Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wa Serikali na hasa anaowateua kuwaheshimu na kuzingatia maagizo yanayotolewa na viongozi wa chama hicho, vinginevyo atawachukulia hatua.
Dk Magufuli aliitoa kauli hiyo jana mara mbili alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa chama hicho asubuhi na akairudia tena alipokuwa anaufunga usiku.
Katika mkutano huo uliofanyika siku nzima na kuonyeshwa muda wote moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa mkutano huo kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kupigiwa kura zote 1,828 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
“Viongozi wa Serikali wanapaswa kutambua kwamba viongozi wa CCM ndio hasa wanaostahili. Kiongozi wa Serikali wa cheo chochote anawajibika kwa viongozi wa CCM,” alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo.
“Viongozi wa Serikali katika ngazi yoyote watambue kuwa waajiri wetu wakuu ni CCM, mimi bila CCM nisingekuwa Rais, CCM ndiyo kimejadili jina langu. Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM na wenye ilani hiyo ni hawa hapa (wajumbe) nendeni mkawasikilize,” alisema.
Dk Magufuli alionya asijitokeze kiongozi yeyote wa Serikali wa kusema hayajui (mambo) ya CCM.
“Kama mimi Rais niliyewateua ninayajua ya CCM asitokee mtu yoyote akasema hayajui mambo ya chama changu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kauli hiyo isiwavimbishe kichwa viongozi wa CCM na kufanya mambo kinyume wakitegemea uongozi wao ndani ya chama hicho tawala.
“Nataka viongozi wa CCM kuheshimu viongozi wa Serikali na viongozi wa Serikali kuheshimu sana sana sana viongozi wa chama,” alisisitiza.
Achaguliwa kwa kura zote
Katika mkutano huo, Magufuli alichaguliwa kwa kupata kura zote 1,828, huku makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula akichaguliwa kwa kura 1,827. Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akichaguliwa kwa kura 1,819.
Viongozi hao watatu walichaguliwa kwa kupata asilimia 100 ya kura zilizopigwa.
Mkutano huo pia uliwachagua wajumbe 30 wa Halmashauri Kuu (NEC) kati yao 15 kutoka Tanzania Bara na 15 wa Zanzibar.
Miongoni mwa waliochaguliwa ni Stephen Wasira, Jerry Silaa, Dk Fenela Mukangara, Angel Akilimali, Jackson Msome, Dk Ibrahim Msengi, Theresia Mtewele, Mwantumu Zodo, Ernest Sungura, Deougratius Ruta, Burton Kihaka, William Sarakikya, Richard Charles, Anna Msuya na Charles Shanda.
Baadhi ya wajumbe wa Zanzibar ni, Nasri Omary Juma, Pereira Ame Silima, Faidha Juma, Sophia Mziray na Amina Omary.
Mbunge wa upinzani atathminiwa
Akifungua mkutano huo jana asubuhi, Magufuli alisema kuna watu wengi wanataka kurejea katika chama hicho ila wanawafanyia tathmini wasije kupokea mamluki.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa CCM jana, Rais Magufuli alisema hicho ni kimbunga na wataisoma namba.
Alisema katika hamahama hiyo kuna mbunge wa upinzani ambaye amemuomba sana kuhamia CCM akiwa na madiwani wanane.
Kauli ya Rais Magufuli imekuja kukiwa na presha upande wa upinzani baada ya wabunge wawili kuhamia CCM wakiachia majimbo yao.
Wabunge hao walioachia nafasi zao ni aliyekuwa wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia na Dk Godwin Mollel wa Siha (Chadema).
Licha ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo wa majimbo matatu, kuna majimbo matano ambayo yapo wazi yakiwemo mawili ya Kinondoni na Siha ambayo wabunge wao walijiuzulu hivi karibuni. Uchaguzi wa Januari 13 mwakani utahusisha majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido.
Akizungumzia uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 43 Novemba 26, Rais Magufuli alisema CCM ilishinda kata 42.
“Katika tathmini ya uchaguzi huu uliofanyika, CCM inakubalika kwa wananchi, uimara na ukomavu wa chama pia umechagia ushindi kwa kuwa ni kikongwe kimetimiza miaka 40 na kinaongoza dola tangu kuanzishwa kwake,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wameshinda kwa sababu wanaCCM wanao umoja na mshikamano mkubwa.
Uchaguzi ndani ya chama
Rais Magufuli alisema wagombea wengi walijitokeza, hiyo inadhihirisha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho.
Aliwataka wajumbe katika mkutano huo kuchagua kwa umakini bila kuangalia udini, ukabila, ukanda au kutegemea kupata masilahi.
“Nawahakikishia katika uchaguzi huu wagombea watakaobainika wameshinda kwa rushwa hatutasita kutengua ushindi wao,” alisema.
“Rushwa ni adui wa haki niwasihi sana wanaCCM wenzangu msichague mtoa rushwa mchague watu waadilifu, wachapakazi na wenye mapenzi na chama, rushwa inatumaliza,” alisema akifungua mkutano asubuhi.
Amshukuru Kikwete
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na marais wastaafu Rais Magufuli alisema, “Ilifika wakati mtu kama hana fedha hawezi kugombea wala kuchukua fomu namshukuru sana mwenyekiti mstaafu Kikwete (Jakaya) ingekuwa mtu anashinda kwa rushwa nisingepita, namshukuru sana mzee Kikwete.”
Uvunjaji makundi
Rais Magufuli aliwataka wana CCM kuvunja makundi yote yaliyokuwapo akisema, “Uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa, uchaguzi usiwe chanzo cha mifarakano na kuvunjika kwa umoja na mshikamano.”
