Friday, 24 November 2017

Kinana, Nape waunganisha nguvu tena



     Arumeru. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wameunganisha nguvu katika Kata ya Makiba ambako wanampigia debe mgombea wa chama hicho, Samson Laizer.

Kinana na Nape wanachukuliwa kama wanasiasa waliofanya kazi kubwa ya kuhuisha nguvu ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kuzunguka karibu nchi nzima kupiga siasa na wakati mwingine kudiriki hata kuwasema hadharani mawaziri wa Serikali ya CCM, wakiwaita mizigo.

Jana wawili hao waliungana na Mrisho Gambo, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Arusha na Alexander Mnyeti (Manyara) kuipigia debe CCM.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Makiba wilayani Arumeru, Kinana alisema ni vigumu vyama vya upinzani kushika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kinana alisema akiwa katibu mkuu wa CCM ametembelea mikoa, wilaya na kata tofauti ambako ameona wananchi wana imani kubwa na chama hicho.

Kinana alisema katika uchaguzi mkuu uliopita wananchi wa eneo hilo walipiga kura kwa kufuata upepo na ushabiki wakidhani upinzani ungeshinda.

“Watu walidhani rafiki yangu yule, mnamjua siwezi kumtaja, atakuwa Rais, lakini hakuweza kupata nafasi hiyo,” alisema Kinana.

Alimpongeza Gambo kwa kufanikisha maendeleo ya mkoa huo na hasa eneo la Makiba.

“Pia mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alifanya kazi kubwa alipokuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru. Anastahili hongera nyingi,” alisema Kinana.

Alisema maendeleo hayana ushabiki hivyo wananchi wa Makiba wanapaswa kumchagua Laizer ili asimamie maendeleo.

Alisema miradi ya maendeleo kama wa umeme vijijini (Rea), maji, ujenzi wa barabara ya Mirerani unapaswa kusimamiwa na diwani wa CCM na si wa upinzani.

Alisema CCM ndicho chama kilichoshinda uchaguzi hivyo kinatekeleza ilani yake na hata wapinzani wanatekeleza ilani hiyo.

Naye Nape, ambaye alizunguka nchini na Kinana wakati akiwa katibu wa itikadi na uenezi, alisema wananchi wa kata hiyo wasirudie makosa kwa kuweka ushabiki na kumchagua mgombea wa upinzani.

Alisema kata hiyo ni ya CCM ndiyo sababu wanaitaka kwa gharama yoyote kiasi cha viongozi kwenda eneo hilo kushiriki katika kampeni. Aliwataja viongozi hao kuwa ni yeye mwenyewe, Kinana na wakuu wa mikoa ya Arusha na Manyara.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer alisema ameshapeleka ombi la wananchi wa mkoa huo kuwa walikosea kwa kuchagua upinzani mwaka 2015.

Laizer alisema salamu hizo ameshazifikisha na Rais Magufuli ameridhia kutoa msamaha kwa wananchi wa eneo hilo ambalo walidhani kanda ya kaskazini inatosha kumchagua Rais wa nchi.

Mgombea Laizer aliwaomba wananchi wa kata ya Makiba kumchagua kwa wingi awe diwani wao kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya eneo hilo.

Laizer aliwaahidi utumishi uliotukuka pindi wakimchagua kwani yeye ni mtu wa maendeleo na anayeweza kutumwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Meru.

Naye Mnyeti, ambaye ametajwa katika kashfa ya tuhuma za kuhonga madiwani wajiondoe CCM na hivyo kusababisha uchaguzi mdogo unaoendelea sehemu mbalimbali nchini ukiwemo wa kata hiyo, alisema wananchi wa eneo hilo walishamuahidi kuwa watamchagua mgombea wa CCM hivyo hana wasiwasi na hilo.

Mnyeti alisema kwa muda wote aliokuwa mkuu wa wilaya hiyo alishirikiana na wananchi wa Makiba, hivyo watamchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane ipasavyo na mkuu mwingine wa wilaya hiyo atakayechaguliwa na Rais.

