Friday, 3 November 2017

Nape Nnauye amfungukia Nyarandu

Baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini kujivua ubunge na kujiondoa katika chama cha Mapinduzi(CCM), Lazaro Nyalandu hatimae Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema kuwa Chama cha siasa ni Itikadi.

Nape kupitia ukurasa wake wa twitter ameweka picha inayomuonyesha mbunge huyo na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ndg Kinana wakiwa wameweka kwa pamoja alama ya kidole gumba.

Chama cha siasa ni ITIKADI, itikadi ni IMANI.Siamini SANA katika kubadili Imani KIENYEJI.Nitashughulikia MAPUNGUFU nikiwa ndani sio NJE!

Nyalandu alikihama chama cha Mapinduzi Oktoba 30 mwaka huu ambapo alieleza kuwa amechoshwa na mwenendo wa siasa wa sasa.

Mahakama yaamuru DC kukamatwa

Mwanza/Bukoba. Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba imetoa hati ya kumkamata na kumfikisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Dennis Mwira kwa kosa la kupuuza amri ya Mahakama.

Amri hiyo imetolewa Novemba 2 na Hakimu Mkazi, Samuel Maweda baada ya mkuu huyo wa wilaya kukaidi amri ya kuachia ng'ombe 541 wa wafugaji wa kitongoji cha Rwenkuba wilayani humo waliokamatwa isivyo halali.

Septemba 22, mahakama hiyo ilitoa amri ya ng'ombe hao kuachiwa baada ya wananchi kufungua shauri la madai namba 21/2017 kupinga ng'ombe wao kukamatwa katika eneo lenye mgogoro unaoendelea katika mahakama kuu kitengo cha ardhi kwa shauri namba 14/2017.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana Alhamisi usiku, Wakili wa wananchi143 waliofungua kesi mahakamani, Danstan Mutagahywa amesema baada ya Mkuu wa Wilaya na mdaiwa mwenzake, Ladislaus Martin ambaye ni Meneja wa Ranchi ya Misenyi baada ya kukaidi kutekeleza amri hiyo, waliwasilisha ombi la watu hao kukamatwa kwa kudharau amri ya Mahakama.

"Siyo tu wamekaidi kutekeleza amri halali ya Mahakama, DC na mwenzake pia wamegoma kupokea hati za wito na kufikia hatua ya kumkamata na kumweka mahabusu dalali wa Mahakama aliyepewa amri ya kutekeleza zoezi la kurejesha ng'ombe wanaoshikiliwa isivyo halali," amesema Mutagahywa.

Amesema amri hiyo inatarajiwa kufikishwa ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), wa Kagera leo Ijumaa Novemba 3.

Amemtaja dalali wa Mahakama aliyekamatwa na kuswekwa mahabusu kwa amri ya DC Oktoba 31, kuwa ni Ignatus Bashemela aliyeachiwa huru baada ya yeye kuwasilisha suala hilo ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera akionyesha nyaraka halali za Mahakama kuhusu jambo hilo.

Wakati shauri la madai dhidi ya DC na mwenzake Ladislaus likitarajiwa kusikilizwa mara watakapokamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama, ile ya ardhi ambayo bado inatajwa mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Seif Musa, itatajwa tena Machi 8, 2018.

Kauli ya DC

Akizungumza kwa njia ya simu mkuu huyo wa wilaya amesema aliagiza kukamatwa kwa dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambaye alifika bila kutoa taarifa yoyote kwa mamlaka za Serikali.

Amesema kuwa mtu huyo alikwenda moja kwa moja katika eneo wanapotunzwa ng'ombe zaidi ya  80 walioingizwa nchini kutoka Uganda bila kufuata utaratibu.

"Hilo suala la dalali wa Mahakama nalisikia kwako niliyeagiza akamatwe ni dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambao tumewakamata alifika bila kufuata taratibu nikaagiza akamatwe,"amesisitiza Kanali Mwila.

Ameongeza kuwa alikamata ng'ombe zaidi ya 400 na wamiliki wake kutoka Uganda walilipa faini na kuwarudisha kwao na kubaki ng'ombe 88 aliosema alipata taarifa kuwa wanataka kuchukuliwa kwa nguvu na watu ambao hata hawakupita kwenye ofisi yake.

