Wednesday, 6 December 2017

Polisi yasema hawataendelea na Kesi ya Dk Shika



Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu yaDar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kesi ya Dk Louis Shika hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba tatu za mfanyabiashara maarufu Said Lugumi alizoahidi kuzinunua zote zipo.

Novemba 9, 2017 kampuni ya udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba mbili za Lugumi zilizoko Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.

Mambosasa akizungumza leo Jumatano, amesema kesi yake haina mashiko hivyo hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba hizo zipo na hajatia hasara .

Amesema Dk Shika alikuwa akitamba kuwa ana fedha kumbe uwezo wake ni mdogo na kusababisha  kushindwa kulipa asilimia 25 kwa kila nyumba hizo.

‘‘Dk Shika ni wa kumuonea huruma hana kitu tulisema tunamchunguza na tutampeleka mahakamani lakini tumeona kesi yake haina mashiko ndiyo maana hatuendelei nayo,” amesema Mambosasa.

Jeshi la polisi kanda hiyo lilimshikilia na kumwachia kwa dhamana Dk Shika ambaye alikuwa akituhumiwa kwa kuharibu mnada baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo ambapo nyumba za Mbweni JKT alifika bei kwa Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni

Mwenyekiti CCM Iringa ataja sababu za kufanya vibaya



Iringa. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Albert Chalamila amesema chama hicho mkoani humo kimepoteza mwelekeo kutokana na baadhi ya wanachama kuendekeza majungu, ufitini na uongo.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, amesema huu ni wakati wa kuijenga CCM mpya na katika uongozi wake hataruhusu mtu ampelekee majungu ofisini.

“CCM Iringa imepoteza mwelekeo kutokana na kuwapo genge la wafitini, kusemana uongo, umbea, kutukana na wapo wachache wapo tayari kukiharibu chama. Katika utawala wangu sitaki mtu wa kuja kuleta majungu ofisini,” amesema Chalamila.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema iliitwaa jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Peter Msigwa. Pia, ilishinda udiwani katika kata nyingi hivyo kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Amesema jukumu lililo mbele yake ni kuwaleta pamoja wanachama wa CCM ili kurejesha heshima ya chama hicho ndani ya Mkoa wa Iringa ambayo kwa sasa imetoweka.

“Iringa leo imepoteza majimbo matatu, jimbo la Iringa Mjini, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kutokana na wingi wa kura wa Chadema wakapata mbunge wa Viti Maalumu. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha tunarejesha majimbo hayo CCM,” amesema Chalamila.

Pia, amesema katika uongozi wake atafanya uhakiki wa mali za CCM na miradi yake ili kuona namna bora ya kukiendeleza chama hicho.

Wakati huohuo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Salim Abri (Asas) amewashukuru wajumbe wa mkutano kwa kumuamini na kumchagua.

Akijifananisha na paka, Abri amesema atatumia fursa hiyo kuwakamata panya  walio ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Waziri Mhagama ameitaka MIVARF kuongeza thamani ya Biashara Longido



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu ) Mhe. Jenista Mhagama ameitaka (MIVARF) kuongeza thamani ya biashara za mifugo wilayani Longido.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo baada ya kukagua soko la kimkakati lililojengwa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Program ya miundombinu ya masoko, uongezaji thamani na huduma za kifedha vijijini (MIVARF).

Soko hilo lililopo wilayani Longido litawanufainisha wananchi wapatao 142,000 wa wilayani humo ambao asilimia 95 ni wafugaji na huzalisha bidhaa zitokanazo na mifugo.

Soko hilo la kimkakati limeingiza mapato ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 106 kwa mwaka 2016/17, na kusaidia wilaya hiyo kuweka rekodi ya kuingiza mapato ya bilioni 1.3 kwa mwaka kitu ambacho hakikuwahi kutokekea hapo awali.
B
MIVARF ni Programu ya Miundombinu ya Masoko na Huduma za kifedha vijijini, iliyobuniwa mwaka 2011 na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na inatekelezwa katika mikoa 29 nchini.

