Tuesday, 5 December 2017

Mtanzania azidiwa na dawa za kulevya na kufariki ndani ya ndege



Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga amethibitisha kupokea taarifa ya Mtanzania kufariki dunia akisafirisha dawa za kulevya.

Amesema alikuwa akisafiri kuelekea nchini China kwa ndege ya Shirika la Ethiopia na alizidiwa kutokana na dawa alizokuwa amemeza.

“Ni kweli kuna Mtanzania amekutwa amekufa kwenye ndege ya Shirika la Ethiopia akiwa amemeza dawa za kulevya. Tunaendelea kufuatilia kujua jina lake na amezitoa wapi hizo dawa,” amesema.

Sianga akizungumza na MCL Digital leo Desemba 5,2017 amesema taarifa hizo walizipata jana na kwamba wanaendelea kufuatilia.

Amesema hivi sasa Watanzania wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wengi wanatumika kupokea mizigo na kuisafirisha kunakohitajika.

Waziri Lukuvi awaonya wenye nyumba wanaotoza kodi ya mwaka



Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaonya wamiliki wa nyumba wanaopangisha na kudai kodi ya mwaka mzima.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 5,2017 akifungua jengo la makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam na sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere, amesema kodi ya nyumba inatakiwa kutozwa kila mwezi.

"Mpangaji anatakiwa kulipa kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja," amesema.

Lukuvi amesema hata NHC inatoza kodi kwa wateja wake kwa mwezi. "Acheni tamaa wenye nyumba chukueni kodi kila mwezi," amesema.

Amesema kuna vijana wanaoajiriwa wanashindwa kukaa jirani na mjini kutokana na kutozwa kodi ya nyumba kwa mwaka.

Mbali ya kauli hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo bungeni alisema Serikali iko katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai kodi ya pango ya zaidi ya mwezi mmoja.

Halima katika swali lake alisema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.

Akijibu swali hilo, Mabula alisema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.

Mabula alisema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.

Zanzibar Heroes yaifumua Rwanda 3-1 CECAFA



Timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rwanda kwenye mchezo wake wa kwanza Kundi A michuano ya CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya.

Zanzibar ambayo imecheza soka safi na kujiamini ilifanikiwa kuandika bao la kuongoza dakika ya 35 kipindi cha kwanza kupitia kwa Abdu-Aziz Makame ambaye alimalizia kwa kichwa krosi nzuri ya Mudathir Yahya. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Rwanda ilianza kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 47 kupitia kwa kijana Hakizimana Niyonzima ambaye ni mdogo wake na nyota wa Simba Haruna Niyonzima.

Bao la pili la Zanzibar limefungwa na Mohammed Juma dakika ya 52 huku bao la tatu likifungwa na Kassim Khamis dakika ya 86. Matokeo hayo sasa yanaiwezesha Zanzibar kushika nafasi ya pili katika kundi A nyuma ya Kenya.

Zanzibar Heroes itacheza mchezo wake wa pili na ndugu zao wa Kilimanjaro Stars siku ya Alhamis Desemba 7. Kilimanjaro ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya taifa ya Libya kwenye mchezo wa kwanza.

Ethiopia: Mtalii kutoka Ujerumani auawa kwa kupigwa risasi



Mtalii mmoja kutoka Ujerumani amepigwa risasi na kuuawa kaskazini mashariki mwa Ethiopia.

Dereva wake pia alijeruhiwa wakati wa tukio hilo, ambalo lilifanyika katika jimbo la Afar, karibu na mpaka wa Eritrea.

Ripoti zanasema raia huyo wa Ujerumani alikuwa miongoni mwa kundi la watalii ambao walikuwa kwenye ziara ya volkano ya Erta Ale - kivutio kikubwa kwa watalii wanaozuru Ethiopia.

Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza anasema hadi kufikia sasa haijabainika ni nani hasaa aliyetekeleza shambulio hilo lakini serikali ya Ethiopia inasema inachunguza mauaji hayo.

Serikali pia inasema vikosi vya usalama vimetumwa kuimarisha usalama huko.

Eneo hilo la mpakani linatumika sana na kundi la waasi linalotaka kujitenga na Ethiopia.

Mnamo mwaka 2012, watalii watano waliuawa na wengine wanne kutekwa nyara baada ya wapiganaji kuwashambulia katika eneo hilo.

Kundi lililojihami la Afar Revolutionary Front lilidai kuhusika kwenye shambulio hilo.

