Tuesday, 12 December 2017

Atiwa mbaroni kwa kubaka watoto wanne



JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, linamshikilia kijana wa miaka 30 kwa tuhuma za kuwabaka watoto wanne, wawili wa familia moja.

Tukio hilo limeripotiwa Desemba 8, mwaka huu, huko Muyuni A, Mkoa wa kusini Unguja na mtuhumiwa huyo anadiwa kuwabaka na kuwalawiti watoto hao ambao ni chini ya umri wa miaka 18.

Kamanda wa Polisi mkoa huo, Makarani Khamis, alisema hapo awali mtuhumiwa  huyo alidaiwa kuwabaka watoto saba, lakini baada ya uchunguzi wa daktari ulibainika kuwa ni watoto wanne ndio walioharibiwa na watatu wakiwa salama.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi seremala alidaiwa kuwafanyia matukio hayo watoto hao kwa siku na nyakati tofauti.

Alisema mtuhumiwa yupo ndani kwa hatua za kiupelelezi na zitapokamilika atafikishwa katika vyombo vingine vya kisheria kwa hatua zaidi.

Aliitaka jamii isiwe mbali na watoto wao kutokana na matukio ya udhalilishaji wanaofanyiwa watoto siku hadi siku.

Aidha, aliwashauri wazazi na walezi kufuatilia nyendo za watoto wao na kuhakikisha wanawaogesha badala ya kuwaacha waoge wenyewe ili kama ana majeraha aweze kugundua mapema.

Watoto hao walitambuliwa kuwa wanafanyiwa vitendo hivyo baada ya mmoja ya wazazi wa watoto hao kumgundua mwanawe akiwa anaharufu mbaya na alipomuhoji ndipo alipomtaja mtuhumiwa huyo.

Baada ya kumuhoji mtoto wake alimtaja mtuhumiwa huyo na kuwataja watoto wenzake ambao wamekuwa wakifanywa na mtuhumiwa huyo na kuwapa Sh. 5,000.

Sheha wa Shehia ya Muyuni ‘A’ Maulid Hassan Zidi, alisema baada ya kutokea tukio hilo kuna wananchi wengine zaidi ya saba wanalalamika watoto wao wameharibiwa na mtu huyo, lakini hakuna aliye kwenda kuripoti.

Aliitaka jamii kuripoti matukio hayo yanapotokea badala ya kulalamika mitaani kwani kufanya hivyo kunachangia watendaji wa makosa hayo kuendelea kuyafanya.Sheha huyo alisema katika shehia yake hilo ni tukio la kwanza kutokea ndani ya mwaka huu, lakini huko nyuma kuna matukio kama hayo yalitokea na watuhumiwa wapo mitaani ndio kinachowafanya wananchi kushindwa kuripoti matukio hayo.

Mbowe ameitaka Serikali kutoa tamko kuhusu Azory


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali kutoa tamko kuhusu aliko mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Azory Gwanda.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mbowe alisema kitendo cha Serikali kukaa kimya kinaleta wasiwasi kwa ndugu na jamii ya wanahabari.

“Sasa ni wiki ya tatu tangu Azory ametoweka nyumbani kwake, lakini Serikali haijatoa tamko lolote, hatuelewi nini kimemtokea,” alisema.

Azory (42), anayefanya kazi za uandishi wa habari Kibiti na Rufiji mkoani Pwani ametimiza siku 22 tangu atoweke kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Novemba 21.

Mbowe alisema kumekuwa na matukio ya kutisha kama watu kupotea na maiti kuokotwa zikiwa zimefungwa kwenye mifuko hali ambayo inawatia wasiwasi wananchi.

“Tunaomba vyombo vya dola kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika ili kufahamu aliko mwandishi huyo,” alisema.

Mbali ya wito huo, mwenyekiti wa Baraza Kuu la CUF, Julius Mtatiro alisema kufungia vyombo vya habari kwa sababu vimekosea kuandika takwimu si halali.