Pia amesema hana taarifa yoyote ya kuwepo kwa hati ya Mahakama dhidi yake na kuwa anaendelea kuwasaka raia wawili wanaodaiwa kushirikiana na wafugaji wa Uganda kuingiza mifugo hiyo bila utaratibu

Mourinho:Nahitaji pongezi kuifunga Tottenham



Meneja wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho

Meneja wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho amesema kikosi chake cha mashetani wekundu (The Red Devils) kinastahili kupongezwa kwa kuifunga Tottenham ambayo imefanya vizuri katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Mourinho ambae nimiongoni mwa makocha wachache wenyemaneno mengi katika ligi ya Uingereza ameyasema hayo hii leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

“Tottenham imeifunga Liverpool mabao 4-1 ikaifunga Real Madrid 3-1,lakini wameshindwa kufanya hivyo dhidi yetu bila shaka wachezaji wamgu wanastahili pongezi,”amesema Mourinho.

Timu ya Tottenham hapo jana usiku imefanikiwa kuchomoza na ushindi wa jumla ya mabao 3-1 mbele ya mabingwa watetezi klabu ya Real Madrid katika dimba la Wembley huku Dele Alli akitupia mawili na Christian Eriksen akimalizia karamu hiyo ya mabao.

Spurs imechomoza na ushindi huo wa kihistoria ndani ya klabu hiyo ikiwa ni sikuchache tu toka ikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Manchester United lilofungwa na Anthony Martial mchezo wa ligi kuu nchini Uingereza.

Mourinho amesisitiza United inastahili pongezi kwa kuishushia kipigo Tottenham ambayo imechomoza na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Liverpool mwezi uliyopita

Maduka yanaodurufu CD za wasanii yafungiwa na TRA

Maduka yanaodurufu CD za wasanii yafungiwa na TRA

       

              



MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) ikishirikiana na kampuni ya Msama Auction Mart ambao ni wasimamizi na wasambazaji wa kazi za muziki wa Injili, chini ya Mkurugenzi wake, Alex Mwita Msama, imefanya oparesheni ya kuwafungia maduka na kuwahoji watu wanaodurufu CD feki yaani zisizofuata utaratibu uliopo.


Akizungumza wakati wa oparesheni hiyo iliyofanyika jana jioni Kariakoo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kodi za Ndani (TRA), Elijah Mwandubya, alisema wamekuwa wakiwatahadharisha watu hao kuachana na kazi hiyo ya kudurufu CD feki hivyo lakini wamekuwa hawaitikii tahadhari hiyo na sasa mamlaka hiyo.

Aliongeza kwamba, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, wamejidhatiti vilivyo kuhakikisha kazi za wasanii nchini zinalindwa na serikali inapata mapato yake kutokana na wengi wao kukwepa kulipa kodi na kuuza CD feki.

Alisema serikali inatengeneza mazingira safi na wafanyabiashara waaminifu wanaofuata utaratibu sahihi, ukiwemo ulipaji wa kodi kwa wakati na hivyo wataendelea
kuhakikisha kazi za wasanii zinalindwa na kuheshimika ipasavyo, kwani zoezi litaendelea maeneo mbalimbali nchin

Dogo Janja anyoosha maelezo kuhusu ndoa yake na Uwoya

Dogo Janja anyoosha maelezo kuhusu ndoa yake na Uwoya

Dar es Salaam. Mwanamuziki Dogo Janja amekiri kuwa amefunga ndoa na mwigizaji Irene Uwoya na kwamba amembadilisha dini kuwa muislamu ingawa amegoma kujibu maswali muhimu ikiwamo uwepo wa wazazi wa mwanamke huyo katika tukio hilo.

Dogo Janja ambaye jina lake halisi ni Abdulaziz Chende wakati akihojiwa na Kipindi cha Leo Tena cha leo Ijumaa kinachorushwa na kituo cha redio Clouds FM, amekiri kufunga ndoa na mwigizaji huyo na kusema kuwa sasa anaitwa Sheillah.

