Friday, 24 November 2017

Breaking Newz: Rais Magufuli amteua Dkt Wilbroad Slaa kuwa Balozi



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amteua Dkt. Wilbrod Peter Slaa kuwa Balozi.

Uteuzi wa Dkt Wilbroad Slaa umefanyika leo Novemba 23 ambapo anategemea kuapishwa baada ya utaratibu kukamilika.

Dkt Slaa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na mwaka 2015 karibu na kipindi cha uchaguzi alitangaza kuachana na siasa.




VIDEO: Kafulila afunguka mazito yaliyomuondoa CHADEMA



Mbunge wa zamani David Kafulila amefunguka sababu ya kujivua uanachama wa Chadema na kusema kuwa chanzo ni "Ajenda" ambazo kwa sasa chama hicho hakifuati misingi na kanuni za Chama.

                               SEHEMU YA PILI..


Robert Mugabe kuhudhuria kuapishwa kwa rais mpya wa Zimbabwe




Robert Mugabe anatarajiwa kuhudhuria kuapishwa kwa rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kulingana na runinga ya habari ya taifa hilo ZBC .

Maandalizi yameanza katika uwanja wa kitaifa wa michezo katika mji mkuu wa Harare ambapo hafla hiyo itafanyika.

Mwandishi wa maswala ya kidiplomasia Judith Makwanya amesema kuwa kiongozi anayeondoka anatarajiwa kukagua gwaride akitoa kwaheri huku kiongozi mpya akilijulisha jeshi katika sherehe hiyo ya gwaride.

Tayari waziri wa Uingereza barani Afrika Rory Stewart amewasili nchini Zimbabwe mapema kulinga na chombo cha habari cha AFP.

Afisa huyo amewasili tayari kuhudhuria kuapishwa kwa rais mpya siku ya Ijumaa.

Bwana Sterwart anatarajiwa kukutana na viongozi wa kisiasa na wale wa kibiashara pamoja na makundi ya haki za kibinaadamu na mashirika yasiokuwa ya kiserikali kulingana na waziri wa maswala ya kigeni nchini Uingereza.

Ametaja mabadiliko hayo ya kihistoria kuwa wakati muhimu baada ya utawala mbaya wa rais wa zamani Robert Mugabe.

Uingereza inataka kuwa mshirika wa kweli wa raia wa Zimbabwe wakati huu ambao wanaanza mwanzo mpya, bwana Stewart aliambia AFP

Angola: Balozi amtaka rais wa zamani Eduardo dos Santos kushtakiwa




Balozi wa Angola nchini Tanzania amemtaka rais wa zamani wa taifa hilo Jose Eduardo dos Santos kushtakiwa kwa madai ya uhalifu aliyotekeleza wakati wa utawala wake wa miaka 38.

Ambrosio Lukoki amesema kuwa bwana dos Santos anafaa kujiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha MPLA kwa kuwa alikuwa anatumia wadhfa wake huo kuzuia kushtakiwa.

Rais mpya wa Angola Joao Lourenco hivi majuzi aliwafuta kazi wakuu wa polisi na vitengo vya ujasusi ,hatua iliokiuka sheria kwamba hatofanya hivyo kwa kipindi cha miaka minane.

Pia alimfuta kazi mwanawe bwana Dos Santos ambaye ni bilionea kama mkuu wa kampuni ya mafuta ya taifa hilo.

Bwana Lourenco kwa jina la utani JLo alichaguliwa na bwana Santos kusimama katika uchaguzi wa mwezi Agosti na wakati huo wachaganuzi walidhani kwamba ataendeleza uongozi wa bwana Santos.

TPA yakamata wezi wa kamba za kutia nanga



Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na Polisi wamewakamata watu saba ambao wamekuwa wakiiba kamba ambazo hutumiwa na meli wakati kutia nanga.

Watuhumiwa hao wamefanya  uhalifu huo kati ya Juni na Septemba mwaka huu kwa kuiba kwenye meli za Mv Northern Decision na Mv MSC Kerry.

Akizungumza  leo Alhamis Novemba 23 Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema wizi huo ulitokea Juni na Septemba.