Alisema makosa ya takwimu yanatakiwa kusahihishwa lakini si kukifungia chombo cha habari kwa kuwa madhara yake ni watu kukosa ajira hata ambao hawakuhusika moja kwa moja na makosa yaliyofanywa.


Dully Sykse atokwa povu kisa Bombardier



Mkongwe wa Bongo Fleva nchini, Dully Sykse.

ETI kisa Bombardier! Mkongwe wa Bongo Fleva nchini, Dully Sykse ametoa povu ikiwemo kutangaza vita na wasanii wa kizazi kipya kwa sababu ya kushindwa kumsapoti kwenye wimbo wake mpya.

Dully Sykes ambaye ameachia wimbo mpya wa Bombardier, alisema wasanii wa sasa ambao wengi ni wapya wana roho mbaya na yeye yuko tayari kupambana nao.

“Wasanii wa sasa wana roho mbaya, hawasapotiani kama wasanii wa zamani, ndiyo maana Bombadier yangu hawajanisaidia kuitangaz, hiyo inaonesha muziki ni vita na mimi niko tayari kupambana nao,” alisema Dully

Wasomi vyuo vikuu watakiwa kumuunga mkono Rais JPM



Ben Kinyaiya anatarajia kusogeza jiko



MTANGAZAJI maarufu Bongo, Ben Kinyaiya amefunguka kuwa anatarajia rasmi kuvuta jiko.

Kinyaiya aliiambia Full Shangwe kuwa, Mungu akijalia hivi karibuni atauaga ukapera rasmi kwa kufunga ndoa na mwenza wake ambaye hakutaka kumuanika wazi.

“Unajua ndoa ni mapenzi ya Mungu, kama mwanadamu sina mamlaka kihivyo, ila Mungu akijalia ‘soon’ ninafunga ndoa na mwandani wangu,”alisema Kinyaiya.

Mzee aliepata msamaha wa Rais Magufuli atoa ya moyoni



Mzee Mganga Matonya (kulia) akisalimiana na ndugu na jamaa zake walipomtembelea nyumbani kwake baada ya kutoka gerezani

       Dar es Salaam. Rais John Magufuli alishangaza wengi alipotaja jina la mfungwa aitwaye Mganga Matonya, mwenye umri wa miaka 85, wakati akitangaza msamaha kwa watu 61 waliohukumiwa kunyongwa na mmoja aliyekuwa na kifungo cha maisha.

Haikuwa kitu cha kawaida kwa mkuu wa nchi kutaja jina la mfungwa, lakini ni mwendelezo wa maajabu yaliyowahi kumkuta Matonya katika maisha yake ya gerezani. Mara ya kwanza alifutiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

“Namshukuru sana  Rais Magufuli,” alisema Matonya alipoongea na mwandishi wetu jana akiwa kijijini kwake Wiliko mkoani Dodoma.

“Sikutegemea kama nitatoka gerezani. Naomba salamu zimfikie kwani sijui namna ya kuonana naye. Ningebahatika kuonana naye siku ile nilipotoka gerezani, ningemkumbatia kwa furaha.”

Matonya alipata taarifa za msamaha akiwa gereza la Kingolwira mkoani Morogoro, lakini awali alikuwa Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa mahabusu baada ya kufanya kosa akiwa na umri wa miaka 39. Aliishi Isanga hadi Mei 10, 1980 wakati alipohukumiwa.

“Hakimu aliamuru ninyongwe mpaka kufa. Wakati nasubiri utekelezaji wa hatua hiyo mwaka 1984, rais wa  wakati huo, Julius Nyerere alinibadilishia adhabu kutoka kunyongwa hadi kifungo cha maisha,” alisema Matonya.

Baada ya kuhukumiwa kunyongwa, Matonya na mwenzake walisubiri kifo kwa miaka mitano, lakini mabadiliko ya tabia waliyoonyesha wakiwa gerezani yalishawishi wasimamizi wao wapendekeze majina yao ili wabadilishiwe adhabu.

Baada ya Rais Nyerere kuwapunguzia adhabu hiyo, wawili hao walihamishwa kutoka Gereza la Isanga mkoani Dodoma na kwenda Kingolwira mkoani Morogoro.

