Sunday, 10 December 2017

Wakili wa Babu Seya afunguka


Wakili Mabere Marando aliyekuwa akimtetea mwanamuziki mkongwe nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, amesema uamuzi wa Rais John Magufuli kuwasamehe umekuwa ni ‘surprise’ (jambo la kushtukiza) kwake.

Babu Seya na Papii Kocha ambaye pia ni maarufu kama Mtoto wa Mfalme walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuwabaka na kuwalawiti watoto 10 wa kike ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.

Tayari walishatumikia kifungo hicho kwa miaka 13 na miezi minne.

Wakili Marando ambaye aliwatetea katika rufaa yao ya pili Mahakama ya Rufani alisema uamuzi wa Rais Magufuli umemshangaza na ameupokea kwa furaha kubwa.

Marando ambaye alifanikiwa kuwatoa kifungoni watoto wawili wa Babu Seya, Mbangu na Francis katika rufaa hiyo alisema hakutarajia uamuzi kama huo.

“Asante sana, asante sana, asante sana, namshukru sana Rais Magufuli kuwasamehe, kwa kweli sikutarajia hili. Hii imekuwa ni surpirise, asante sana,” alisema Wakili Marando ambaye alikuwa hajapata taarifa za uamuzi huo hadi alipoulizwa na mwandishi wetu.

Mwananchi

Mnyika awaombea askari 14 wa JWTZ



Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amejitoa na kuwaombea askari 14 wa JWTZ ambao wamefariki dunia nchini Congo wakati wakilinda amani huku askari wengine 44 wakiwa wamejeruhiwa.

Mbunge wa Kibamba ameitumia Jumapili ya leo Disemba 10,2017  kuwaombea mashujaa hao na kuwapa pole wanafamilia wote ambao ndugu zao wamepoteza maisha katika tukio hilo.

"Kwa kipekee naitoa ibada ya leo kuwaombea Mashujaa wetu,askari 14 wa JWTZ waliojitoa mhanga na maisha yao kuitetea amani Congo, 44 ambao wamejeruhiwa na wale wawili (2) ambao hawajulikani walipo. Mungu awajalie pumziko jema kwa wale waliopoteza uhai kupigania amani"
Mnyika aliendelea kusema kuwa
"Awape uponyaji majeruhi na kusaidia kupatikana kwa Askari wawili. Aijalie faraja na ustawi familia za wahanga na wote ambao wameguswa kwa moja kwa moja au namna ingine yeyote na tukio baya hilo" aliandika John Mnyika 

Wachezaji Zanzibar Heroes kupimwa mkojo kama wanatumia dawa



Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaingiwa na hofu kwa kiwango bora wanachoonyesha timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) katika Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup yanayoendelea nchini Kenya.

Hofu hiyo imekuja jioni ya leo katika uwanja wa Kenyatta Mjini Machakos mara baada ya kutoka sare ya 0-0 na Wenyeji Kenya na kupelekea Zanzibar kutinga moja kwa moja nusu fainali wakiwa na alama 7 wakiongoza kundi lao A lenye Mataifa kama Kenya, Libya, Rwanda na kaka zao Tanzania bara.

Baadhi ya wajumbe wa CECAFA wakiongozana na wakaguzi wanaopinga dawa za kuongeza nguvu Michezoni walikwenda kwenye vyumba vya kubadilisha nguo vya Zanzibar Heroes kwa kusema haiwezekani timu ya Zanzibar icheze michezo mitatu mfululizo bila ya kuonekana kuchoka.

“Mechi tatu mfululizo Zanzibar wanacheza kwa kiwango bora, tena wachezaji wao ndo wale wale kila siku wanaoanza labda abadilike mmoja tu, itakuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu lazima wachunguzwe”. Alisema mmoja wa Afisa.


Uongozi wa Zanzibar Heroes ukakubali wachezaji wake kwenda kupimwa kama kweli wanatumia dawa za kuongeza nguvu au kiwango chao tu,ukatokea mtafaruku baina yao wenyewe viongozi wa CECAFA na mwisho wakakubali kuwaachia wachezaji hao waende zao wachezaji ambao walishangazwa mno kusikia kuwa wanatumia dawa.

Mbunge Lema atuma ombi hili kwa Rais Magufuli



 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. John Magufuli kuwafuatilia mahabusu waliokaa magereza muda mrefu bila kesi zao kukamilika.

Mh. Lema amefunguka hayo kwenye ukurasa wake Twitter ambapo amechukua hatua hiyo baada ya kumshukuru rais Magufuli kwa kitendo cha kutoa msamaha kwa watu 8157.... waliokuwa wamehukumiwa katika magereza tofauti nchini.