Naye Gambo alisema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kumchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane naye kuleta maendeleo.

Gambo alisema awali walifanya makosa kwa kumchagua mpinzani hivyo wasifanye tena makosa.

Alichokisema Dk Slaa baada ya kuteuliwa



Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo, Dkt. Wilbroad Peter Slaa, amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa Balozi wa Tanzania na kusema kuwa yuko tayari kutoa mchango wake katika kulijenga taifa la Tanzania.

“Kwa sababu Ubalozi uko kwenye Idara za moja kwa moja za mkuu wa nchi, na bila shaka hakukuwa na sababu mkuu wangu kutotaka kuniteua, ninamshukuru kwa uteuzi huo kwa kuniona, ninachoweza tu kusema katika hatua hiyo ni kwamba ninao wajibu mkubwa hasa katika kipindi hichi cha kulijenga taifa letu,” amesema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, na ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Urasi kupitia chama hicho, alijiuzulu nafasi yake hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuondoka nchini.

Muda mfupi baadaye Dkt. Slaa alitangaza kutojihusisha tena na siasa za hapa nchini na akawa anaishi nchini Canada pamoja na mpenzi wake Josephine Mushumbusi.

Dk. Slaa, ambaye kwa sasa anaishi nchini Canada alikokwenda kwa masomo, tangu alipotangaza kuachana na siasa Septemba 1, mwaka 2015 aliweka wazi kuwa anafanya kazi zaidi ya mbili ili aweze kujipatia kipato kitakachomuwezesha kumudu gharama za maisha nchini humo.

Alitaja kuwa kwa sasa anafanya kazi ya Mshauri wa Mauzo (sales Advisor) pamoja na kutoa ushauri (consultancy).

“Mimi ninafanya kazi PWD/CDS/COSTCO kama Sales Advisor, baada ya kumaliza masomo yangu hasa Interpersonal Communication. Costco ninakofanya kazi ina members (wanachama) 10,000. Kwa siku wanaofika Warehouse ni kati ya 5,000 hadi 7,000,” alisema Dk. Slaa.

Kufuatia uteuzi huo wa Dkt. Slaa kuwa Balozi uliofanywa na Rais Magufuli, taaarifa kutoka ikulu imeeleza kuwa zoezi la kuapishwa kwake litafuata baada ya kukamilishwa kwa taratibu.

Wolper awafungukia Mastaa




Jacquline Wolper.

STAA wa Bongo Movies, Jacquline Wolper amesema kuwa mastaa wengi hawapendi kupeana ‘sapoti’, kiasi kwamba hata kama staa mwenzao akiwa na biashara yake wapo radhi kununua kwingine lakini si kwake, ili tu wamkomoe.

Akichonga na gazeti hili, Wolper alijitolea mfano kwa kusema kuwa tangu amejiingiza kwenye biashara ya ushonaji, watu wengi ambao wamekuwa wateja wa biashara zake ni wa kawaida tu na wasanii wenzike hawazidi hata watatu. “Unapofanya maendeleo kwa sisi mastaa wenzako si kwamba wanapenda.

Wananuna ndiyo maana huwezi kuwaona wakikusapoti,” alisema Wolper.

Tanroads yatoa sababu ya ubomoaji Barabara ya Morogoro



      Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umesema kutofautiana kwa mita zinazotumika katika ubomoaji nyumba zilizoko kuanzia eneo la Ubungo na Kiluvya, kunatokana na Sheria ya Hifadhi ya Barabara ta Mwaka 1932 na mipango ya Serikali.

Tanroads imesema sheria hiyo inataja umbali tofauti wa hifadhi ya barabara katika baadhi ya maeneo na imeendelea kuwa mwongozo kwa Barabara ya Morogoro.

Nyumba zinazobomolewa kati ya Ubungo na Kimara ziko ndani ya mita 90 kutoka katikati ya barabara, wakati zilizobomolewa kutoka Kimara Stop Over hadi Kiluvya ziko ndani ya mita 121.9.