Finland yaipa shavu Klabu ya Tanzania


Klabu ya soka ya Kiluvya United ya Mkoa wa Pwani imefanikiwa kupata klabu rafiki inayofahamika kama Tampere inayoshiriki ligi kuu nchini Finland.

Katibu wa klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Omary Masawilla amethibitisha hilo, ambapo ameeleza kuwa urafiki huo umefanikishwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.

“Ni kweli tumepata klabu rafiki ya huko Finland inashiriki ligi kuu na wameona sisi tuna mipango mizuri na uwezo wa kupanda ligi kuu hivyo wakaomba tushirikiane katika mambo mabalimbali, tayari mkuu wa mkoa ameshatupa maelekezo na kinachosubiriwa ni wao kuja kukutana na sisi ili kuanza utekelezaji”, amesema Masawilla.

Ushirikiano huo utahusisha maeneo kadhaa ikiwemo  kukuza vipaji, mbinu za uchezaji na benchi la ufundi ili kuinua soka mkoani humo. Ushirkiano huo utaleta manufaa makubwa kwa vipaji vya soka hususani vijana katika mkoa wa Pwani.

Kwa upande mwingne Mkuu wa mkoa ametoa kiasi cha shilingi milioni moja kwa timu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza ili kuhakikisha inapunguza changamoto mbalimbali na hatimaye kutimiza lengo la timu kuingia ligi kuu.

Mhandisi Ndikilo ametoa mchango huo baada ya kutembelea kambi ya  timu hiyo iliyopo kwenye shule ya Filbert Bayi wilayani Kibaha. Kiluvya United inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 14 kwenye kundi A ligi soka daraja la kwanza nyuma ya vinara JKT Ruvu yenye alama 23 wakati African Lyon inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 17.

Madabiba afutiwa Mashtaka



ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefutiwa mashtaka ya kusambaza dawa feki za kufubaza makali ya ukimwi (ARV) na kujipatia Sh milioni 148 kwa njia ya udanganyifu na kukamatwa tena, kusomewa mashtaka mapya.

VIDEO: Kubenea afunguka kutohamia CCM



Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hana sababu za msingi zinazomfanya kujiuzulu nafasi hiyo.



Pia, amewaonya wanaoeneza uzushi huo akitaka waache tabia hiyo.

Kubenea ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani amesema leo Jumatano Desemba 6,2017 saa saba mchana katika ofisi za kanda hiyo Magomeni Dar es Salaam, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Ametoa kauli hiyo baada ya taarifa kuenea kuwa ni miongoni mwa wabunge wa upinzani watakaohama vyama vyao katika dhana ya kuunga mkono utendaji wa Rais John Magufuli.

Akizungumza na MCL Digital, Kubenea amesema hajawahi kumweleza yeyote kwamba ana mpango wa kuhama na hafikirii kufanya hivyo.“Sijawahi kukaa kuzungumza na CCM, hayo mambo ninayaona kwenye mitandao ya kijamii, kama kuna mtu ana ushahidi wa mimi kuzungumza na CCM autoe. Sina sababu za kuhama Chadema,” amesema Kubenea.

Amesema, “Imani niliyopewa na wananchi wa Ubungo ni kubwa, siwezi kuichezea.”

Kilimanjaro Stars yafundishwa mbinu mpya za kukabiliana na Adui



Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ Ammy Ninje amesema anafurahishwa na mwenendo wa mazoezi ya timu yake ambayo yanatoa taswira ya kufanya vizuri kwenye mchezo ujao.

Kilimanjaro Stars imeendelea na mazoezi yake leo asubuhi kwenye Uwanja wa Machakos Academy, ambapo kocha Ninje ameanza kufanyia kazi namna ya kukaba wakati mpira unapokuwa kwa adui au timu inapopoteza mpira. Sambamba na hilo Ninje pia amefanyia kazi namna ya kutengeneza mashambulizi.