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na sehemu ya kamba zilizoibwa ambayo ni mita 150.“Tumewakamata watuhumiwa wakiwa na kamba yenye urefu wa mita 100 kwa kuwa mita 50 walikuwa wameshaiba,” amesema

Amesema wizi huo ulifanyika wakati meli hizo zikiwa zimeegesha nje ya bandari ya Dar es Salaam zikisubiri kuruhusiwa kutia nanga.

Amesema kamba hizo zimekuwa zikitumika kutengenezea nyavu za kuvulia na kuezekea makuti kwa kuwa huwa haziozi.

Amesema watuhumia hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kigamboni na Zanzibar wakiwa katika harakati za kuziuza.

Amesema mbali na kamba, pia wamekamata gari dogo ambalo lilikuwa limebeba kamba hizo.Amesema watuhumiwa hao watafikishwa hivi karibuni mahakamani.

Amesema mamlaka hiyo imeongeza ulinzi bandarini ili kuhakikisha kwamba vitendo vya uhalifu vinakomeshwa.

“Tunachukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa hawa ili kuwaonyesha wenye meli na mawakala kuwa tunadhibiti matukio ya aina hii,” amesema.

Hivi karibuni, uongozi wa bandari ulisema ili kuimarisha usalama, umefunga camera maalum zaidi ya 400 ambazo zinaonyesha kila shughuli inayoendelea katika bandari.

Kafulila asema ndoa yake haihusiani na siasa



Daudi Kafulila ambaye hapo jana amekihama chama cha CHADEMA, amesema suala la mke wake kuridhia au kutoridhia kwa yeye kuhama chama wakati yeye ni Mbunge wa chama hiko, ni suala ambalo halihusiani na ndoa yao.

Kafulila ameyasema hayo leo na kueleza kwamba linapokuja suala la ndoa hapo ndio huwa lazima wafikie makubaliano, lakini ikija suala la kisiasa kila mtu ana uamuzi wake ambao hawaingiliani kwani ndoa yao ilifngwa kanisani na sio kwenye chama.

“Haya ni maamuzi ya kisisasa, sisi ndoa yetu ilifungwa kanisani haikufungwa kwa mwenyekiti wa chama au kwenye chama, kwa hiyo ndoa ni jambo jingine na harakati ni mjambo jingine, yeye ni mke wangu lakini haimaanishi tunakubaliana kwenye kila kitu, tunakubaliana kwenye mambo ya ndoa, kwenye siasa kila mtu anaweza akatazama jinsi anavyotazama yeye na sio shida”, amesema Kafulila.

Hivi sasa kumekuwa na mvutano kati ya wanandoa hao baada ya Kafulila kuhama CHADEMA, huku mke wake akisema hakuwa na taarifa zozote, na hata hizo sababu zake za kuhama hazina ukweli na kumtaka aweke wazi sababu rasmi za kufanya hivyo

Waziri Mkuu akipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi Kukodi Makampuni



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi makampuni ya kufanya kazi mbalimbali kwa niaba yake, akisema kuwa kitendo hicho kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya makampuni wanayoyapa kazi hayakidhi vigezo.

Waziri Mkuu  ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 23, 2017) kwenye ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu Ardhi.

“Kama kuna umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi vizuri ili kujiepusha na matatizo," amesema na kukiagiza chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia. Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela, uharibifu wa mazingira na majanga ya asili kama mafuriko.

Amesema Serikali inaamini kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa imeweka mkazo wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kupato cha kati ifikapo 2025, hivyo wanahitajika wataalamu wa kutosha na wenye weledi.

