda kata 42.
“Katika tathmini ya uchaguzi huu uliofanyika, CCM inakubalika kwa wananchi, uimara na ukomavu wa chama pia umechagia ushindi kwa kuwa ni kikongwe kimetimiza miaka 40 na kinaongoza dola tangu kuanzishwa kwake,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wameshinda kwa sababu wanaCCM wanao umoja na mshikamano mkubwa.
Uchaguzi ndani ya chama
Rais Magufuli alisema wagombea wengi walijitokeza, hiyo inadhihirisha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho.
Aliwataka wajumbe katika mkutano huo kuchagua kwa umakini bila kuangalia udini, ukabila, ukanda au kutegemea kupata masilahi.
“Nawahakikishia katika uchaguzi huu wagombea watakaobainika wameshinda kwa rushwa hatutasita kutengua ushindi wao,” alisema.
“Rushwa ni adui wa haki niwasihi sana wanaCCM wenzangu msichague mtoa rushwa mchague watu waadilifu, wachapakazi na wenye mapenzi na chama, rushwa inatumaliza,” alisema akifungua mkutano asubuhi.
Amshukuru Kikwete
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na marais wastaafu Rais Magufuli alisema, “Ilifika wakati mtu kama hana fedha hawezi kugombea wala kuchukua fomu namshukuru sana mwenyekiti mstaafu Kikwete (Jakaya) ingekuwa mtu anashinda kwa rushwa nisingepita, namshukuru sana mzee Kikwete.”
Uvunjaji makundi
Rais Magufuli aliwataka wana CCM kuvunja makundi yote yaliyokuwapo akisema, “Uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa, uchaguzi usiwe chanzo cha mifarakano na kuvunjika kwa umoja na mshikamano.”
“Kafanyeni kazi kwa bidii kwa kuwaunga mkono waliochaguliwa, tuvunje makundi yote yalikuwapo wakati wa uchaguzi.”
Alisema chama hicho kamwe hakitamvumilia yeyote atakayeendeleza makundi awe kiongozi aliyechaguliwa au mwanachama wa kawaida aliyeshindwa.
Mageuzi ndani ya CCM
Rais Magufuli alizungumzia mageuzi katika chama hicho akieleza, “Mkutano unafanyika katika mazingira ya kipekee na kufuatia majadiliano ya kina tumefanya mageuzi ya mfumo, muundo na utendaji ili kukirudisha chama kwa wananchi.”
“Mageuzi haya yameleta uadilifu, uwajibikaji wa viongozi na wanachama,” alisema.
Aliongeza kuwa mabadiliko huwa yana changamoto zake, mageuzi yaliyofanyika ni makubwa lazima wasimamie na hasa viongozi ambao wamechaguliwa.
“Viongozi waendelee kusimamia mageuzi kwa kuimarisha na kuongeza idadi ya wanachama,” alisema. “Tunataka ikifika wakati wa uchaguzi washindani wetu wasiambulie chochote.”
Akiba ya fedha
Rais Magufuli alisema Tanzania ina akiba ya fedha za kigeni Dola 5,820.4 milioni za Marekani ambazo zinaweza kulipia bidhaa kwa miezi mitano hata kama Watanzania watakaa bila kufanya kazi kwa muda huo.
Mangula na Kinana wapeta
Akiwazungumzia Philip Mangula na Abdulrahman Kinana, Rais Magufuli alisema wamemsaidia sana akieleza kuwa kuna watu walijua hatamchagua Mangula, wengine wakiwa wanamuita Mangula ni mzee Mugabe.
“Hakuna kazi ya kukitumikia chama bila kutegemea wazee, ni muhimu sana busara zao zinahitajika sana,” alisema.
“Mangula amenisaidia sana mimi ni kijana wakati mwingine nakuwa nachemka, hawa makamu wangu Shein (Dk Ali Mohammed) na Mangula wananisaidia sana. Hawa wazee ni muhimu sana katika kunifanya niwe kiongozi mzuri.”
“Kinana amenisaidia sana kufanya mambo ya mageuzi ndani ya chama na mategemeo yangu makubwa ataendelea kunisaidia sana.”
Akizungumza baada ya Rais Magufuli, Kinana alisema anakubali kuendelea na nafasi hiyo katika chama hicho na kuahidi kuwa atafanya kazi kwa bidii na uaminifu.
“Haiwezekani kumkatalia mwenyekiti wako na Rais wako. Imani huzaa imani na uhakika umenitaka niendelee kuchapa kazi ndani ya chama chetu,” alisema Kinana.
“Kwa kuwa una imani nina uwezo wa kufanya kazi vizuri kauli ni amri, nakuhakikishia nitakitumikia chama changu kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu.”
Akifunga mkutano huo, Mafuguli alisema sekretarieti itaendelea hiyohiyo iliyokuwepo.
amempa uhuru katika baadhi ya maeneo na wakati mwingine akimwambia mambo magumu hucheka, jambo ambalo linampa faraja.
Akizungumzia suala la Rais Magufuli kubadilisha Katiba, alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakibadilisha mambo yaliyofanywa na chama hicho kwa lengo la kumchafua mwenyekiti wa chama hicho.
Alitoa mfano kuwa wapo wanaosema kuwa wamebadilisha Katiba na kwamba Rais Magufuli atakapomaliza kipindi cha miaka mitano hakuna wa kumpinga ataendelea.
“Mimi sijawahi kuona hiyo, wala kwenye mageuzi hayapo lakini hiyo yote ni kutaka kumchafua mwenyekiti, lazima tukatae, msiyakubali ,” alisema.
Kinana alisema katika awamu zote Serikali zilikuwa zikipambana na rushwa lakini tofauti yake ni kwamba kwa awamu hii hatua kali zinachukuliwa papo hapo.
Shibuda, Cheyo wamsifia JPM
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo aliiomba CCM kuongoza vyama vingine kuamini kuwa siasa si vita.
Cheyo alisema hayo akitoa salamu katika mkutano huo akisema anashangazwa na watu ambao wanaamini siasa ni uadui.
Mwanasiasa huyo alianza kwa kauli ya kuwaita CCM ndugu zake, “Najua kuwaita ndugu zangu kesho nitashambuliwa kwenye vyombo vya habari, lakini ukweli ni kwamba mimi ni muumini wa kuwa siasa si uadui.”
“CCM ituongoze kuvifanya vyama vyetu vya siasa visiwe viwanda vya matusi.”
“Niwaambie wenzangu wanaojaribu kushindana na CCM kuwa CCM inatisha. Tusitumie muda mwingi kujaribu kuiangusha. Naomba wenzangu watambue kuwa Tanzania kwanza tuache mchezo wa susiasusia kila wakati.”
Aliongeza kuwa: “Tunaona kazi unayoifanya, tunakuhitaji, endelea kutusukuma kwenye maendeleo.”
Katibu Mkuu wa Ada Tadea na Mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa, John Shibuda alipongeza utendaji kazi wa Magufuli.
Shibuda alitumia fursa hiyo kuomba Sh20 milioni alizosema zinahitajika kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Januari 13.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alimpongeza Rais Magufuli kwa kuwasamehe wafungwa zaidi ya 1,800 katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mrema pia ni mwenyekiti wa bodi ya Parole.