“Timu inaendelea vizuri na mazoezi na nafurahi kuona vijana wanafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza tulipocheza na Libya na tunaamini hayatajirudia kwenye mechi ijayo, tutashinda dhidi ya Zanzibar Heroes”, amesema Ninje.

Kilimanjaro Stars, ilicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Libya Jumapili Desemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kenyatta na kutoka sare tasa katika mfululizo wa mechi za michuano ya CECAFA inayoendelea nchini Kenya ikiwa katika hatua ya makundi.

Timu hiyo ipo kundi A pamoja na timu za Rwanda, Zanzibar, Libya na wenyeji Kenya. Hadi sasa Kenya ndio vinara wa kundi hilo wakiwa na alama nne baada ya michezo miwili huku Zanzibar Heroes ikishika nafasi ya pili ikiwa na alama tatu ikifuatiwa na Libya yenye alama mbili. Tanzania ina alama moja huku Rwanda ikiburuza mkia ikiwa haina alama.

Lissu afurahi kutembelewa na Rais mstaafu Mwinyi


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya umri wa miaka 93 alionao Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi bado amediriki kufunga safari kwenda kumtembelea na kumpa pole.

Lissu, ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutembelewa na Mzee Mwinyi katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako anaendelea na matibabu.

Lissu amelazwa hospitalini hapo tangu Septemba 7 anakotibiwa akiuguza majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma akitokea kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu kuhusu kutembelewa na Mzee Mwinyi, mwanasheria huyo wa Chadema pamoja na mke wake, Alice walisema wamefurahi kutembelewa na kiongozi huyo.

“Nimefurahi sana kwamba umri wote alionao wa miaka 93 si kidogo, ametafuta muda kuja kunipa pole hospitalini ni kitu kizuri sana, ni ubinadamu mkubwa sana,” alisema Lissu ambaye alionekana mwenye furaha.

Rais mstaafu Mwinyi anakuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali waliomtembelea Lissu kwani hivi karibuni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye alifika hospitalini hapo kumjulia hali.

Mzee Mwinyi akiambatana na mke wake na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya walifika hospitalini hapo kumjulia hali mbunge huyo na picha zinawaonyesha wawili hao wakizungumza huku nyuso zao zikiwa na tabasamu

Kubenea afunguka kutohama Chadema


Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hana sababu za msingi zinazomfanya kujiuzulu nafasi hiyo.

Pia, amewaonya wanaoeneza uzushi huo akitaka waache tabia hiyo.

Kubenea ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani amesema leo Jumatano Desemba 6,2017 saa saba mchana katika ofisi za kanda hiyo Magomeni Dar es Salaam, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Ametoa kauli hiyo baada ya taarifa kuenea kuwa ni miongoni mwa wabunge wa upinzani watakaohama vyama vyao katika dhana ya kuunga mkono utendaji wa Rais John Magufuli.

Akizungumza na MCL Digital, Kubenea amesema hajawahi kumweleza yeyote kwamba ana mpango wa kuhama na hafikirii kufanya hivyo.“Sijawahi kukaa kuzungumza na CCM, hayo mambo ninayaona kwenye mitandao ya kijamii, kama kuna mtu ana ushahidi wa mimi kuzungumza na CCM autoe. Sina sababu za kuhama Chadema,” amesema Kubenea.

Amesema, “Imani niliyopewa na wananchi wa Ubungo ni kubwa, siwezi kuichezea.”

ACT kufanya maandamano


dara ya vijana ya Chama Cha ACT-Wazalendo imesisitiza kuwa itafanya maandamano yake ya amani yenye lengo la kupinga vitendo vya utumwa wanavyofanyiwa vijana wa Afrika nchini Libya.