“Hivyo Chuo Kikuu cha Ardhi kama taasisi ya Serikali inawajibu mkubwa wa kutayarisha wataalamu mbalimbali wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira," amesema Waziri Mkuu na kukitaka chuo kitumie fursa hiyo ya kuadhimisha miaka 10 ya chuo hicho kujitafakari na kuona ni kwa namna gani wanaweza kuwekeza zaidi ili kuongeza tija ya uwepo wa taasisi hiyo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Wekeni mikakati madhibuti itakayowezesha chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Siku zote mjikite katika kutafuta kuwa na ubora zaidi ya wakati uliopita," alisisitiza.
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali inakkitegemea chuo hicho katika kufanikisha ajenda yake ya uchumi wa viwanda kwa kuwa kinatoa wataalamu wengi.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya, Mwenyekiti wa Baraza la chuo Bibi Tabitha Siwale, Makamu Mkuu wa chuo Profesa Evaristo Liwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.

Yanga yasema Uwanja wa Kaunda lazima ukamilike



Yanga haitanii bwana! Hakika ndilo neno sahihi la kulitumia baada ya wanachama wa klabu hio kuungana na uongozi wao kujaza vifusi kwenye Uwanja wao wa Mazoezi wa Kaunda ikiwa ni matengenezo ya hatua ya kwanza.

Mchakato huo wa kujaza vifusi kwenye sehemu ya kuchezea ya uwanja huo unaotuamisha maji wakati wa mvua nyingi, unafanikishwa kwa asilimia kubwa na nguvu za wanachama wa klabu hio walioamua kujitolea.

Hio ni awamu ya kwanza kabla ya mchakato huo kuhamia kwenye awamu ya pili na tatu ili kukamilisha mchakato mzima unaoaminika kuwa utapunguza gharama kwa klabu hio, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwassa amethibitisha juu ya hilo.

“Tumeanza mchakato wa kupajaza, kwa ushirikiano wa wanachama, tunaamini malengo yetu yatatimia, malengo yetu ni kupajaza hapa ili kupunguza gharama, tunafanya kazi na wanachama, hatujaweka mikakati ya kumpa mkandarasi yeyote kwa sasa,” amethibitisha Mkwassa.

Okwi bado hana nafasi ya kuivaa Lipuli



Simba imeendelea kujifua lakini kiungo mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi bado hajawa fiti na tayari kuichezea Simba katika mechi dhidi ya Lipuli.

Simba itaivaa Lipuli katika mechi yake ya 11 ya Ligi Kuu Bara katika msimu huu. Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Okwi ambaye ni kinara w akufunga mabao aliumia enka na inaonekana bado hajawa fiti kwa kuwa hakushiriki mazoezi ya Simba leo.

AFYA:Faida Zitokanazo Na Matumizi Ya Mapapai



ASILI ya mpapai ni Amerika ya Kati, ambapo kuanzia matunda, majani na utomvu wa mmea huu hutumiwa kama dawa maeneo mbalimbali duniani. Vile vile, matunda na utomvu wake yamekuwa yakitumika kutengeneza pombe na mvinyo katika baadhi ya nchi, huku wengine wakitumia mpapai kama dawa kwa mifugo na binadamu.

Inaelezwa kuwapo na tafiti zilizowahi kufanyika na kuchapishwa katika jarida lijulikanalo kwa jina la ‘Archieve’ la nchini India mnamo Oktoba 27 mwaka 2010, ambapo jarida hilo lilieleza kwamba juisi ya majani ya mpapai iliweza kusaidia wagonjwa watano waliowahi kupata homa ya dengue.

Mbali na utafiti huo, pia kuna tafiti zilizowahi kufanywa na madaktari wa nchini Marekani na Japani na kubaini kuwa, juisi ya majani ya mpapai ina uwezo wa kutibu malaria na saratani, japokuwa tafiti hizo hazikukubawaliwa kisayansi.
Faida za kiafya za tunda la papai

Aidha, wataalam wa lishe nao wanaeleza kwamba, watu wenye matatizo ya kupatwa na majipu, uvimbe na vidonda mara kwa mara huwa na upungufu wa virutubisho muhimu, ambavyo huweza kupatikana ndani ya papai, hivyo imegundulika watu wenye matatizo hayo wakitumia papai hupata nafuu na kupona haraka.

Pia papai husaidia kuleta nuru ya macho, kama inavyoaminika kwa karoti, hali kadhalika papai pia husaidia kupunguza madhara yatokanayo na moshi wa sigara.