Akisaidiwa kutoa maelezo na mwanamuziki Keisha amesema ndoa hiyo ilifungwa kwa kupata baraka kutoka kwa ndugu wa pande zote baada ya kutoa posa wiki mbili zilizopita.

Amesema Uwoya alibadili dini wiki tatu kabla ya ndoa na kwamba barua ya posa, mahari na ndoa vilichukua muda wa wiki tatu tu.

Mtangazaji wa kipindi hicho, Husna Abdul maarufu Da Huu amemuuliza mwanamuziki huyo mahali ilipofungwa ndoa hiyo naye alijibu kwa Madee lakini Keisha aliingia kati na kusema ilikuwa eneo la siri.

Mtangazaji huyo aliendelea kuwabana kwa maswali kuwa inawezekana vipi ndoa ikafungwa eneo la siri wakati ilipaswa kufanyika nyumbani kwa wazazi wa Irene, Keisha amesema walikwenda kumchukua bibi harusi na kwenda kufunga ndoa katika eneo hilo.

Kitilya na wenzake waendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia  uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na waliokuwa maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon bado wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi inayowakabili  bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa  leo Ijumaa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Soma: Wakili aomba kesi ya utakatishaji fedha dhidi ya akina Kitilya ifutwe

Pia ameeleza kuwa bado wanasubiri awamu ya pili ya upelelezi kutoka nchini Uingereza, kutokana na hilo ameomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya ombi hilo Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la

Mmiliki wa timu ya Chelsea na kocha mkuu hawaongei

Mmiliki wa timu ya Chelsea na kocha mkuu hawaongeiTaarifa zinaeleza hali si shwari katika klabu ya Chelsea na sasa mmiliki wa klabu hiyo Roman Abromovich hana maelewano mazuri na kocha Antonio Conte na siku za usoni hawajawahi kuonana.


Mmiliki wa Chelsea Roman Abromovich huwa ana mahusiano ya karibu sana na makocha wa timu yake na hupenda kuwaweka karibu yake na ndivyo alivyofanya wakati Antonio Conte akijiunga na Chelsea.

Gazeti maarufu la masuala ya michezo la Marca limechapisha habari inayosema kwamba watu hao wawili hawaongei moja kwa moja kwa sasa na kama Conte akitaka kuongea na Abromovich ni lazima amtumie Secretary wake.

Mahusiano kati ya wawili hao yalianza kuwa katika hali mbaya wakati wa dirisha la usajili huku sababu kubwa ikidaiwa ni Conte kutoridhishwa na namna ambavyo klabu ya Chelsea inaendesha dirisha la usajili.

Mbaya zaidi Marca wamesema tayari kuna kikundi cha wachezaji ndani ya Chelsea ambao hawamuungi mkono Antonip Conte na wengi wakichukizwa na kitendo alichomfanyia Diego Costa baada ya msimu kuisha.

Kwa mambo yanayoendelea Chelsea inaonesha wazi huenda huu ukawa msimu wa mwisho kwa Conte kuitumikia Chelsea na kipigo cha bao 3 kwa 0 toka kwa As Roma kimezidi kuchafua hali ya hewa kwa meneja huyo.

Chelsea wana kibarua kigumu zidi ya Manchester United mchezo ambao utamlazimu Conte kushinda laa sivyo muda wake wa kuwa Chelsea unaweza kuisha mapema zaidi kuliko watu wanavyoamini.m

Tazama full video ya harusi ya Dongo Janja na Irene Uwoya


Wakati mjadala ukiendelea kuhusu taarifa zinazodai Dogo Janja na Irene Uwoya kufunga ndoa, hatimaye Dogo Janja ametuletea video hii inayoonyesha tukio zima la sherehe yake.

Tazama video hapa chini

Anaswa na wananchi akimbaka mtoto wa miaka miwili

Anaswa na wananchi akimbaka mtoto wa miaka miwili



Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba 

Polisi wanamshikilia mkazi wa Kijiji cha Magamba wilayani hapa kutokana na tuhuma za kumbaka mtoto mwenye miaka miwili.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, tukio hilo lilitokea juzi Kitongoji cha Komkola Chang’ombe.