Akizungumza na Mwananchi jana, kaimu mkuu wa Idara ya Mipango Tanroads, mhandisi Elson Mwelanzi alisema tofauti hiyo inatokana na mipango ya Serikali.

“Katika sheria hii iliyoanza eneo la Faya hadi Ubungo ni mita 22.5, kutoka Ubungo hadi Kimara Mwisho ni mita 91.7 na kutoka Kimara Stop Over hadi Kiluvya ni mita 121.9 hayo ndiyo maeneo ya hifadhi ya barabara,” alisema Mwelanzi.

Alisema sababu ya Kimara Stop Over hadi Kiluvya kuwa na umbali wa mita 121.9 ni kutokana na mpango wa Serikali wa kuwa na hifadhi kubwa ya barabara.

“Hii sheria ilibadilishwa katika maeneo mengine mwaka 1967 na baadaye mwaka 2000, lakini katika hifadhi ya Barabara ya Morogoro haijawahi kubadilishwa. Sababu mojawapo ni kwamba hii ni barabara kuu hapa nchini,” alisema.

Alisema sheria hiyo ni nzuri kwa sababu inapunguza gharama za malipo kwa wakazi waliojenga ndani ya hifadhi.

“Ujenzi ndani ya hifadhi ya barabara unasababisha miradi kuwa na gharama nyingi si tu kwa ajili ya ujenzi, bali pia kulipa wakazi waliovamia maeneo,” alisema.

“Nakumbuka watu walilalamika na wakashauri sheria hii ibadilishwe, lakini mimi sishauri hii ibadilishwe ibaki kwa sababu watu hawatajenga ndani ya hifadhi ya barabara na miundombinu itapangwa vizuri,” alisema.   

Mama Kanumba kumtembelea Lulu Mahakamani



 

 Frola Mtegoa.

MAMA wa staa wa filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba, Frola Mtegoa amesema kuwa, kutokana na matatizo yaliyompata staa wa filamu Bongo Elizabeth Michael ‘Lulu’ baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili, amekuwa akimuonea huruma na anajipanga kumtembelea gerezani.

Akipiga stori na Ijumaa, Mtegoa alisema watu wengi wamekuwa wakihisi kuwa ana chuki na Lulu, lakini moyo wake unampenda na kama isingekuwa sheria kuhitaji Lulu kufungwa basi yeye asingekuwa na tatizo naye.



Staa wa filamu Bongo Elizabeth Michael ‘Lulu’

“Sina chuki na Lulu, tulikuwa karibu lakini nafikiri watu wake wanaozunguka ndiyo waliosababisha ukaribu wetu kuparanganyika. “Lakini moyoni ninampenda na kiimani mimi ni Mkristo.

Kwa hiyo siwezi kufurahi kuona mwenzangu anapata matatizo, ipo siku nitamtembelea gerezani!” alisema mama huyo.

Emmerson Mnangagwa kumrithi Mugabe



Emmerson Mnangagwa anatarajiwa kuapishwa kama rais wa Zimbabwe, kufuatia kuondoka kwa rais kuondoka kwa Robert Mugabe madarakani baada ya miaka 37 ya utawala wa kiimla.

Makamu huyo wa zamani wa rais ambaye alirejea kutoka uhamishoni Jumatano -ataapishwa kaka uwanja wa ndege wa Harare.

Kufutwa kwake kazi mwezi huu kulipelekea chama tawala cha Zanu-PF na jeshi kuingilia kati na kumlazimisha Mugabe ang'atuke .

Upinzani unamtaka Bwana Mnangagwa, ambae amekuwa mmoja wa watawala kumaliza "utamaduni wa ufisadi".

Taarifa ya kuondoka madarakani kwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 hapo siku ya Jumanne iliibua sherehe kubwa kote nchini Zimbabwe

Ilitolewa kwa njia ya barua bungeni na kikao cha kumpigia kura ya kutokuwa na imani nae kikakatizwa.