Kenya inampango wa kuzalisha kawi ya nyuklia kufikia 2027



Kenya imesema kwamba itaendelea na mpango wake wa kuhakikisha kwamba ina kiwanda cha kuzaliwa umeme kwa kutumia nguvu za nyuklia kufikia 2027.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Umeme wa Nyuklia ya Kenya Collins Juma ameambia mkutano wa wadau kuhusu kawi jijini Nairobi kwamba ujezi wa kiwanda cha kuzalisha kawi hiyo unatarajiwa kuanza 2024.

Bodi hiyo imesema nishati hiyo itatumiwa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini humo na si kuchukua nafasi ambayo imekuwa ikitekelezwa na vyanzo vingine vya kawi nchini humo.

Kufikia mwaka 2030, ambapo Kenya inatazamia kuwa taifa lenye viwanda la mapato ya wastani kufikia wakati huo, Kenya itakuwa ikihitaji megawati 17,000.

Kawi ya mvuke itachangia megawati 7,000. Kwa sasa, kawi hiyo kwa sasa hutumiwa kuzaliwa megawati 2,400 za umeme nchini humo.

Kaimu afisa mkuu mtendaji wa kukinga dhidi ya miali nururishi nchini Kenya Joseph Maina amesema Wakenya hawafai kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa nishati ya nyuklia.

"Kumekuwa na ajali tatu pekee kubwa za nyuklia katika historia. Kisiwa cha Three Mile Marekani, 1978; Chenorbyl nchini Ukraine, 1986 na Fukushima nchini, Japan, 2011. Usalama umeimarishwa kutokana na mafunzo kutoka kwa mikasa hiyo," amesema.

Kenya imekuwa na mpango wa kuzalisha kawi ya nyuklia kwa muda.

Machi mwaka huu, Waziri wa nishati na mafuta wa nchi hiyo Bw. Charles Keter alisema Kenya itatimiza vigezo vikali vilivyowekwa na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA kabla ya kutekeleza mpango huo.

Alikadiria kwamba Kenya itatumia dola 5 bilioni za Marekani kujenga kiwanda cha kuzalisha kawi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA ya mwaka 2015, zaidi ya nchi 30 duniani, theluthi moja zikitoka Afrika zinajiandaa kuanzisha mipango ya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa usaidizi wa wataalamu kutoka shirika hilo.

VIDEO: Walichosema Witness na Tea kuhusiana na uzalendo

Hiki ndicho walichokisema Witness A.K.A kibonge mwepesi na Ndumbagwe misayo A.KA Tea kuhusiana na uzalendo ambapo waziri wa habari utamaduni sanaa na michezo Mh. Harrison Mwakyembe

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI.........USISAHAU KUSUBSCRIBE.

VIDEO: Polisi wamnasa komandoo wa Burundi akiwa na AK.47 akifanya matukio ya ujambazi


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es alaam mnamo tarehe 28/11/2017 na tarehe 30/11/2017 askari walifanya oparesheni maalum ambayo ilifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa watatu ambao wanajihusisha na matukio ya uporaji na mauaji mbalimbali katika jiji la Dar es salaam.

TAZAMA FULL VIDEO HAPO CHINI.....USISAHAU KUSUBSCRIBE

Kamanda SACP Lazaro Mambosasa amesema hayo leo  alipozungumza na waandishi wa habari, na kusema kuwa baada ya  mahojiano name watuhumiwa hao walikubali kuonyesha silaha moja aina ya AK.47, Magazine mbili 2 na risasi 57 ambayo walikuwa wameificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano, pia walionyesha pikipiki mbili aina ya Boxer zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE  rangi nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali.


Pia Kamanda Mambosasaaliongeza kuwa walipohojiwa zaidi walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda kuonyesha silaha hizo, walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari jambazi mmoja raia wa Burundi aliyefahamika kwa jina la Fanuel Luchunda Kamana @Mrundi alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha huku wenzake wawili wakijaribu kutoroka na ndipo walijeruhiwa kwa risasi.

Aidha majambazi hao waliwahishwa katika hospitali ya Mwananyamala ili kupatiwa matibabu na ndipo madaktari wakabaini kuwa tayari wameishafariki dunia.