Anasema hakuwahi kufikiria kuwa kuna siku angetoka gerezani, zaidi ya kujipa matumani na kumuomba Mwenyezi Mungu amnusuru na adhabu ya kufia ndani ya kuta za majengo hayo.

Jana ilikuwa siku ya furaha kwa Matonya, familia yake, ndugu na wanakijiji wa Wiliko, kijiji ambacho kiko takriban kilomita 85 kutoka Dodoma Mjini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Matonya alionyesha furaha, mwenye kutafuta maneno asijue la kusema zaidi ya shukrani nyingi kwa Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kumsamehe adhabu ambayo ni nadra kunusurika isipokuwa kwa kushindana kisheria.

“Natamani kuonana na Rais Magufuli na kuongea naye mambo mbalimbali, lakini sina uwezo,” alisema Matonya.

“Lakini kupitia gazeti hili naamini ujumbe utamfikia. Kwa kweli, namshukuru sana kwa hili.”

Pamoja na Rais kumtaja jina, Matonya anasena hakuwa anafahamu lolote kuhusu msamaha huo.

“Taarifa zilinifikia ghafla,” alisema.

“Siku hiyo nilikuwa nimepumzika gerezani na wenzangu walikuwa wanaangalia televisheni. Mara nikasikia wenzangu wakiniita. ‘Mzee Matonya, Mzee Matonya. Njoo uone huku jina lako limetajwa na Rais Magufuli kuwa umeachiwa huru’.

“Sikuamini na sikula chakula kwa furaha niliyokuwa nayo.”

Kosa mpaka kufungwa

Matonya na mwenzake anayeitwa Myeya Nyagalo walikamatwa Oktoba 1974 wakati walipoenda kuuza ng’ombe wa wizi kwenye mnada katika Kijiji cha Nyang’oro kilichopo kati ya Iringa na Dodoma. Walikuwa wamemuua mwenye mifugo hiyo kwa mkuki wakati wakiiba na hivyo walikuwa wanasakwa hadi walipoibuka mnadani.

Matonya na Nyagalo walikuwa miongoni mwa watu 12 walioorodheshwa kuwa walihusika katika mauaji hayo.

Akikumbuka tukio hilo, Matonya alisema wakati huo alikuwa kijana na mwenye tabia ya wizi wa mifugo.

Anasema siku alipofanya kosa hilo, alikuwa na Nyagalo na vijana wengine wawili wa kabila la Kimasai walioshirikiana kuiba ng’ombe hao.

“Tuliandaa mpango wa kujiongezea mifugo. Baada ya kujiridhisha wapi tunaenda kuiba mifugo hiyo, tuliamua kwenda,” alisema Matonya.

“Haikuwa mara yetu ya kwanza. tulishafanya matukio kama hayo maeneo mengine. Lakini, kwa hili, arobaini za mwizi zilikuwa zimefika. Tulipata upinzani mkubwa uliosababisha mapigano na kifo cha mwenye mali.

“Mimi na mwenzangu Nyagalo hatukufahamu kama mtu yule amefariki. Tulijua tumemjeruhi tu.”

Alisema wenzao walifahamu kwamba mwenye mali hangepona. Alisema tofauti na matukio ya awali, wenzao walitaka wagawane mifugo waliyoiba na kila mmoja ashike njia zake.

“Tulishangaa, lakini mwisho wa siku tuligawana, tukaachana,” alisema.

Alisema baada ya muda hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kupeleka mifugo mnadani kuiuza bila kujali kama Jeshi la Polisi lilikuwa linawatafuta. Ndio maana walikamatwa kirahisi.

Familia ya Matonya

Leo hii, Matonya amerejea mtaani ambako ana watoto sita, wajukuu 33 na vitukuu ambao idadi yake haikuweza kupatikana mara moja. Lakini alimuacha mkewe akiwa na watoto wawili na ujauzito wa miezi nane, hivyo watoto waliozaliwa wakati akiwa jela wanahesabika kuwa wake.