“Kafanyeni kazi kwa bidii kwa kuwaunga mkono waliochaguliwa, tuvunje makundi yote yalikuwapo wakati wa uchaguzi.”
Alisema chama hicho kamwe hakitamvumilia yeyote atakayeendeleza makundi awe kiongozi aliyechaguliwa au mwanachama wa kawaida aliyeshindwa.
Mageuzi ndani ya CCM
Rais Magufuli alizungumzia mageuzi katika chama hicho akieleza, “Mkutano unafanyika katika mazingira ya kipekee na kufuatia majadiliano ya kina tumefanya mageuzi ya mfumo, muundo na utendaji ili kukirudisha chama kwa wananchi.”
“Mageuzi haya yameleta uadilifu, uwajibikaji wa viongozi na wanachama,” alisema.
Aliongeza kuwa mabadiliko huwa yana changamoto zake, mageuzi yaliyofanyika ni makubwa lazima wasimamie na hasa viongozi ambao wamechaguliwa.
“Viongozi waendelee kusimamia mageuzi kwa kuimarisha na kuongeza idadi ya wanachama,” alisema. “Tunataka ikifika wakati wa uchaguzi washindani wetu wasiambulie chochote.”
Akiba ya fedha
Rais Magufuli alisema Tanzania ina akiba ya fedha za kigeni Dola 5,820.4 milioni za Marekani ambazo zinaweza kulipia bidhaa kwa miezi mitano hata kama Watanzania watakaa bila kufanya kazi kwa muda huo.
Mangula na Kinana wapeta
Akiwazungumzia Philip Mangula na Abdulrahman Kinana, Rais Magufuli alisema wamemsaidia sana akieleza kuwa kuna watu walijua hatamchagua Mangula, wengine wakiwa wanamuita Mangula ni mzee Mugabe.
“Hakuna kazi ya kukitumikia chama bila kutegemea wazee, ni muhimu sana busara zao zinahitajika sana,” alisema.
“Mangula amenisaidia sana mimi ni kijana wakati mwingine nakuwa nachemka, hawa makamu wangu Shein (Dk Ali Mohammed) na Mangula wananisaidia sana. Hawa wazee ni muhimu sana katika kunifanya niwe kiongozi mzuri.”
“Kinana amenisaidia sana kufanya mambo ya mageuzi ndani ya chama na mategemeo yangu makubwa ataendelea kunisaidia sana.”
Akizungumza baada ya Rais Magufuli, Kinana alisema anakubali kuendelea na nafasi hiyo katika chama hicho na kuahidi kuwa atafanya kazi kwa bidii na uaminifu.
“Haiwezekani kumkatalia mwenyekiti wako na Rais wako. Imani huzaa imani na uhakika umenitaka niendelee kuchapa kazi ndani ya chama chetu,” alisema Kinana.
“Kwa kuwa una imani nina uwezo wa kufanya kazi vizuri kauli ni amri, nakuhakikishia nitakitumikia chama changu kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu.”
Akifunga mkutano huo, Mafuguli alisema sekretarieti itaendelea hiyohiyo iliyokuwepo.
amempa uhuru katika baadhi ya maeneo na wakati mwingine akimwambia mambo magumu hucheka, jambo ambalo linampa faraja.
Akizungumzia suala la Rais Magufuli kubadilisha Katiba, alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakibadilisha mambo yaliyofanywa na chama hicho kwa lengo la kumchafua mwenyekiti wa chama hicho.
Alitoa mfano kuwa wapo wanaosema kuwa wamebadilisha Katiba na kwamba Rais Magufuli atakapomaliza kipindi cha miaka mitano hakuna wa kumpinga ataendelea.
“Mimi sijawahi kuona hiyo, wala kwenye mageuzi hayapo lakini hiyo yote ni kutaka kumchafua mwenyekiti, lazima tukatae, msiyakubali ,” alisema.
Kinana alisema katika awamu zote Serikali zilikuwa zikipambana na rushwa lakini tofauti yake ni kwamba kwa awamu hii hatua kali zinachukuliwa papo hapo.
Shibuda, Cheyo wamsifia JPM
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo aliiomba CCM kuongoza vyama vingine kuamini kuwa siasa si vita.
Cheyo alisema hayo akitoa salamu katika mkutano huo akisema anashangazwa na watu ambao wanaamini siasa ni uadui.
Mwanasiasa huyo alianza kwa kauli ya kuwaita CCM ndugu zake, “Najua kuwaita ndugu zangu kesho nitashambuliwa kwenye vyombo vya habari, lakini ukweli ni kwamba mimi ni muumini wa kuwa siasa si uadui.”
“CCM ituongoze kuvifanya vyama vyetu vya siasa visiwe viwanda vya matusi.”
“Niwaambie wenzangu wanaojaribu kushindana na CCM kuwa CCM inatisha. Tusitumie muda mwingi kujaribu kuiangusha. Naomba wenzangu watambue kuwa Tanzania kwanza tuache mchezo wa susiasusia kila wakati.”
Aliongeza kuwa: “Tunaona kazi unayoifanya, tunakuhitaji, endelea kutusukuma kwenye maendeleo.”
Katibu Mkuu wa Ada Tadea na Mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa, John Shibuda alipongeza utendaji kazi wa Magufuli.
Shibuda alitumia fursa hiyo kuomba Sh20 milioni alizosema zinahitajika kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Januari 13.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alimpongeza Rais Magufuli kwa kuwasamehe wafungwa zaidi ya 1,800 katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mrema pia ni mwenyekiti wa bodi ya Parole.
No comments:
Post a Comment