Hivyo wavutaji wa sigara ni vyema wakatumia tunda hili mara kwa mara ili kujipunguzia madhara ya moshi wa sigara, ingawaje ni vyema wakakumbuka matumizi ya sigara si mazuri kwa afya hivyo ikibidi ni vizuri kuacha kabisa.

Ni wazi kuwa papai ni tunda lililosheheni kila aina ya utajiri wa vitamin kuliko matunda mengine, kwani lina vitamin A, B, C, D na E.

Wataalam wa tiba za asilia pia wanaeleza kwamba tunda hili linauwezo wa kutibu tatizo la usagaji wa chakula tumboni pia hutibu kisukari na pumu na mara nyingine hata kifua kikuu.

Tunda la papai lina faida nyingi sana kwa afya ya mwanadamu. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na kuwa na uwezo wa:


  • Kutibu tatizo la Shida ya kusaga chakula tumboni
  • Kutibu Udhaifu wa tumbo
  • Kutibu Kisukari na asthma au pumu.
  • Kutibu Kikohozi kitokacho mapafuni
  • Kutibu Kifua kikuu
  • Tunda hili huleta afya nzuri ukitumia kila siku
  • Maziwa yanayotoka katika jani lake huponya vidonda
  • Vilevile yanasaidia kutibu sehemu palipoungua moto
  • Kama hiyo haitoshi, maziwa yanayotoka katika jani la mpapai yanatibu kiungulia na Ugonjwa wa colon (njia ya haja kubwa ndani)

Pia yanasaidia kutofunga choo
Maganda ya tunda la papai yanasaidia kutibu tatizo la kuungua, vipele na saratani ya ngozi.
Mbegu zake zinatibu ini zikitafunwa 10 – 12 kwa siku 5.
Majani yake yakaushie ndani, yanatibu pumu. Inapoanza kubana yachome majani yaliyokaushwa kisha jifukize, kule kubanwa kutakisha.
Majani yake yanasaidia katika kutibu shinikizo la damu.
Papai likimenywa na kupondwa linafaa Sana katika masuala ya urembo kwani linaweza kutumika Kama vile unavyotumia lotion kulainisha uso.
Mbegu za papai zina uwezo wa kutibu homa. Meza mbegu za papai kiasi cha kijiko cha chakula mara 3 kwa ajili ya kutibu homa.
Mbegu za papai zilizokaushwa ndani kisha zikasagwa kuwa unga zinatibu malaria, tumia kijiko 1 cha chai changanya na uji, kunywa mara 3 kwa siku 5 Mgonjwa wa kifua kikuu akila matunda haya kwa muda mrefu atapona bila dawa nyingine.
Mizizi yake ikipondwa na kulowekwa katika maji yaliyochemshwa, lita 2 na nusu kwa dakika 15, yanatibu figo, bladder, yanazuia kutapika. Nusu kikombe cha chai kutwa mara 3 kwa siku 5.

Tikiti maji


TIKITI MAJI ni moja ya matunda yanayolimwa sana katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania tofauti na miaka iliyopita.

Hii inaashiria kwamba tunda la tikiti maji linaliwa sana katika maeneo hayo kutokana na faida inayopatikana kwenye tunda hilo.


Faida ya kutafuna mbegu za tikiti maji
Pamoja na kuongezeka kuliwa kwa tunda la tikiti maji lakini wengi wa wateja wanaokula tunda hilo huwa hawajui faida ya mbegu za tunda hilo.
Kutokana hali hiyo wengi wanaokula tikiti maji wanatema mbegu hizo na huenda wengi walikuwa na imani potofu inayokataza kula mbegu za tunda.
Hivyo badala ya kuzitafuna mbegu hizo wengi huzitema na kuona ni kitu kisicho na faida yoyote katika mwili wa binadamu.


Lakini mbegu hizo zinatakiwa kutafunwa wakati unapokula tunda lenyewe na hii ni kutokana na faida zake kiafya.

Unapokula tunda la tikiti maji unachotakiwa kufanya ni kuzitoa mbegu zake na kuziweka kwenye chombo kimoja mpaka zichipue yaani kuanza kutoa mizizi.