Kama ilivyokuwa kwa Nguza Mbangu Vicking na mwanae Papii Kocha waliotoka gerezani saa chache baada ya kutangaziwa msamaha, ndivyo ilivyokuwa kwa Matonya na mwenzake waliotoka gerezani juzi.

Mzee Matonya alisema anaangalia uwezekano wa kujikita kwenye kilimo, shughuli aliyokuwa akiifanya kabla ya kuhukumiwa, lakini anasema umri ushaenda.

Baada ya kuishi gerezani mwezi mmoja, alizaliwa mtoto ambaye mkewe alimuita Aron (45) ambaye akiwa shule ya msingi, alikuwa akipokea barua za baba yake kutoka kwa wafungwa waliokuwa wanamaliza kutumikia adhabu zao au mahabusu walioshinda kesi.

Aron ambaye kwa sasa ni baba wa watoto wanne na wajukuu, alisema alijisikia furaha baada ya kupata taarifa za kuachiwa kwa baba yake kwa kuwa hakuamini kama angekuwa huru tena.

“Tulikataa tamaa kama Mzee angetoka gerezani,” alisema Aron.

“Niliwahi kwenda kumuona mara nne na mwisho ilikuwa ni mwaka 2014. Ninapozungumza naye. Najisikia furaha iliyopitiliza. Kila mtu hapa kijijini haamini kilichotokea,” alisema Aron.

Baada ya kuongezeka kwa mzee wao, Aron anasema watu hawakauki nyumbani kwao kwa kuwa kila mtu anataka kumuona na kumshika mkono. Hapo nyumbani, anasema watu hawalali, wanashangilia huku wengine wakifanya maombi  ya kumshukuru Mungu na Rais Magufuli aliyempa msahama.

Source: Mwananchi

Waziri Jafo ampa wiki sita Mkandarasi wa mradi wa maji Muheza



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mh. Selemani Jafo amempa wiki sita Mkandarasi wa mradi wa maji wa Kivindo Wilayani Muheza mkoani Tanga, kuhakikisha anakamilisha mradi huo na uanze kutoa huduma.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Muheza,  ambapo alikagua miradi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo ukiwemo mradi huo wa maji.

“Sitegemei kusikia sababu zozote zitakazofanya mradi huu usikamilike ndani ya wiki sita, ni mategemeo yangu wananchi wataanza kufaidi matunda ya mradi huu baada ya muda mfupi tu kuanzia sasa, Mkandarasi fanya kazi yako” amesema Jafo.

Aidha Waziri Jafo alimtaka Mkandarasi wa Mradi huo ambao umefikia asilimia 90 ya utekelezaji wake kuwaahidi wananchi kuwa ataukamilisha ndani ya muda wa wiki sita ambao amepewa na waziri.

Mbali na mradi huo wa maji wa Kivindo pia Waziri Jafo amefanikiwa kutembelea Miradi ya afya na
 elimu katika kituo cha afya Mkuzi na Ubwari pamoja na kutembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kilulu.

elimu katika kituo cha afya Mkuzi na Ubwari pamoja na kutembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kilulu.

Hili ndilo Kombora jipya la korea Kaskazini Linaloweza Kuitandika Marekani


Korea Kaskazini imetoa picha za jaribio la kombora lake jipya ambalo inadai kuwa linaweza kushambulia popote pale nchini Marekani.

Picha hizo zinaonyesha kiongozi wa Korea Kaskazini Ki Jong un na maafisa wengine kadha ya ngazi za juu jeshini wakisherehekea kombora la Hwasong-15 wakati likipaa.

Wengi wameshangazwa na ukubwa wa kombora hilo. Picha hii ambayo haijulikanai ilichukuliwa lini na iliyotolewa na vyombo vya habari vya taifa inaonyesha Kim akilikagua kombora hilo.

Michael Duitsman, mtafiti katika kituo kimoja alisema kuwa kombora hilo ni kubwa kuliko kombora la kwanza la Hwasong-14 "ni nchi chache tu zinaweza kuunda kombora kama hilo na Korea Kaskazini imejiunga nazo."