Pamoja na kutojibiwa barua yao ambayo wameliandikia jeshi la Polisi kwenye mkoa wa kipolisi Kinondoni kwaajili ya kuomba kibali cha maandamano hayo lakini wamesisitiza kuwa watafanya hivyo

“Polisi Kinondoni wanasema barua yetu ya maandamano ya tarehe 8/12/17 imetumwa KANDA na mpaka sasa majibu hawajaletewa, wanasema tuulizie tena kesho tunapenda kuujulisha umma kuwa ratiba ya maandamano yetu haijabadilika”, imesema Taarifa ya hiyo kutoka idara ya vijana ACT-Wazalendo.

Idara hiyo ya vijana imepanga kuandamana siku ya Ijumaa Disemba 8 kuanzia saa 4 asubuhi ambapo wataanzia eneo la Leaders Club jijini Dar es salaam na kuishia ofisi za Ubalazi wa Libya nchini zilizopo Upanga jijini Dar es salaam na watatumia barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Hivi karibuni nchini Libya kumeibuka vikundi vya watu ambavyo vinafanya biashara ya utumwa kwa baadhi ya wageni wanaoingia nchini humo hususani wale wahamiaji ambao hufika nchini humo kwa lengo la kuvuka na kuelekea barani Ulaya.



Nigeria wateua Waziri wa kushughulikia furaha, mahusiano kifamilia



Gavana wa Jimbo la Imo, Rochas Okorocha (kushoto).

Serikali ya Jimbo la Imo nchini Nigeria imeteua waziri atakayeshughulikia masuala ya furaha na mahusiano ya kifamilia.

Uteuzi wa waziri huyo unaelezwa ni mkakati wa kuwasahaulisha wananchi adha za kisiasa na mapigano ya makundi haramu.

Gavana wa jimbo hilo, Rochas Okorocha amesema uteuzi huo ni wa kwanza kufanyika katika Taifa hilo lililopitia kipindi kigumu cha mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram na hali mbaya ya kisiasa.

Okorocha amemteua ndugu yake, Ogechi Ololo kuwa waziri wa masuala ya furaha na mahusiano mema ndani ya familia.

Kabla ya uteuzi huo, Ogechi alikuwa msaidizi wa Gavana Okorocha na mshauri wake maalumu wa masuala ya nyumbani. Pia, anahusika na mapambo wakati wa sikukuu ya Krismasi.

Hata hivyo, msemaji wa gavana huyo, Sam Onwuemeodo hakutoa maelezo zaidi kuhusu majukumu ya waziri huyo.

Akizungumza na Shirika la Habari la AFP alisema, “Hakuna kitu kipya zaidi katika uteuzi huo.”

“Gavana ni mtu mbunifu ambaye kila wakati huanzisha vitu vipya serikalini. Jukumu kubwa la waziri huyu ni kuleta ubunifu ambao utaweza kuigwa na magavana wengine. Gavana anataka kuwafanya watu wawe na furaha kila wakati na ndiyo maana ameunda wizara hii kwa lengo hilo,” amesema.

Urusi Imefungiwa kushiriki michuano ya Olimpiki


Kamati ya kimataifa ya Olimpiki, imeifungia nchi ya urusi kushiriki michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itayofanyika katika jiji la Pyeongchang nchini Korea kusini mwakani.

Rais wa IOC Thomas Bach na bodi yake walitangaza adhabu hiyo jana jioni baada ya kukutana katika mji wa Lausanne nchini Switzerland, maamuzi hayo yamefikiwa baada ya uchunguzi wa miezi kumi na saba.

Serikali ya Urusi ilihusika katika udanganyifu wa kuanda michuano ya olimpiki iliyofanyika nchini humo mwaka 2014 pamoja na udanganyifu kuhusu matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Uchunguzi huo ulikuwa ukiongozwa na Rais wa zamani wa IOC Samuel Schmid, Licha adhabu hiyo wanariadha wa Urusi wanaweza shiriki michuano ya majira ya baridi kama wanaridha huru ambao watakuwa wakiwakilisha nchi.

Nafasi za kazi leo Dec 6