Baada ya hapo unatakiwa uzikaushe tayari kwa kuzitumia kutoka na faida hizi zifuatazo:
Mbegu za tikiti maji zina protini nyingi hivyo kuzitafuna kunaweza kumpatia mlaji chanzo cha protini.
Pia aunzi mmoja tu (takriban ujazo wa 1/8 wa kikombe) inakupa virubutisho vya protini vya gramu 10.


Hii ni sawa sawa na kiwango kinachopatikana kutoka katika yogati ya Kigiriki wakati wa kustaftahi. 
Mbegu ‘zilizochipua’ zimemea na mara nyingi zina virutubisho vya hali ya juu kuliko zile ambazo hazichipua.

Kuchipua kunaondoa mchanganyiko katika chakula ambacho husababisha ugumu wa kufyonza virutubisho vyote.

Mbegu za tikiti maji zilizochipua zikitafunwa huongeza msongamano wa virutubisho na kusababisha urahisi kumeng’enya chakula. 
Kuhusu tikitimaji, mbegu hutolewa ngozi nyeusi ya juu na kubaki ikifanana na mbegu zilivyo.
Katika mbegu za zamani hili halipatikana lakini umegundulika kwamba kweli mbegu hizi zinaleta afya kwenye mlo.


Mbegu za tikiti maji zilizochepua zina protini, vitamin B, Magnesia, na mafuta ambayo hayakoleza.
Wataalamu wa masuala ya chakula wanasema mafuta yaliyokolezwa mara nyingi hayana viwango vya lehemu na muasho na yanaondoa hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na kiharusi.



Kama umeshawahi kutafuna mbegu za matikiti maji wakati ukila tunda hilo uligundua ladha yake ni sawa na tunda lenyewe. 
Mbegu za matikiti maji ni sawa na mbegu za alizeti kwa ladha, lakini haina lozi kubwa. 


Zinakuwa na ladha nzuri zaidi zikiwa kwenye kachumbari, iliyochanganywa pamoja au ukiila ikiwa mkononi mwako.
Jungu na mbegu nyingi ni nzuri kwa mwili wa mwanadamu, lakini ukilinganisha ukubwa wa lishe unaopatikana basi mbegu za matikiti maji
Kama vile haitoshi tunda hili limejaaliwa virutubisho kadha wa kadha vyenye faida kubwa katika afya ya mwanadamu.

Licha ya 92% ya tikiti maji kuwa ni maji, bado zile 8% zilizobaki zina faida kubwa sana kiafya jambo linaloonekana kutofahamika kwa wengi. Zifuatazo ni baadhi tu ya faida chache kati ya nyingi za tunda hili la tikiti maji:

Tikiti maji ni chanzo kizuri cha vitamini. Katika tunda hilo kuna Vitamin A, inayosaidia kuboresha afya ya macho na pia kuondosha sumu mwilini; Vitamin C, inayosaidia kuboresha kinga, kuponya majeraha, kukinga uharifu wa seli, kuboresha afya meno na fizi; na vitamini B6, inayosaidia ubongo kufanya kazi na pia kuibadilisha protini kuwa nishati.

Tabia 6 za kufuata kupata ngozi laini bila madoa/beauty habits to get glowing skin



1.TUMIA ANTIOXIDANT SERUM.
Sio kila mtu ana bahati ya kupata ngozi laini na nyororo bila kuifanyia kazi. Kwa wengine it a must to work hard ili kupata that perfect skin you have always wanted.

So Ladies you have to change your beauty routine, unatakiwa uanze asubuhi yako in a healthy way. Jinsi unavyoanza siku yako itaonesha kwenye uso wako.

Antioxidants kama vile Vitamin C&E hulinda ngozi yako ili isi dehydrate na pia zile aging radicals zitalindwa from UV-ray pollution na bad dietary habits(kula vibaya). Paka antioxidant serum baada tu ya kutoka kuoga, subiri dakika chache then paka moisturizer yako.