Pia linaonekana kuwa na kichwa kikubwa ikimaanisha kuwa linaweza kubeba bomu zito la nyuklia kwenye kichwa chake.

Yote haya yanaashiria kuwa kombora hilo lina uwezo kwa kusafirisha bomu la nyuklia kwa muda mrefu.

Lilisherehekewa kwa sigara

Kim mwenye furaha anaonekana akicheka kwa furaha  wakati kombora hilo linapaa. Linaaminiwa kuwa kombora la kwanza la Korea Kaskazini lililopaa mbali zaidi katika kilomita 4,475.

Bw Kim na wenzake walionekana wakisherehekea  mafanikio ya jaribio hilo kwa sigara.

Credit: BBC


Askari wa usalama Barabarani wazuia magari zaid ya 10 kusafiri




Dar es Salaam. Askari wa usalama barabarani wamezuia magari zaidi ya 10 kufanya safari za mikoani kwa ajili ya ukaguzi katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Usalama Barabarani Ubungo, Said Ibrahimu akizungumza na MCL Digital leo Jumanne Desemba 12,2017 amesema wanaendelea na ukaguzi na kwamba magari yaliyozuiwa ni mabovu.

Katika kituo hicho idadi ya abiria imeongezeka ikielezwa ni kutokana na sherehe za mwishoni mwa mwaka.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) jana Jumatatu Desemba 11,2017 kupitia taarifa kwa umma imetangaza kutoa leseni za muda mfupi katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

Sumatra imewaalika wamiliki wenye mabasi ya ziada kuwasilisha maombi ya leseni za muda mfupi kwa ajili ya kuongeza huduma katika njia za mikoani zenye mahitaji zaidi kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Mamlaka hiyo pia imewakumbusha wananchi wanaotarajia kusafiri kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kupanga safari mapema ili kuepusha usumbufu unaotokana na changamoto za usafiri.

Ofisa Mtendaji Mkuu NMG kujiuzulu



  Dar es Salaam. Bodi ya kampuni ya Nation Media Group (NMG) imetangaza kujiuzulu kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Joseph Muganda kuanzia Januari 31, 2018.

Taarifa iliyotolewa jana na mwenyekiti wa Bodi ya NMG, Wilfred Kiboro inaeleza kuwa kutokana na kuondoka kwake, Mkurugenzi wa Fedha wa NMG, Stephen Gitagama atakaimu nafasi hiyo wakati bodi ikitafuta mtu atakayemrithi Muganda.

Muganda alijiunga na NMG Julai, 2015 na amefanikiwa kuongoza mkakati wa kuifanya kampuni ikue vizuri katika safari mpya ya kidigitali.

“Muganda ameongoza kwa ujasiri kutathmini biashara ya bidhaa zetu, ameongoza kufanya mageuzi ya kimfumo na kuielekeza tena kampuni katika kutumia fursa zilizojitokeza kutokana na mitandao ya jamii kuvuruga sekta ya habari,” anasema Kiboro katika taarifa yake.

“Ataiacha kampuni ikiwa inawaelewa wateja na iliyobadilika kwa haraka na ambayo mafanikio yake kibiashara tayari ni dhahiri kwa kuangalia matarajio ya faida kutokana na uwekezaji katika mikakati ya kidigitali. Tunamtakia mafanikio katika mipango yake ya baadaye.”

Kiboro amewahakikishia wanahisa na wadau wote wa NMG na umma kwamba kwamba kipindi cha mpito cha mabadiliko ya uongozi hakitakuwa na matatizo na kitafanyika kwa haraka.

NMG, ambayo inamilikiwa na umma, ni kampuni yenye mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na inajivunia mafanikio ya kidigitali, ikiwa na watu milioni 30 wanaotembelea kurasa zake.

NMG inachapisha magazeti ya Nation na Taifa Leo nchini Kenya, The EastAfrican ambalo ni la kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Daily Monitor la Uganda, na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ya Tanzania na pia matoleo ya kielektroniki.

Pia inamiliki vituo vya televisheni vya NTV Kenya, na NTV na Spark pamoja na vituo vya redio vya KFM na Dembe nchini Uganda. Pia inamiliki kituo cha redio cha Nation FM cha Kenya.