Miili hiyo imehifadhiwa hospitalini hapo kwa hatua za uchunguzi wa kitaalamu, aidha majambazi hao walikiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji na mauaji likiwemo tukio la mauaji huko Kunduchi Mtongani la tarehe 19/11/2017 ambapo huwaua madereva bodaboda na kupora pikipiki zao na kuziuza kwa TSHS.800, 000/=.

Majambazi wengine waliofariki ni Gallus Clement, (31) na Fredrick Wilbord Acholo mkazi wa Gongo la Mboto.

VIDEO: Waziri Mwakyembe amkabidhi Ibrahim Classic TSH 18 Milioni


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo ameonesha uzalendo wake baada ya kumkabidhi Bondia Ibrahim Classic kiasi cha Tsh Milioni 18 kama malipo yake ya pambano na Bondia Koos Sibiya kutoka Afrika Kusini ambapo Ibrahim alishinda pambano hilo na kutetea ubingwa wake wa Dunia wa CBG.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI.......USISAHAU KUSUBSCRIBE

Dhamana ya Wabunge Lijualikali na Susan Kiwanga kujulikana kesho


Morogoro. Wabunge Susan Kiwanga na Peter Lijualikali waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro pamoja na washtakiwa wengine 36 wamerejeshwa rumande.

Mahakama iliyokuwa itoe uamuzi wa dhamana leo Jumanne Desemba 5,2017 imekwama kufanya hivyo kutokana na kuibuka hoja za kisheria.

Upande wa mashtaka na ule wa utetezi unavutana kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Ivan Msack ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Kata ya Sofi iliyopo wilayani Malinyi.

Washtakiwa wanatetewa na mawakili Peter Kibatala, Ignas Punge, Fredrick Kiwelo na Bartholomew Tarimo.

Upande wa mashtaka unawakilishwa na mawakili wa Serikali, Edga Bantulaki na Sunday Hyera.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Frederick Sumaye walihudhuria mahakamani.

Wengine waliofika mahakamani ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Viti Maalumu, Devota Minja.

Usiku wa Kitendaliwili kuzinduliwa Disemba 8 Dodoma


Usiku wa Kitendawili unaotarajiwa kufanyika Disemba 8 mwaka huu huko mkoani Dodoma ndio habari ya mjini kwa sasa, kwani watanzania wanashahuku kubwa ya kusikia kauli za viongozi mbalimbali wastaafu na walioko madarakani kuhusu harakati za Tanzania kupata uhuru pamoja na jinsi watanzania walivyoonganika na kuwa kitu kimoja licha ya kuwa na makanila 120.

Viongozi wa zamani wa serikali, walipo madarakani pamoja na wadau wakiwa wamekaa chini kwenye mikeka ya asili na vigoda watapata fursa ya kueleza namna serikali kupitia viongozi wake ilivyoweza kuondoa mambo ya ukabila ambayo yanayatesa mataifa mengi ya Afrika.

Akiongea na TBC katika kipindi cha Tanzania Mpya, Mrisho Mpoto amesema kuwa siku hiyo mgeni rasmi ambaye ni Rais John Pombe Magufuli atapata fursa ya kueleza maisha yake ya utoto na namna alivyoweza kusimama katika mstari ambao kila mmoja kwa sasa akiangalia matendo yake anaona rais kweli ni mzalendo wa kweli.

“Usiku wa Kitendawili ni ukurasa mpya wa kujifunza mambo mapya kuhusu uzalendo na kuanza utekelezaji mara moja, na kama unavyojua tutakuwa na viongozi mbalimbali katika huo usiku, Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu pamoja na Waziri Mkuu na wote watapata fursa ya kueleza mawili machache kuhusu uzalendo, wao waliwezaje kuwa wazalendo wa kweli, tunapokuwa kuna jambo la kitaifa tuungane kwa pamoja kama watanzania, wanapotokea watu wachache wakajitenga huo sio uzalendo ndio maana nikasema hiyo siku tutamsikiliza Rais wetu amewezaje kuwa mzalendo ambaye kila mtu akimuangalia anaona kabisa huyo ni mzalendo na apaswa kuungwa mkono na watanzania wote kwa manufaa ya taifa leo na la kesho,” alisema Mpoto.

Aliongeza, “Lakini pia tumeomba protocol zisiwe kali sanaa kwa upande watanzania na viongozi ili watu wafunguke, tunataka Rais wetu atuambie kwanini yupo vile, kwa nini anakuwa na uchungu na watanzania hasa watanzania wa chini, kwa nini anawafikiria wanyonge zaidi.