2.KULA PROTEIN YA KUTOSHA.
Kula breakfast ambayo ipo high in protein, husisha mayai, karanga, yogurt nk. Hivi husaidia kujenga collagen ambayo ndio kitu kikubwa ambacho hukusaidia ngozi yako isizeeke mapema. Ngozi yako haitokuwa na mikunjo wala kutepeta. Watu ambao hula protein for breakfast hula kidogo for the rest of the day, na pia protein husaidia kukuza nywele zako.

3.TUMIA SPF.

SPF ni lazima. Kila mmoja weto anapaswa kutumia SPF, hata kama wewe ni mweusi. Na kama hutumii kisa tu unaona kuwa makeup yako na moisturizer yako ina SPF, hiyo haitoshi. Paka SPF usoni, kwenye shingo, juu ya macho, kwenye lips, nyuma ya mikono, yani paka sehemu zote ambazo huwahi kuanza kuzeeka.

 4. HYDRATE! KUNYWA MAJI YA KUTOSHA.
Maji ni part kubwa sana ya urembo wa kila mtu. Kila asubuhi baada tu ya kuamka chukua maji ya uvuguvugu kamulia ndimu nusu kisha kunywa. Hii itasaidia kujenga more collagen..na ku-replenish ngozi yako.



5. MOVE YOUR BODY! EXERCISE
Si lazima kufanya yale mazoezi ya kufa mtu, No. Lakini ni lazima angalau uufanyishe mwili wako kazi kidogo. Unaweza hata ukaanza tu na mazoezi ya dakika 10-15 kila siku hadi utakapozoea.

Unaweza ukachagua kufanya Yoga. Kwa kifupi ni fanya kitu chochote ili kufanya heart rate yako ipande asubuhi, kunyoosha viungo vyako, ku-sweat kidogo. Lakini kama unajiweza si mbaya kufanya mazoeze haswa.

Mazoezi yatakupa nguvu for the rest of the day, pumps your blood na kukupa a glow kwa uso wako.

6. KUNYWA GREEN TEA
Yes Loves, green tea sio kwa ajili ya kukufanya upungue tu, bali husaidia pia ngozi yako. Ina-slowdown ageing process ya ngozi yako na kuifanya ionekane bado nzuri.



Lissu yupo tayari kutaja waliomshambulia



 Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu mwezi mmoja kuanzia sasa.

Familia yake imesema Lissu baada ya kupata matibabu nje ya nchi amepanga kufanya mambo matano akirejea salama

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23, kaka wa Tundu Lissu, Wakili Alute Mughwai alisema taratibu za kumsafirisha nje ya nchi zimeanza.

Lissu, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu na mwanasheria mkuu wa chadema amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba7.

“Awamu ya tatu ya matibabu yake ni maalumu sana kwani itahusu pia mazoezi ambayo kama haitafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa kudumu,”alisema.

Hata hivyo, alisema Lissu atapelekwa nje kwa ndege ya kawaida tofauti na hali yake ya awali alipotakiwa kusafirishwa na ndege maalumu za wagonjwa.

“Itatolewa taarifa ni lini ataondoka kwa matibabu na atakwenda nchi gani, hasa baada ya kupata ushauri wa mwisho wa madaktari katika hospitali Nairobi,” alisema.

Mambo matano ya Lissu akirejea nchini

Mughwai alisema amezungumza na Lissu akiwa Hospitali Nairobi na amemueleza kuwa akirejea tu nchini, kuna mambo makubwa matano ambayo atafanya.

Alisema jambo la kwanza, ambalo atafanya ni kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kuokoa maisha yake siku aliyopigwa risasi.

Wakili Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na msikitini kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada maalumu.

“Baada ya ibada, tutaangalia utaratibu kifamilia kama itawezekana kwenda kufanya matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika vita miaka 200 iliyopita,” alisema.

Alisema baada ya hapo, anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale alipoishia kwa ari kubwa .

Wakili Mughwai alisema jambo la tano atahakikisha anasimama na kupambana kisheria na watu waliotaka kukatisha maisha yake baada ya kumpiga risasi.

“Amesema atahakikisha anasimamia jambo hili kwa uwezo wake wote ili kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria waliohusika na uovu huo,” alisema.