"Mh Rais Magufuli, Mungu akubariki sana kwa msamaha uliotoa jana kwa wafungwa haswa wale waliokaa magereza muda mrefu pamoja na wazee, msamaha ni ibada, pia wako mahabusu wamekuwa magereza kwa muda mrefu sana bila kesi zao kukamilika. Mh Rais fuatilia watu kama hawa pia" Lema.

Jana katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa miaka 56 ya Tanganyika yaliyofanyika Mkoani Dodoma Rais Magufuli alitangaza  msamaha kwa wafungwa 8,157.  ambapo baada ya msamaha huo, 1828 watatakiwa kuondoka Magereza kabisa na wengine 6329 wamepunguziwa muda wa kukaa gerezani.


Takukuru yamshikilia mwenyekiti wa UVCCM



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma inamshikilia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis kwa tuhuma za kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi.

UVCCM leo Jumapili Desemba 10,2017 inachagua viongozi wapya wa ngazi ya Taifa watakaoongoza jumuiya hiyo ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano.

Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, Zanzibar amekamatwa nyumbani kwake karibu na mnada wa zamani mkoani Dodoma.

Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kihanga amethibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo na kwamba watatoa taarifa zaidi baadaye.

"Ni kweli tumemkamata tangu jana usiku tumekesha tunafanya uchunguzi, nitatoa taarifa baadaye kuhusu tukio hilo," amesema.

Mkutano mkuu wa uchaguzi wa UVCCM unaendelea mjini Dodoma na miongoni mwa waliohudhuria ni Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akifunga mkutano mkuu wa uchaguzi wa Umoja wa Wanawake (UWT) jana Jumamosi Desemba 9,2017 alisema hawajapokea malalamiko mengi kutoka umoja huo na kuzitaka jumuiya nyingine za CCM kujifunza UWT.

Manchester United v Manchester City, nani kutoka kifua mbele leo


Manchester United wanawakaribisha majirani zao Manchester City hii leo katika mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa sana, vilabu hivi viwili vinaongoza mbio za ubingwa jambo ambalo linaufanya mchezo huu kuwa mgumu sana.

Mchezo hii sio mrahisi kwa upande wowote ule na United wamepoteza michezo saba kati ya michezo kumi na mbili ambayo wamekutana na katika siku za hivi karibuni Man City wanaonekana kuimarika kuliko United.

Derby ya leo ni tofauti sana na derby nyingi zilizopita kati ya timu hizi kwani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013 Manchester United na Manchester City zinakutana huku wakiwa katika nafasi mbili za juu.

Wakati City wakiwa wamefunga mabao mengi ugenini (27) msimu huu, wenzao United wanaringa na rekodi ya uwanja wao wa nyumbani ambapo michezo 42 hawajafungwa huku wakiwa wameshinda 30.

Jose Mourinho anaonekana kuijenga na kuiimarisha sana United katika eneo lao la ulinzi ambapo hadi sasa wameruhusu nyavu zao kuguswa mara 9 tu katika uwanja wao wa Old Traford msimu huu.

Tayari Manchester City wameshashinda michezo 13 mfululizo na kama watakwenda kushinda mchezo wa leo dhidi ya United baasi wataifikia rekodi waliyoweka Arsenal 2001/2002 ya kushinda michezo 14 mfululizo.

Lakini Jose Mourinho ana rekodi mbovu mbele ya Pep Gurdiola ambapo michezo 19 waliyokutana Mou ameshinda 4 tu na tena ni mchezo 1 tu wa ligi alioshinda, akisuluhu 7na vipigo 8.

Mkuu wa mkoa aagiza waliotia mimba wanafunzi 20 wakamatwe



MKUU wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameitaka polisi mkoani humo kuwakamata watu waliowatia mimba wanafunzi 20 ambao walishindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba mwaka huu.

Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kikao cha bodi ya uteuzi wa wanafunzi waliofaulu na wanaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2018 na kuongeza kuwa wanafunzi hao wa kike ndiyo walioshindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba kutokana na kupata ujauzito kwenye mkoa huo.

“Naagiza polisi kuwakamata watu hao waliowatia mimba wanafunzi wakashindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba mwaka huu,” alisema Ndikilo na kuongeza kuwa sheria ziko wazi kwa wanaowatia mimba wanafunzi hivyo wahusika hao wakamatwe wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Alisema haiwezekani kuwakalia kimya wahusika kwani wamewaharibia maisha watoto hao ambao ndoto zao zimeyeyuka kwa kukatishwa na watu wasio na utu hivyo.

