MAOFISA watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wamehukumiwa kifungo kwenda jela mwaka mmoja na nusu kwa kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.
Waliopata adhabu hiyo walikuwa wajumbe wa bodi ya zabuni ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Kabla ya kuhukumiwa kwenda jela, watumuhiwa hao walikuwa wamepewa adhabu hiyo au kulipa faini ya Sh. milioni 1. 5.
Watumishi hao ni Ramadhani Zongo aliyekuwa ofisa maendeleo ya jamii (amestaafu), Stephen Mayani (ofisa ugavi), Maduhu Magili (mhandisi wa maji), Joachim Leba (ofisa utumishi) na Leonard Batigashaga (ofisa biashara).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya mkoa wa Simiyu, John Mkwabi.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Simiyu, Polycarp Mtega, aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 30 ya 2016 chini ya kifungu cha 31 cha sheria ya makosa ya rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mtega alidai kuwa washtakiwa wote wanatuhumiwa kwa kosa la kubadilisha maamuzi ya timu ya tathmini ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa bwawa katika halmashauri hiyo kinyume cha kifungu cha 75 cha sheria ya manunuzi namba 07 ya mwaka 2011.
Alidai kuwa maofisa hao kwa kujua kuwa wanatenda kinyume cha sheria, walitumia madaraka yao vibaya, kubadilisha mkandarasi aliyepitishwa na timu hiyo katika ujenzi wa bwawa la umwagiliaji lililoko katika Kijiji cha Ikungulyambeshi kwa Sh. bilioni 1.8.
Alisema Mei 7, 2012 maofisa hao wakiwa chini ya Mwenyekiti wa bodi ya zabuni ya halmashauri ambaye ni makamu mwenyekiti pamoja na wajumbe walimbadilisha mkandarasi GAT Engineering Co.Ltd aliyepitishwa na timu ya tathmini, badala yake kumpatia Jossam & Company Ltd kinyume cha utaratibu.
Aliongeza mkandarasi aliyepitishwa na maofisa hao kampuni yake ilikuwa na uwezo wa daraja la tano (v), wakati tangazo la zabuni lilihitaji mkandarasi mwenye darasa la nne hadi moja (1V-1) ambaye alikuwa GAT Engineering Co.Ltd.
Baada ya maelezo hayo, mwendesha mashtaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuacha kutumia madaraka yao vibaya.
Kwa upande wao washtakiwa hao waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia kifungo kutokana na kosa hilo kuwa la kwanza, huku wengine wakidai wana umri mkubwa na wanategemewa na familia zao.
Baada ya utetezi huo, kila mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu au kulipa faini Sh. milioni 1.7. Hata hivyo, wote walipelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa.
No comments:
Post a Comment