Aliyekuwa Mbunge Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia ambaye amehamia CCM ametangaza nia ya kugombea tena ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Desemba 2 Mtulia amejiuzulu nafasi ya ubunge, huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishiwa mtu yeyote na amebaini Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani iliahidi kuyatekeleza.
Baada ya hatua hiyo, chama cha CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza kuwaomba radhi wapiga kura wa Kinondoni kwa Mtulia kujiuzulu uanachama kisha ubunge.
Lakini leo Jumanne Desemba 19, 2017 kupitia andiko lake alilolituma kwa vyombo vya habari, Mtulia amesema atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa ndani ya CCM ili agombee tena nafasi hiyo.
“Chama changu kikiridhia nitakwenda mbele ya Wanakinondoni kuomba ridhaa ya kuwatumikia katika nafasi ya ubunge kupitia CCM. Pia nawapa pole sana kwa maumivu mliyoyapata kutokana na uamuzi wangu wa kujiuzulu ubunge wa Kinondoni,” amesema Mtulia.
Hata hivyo, Mtulia amewahakikishia wakazi wa Kinondoni kuwa bado anawapenda na yupo tayari kutumikia tena kwa lengo la kuleta maendeleo ya jimbo hilo ambalo awali lilikuwa likishirikiliwa na CCM kwa kipindi cha muda mrefu.
No comments:
Post a Comment