Mvua yaharibu makazi Mtwara



Baadhi ya wakazi wa Kiangu na Chuno mjini Mtwara wamelazimika kuyahama makazi yao yaliyojaa maji baada ya mvua kunyesha.

Mvua ilinyesha usiku wa kuamkia jana Jumamosi Desemba 9,2017 saa nane usiku pasipo kukata hadi saa kumi na moja jioni. Mvua ilikata kwa muda na kuendelea kunyesha usiku hadi leo Jumapili Desemba 10,2017.

Katika maeneo hayo MCL Digital imeshuhudia wananchi wakiokoa mali zao ambazo zilikuwa zimelowa.

Miongoni mwa mali zilizoharibika ni magodoro, samani, majokofu na televisheni.

Baadhi ya vijana wamekuwa wakiwasaidia wazee kuhamisha mali na kuwaondoa maeneo yaliyozingiwa maji.

Mkazi wa Kiangu, Edith Mboni ameiomba Serikali kujenga mitaro itakayopeleka maji baharini ili kuwaondolea adha hiyo.

Amesema mtaro uliopo ni mdogo hivyo kutokana na wingi wa maji unashindwa kuhimili.

Mkazi mwingine, Hassan Mbarali  ameiomba Serikali kujenga miundombinu imara ili kuwaepusha na maafa ambayo yamekuwa yakijirudia mvua kubwa inaponyesha.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Desemba 8,2017 ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwapo vipindi vya mvua kubwa katika  maeneo ya ukanda wa Pwani.

Maeneo hayo ni mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Pia,  visiwa vya Unguja na Pemba.

Viongozi wakuu wa TFF kumzika Bendera



Viongozi wakuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais Wallace Karia na Makamu Rais Michael Wambura wataongoza ujumbe wa shirikisho katika mazishi Kocha wa zamani wa Taifa Stars, marehemu Joel Nkaya Bendera.

Bendera aliyefariki dunia Desemba 6, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, atazikwa leo Jumapili Desemba 10, 2017 makaburi ya Kijiji cha Manundu, Korogwe mkoani Tanga.

Ujumbe huo pia utamjumuisha Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la TFF, Mhe. Mohammed Abdulaziz, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Vedastus Lufano pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Kanda ya 12 (Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro), Khalid Mohammed.

Khalid Mohammed atakuwa na wenyeji wengine ambao ni viongozi wa mpira wa miguu mkoa na wilaya za Tanga ambao wataungana familia pamoja na waombolezaji wengine kumpumzisha Mbunge huyo wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1995 hadi 2005) katika Jimbo la Korogwe Mjini.

Mwili wa marehemu Bendera umeagwa Jumamosi Desemba 9, mwaka huu asubuhi kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Lugalo, Dar es Salaam. Enzi zake Joel Nkaya Bendera alifikia cheo cha Naibu Waziri Michezo mbali ya kuongoza mikoa ya Morogoro na Manyara kwa cheo cha Mkuu wa  mkoa.

Alberto Msando aikosoa UVCCM




Wakili msomi, Alberto Msando ambaye alijiunga na (CCM) amefunguka na kuwachana vijana wa chama hicho UVCCM baada ya viongozi wake kumdanganya  Dkt. John Pombe Magufuli juu ya idadi wa vijana wao.

Albert Msando aliomba nafasi kwa Rais Magufuli ili aweze kuwasema vijana wa CCM baada ya moja ya taarifa yao kusema wapo vijana wa CCM zaidi ya milioni sita jambo ambalo linapingana na taarifa zao wenyewe.

"Nimeazima taarifa ya utekelezaji na mpango mkakati naona mmesema kwamba UVCCM mpo milioni sita, je ni kweli? Kama vijana mtakuwa mnafanya mambo kama haya tutakuwa na nchi ya hovyo sana na chama cha hovyo sana, mmeandika takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya 14-35 ni asilimia 34 ya watu wote nchini. mara tu baada ya ukurasa wa nane, ukurasa wa tisa mmeandika kundi la vijana ni kubwa takwimu zinaonyesha sasa wamefikia asilimia 65 ya idadi ya watu nchini ina maana hatujijui tupo wangapi? alihoji Msando

Wakili Msomi Msando aliendelea kuonyesha mapungufu hayo ambayo yalikuwa na lengo la kumdanganya Rais John Pombe Magufuli

"Kwenye kitabu hiki mmemwambia Rais Magufuli kuwa vijana wa UVCCM mnafika milioni sita lakini kwenye jedwali la kweli mmeandika idadi ya vijana wa UVCCM kila mkoa 2013/2017 jumla walio hai ni milioni moja laki sita wasio hai ni laki nne sasa kwanini mumdanganye Rais?  Tukafanye kazi na hizi ndiyo takwimu zenu sasa hivi mnamwambia Rais tunakaribia milioni sita mnataka Rais aondoke akiwa na picha ya kuwa mpo zaidi ya milioni sita wakati mpo milioni moja laki tano, jamani hatuendi hivyo tunakata CCM mpya ya vijana wachapa kazi, wanachama wote ambao hawapo hai warudi, tupate wanachama wapya" alisema Msando.