Katika barua hiyo Bwana Mugabe alisema anajiuzulu ili kuruhusu mchakato rahisi na wa amani wa ukabidhianaji mamlaka na kwamba uamuzi wake ulikuwa wa hiari.

Bwana Mugabe na mkewe Grace hawajaonekana hadharani tangu Jumapili, na haifahamiki wako wapi .

Alhamis , taarifa zilielezea kuwa Bwana Mugabe amepewa kinga ya kutoshtakiwa.

Televisheni ya taifa imesema kuwa atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Bwana Munangagwa.

Sherehe hizo zitafanyika katika uwanja wa michezo mjini Harare wenye viti 60,000- huku waandalizi wakiwataka waZimbabwe kuhudhuria kwa wingi sherehe hizo.

Alhamisi Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini (MDC ) alitoa wito wa kufanyika kwa mageuzi makubwa ya kisiasa ili kuondoa masuala yaliyoweka madarakani kwa muda mrefu utawala wa Bwana.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement fo Democratic Change (MDC) Morgan Tsvangirai
Bwana Munangagwa alikimbilia nchini Afrika Kusini wiki mbili zilizopita- na kurejea nchini Jumatano wiki hii ambapo alipokelewa kama shujaa.

Bwana Mnangagwa aliahidi kubuni ajira ambapo baadhi wanakadiria kuwa 90% ya watu hawana ajira.

"Tunataka kukuza uchumi wetu, tunataka amani, tunataka kazi, kazi, kazi ," aliuambia umati wa watu uliomshangilia mjini Harare.

Jumatano chama tawala cha ZANU PF kilisema kitafanya mageuzi kuondoa sheria zilizomfanya Mugabe kuwepo madarakani kwa muda mrefu.

Mbunge wa Songea mjini afariki dunia





Mbunge wa Songea Mjini kupitia CCM, Leonidas Gama amefariki dunia katika hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma akipatiwa matibabu.

Taaifa za kifo cha mbunge huyo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, na kusema kwamba marehemu alifariki dunia usiku wa saa 6 kuamkia leo.

Oddo Mwisho ameendelEa kwa kusema kwamba alipata taarifa kwamba Leonidas Gama alianguka ghafla usiku wa jana kutokana na tatizo la presha na kukimbizwa hospitali ya Peramiho, mpaka pale umauti ulipomkuta.

LeonidaS Gama amewahi kuhudumu kama mkuu wa WIlaya sehemu mbali mbali hapa nchini, na mwaka 2015 kugombea ubunge wa jimbo la Songea Mjini kupitia CCM.

Ikulu yakanusha taarifa hii



 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imekanusha taarifa za uteuzi zinazosambaa mitaondaoni ikiwa na majina ya wafuasi wa Chadema

Taarifa iliyotolewa asubuhi hii na Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu  Gerson Msigwa imesema kwamba Rais Magufuli hajafanya uteuzi.

"Taarifa hii ni ya uongo imetengenezwa na wahalifu ipuuzeni Mhe. Rais Magufuli hajafanya uteuzi huu" -  Msigwa


MAGAZETI YA LEO 24/11/2017

MAGAZETI YA LEO 24/11/2017



Thursday, 23 November 2017

Jokate: Rais Magufuli ni kama Musa Mkombozi wa Israeli


 Jokate Mwegelo ‘Kidoti’.

Kaimu Katibu Idara Ya Uhamasishaji, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ leo ameandika ujumbe mrefu mtandaoni ambao unasifia kazi na majukumu kadhaa aliyoyafanya Rais John Magufuli katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani.




Rais John Magufuli.