Haya ndo Maajabu aliyoshudia Vanessa Mdee



Malkia wa Bongo Fleva anayefanya vizuri ndani na nje ya nchi, Vanessa Mdee amekiri kushuhudia maajabu ya Mungu baada ya kupitia changamoto miezi ya mwanzo wa mwaka na hatimaye kumaliza mwaka kwa kusaini mkataba mnene na Kampuni ya usambazaji wa muziki 'Univesal Music Group'.
Kupitia ukurasa wake wa Istagram Vanessa ameweka furaha yake na kushangilia na mashabiki wake ambapo amewaambia kwamba huo ni mwanzo tu na kwamba mambo mengine makubwa yapo njiani.
"Nimeona niitumie siku na fursa hii kuwajulisha wapendwa mashabiki zangu mwanzoni mwa mwaka huu. Nilipitia changamoto nyingi Sana. Lakini kwa neema za Mungu. Nilitoka mahali pale na sio kuona baraka tu bali na maajabu mengi yaliyotokea kwenye maisha yangu i kiwemo kuwa mmoja wa familia ya Universal Music Group in a unique joint signing between Universal Music Germany, Airforce1 na Universal Music Group. Vanessa Mdee.
Ameongeza "hii ni mara ya kwanza kwa msanii wa kiafrika kupata deal ya aina hii yenye mkwanja mrefuu sana...Hii ni habari njema kwa mashabiki wangu na ndiyo kwanza tumeanza. Mambo makubwa zaidi yanakuja. Kumbuka kila mwisho wa Jumapili ndiyo mwanzo wa Jumatatu, usiogope kuanza upya"
Vanessa amewashukuru mashabiki zake, ndugu jamaa na marafiki ambao walikuwa pamoja na yeye kuanzia mwaka kuanza japo ulikuwa na changamoto mpaka sasa anbapo mwaka unaelekea kuisha.