NMG imejisajili katika masoko ya hisa ya Kampala, Dar es Salaam na Kigali.

Idara ya Uhamiaji yamuhoji Askofu wa Katoliki kuhusu uraia wake



Askofu Severine Niwemugizi.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, Severine Niwemugizi (61), amehojiwa na Idara ya Uhamiaji kuhusiana na uraia wake. Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Askofu Niwemugizi alisema mara ya kwanza alihojiwa Novemba 28 mwaka huu na mara ya pili alihojiwa Desemba 4, mwaka huu.

“Mara ya kwanza niliitwa na kufika ofisi za uhamiaji Ngara, Novemba 28 na mara ya pili niliitwa Desemba 4.

“Niliombwa kibali kinachoniruhusu kuwa nchini, nikashangaa, nikasema mimi ni Mtanzania, nikaambiwa nilete document (nyaraka).

“Nilipeleka hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa, wakasema wataniita tena.

“Baada ya kuitwa mara ya pili, nilipewa fomu ya kujaza ambayo bado naendelea kuijaza hadi sasa.

“Waliniita tena wakasema bado wanataka kujiridhisha ndio maana wanataka nijaze fomu,
ninaendelea kuifanyia kazi mpaka nitakapokuwa nimeikamilisha yote,” alisema Askofu Niwemugizi ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC).

Mahojiano kati yake na Mwandishi wa Mtanzania yalikuwa hivi.

Swali: Je, ulizaliwa wapi?

Jibu: Nilizaliwa katika Kitongoji cha Kayanza, Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo, Wilaya ya Biharamulo.

Swali: Ulizaliwa tarehe ngapi?

Jibu: Nilizaliwa Juni 3, mwaka 1956.

Swali: Ulibatizwa wapi?

Jibu: Nilibatizwa katika Parokia ya Katoke, Biharamulo.

Swali: Elimu ya Msingi na Sekondari ulisoma wapi?

Jibu: Nilisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo na Shule ya Sekondari Nyakato Bukoba (O-level).

Baada ya kumaliza ‘O-level’ niliingia Seminari Kuu ya Ntungamo Bukoba halafu nikatoka hapo nikaenda Kipalapala Tabora.

Swali: Wazazi wako walizaliwa wapi?

Jibu: Walizaliwa sehemu mbalimbali, mama alizaliwa Lusahunga na baba alizaliwa katika Tarafa ya Nyarubungo, Kijiji cha Kabukome Kitongoji cha Kayanza.

Swali: Katika maisha yako yote je, ulishawahi kuhisiwa kuhusu uraia wako?

Jibu: Sijawahi kuulizwa, muda wote nimetumia passport (hati ya kusafiria) ya Tanzania na hakuna aliyewahi kuniuliza suala la uraia.

Swali: Je, unafikiri kwanini hili linajitokeza sasa?

Jibu: Baada ya hivi karibuni kutoa ushauri, kwamba ni vizuri mchakato wa Katiba ukarejewa, watu wali-react, sasa naweza kupata picha nini kimesababisha nianze kuhojiwa.

Swali: Je, Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC) wana taarifa kwamba umeitwa uhamiaji?
Jibu: Sijawataarifu kwa sababu suala hili lilionekana bado liko chini chini, lakini nafikiri nitatafuta namna ya kuwafahamisha juu ya jambo hili.

Swali: Je, mbali na kuwa Askofu, uliwahi kushika nafasi gani katika Kanisa Katoliki?

Jibu: Niliwahi kuwa Rais wa TEC, kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 na baadaye nikawa Mkamu wa Rais kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.

Swali: Je, una hofu yoyote juu ya usalama wako?

Jibu: Mimi sina hofu na usalama kwa sababu ninajua kufa ni mara moja. Kwa hiyo, ninabaki kivulini, ninazungumza tu ninavyowajibika kama askofu.

UHAMIAJI

MTANZANIA lilizungumza na Msemaji Mkuu Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, ambaye alikiri askofu huyo kuhojiwa.