Katika ujumbe huo, Mwegelo ameifananisha kazi hiyo ya Magufuli na jukumu alilolifanya Nabii Musa la kuwatoa wana wa Israel kwenda Canaan, nchi ya ukombozi wao.  Ufuatao ndiyo ujumbe kamili aliouandika:

Musa alipitia vitu vingi ikiwemo kejeli, kujaribiwa na hatimae kufanikiwa kuwavusha Wana wa Israeli kuelekea nchi ya ahadi. Lakini kuna wakati wafuasi wake hao walipojaribiwa kidogo tu wakaanza kunung’unika na kumkebehi Musa kwamba ni kheri maisha waliyokuwa wanaishi Misri kwa Farao.

Rais John Pombe Magufuli ameianza safari yake nyingine baada ya Novemba 5 mwaka huu kufikisha miaka miwili madarakani. Napenda kuifananisha safari yake hiyo iliyosheheni mageuzi makubwa sawa na ile ya Wana wa Israeli walipokombolewa na Nabii Musa kutoka kwenye mikono ya utumwa chini ya Farao wa Misri.

Uwajibikaji, Uzalendo, Utendaji
Kumekuwa na tatizo tatizo la watumishi wa Serikali kutokuheshimu misingi ya kazi zao katika utumishi wao wa umma, nidhamu ya kazi ilikuwa haipo. Ilifikia wakati watu walitunga safari za nje ilimradi tu wapate posho za kujiendeleza wao na familia zao.

Uzalendo wa nchi ukageuka kuwa uzalendo unaokimu mtu na familia yake na watu wake wa karibu. Fedha nyingi zikawa zinapotea angani na hata matunda ya safari tulikuwa hatuyaoni. Bado barabara na miundimbinu muhimu ilikuwa kasi yake ya kuimarishwa haikuwa nzuri sana.

Utendaji na ubunifu ulikuwa wa chini kwani hakukuwa na kitu kipya katika utendaji wa kazi kwa wengi zaidi ya kujitajirisha kupitia kodi za wananchi bila sababu zozote zile za msingi.

Manung’uniko yalikuwa mengi juu ya rasilimali za taifa. Kulikuwa na makundi mengi yakizungumza kwa lawama namna rasilimali zilikuwa zinatumika vibaya. Makundi haya yakihusisha Wanasiasa, Wasomi na hata baadhi ya Wananchi wenye kufuatilia maslahi na rasilimali za taifa. Nchi yetu pendwa ya Tanzania ‘kuibiwa’ umekuwa ni mjadala wa muda mrefu bila utatuzi au hatua yoyote kuchukulliwa.

Kuna wakati, nikiamini kwa nia njema na uchungu wa nchi yao na si siasa, baadhi ya wanasiasa walipaza sauti kusema kuwa ni aibu kubwa kwa nchi yetu kushindwa hata kumiliki ndege yetu. Walihoji: “Tutatangazaje utalii bila ya kuwa na ndege yetu?” Kwa ufupi kila kitu kilikuwa kikionekana kwenda sivyo. Na hapa sijagusia issue ya “mafisadi”

Kuingia kwa Magufuli madarakani miaka miwili iliyopita, ukiyatazama maisha yake, utakubaliana nami kuwa huyu ni kiongozi anayeishi na kujituma kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Hii inanikumbusha nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka kadhaa ya nyuma, niliwahi kumuona Rais wetu ambaye kipindi kile alikuwa ni Waziri akila sehemu mmoja wanafunzi katika kijiwe maarufu cha misosi kiitwacho “Harvard”.

Pale chakula ni cha bei ya chini kabisa, mlo kamili mzuri ulikuwa hauzidi elfu 1000. Ilikuwa ni sehemu ya sisi wanafunzi wa kawaida kula kwa sababu ya bajeti zetu ndogo. Kumuona yeye kama waziri pale kulipelekea mimi kuanza kuelewa Dkt. Magufuli ni mtu wa aina gani. Ni wazi kwamba ni mtu wa watu, hana makuu, hajikwezi na anapenda “ku-budget.”