Polisi wamshikilia Daktari Feki



Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja kwa kosa la kujifanya daktari, katika hospitali ya mkoa Sekou Toure.
Joseph Mbagata 25,mkazi wa mtaa wa Mabatini jijini humo amekamatwa leo Desemba 18 na jeshi hilo baada ya kubainika kwamba sio mwanataaluma na alikuwa akiwatapeli wagonjwa kwa kuwaomba hongo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Taarifa kutoka kwa jeshi hilo zimesema kwamba mtuhumiwa alikuwa akiwaomba hongo, huku akiahidi kuleta dawa muhimu na pia kufanya mipango ili mgonjwa apate huduma kwa haraka.
Awali zilipatikana taarifa kuwa siku chache zilizopita alionekana mtu aliyevalia mavazi ya udaktari na kujifanya daktari, kisha anapita wodini kuwaona wagonjwa. Pia ilisemekana kuwa mtu huyo tayari amechukua Sh30,000 kwa mgonjwa ili aweze kumpatia matibabu.
Aidha baada ya tuhuma hizo kufika katika uongozi wa hospitali waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa, akiwa amevalia mavazi ya udaktari huku akiwa amesimama nje ya wodi ya upasuaji.
“Tumekuwa tukilalamikiwa kwamba kuna baadhi ya madaktari hapa hawana ujuzi wala hawajitambui, kumbe ni dhahiri kwamba hao watu wapo na kuanzia sasa lazima tufanye ukaguzi wa hali ya juu ili hali hiyo isije ikajitokeza tena maana ni sehemu ya kuhatarisha maisha,” amesema mmoja wa madakatri katika hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa majina.
Baada ya daktari huyo feki kukamatwa, uongozi wa hospitali ulitoa taarifa polisi, ambapo askari walifika eneo la tukio na kumuweka mtuhumiwa chini ya ulinzi kisha kumfanyia upekuzi kwenye begi alilobeba na kukuta mavazi yanayotumiwa na madaktari katika vyumba vya upasuaji.
Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi ametoa wito kwa wananchi hususani wagonjwa waliopo hospitalini akiwaomba kuwa makini na watu ambao ni matapeli wa aina kama hiyo wenye nia ovu dhidi yao.
Aidha pia aliwaomba viongozi wa hospitali zote kuendelea kutoa taarifa kwa polisi kuhusiana na watu wanao watilia shaka hospitalini, ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Moyes asema anauwezo Wa kufundisha timu Yoyote duniani



Meneja wa wagonga nyundo wa London West Ham United David Moyes, amesema uwezo alionao kwa sasa anaweza kuifundisha timu yoyote duniani na anataka kuonesha kama ana uwezo huo akiwa na klabu yake ya West Ham United.
Tangu alipoteuliwa kuwa kocha wa West Ham United Moyes, ameisaidia timu hiyo kutoka katika mstari wa timu zinazotakiwa kushuka daraja kwa kutokufungwa michezo mitatu.
"Nina uwezo wa kufanya kazi hii katika klabu yoyote duniani na nina uhakika nitalifanya hili nikiwa na West Ham," alisema kocha huyo.
Kocha huyo raia wa Scotland mwenye umri wa miaka 54, anajaribu kurudisha heshima yake baada ya kufanya vibaya alipoviongoza vilabu vya Manchester United, Real Sociedad na Sunderland.
West Ham kwa sasa iko nafasi ya kumi na tano katika msimamo wa ligi kuu ya nchini England.

Diwani wa Chadema afunguka kuhama chama kwa masharti




Diwani wa (CHADEMA), Kata ya Sombetini, Ally Bananga amesema yupo tayari kurudi (CCM) ikiwa viongozi wa chama hicho ambao wanataka kumnunua ikiwa watamuonyesha watu waliowatuma kumuua Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.
Mbunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika (kushoto) Diwani wa Sombetini Ally Banaga (Katikati) akiwa na Mstahiki Meya wa Ubungo Mhe. Boniface Jacob (Kulia).
Ally Banaga amedai kuwa yeye yupo tayari kurudi CCM kama viongozi hao watatimiza jambo hilo na kusema hiyo ndiyo itakuwa gharama yake kurudi CCM na siyo fedha au mali kama ambavyo wengine wanadaiwa kupewa.
"Ma CCM wanaotaka kuninunua, leo nataja gharama za kurudi CCM. Nionyesheni mliowatuma kumuuwa Mawazo, nitajiunga nanyi siku hiyo hiyo" alindika Ally Banaga
Aidha Banaga ameonyesha masikitiko yake makubwa kwa watu ambao wanakisaliti chama hicho na kusema kuwa wamesahau kuna watu kama kina Mawazo ambao wamekufa wakikipigania chama hicho.
"Nilishika jeneza lako nikikuangalia mwamba umelala. Ndipo nilipoamini kuwa sio stori, mwanaume wa kweli uliyefia vitani ukikitetea chama ambacho kuna Mambwa Koko yanakisaliti, yanakichezea yanakinajisi bila kuhisi maumivu yako ulipotoka roho kukipigania. Nilikuita kwangu Dar es Salaam tupumzike baada ya uchaguzi mkuu ambao CCM walikupora kwa nguvu ushindi wako, kaka ukakataa kwa neno moja " Nikiondoka Makanda watakufa moyo, ngoja niwape tafu, Tukutane Dodoma.....dah! Tukakutania Mwanza kwenye jeneza" alisema Banaga
Novemba 14, 2015 aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Busanda kupitia CHADEMA na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita aliuawa kwa kupigwa mapanga na watu wasiojulikana na kupelekea kifo chake.