Wakazi wa kitongoji hicho waliozungumza na gazeti hili, walisema walisikia mtoto akilia nyumbani kwa mtuhumiwa na walipokwenda walikuta akimbaka mtoto huyo.

“Huu ni unyama umevuka kiwango kijana anathubutu kumbaka mtoto mdogo kama yule, sijui tunaelekea wapi vijana wa namna hii hawastahili kuishi na jamii,” alisema Hussen Juma.

Kamanda Wakulyamba alisema mtoto aliyebakwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni akiendelea na matibabu na kwamba, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Alitoa wito kwa wazazi kutowaacha watoto wao kuzurura mitaani, ili kuwalinda wasitendewe vitendo vya kikatili kama hivyo

Akaunti ya Twitter ya rais Trump ''yapotea kwa muda




Akaunti ya mtandao wa Twitter ya rais Donald Trump ilipotea kwa muda siku ya Alhamisi lakini, ikarudishwa baadaye , kampuni hiyo imesema.

Twitter imesema kuwa akaunti hiyo kwa jina @realdonaldtrump iliondolewa na mfanyikazi mmoja na baadaye kuelezea kuwa ilikuwa siku yake ya mwisho kazi.

Akaunti hiyo iliondolewa kwa muda wa dakika 11 na sasa kampuni ya Twitter inachunguza.
Bwana Trump ambaye ni mtumizi wa mtandao wa Twitter wa mara kwa mara akiwa na wafuasi milioni 41.7 hajatoa tamko lolote kuhusu swala hilo.

Siku ya Alhamisi jioni, wale waliotembelea akaunti ya rais Trump waliona ujumbe uliosema ''pole ukurasa huu hauko kwa sasa!''

Baada ya akaunti kurejeshwa , ujumbe wa kwanza wa bwana Trump ulikuwa kuhusu ule mpango wa Republican wa kupunguza kodi.

Hatahivyo@POTUS ambayo ndio akaunti rasmi ya rais Trump haukuathiriwa.

Twitter imesema kuwa inachunguza tatizo hilo na kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kisa kama hicho hakitokei tena.

Kampuni hiyo ilisema katika ujumbe wake kwamba wamebaini katika uchunguzi wao kwamba kisa hicho kilifanywa na mfanyikazi anayewahudumia wateja ambaye alifanya hivyo katika siku yake ya mwisho ya kazi.

Tunatathmini kisa chote kikamilifu.

Bwana trump alijiunga na mtandao wa twitter mnamo mwezi Machi 2009.

Amekuwa mtumiaji mkubwa wa mtandao huo kwa kukuza sera zake mbali na kuwashambulia wapinzani wake wakati wa kampeni za urais 2016 na hata baada ya kuchukua mamlaka mnamo mwezi Januari

Wahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mpwa wao



Mahakama moja nchini India imewahukumu watu wawili kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mpwa wao mwenye umri wa miaka 10 ambaye alijifungua mtoto wa kike mnamo mwezi Agosti.

Wanaume wote wawili walikuwa wajomba wa smichana huyo.

Walihukumiwa kwa kumbaka msichana huyo siku ya Jumanne.

Uja uzito wa msichana huo ulibainika katikati ya mwezi Julai wakati alipopelekwa hospitalini baada ya kulalamikia maumivu ya tumboni.

Mjombake wa pili alikamatwa baada ya chembechembe za DNA za mtoto huyo kutofanana na kakake mkubwa ambaye ndio mshukiwa wa kwanza .

Kesi ya mshukiwa wa kwanza ilichukua mwezi mmoja huku mjombake mdogo akihukumiwa baada ya kesi hiyo kuchukua siku 18.

Kesi hiyo ya msichana wa miaka 10 imegonga vichwa vya habari kwa wiki kadhaa nchini India na kote duniani.

Alikuwa na uja uzito wa wiki 30 wakati mahakama moja ya Chandigarh ilipokataa ombi la kuavya mimba, kwa sababumimba hiyo ilikuwa kubwa.

Jopo la madaktari lilisema kuwa kutolewa kwa mimba hiyo ni hatari .