Familia yataka Lissu akahojiwe Nairobi

Akizungumzia juu ya upelelezi wa shauri la Lissu, Mughwai alisema bado msimamo wao upo palepale wanaomba wapelelezi kutoka nje ya nchi washirikiane na wapelelezi wa ndani kuwakamata watuhumiwa.

Alisema ingawa familia ya Lissu iliandika barua tangu Septemba 16, kutaka wapelelezi wa kimataifa na kujibiwa na mwanasheria mkuu Septemba 20 kuwa jukumu la upelelezi ni la polisi.

“Tunataka wapelelezi wa nje kushirikiana na wa ndani kwa sababu hatuna imani na upelelezi kutokana na kasi ndogo kwani hadi sasa wamekuwa wakieleza kukwama upelelezi kutokana na kutomuhoji dereva wa Lissu,”alisema.

Hata hivyo, alisema kwa sasa Lissu anaweza kuongea mwenyewe hivyo, jeshi la polisi linaweza kwenda Nairobi kumuhoji na atawapa maelezo yote ikiwepo watu ambao aliwatambua.

“Bila shaka Lissu atawaeleza watu hao, walimshambulia kwa sababu gani,”alisema.

Familia yaelezea gharama

Katika hatua nyingine, Mughwai alisema Oktoba 2, familia ya Lissu ilikutana na viongozi wa bunge kujadili matibabu yake ambayo ni haki yake kisheria.

Alisema baada ya mazungumzo hayo, Oktoba 8, familia iliandika barua rasmi kwa katibu wa bunge kwa kuzingatia sheria ya bunge namba 14 kifungu cha 24 kuhusu stahiki za mbunge.

Alisema barua hiyo, ilipelekwa bungeni kwa kutumia shirika la kubeba mizigo na vifurushi la DHL na kupokelewa Oktoba 19 na baadaye aliwasiliana na Spika Job Ndugai na kumweleza juu ya barua hiyo na aliahidiwa kuwa suala hilo litashughuliwa.

Hata hivyo, alisema familia haijapata mrejesho tangu wakati huo hadi Novomba 11, alipoamua kumpigia katibu mpya wa bunge baada ya kushauriwa na Spika Ndugai ambaye aliahidi kufuatilia.

“Hivyo hadi sasa bado Bunge halijaanza kugharamia matibabu ya Lissu kama sheria inavyosema na Lissu amekuwa akitibiwa kwa michango ya watu mbali mbali,” alisema

Alisema michango hiyo ambayo inakusanywa katika akaunti maalumu ya Chadema na pia kupitia chama cha mawakili(TLS) ndio hadi sasa inatumika.

“Tutaendelea kulitaka Bunge kugharamia matibabu kwani sio suala la hiari, ni haki ya mbunge lakini pia tunaomba wananchi waendelee kuchangia matibabu ya Lissu kupitia akaunti iliyotolewa na Chadema, chama cha TLS na kwa familia”alisema

Akanusha mgawanyiko juu ya matibabu

Katika hatua nyingine, Mughwai alisema, familia ya Lissu, Chadema na chama cha Mawakili wa Tanganyika(TLS), hawana mgawanyiko wowote juu ya matibabu ama hatua zinazoendelea za kumtibu Lissu.

Wakili Mughwai alisema wanasikitishwa na taarifa kuwa familia imegawanyika juu ya uamuzi wa kuliomba bunge kugharamia matibabu ya Lissu.

“Tupo kitu kimoja wote familia yetu tupo pamoja kwa yote na Lissu anajua hatua zote kwani hata makamishna wa bunge walipomtembelea Oktoba 23 aliwauliza kuhusu stahiki zake kama mbunge,”alisema.

Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nje ya nyumba yake akirejea kutoka vikao vya bunge Dodoma, Septemba 7 na kukimbizwa hospitali ya Nairobi kwa matibabu ambapo hadi sasa anapatiwa matibabu.

Kinana, Nape waunganisha nguvu tena



     Arumeru. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wameunganisha nguvu katika Kata ya Makiba ambako wanampigia debe mgombea wa chama hicho, Samson Laizer.