ACT -Wazalendo wasitisha mchakato wa uchaguzi mdogo



Chama cha ACT -Wazalendo kimesitisha mchakato wa uchaguzi mdogo wa majimbo matatu na kata sita kikisubiri uamuzi wa Kamati Kuu.

Kaimu Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Dorothy Semu katika taarifa kwa makatibu wa mikoa ya Tanga, Tabora, Ruvuma, Arusha, Iringa, Pwani na Singida amesema kamati ya uongozi ya chama hicho katika kikao cha dharura cha Desemba 8,2017 mjini Dar es Salaam imetoa maelekezo mawili.

Amesema mosi; kwamba viongozi wa mikoa, majimbo na kata zenye uchaguzi wasitishe mchakato wa kushiriki uchaguzi mdogo.

Pili; Dorothy amesema mikoa itapokea maelekezo kuhusu uchaguzi mdogo kutoka ofisi ya katibu mkuu baada ya Kamati Kuu ya ACT -Wazalendo kukutana hivi karibuni.

Amesema kamati ya uongozi ya Taifa imefikia uamuzi huo kutokana na hali iliyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa kata 43 uliofanyika Novemba 26,2017.

Baadhi ya yaliyojitokeza amesema ni pamoja na kubinywa kwa demokrasia na vurugu zilizotokea katika maeneo mbalimbali.

“Hivyo, kamati kuu itafanya tathmini ya uchaguzi mdogo wa kata 43 na kutoa mwelekeo wa chama juu ya uchaguzi wa majimbo matatu na kata sita unaoanza mchakato Desemba 12,2017 na kukamilika Januari 13,2018,” amesema.

Mwananchi:

Hii ndio zawadi ya Manara kwa Papii Kocha baada ya kutoka jela



 Jumamosi ya December 9 2017 ni siku ya furaha kwa watanzania na wapenzi wa muziki wa dansi kwa ujumla, hiyo inatokana na Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli kutangaza msamaha kwa wafungwa wakiwemo msanii Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na Mwanae Papii Kocha.

Rais Magufuli ametangaza msamaha kwa Babu Seya na mwanae Papii Kocha akiwa mjini Dodoma katika maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania na muda mchache baada ya taarifa hizo kutoka watu mbalimbali tumeona wakioneshwa kufurahishwa na uamuzi huo wa Rais Maguli.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa club ya Simba Haji Manara ni moja kati ya watu waliooneshwa kufurahishwa na maamuzi hayo na kaamua kuandika hivi kupitia ukurasa wake wa instagram katika picha ya Papii Kocha akiwa kavaa jezi ya Simba.

“Nchi imezizima sababu yenu . Mungu ametenda miujiza kupitia kwa Rais wetu..uliitangaza Simba hadi gerezani..ntakuvalisha jezi mpya iliosainiwa na wachezaji wote🙏🙏…ila Wenger bado hajatwaa taji…. kama ulivyomuacha🙇🙇”>>> Haji Manara

Huo ni ujumbe wa Haji manara kupitia ukurasa wake wa instagram, kama utakuwa unakumbuka vizuri Babu Seya na watoto wake watatu akiwemo Papii Kocha walihukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2004 baada ya kukutwa na hatia ya kesi ya kubaka na kunajisi watoto 10.

Umoja wa kiarabu waitaka Marekani kufuta uamuzi wake kuhusu Jerusalem



Umoja wa kiarabu katika mkutano wake uliofanyika mjini Cairo umetolea wito Marekani kutupilia mbali uamuzi uliochukuliwa kuhusu jiji la Jerusalem.

Mawaziri wa mambo ya nje katika Umoja wa Kiarabu wametolea wito Marekani kutupilia mbali uamuzi kuhusu Jerusalem , uamuzi ambao unakiuka mikataba ya kimataifa iliyosainiwa kuhusu mji wa Jerusalem.

Umoja wa kiarabu unasema kuwa uamuzi wa Trump ni hatari na una kiuka mikataba ya kimataifa.

Wito umetolewa kwa ulimwengu mzima kukemea uamuzi wa Trump.

Kufuati uamuzi huo, Marekani haina vigezi kuwa mpatanishi katika mzozo baina ya Israel na Palestina.