Mageuzi na Mabadiliko
Sishangai miaka miwili tu ya uongozi wake akiwa ameacha tayari alama na mageuzi makubwa ya kukumbukwa. Kwa kifupi tu ametenda yafuatayo ya kukumbukwa:

· Kuwezesha elimu bure kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari;

· Kufufua shirika la ndege la ATCL kwa nunua ndege mpya sita;

· Kuongeza mapato ya ndani toka trilioni 9.9 kwa mwaka hadi trilioni 14 kwa mwaka;

· Kurejesha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma;

· Ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania

· Kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma;

· Kutimiza ahadi ya Serikali kuhamia Dodoma;

· Kukamilisha miradi mikubwa wa umeme wa Kinyerezi I-extension na Kinyerezi II;

· Kuanza ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge;

· Uzalendo kusimamia raasilimali za taifa yakiwemo madini;

· Kuanza ujenzi wa barabara za juu Tazara, Ubungo na daraja la wapiti kwa miguu Furahisha;

· Ujenzi wa madaraja ya kisasa mfano la daraja la Kilombero;

· Kusimamia uhakika wa madawati maabara na maktaba katika shule zote nchini;

· Ujenzi wa maduka ya kisasa ya dawa za ndani ya kila hospitali ya Serikali;

· Kupambana vikali dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini;

· Kutoa bima za afya za matibabu ya bure kwa wazee

· Kuhakikisha wanafunzi wanaostahili kupata mikopo ya elimu ya juu wanapatiwa

· Kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwanda vya kutosha nchini

· Kufuta kodi na urasimu kwenye kilimo na uwekezaji nchini

· Kuhakikisha serikali inasimamia uuzwaji wa mazao ya wakulima masokoni na kupata faida. Mfano wakulima walikuwa wakiuza korosho zao kwa tsh 800 kwa kilo mpaka tsh 4000 kwak kilo.

Nimesukumwa kuzungumzia na kuorodhesha mafanikio haya kwa ufupi ili tujue shabaha ya rais wetu. Rais wetu anataka kurudhisha heshima. Heshima hailetwi kwa blah blah, heshima huletwa kwa vitendo na kufanya vitu kwa njia ya kuwa “disruptive”-kutokufanya vitu kikawaida au kwa mazoea.

Msimamo mkali wa rais

Rais Magufuli anataka kuona watu wakijituma na kuleta matokeo chanya. Hata ukiangalia safu zake za uongozi ni viongozi walioshiba kwenye nafasi zao. Na wanaonekana hawafai wanaondolewa. Ila bado kuna makundi ya watu kwenye jamii wanaona anachofanya ni kazi bure na kufikia hatua ya kuaminisha umma kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya hali imekuwa ngumu na eti haina malengo na kuwa imepoteza dira.

Hakuna ukombozi uliofanyika bila kutoa jasho, kutokwa damu na kutumia mbinu za kujifunga mikanda. Mheshimiwa Rais anafanya hilo, ni lazima kujitoa mhanga kwa kipindi hiki kwa ajili ya mafanikio ya muda mrefu. Nilifikiria viongozi wetu hasa wa upinzani wangefurahia mabadiliko haya kwa maana ndio kitu hasa walichokuwa wakikitamani na wakishiriki kikamilifu katika kutoa mawazo yenye kujenga ila hali imekuwa ni tofauti.

Hapa ndio maana nimekikumba kisa cha safari ya Mussa-maana nalifananisha hili na kadhia ya wale Wana wa Israeli kufikia hatua mpaka kumkufuru Mwenyezi Mungu na wakaona kuwa ni kheri wangebaki kule Misri. Kama kumbukumbu ya kuku, nao walisahau walipotoka.