 Kuna wakati Mhe Rais anasema Tanzania ya Viwanda watu wanaona kama haeleweki, lakini sasa hivi viwanda vimeongezeka kila mtu amenza kuamini kwamba Tanzania ya Viwanda inawezekana, kwa sababu imetoka kwenye ubongo kama wazo imeenda kwenye uhalisia.

 Kwahiyo ninachosema kwamba tutakaa kwenye mikeka na vigoda, tutakula ugali ya muhogo, kisamvu na madafu , Majaliwa pale, Mama Samia pale , tunakaa pale na ule ukumbi umetengenezwa kama kuna vijiji na mitaa, Mhe atapita pale kwenda kusalimia kijiji cha jirani watuambie tu wamewezaje kuondoa suala la ukabila, nchi za wenzetu wanapigana kila siku, kwahiyo kama tukitumia nguvu iliyotumiaka kuwaonganisha watanzania ambao kwa wingi wetu tuna makabila 120, lakini wote tukawa kitu kimoja kwanini tushindwe watanzania na wote tuimbe wimbo mmoja wa Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’,”

Mpoto amesema kwa sasa kuna haja ya kuwa na nyimbo za hamasa ambazo zitawajenga watanzania kuwa wazalendo na kukataa rushwa pamoja na kuacha kufanya kazi kizembe.

Usiku wa Kitendawili umeanzishwa na msanii wa huyo wa muziki wa asili nchini baada ya kuachia wimbo wake ‘Kitendawili’ na baadaye kufikiria kuanzisha usiku wa wimbo huo kwaajili ya kuwakutanisha wadau na kujadili kuhusu Uzalendo.

Alisema baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo, itayokuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julis Kambarage Nyerere, wataanza kuzungumza katika mikoa mbalimbali kupaza sauti kuhusu uzalendo.

Mpoto alisema mambo yatayopambaniwa katika kampeni hiyo ni pamoja na kudhibiti na hatimaye kukomesha kabisa mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma, kupunguza tuhuma za rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma pamoja kuongeza hari ya kufanya kazi na Uzalendo.

Rais Mwinyi amtembelea Lissu, Nairobi


RAIS Mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi leo Desemba 5, 2017 amemtembelea Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Tundu Lissu katika Hospitali ya Nairobi anakotibiwa baada kushambuliwa kwa risasi nyumbani kwake Area D, Mjini Dodoma.


Rais Mstaafu Kikwete afanya uteuzi huu


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete amemteua Profesa William-Andey Anangisye kuwa makamu mkuu wa chuo hicho.

Prof. Anangisye ameteuliwa katika nafasi hiyo kuitumikia kwa miaka mitano kuanzia leo Desemba 5, 2017. Makamu mkuu huyo mpya wa chuo anachukua nafasi ya Profesa Rwekaza S. Mkandala ambaye anamaliza muda wake.

Mkuu huyo wa chuo Dkt. Kikwete amefanya uteuzi huo baada ya kushauriana na bodi ya chuo kwenye kikao kilichofanyika Novemba 30 na baadae kumjulisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Kampuni ya CNBM Group yaunga mkono jitihada za Makonda



Kampuni ya China Nationali building Material Group leo imekabidhi hundi ya Shilingi Milioni kumi ili kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kusaidia Watu wenye uhitaji wa miguu bandia na zoezi la upimaji afya.


Akizungumza na Waandishi wa habari leo mara baada ya kupokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa,  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dakta Grace Magembe amesema Serikali ya Mkoa imekusudia kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi pamoja na kusaida watu wenye ulemavu,ambapo amebainisha kuwa hapo awali Serikali ya Mkoa ilikusudia kusaidia watu wenye ulemavu miambili lakini idadi ya wenye uhitaji wa miguu ni zaidi ya watu elfu moja hivyo amewataka wadau kuendelea kujitokeza kusaidia.

Dakta Magembe ameongeza kuwa tokea kuingia madarakani Serikali ya awamu ya tano iliyo chini ya Rais Dakta John Magufuli imekuwa ikishughulikia changamoto mbalimbali za wananchi hivyo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya China National building Material Group Wang Shupeng amesema kampuni hiyo imeridhishwa na juhudi zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na imetambua umuhimu wa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo miguu bandia hivyo mbali na msaada huo wa shilingi milioni kumi za kitanzania itaendelea kutoa misaada mbalimbali kuunga mkono serikali.