Kinana na Nape wanachukuliwa kama wanasiasa waliofanya kazi kubwa ya kuhuisha nguvu ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kuzunguka karibu nchi nzima kupiga siasa na wakati mwingine kudiriki hata kuwasema hadharani mawaziri wa Serikali ya CCM, wakiwaita mizigo.

Jana wawili hao waliungana na Mrisho Gambo, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Arusha na Alexander Mnyeti (Manyara) kuipigia debe CCM.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Makiba wilayani Arumeru, Kinana alisema ni vigumu vyama vya upinzani kushika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kinana alisema akiwa katibu mkuu wa CCM ametembelea mikoa, wilaya na kata tofauti ambako ameona wananchi wana imani kubwa na chama hicho.

Kinana alisema katika uchaguzi mkuu uliopita wananchi wa eneo hilo walipiga kura kwa kufuata upepo na ushabiki wakidhani upinzani ungeshinda.

“Watu walidhani rafiki yangu yule, mnamjua siwezi kumtaja, atakuwa Rais, lakini hakuweza kupata nafasi hiyo,” alisema Kinana.

Alimpongeza Gambo kwa kufanikisha maendeleo ya mkoa huo na hasa eneo la Makiba.

“Pia mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alifanya kazi kubwa alipokuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru. Anastahili hongera nyingi,” alisema Kinana.

Alisema maendeleo hayana ushabiki hivyo wananchi wa Makiba wanapaswa kumchagua Laizer ili asimamie maendeleo.

Alisema miradi ya maendeleo kama wa umeme vijijini (Rea), maji, ujenzi wa barabara ya Mirerani unapaswa kusimamiwa na diwani wa CCM na si wa upinzani.

Alisema CCM ndicho chama kilichoshinda uchaguzi hivyo kinatekeleza ilani yake na hata wapinzani wanatekeleza ilani hiyo.

Naye Nape, ambaye alizunguka nchini na Kinana wakati akiwa katibu wa itikadi na uenezi, alisema wananchi wa kata hiyo wasirudie makosa kwa kuweka ushabiki na kumchagua mgombea wa upinzani.

Alisema kata hiyo ni ya CCM ndiyo sababu wanaitaka kwa gharama yoyote kiasi cha viongozi kwenda eneo hilo kushiriki katika kampeni. Aliwataja viongozi hao kuwa ni yeye mwenyewe, Kinana na wakuu wa mikoa ya Arusha na Manyara.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer alisema ameshapeleka ombi la wananchi wa mkoa huo kuwa walikosea kwa kuchagua upinzani mwaka 2015.

Laizer alisema salamu hizo ameshazifikisha na Rais Magufuli ameridhia kutoa msamaha kwa wananchi wa eneo hilo ambalo walidhani kanda ya kaskazini inatosha kumchagua Rais wa nchi.

Mgombea Laizer aliwaomba wananchi wa kata ya Makiba kumchagua kwa wingi awe diwani wao kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya eneo hilo.

Laizer aliwaahidi utumishi uliotukuka pindi wakimchagua kwani yeye ni mtu wa maendeleo na anayeweza kutumwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Meru.

Naye Mnyeti, ambaye ametajwa katika kashfa ya tuhuma za kuhonga madiwani wajiondoe CCM na hivyo kusababisha uchaguzi mdogo unaoendelea sehemu mbalimbali nchini ukiwemo wa kata hiyo, alisema wananchi wa eneo hilo walishamuahidi kuwa watamchagua mgombea wa CCM hivyo hana wasiwasi na hilo.

Mnyeti alisema kwa muda wote aliokuwa mkuu wa wilaya hiyo alishirikiana na wananchi wa Makiba, hivyo watamchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane ipasavyo na mkuu mwingine wa wilaya hiyo atakayechaguliwa na Rais.

Naye Gambo alisema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kumchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane naye kuleta maendeleo.

Gambo alisema awali walifanya makosa kwa kumchagua mpinzani hivyo wasifanye tena makosa.