Ushauri

Natambua ni vigumu kumuaminisha kila mtu ukweli kama tayari anaamini uongo, kama ilivyo vigumu kumuaminisha uongo yule ambaye anaamini ukweli. Ila kama vijana na taifa lililo la vijana, imefika wakati wa kila mmoja kusimamia kila anachokiamini, LAKINI asiamini kile alichoaminishwa. Vijana tuache siasa za kupikwa na kuungaunga, tusimame katika ukweli na mambo yale ambayo yana maslahi kwa taifa letu na si maslahi binafsi. Tujiulize: Inakuwa vipi, wanasiasa na wanaharakati wale wale ambao walikuwa wanapigania vitu flani vifanyiwe kazi, sasa vinafanyiwa ndiyo wa kwanza kununa na kufanya ‘confusion’ mbele ya Jamii?

Ndani ya chama cha Mapinduzi tunaamini Umoja ni Ushindi. Huu ni wakati wa kuungana na Mheshimiwa Rais katika ukombozi wa Watanzania, lazima tuelewe shabaha ya Rais wetu kuwa ana nia njema na maendeleo ya nchi yetu.

Hii safari sio rahisi, hakuna aliyemkamilifu ila wote tunaitumainia Tanzania yenye neema. Vijana tuache kupokea mapokeo ya wanasiasa wasio na nia njema na nchi yetu, tufanye kazi kwa kushirikiana katika kuiletea nchi hii neema.

Hapa Kazi Tu!
Jokate Mwegelo
Kaimu Katibu Idara Ya Uhamasishaji,
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) makao makuu


Mgombea azuiwa kufanya kampeni



Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kufanyika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini, mgombea wa Chadema wa Saranga amewekewa pingamizi la kufanya kampeni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga uchaguzi mdogo wa udiwani kufanyika Novemba 26,2017.

Mgombea huyo, Ephraim Kinyafu wa Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam amewekewa pingamizi na Chama cha Wananchi (CUF) la kutofanya kampeni kwa siku zilizobaki.

Kampeni za uchaguzi huo zitahitimishwa Novemba 25,2017.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni mtendaji wa Kata ya Saranga, Dandasi Kijo amesema leo Alhamisi Novemba 23,2017 kuwa mgombea huyo amewekewa pingamizi baada ya kukiuka masharti ya kampeni.

Kijo amesema kanuni aliyokiuka ni kutamka akiwa jukwaani kuwa CUF haijasimamisha mgombea katika kata hiyo.

Akizungumzia pingamizi hilo, Kinyafu amesema hajashirikishwa kwa lolote hivyo hatambui uamuzi huo wa Jumanne Novemba 21,2017.

Kinyafu ambaye amekata rufaa ngazi ya wilaya, amesema katika kikao kilichofikia uamuzi huo Chadema iliwakilishwa na mjumbe badala ya katibu wa wilaya.

Mgombea huyo amesema hajawahi kupewa barua ya malalamiko wala muda wa kujitetea. Amesema rufaa aliyokata ngazi ya wilaya inasikilizwa leo.

Raila arejea Kenya baada ya mapumziko mafupi



Zanzibar/Nairobi. Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa nchini Kenya, Raila Odinga amerejea nyumbani baada ya kujichimbia kwa siku nne Zanzibar nchini Tanzania.

Mwanasiasa huyo ambaye amegoma kuutambua ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa visiwani Zanzibar kwa mapumziko baada ya kumaliza ziara ya siku 10 nchini Marekani.

Taarifa za kurejea nyumbani kiongozi huyo zimethibitishwa na msemaji wake, Dennis Onyango ambaye aliliambia gazeti la Nation kuwa Odinga amerejea Kenya.

Pia, mkurugenzi wa mawasiliano wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Philip Etale amezungumzia kuwasili kwa Odinga mjini Nairobi.

Ingawa baadhi ya picha zimekuwa zikimuonyesha mwanasiasa huyo akiwa mapumzikoni katika hoteli moja Zanzibar lakini ziara yake imehusishwa na hali ya kisiasa nchini mwake.

Mapokezi ya Odinga mwishoni mwa wiki aliporejea Kenya baada ya kuwa nje ya nchi kwa siku 10 yalikumbwa na taharuki baada ya kutokea ghasia zilizohusisha wafuasi wake na polisi.