Tuesday, 12 December 2017

Atiwa mbaroni kwa kubaka watoto wanne



JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, linamshikilia kijana wa miaka 30 kwa tuhuma za kuwabaka watoto wanne, wawili wa familia moja.

Tukio hilo limeripotiwa Desemba 8, mwaka huu, huko Muyuni A, Mkoa wa kusini Unguja na mtuhumiwa huyo anadiwa kuwabaka na kuwalawiti watoto hao ambao ni chini ya umri wa miaka 18.

Kamanda wa Polisi mkoa huo, Makarani Khamis, alisema hapo awali mtuhumiwa  huyo alidaiwa kuwabaka watoto saba, lakini baada ya uchunguzi wa daktari ulibainika kuwa ni watoto wanne ndio walioharibiwa na watatu wakiwa salama.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi seremala alidaiwa kuwafanyia matukio hayo watoto hao kwa siku na nyakati tofauti.

Alisema mtuhumiwa yupo ndani kwa hatua za kiupelelezi na zitapokamilika atafikishwa katika vyombo vingine vya kisheria kwa hatua zaidi.

Aliitaka jamii isiwe mbali na watoto wao kutokana na matukio ya udhalilishaji wanaofanyiwa watoto siku hadi siku.

Aidha, aliwashauri wazazi na walezi kufuatilia nyendo za watoto wao na kuhakikisha wanawaogesha badala ya kuwaacha waoge wenyewe ili kama ana majeraha aweze kugundua mapema.

Watoto hao walitambuliwa kuwa wanafanyiwa vitendo hivyo baada ya mmoja ya wazazi wa watoto hao kumgundua mwanawe akiwa anaharufu mbaya na alipomuhoji ndipo alipomtaja mtuhumiwa huyo.

Baada ya kumuhoji mtoto wake alimtaja mtuhumiwa huyo na kuwataja watoto wenzake ambao wamekuwa wakifanywa na mtuhumiwa huyo na kuwapa Sh. 5,000.

Sheha wa Shehia ya Muyuni ‘A’ Maulid Hassan Zidi, alisema baada ya kutokea tukio hilo kuna wananchi wengine zaidi ya saba wanalalamika watoto wao wameharibiwa na mtu huyo, lakini hakuna aliye kwenda kuripoti.

Aliitaka jamii kuripoti matukio hayo yanapotokea badala ya kulalamika mitaani kwani kufanya hivyo kunachangia watendaji wa makosa hayo kuendelea kuyafanya.Sheha huyo alisema katika shehia yake hilo ni tukio la kwanza kutokea ndani ya mwaka huu, lakini huko nyuma kuna matukio kama hayo yalitokea na watuhumiwa wapo mitaani ndio kinachowafanya wananchi kushindwa kuripoti matukio hayo.

No comments:

Post a Comment