“Ni kweli anahojiwa na ofisi yetu ya Wilaya ya Ngara, ni suala tu la tuhuma si kwamba ni kweli au la, hivyo itakapothibitika basi itajulikana,” alisema Mtanda.

Peter Msigwa awajia juu CCM



Mbunge wa Iringa Mjini  CHADEMA, Peter Msigwa amewavaa baadhi ya viongozi wa CCM ambao wamekuwa wakisema upinzani Tanzania unakufa na kuwahoji kuwa endapo upinzani ukifa ndiyo maendeleo ya nchi yatapatikana.

Msigwa amesema hayo jana kupitia ukurasa wake wa Facebook baada ya juzi baadhi ya viongozi wa CCM waliokuwepo kwenye Mkutano Mkuu UVCCM wa 9 ambao ulifanyika mjini Dodoma Disemba 10, 2017 ambapo wapo baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho walikuwa wakisema kuwa kwa sasa upinzani nchini unakufa.

"Mkutano wa UVCCM ulibebwa na kibwagizo cha upinzani kuwa unakufa ! Fine, tukubaliane kuwa upinzani unakufa! Ukifa upinzani zitaongezeka ajira ngapi! Umaskini utapungua kwa kiwango gani?

Haki za binadamu zitalindwa kwa kiwango gani? Utawala bora utaimarika kwa kiwango gani ?

Demokrasia itaimarishwa kwa kiwango gani? Uhuru wa kutoa mawazo na vyombo vya habari utaimarika kwa kiwango gani! Haya yote hayana chama! Nilitegemea CCM mje na majibu ya haya sio upinzani unakufa" alisisitiza Msigwa

Mpanda majengo marefu China afariki akionyesha ujuzi wake



Mpanda mijengo mirefu ambaye ni maarufu sana nchini China amefariki akionyesha moja ya ujuzi wake hatari.

Wu Yongning alikuwa amejizolea maelfu ya mashabiki kwenye mtandao ya kijamii wa Weibo, kutokana na video zake fupi za kutisha akiwa juu ya majengo marefu bila ya kuchukua tahadhari zozote za kiusalama.

Wasi wasi uliwaingia mashabiki wake wakati aliacha kuchapisha video zake mwezi Novemba.


Jiwe kubwa linalocheza nchini Tanzania
Mzee mwenye watoto 70 na wajukuu 300 Tanzania
Pacha waliotungwa siku tofauti Australia


Sasa imeibuka kuwa alikufa baada ya kuanguka kutoka jumba la ghorofa 62 kwenye mji wa Changsha.

Vyombo vya habari nchini China vinasema kuwa alikuwa akishiriki kwenye mchezo wa kushinda pesa nyingi


























 Facebook  Twitter  Google+  Pinterest  Linkedin
Newer Post Older Post
POPULAR
Mama Mzazi wa Diamond: "Nimeolewa na Diamond asubiri mdogo Wake"
Mama Mzazi wa Diamond: "Nimeolewa na Diamond asubiri mdogo Wake"
Jeshi la Malaysia lipo tayari kuukomboa mji wa Jerusalem
Jeshi la Malaysia lipo tayari kuukomboa mji wa Jerusalem
FULL VIDEO: Babu Seya na Papi Kocha wakitoka Gerezani
FULL VIDEO: Babu Seya na Papi Kocha wakitoka Gerezani
Breaking News: Rais Magufuli afanya uteuzi kwa watu 6
Breaking News: Rais Magufuli afanya uteuzi kwa watu 6
Sababu ya kuaachiwa Babu Seya yatajwa
Sababu ya kuaachiwa Babu Seya yatajwa
MAGAZETI YA LEO 10/12/2017
MAGAZETI YA LEO 10/12/2017
Kisa Babu Seya mashabiki wamvaa Zitto
Kisa Babu Seya mashabiki wamvaa Zitto
Rais Kenyatta amuandikia barua Rais Magufuli
Rais Kenyatta amuandikia barua Rais Magufuli
Walimu wapigana ofisini
Walimu wapigana ofisini
MAGAZETI YA LEO 8/12/2017