Baadaye mahakama ya juu ya India pia ilikataa kutolewa kwa mimba hiyo kwa sababu kama hizo za kimatibabu.

Sheria ya India hairuhusu kutolewa kwa mimba baada ya wiki 20 hadi pale daktari aweze kubaini kwamba maisha ya mama yapo hatarini.

Mtoto huyo hakujua kwamba alikuwa akibeba uja uzito na kwamba alielezewa kwamba tumbo lake likuwa na jiwe, kulingana na mwamndishi wa BBC Geeta Panday mjini Delhi.

Alijifungua mwezi Agosti na mtoto huyo kukabidhiwa mamlaka ya kuangalia watoto ili kulewa.

Awali msichana huyo aliwaambia maafisa wa polisi na wanaharakati wa maslahi ya watoto kwamba alibakwa mara kadhaa katika kipindi cha miezi saba iliopita na mjombake mkubwa ambaye yuko katika umri wake wa 40

Steve Nyerere amwagia sifa Aunt Ezekiel


Mchekeshaji maarufu Bongo, Steve Nyerere.

MCHEKESHAJI maarufu Bongo, Steve Nyerere amefunguka kuwa mwanamke anayemheshimu Bongo Muvi kwa sasa ni Aunt Ezekiel pekee.



Msanii wa Bongo Muvi, Aunt Ezekiel pekee.

Akizungumza na Star Mix Steve alisema kuwa, anamheshimu kwa sababu ni mwanamke ambaye hajabweteka na amejitahidi sana kukusanya hela anazopata kufanya mambo ya maana kama alivyojenga nyumba maeneo ya Kigamboni tofauti na mastaa wengine.

“Yaani kwa kweli Bongo Muvi kwa wanawake nampa heshima kubwa Aunt,ni mdada ametulia na mzazi mwenziye amepata watoto lakini pia ameweza kujituma mpaka kujenga nyumba tofauti na wengine,”alisema Steve

Shahidi adai kufungiwa tofali sehemu za siri


MSHTAKIWA wa pili wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri na bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, Shaibu Said (Mredii), amedai mahakamani kuwa alipelekwa Kituo cha Polisi kinachoitwa Guantamano, nje kidogo ya Jiji la Arusha na kuteswa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Pia alidai kuwa baada ya kuhamishiwa Moshi alifungiwa nusu ya kipande cha tofali kwenye sehemu zake za siri, ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la mauaji.

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi katika kesi ndani ya kesi, aliieleza mahakama hiyo kuwa wakati analazimishwa na polisi kusaini maelezo hayo akiwa Moshi, alinyweshwa pia maji ambayo yanafanya tumbo kuwaka moto na mwili mzima kuwasha.

Akitoa utetezi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mredi alidai kuwa mateso mengine aliyokutana nayo ni kufungiwa bomba la chuma katikati ya miguu na kuning’inizwa kwenye paa la nyumba akiwa amefungwa pingu mkononi, kuchomwa na singe ya bunduki ya SMG kwenye fundo la mguu karibu na unyayo na kuchokonolewa na singe hiyo ndani yake ili akubali kosa na baadaye kuchomwa na pasi ya umeme miguuni.

Alidai mateso hayo ya polisi yamemfanya awe mlemavu mkono wake wa kushoto ambao kutokana na madhila hayo, hivi sasa anatumia dawa za mifupa na maradhi mengine tangu alipokamatwa mwaka 2013 hadi leo.

Aidha, alidai kutokana na madhila hayo, askari polisi waliokuwa wakimtesa ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la kumuua Msuya, walikuwa wakimkanda kila siku kwa maji ya moto ili apate nafuu na kutia saini kama walivyotaka.

Akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, Mredii aliieleza mahakama hiyo kwamba wakati anakamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Bilionea Msuya, hakuwapo Mererani, Arusha wala Orkolili kulikofanyika mauaji hayo, kwa vile alikuwa shambani kwake mkoa wa Manyara.

Alidai kwamba hata taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi, Erasto Msuya (Bilionea), alizipata kwa njia ya simu akiwa shambani kwake baada ya kupigiwa simu na shemeji wa marehemu, aliyemtaja kwa jina moja la Shujaa.

Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kandokando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mbali na Mredii, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu.

Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Majeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Kesi hiyo ndani ya kesi iliibuliwa wiki iliyopita na Wakili wa Utetezi, Majura Magafu, baada ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, kudai aliteswa na kulazimishwa kutia saini maelezo bila ridhaa yake.

Madai hayo ya mateso yaliyosababisha afya ya mteja wake (Mredii) kuwa mbaya na kulazimika kupelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC kwa matibabu zaidi, ndiko kulikoibua mgongano wa kisheria na kuanza kesi ndani ya kesi.

Shahidi huyo wa upande wa utetezi (Mredii), aliongozwa kutoa ushahidi na Wakili wake Majura Magafu kuhusu uelewa wake tangu alipokamatwa hadi kufanyiwa mateso hayo na kisha kulazimishwa kusaini maelezo ya kukubali kushiriki mauaji ya Bilionea Msuya. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Magafu: Walipokuchukua askari kutoka Mererani kuja KIA, ulipofika hapo kulitokea kitu gani?

Shahidi: Walipaki gari chini ya mti wa mjohoro na kuniamuru nilale chini kifudifudi.

Wakili Magafu: Baada ya hapo ikawaje?

Shahidi:  Nililala hivyo hadi saa 12 jioni nikasikia wanasema twende hivi na nilihisi wanakwenda barabara ya Arusha.

Wakili Magafu: Ulijuaje uko barabara ya KIA kuelekea Arusha?

Shahidi:  Nimeizoea hiyo barabara kwa sababu naipita kila siku.

Wakili Magafu: Mlienda mpaka wapi?

Shahidi: Nilipelekwa mpaka Arusha

Wakili Magafu: Ulipofikishwa Arusha nini kilifanyika?

Shahidi: Nilikaa kwenye gari la Polisi kwa saa mbili hivi hadi waliponishusha kwa amri ya afande Samuel ambaye alitoa ushahidi
hapa mahakamani.

Wakili Magafu: Umesema Arusha ulipelekwa ukumbini, hebu tuambie ni jambo gani lilifanyika?

Shahidi: Nilimkuta RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) Arusha na baadhi ya askari wengine wenye vyeo vikubwa.

Wakili Magafu: Huyo RPC ulikuwa unamfahamu majina yake kabla?

Shahidi: Hapana, nilikuwa namfahamu kwa sura tu

Wakili Magafu: Wakati unapelekwa pale ukumbini Arusha, kulikuwa na askari wangapi?

Shahidi: Walikuwa kama sita au saba

Wakili Magafu: Tusaidie, wakati huo ulikuwa katika hali gani?

Shahidi: Nilikuwa katika hali nzuri, lakini walikuwa wamenifunga pingu za mikono na miguu.

Wakili Magafu: Ulipofikishwa ukumbini uliambiwa nini na hao uliowakuta?

Shahidi: RPC Arusha aliniambia Shaibu tunachotaka hapa ni ushirikiano wako.

Wakili Magafu: Alikwambia anaomba ushirikiano kuhusiana na jambo gani?

Shahidi:  Mauaji ya Erasto Msuya

Wakili Magafu: Huyo Erasto Msuya ulikuwa ukimfahamu?

Shahidi: Ndiyo nilikuwa namfahamu ingawa sikuwa na ukaribu naye.

Wakili Magafu: Ulipowajibu kwamba hutambui chochote kuhusiana na tukio hilo, walikuambiaje?

Shahidi: Niliwaambia kwamba sifahamu jambo hilo na siku ya tukio linapofanyika mimi sikuwapo Mererani, Kia wala Arusha.

Wakili Magafu: Baada ya kuwaambia hivyo walikujibu nini?

Shahidi: Waliniuliza taarifa za kuuawa kwa Erasto nilizipata wapi.

Wakili Magafu: Ukawajibu nini?

Shahidi: Niliwaambia nilizisikia baada ya kupigiwa simu kwamba Erasto ameuawa.

Wakili Magafu: Unaweza kukumbuka ni nani alikwambia kwamba Erasto ameuawa?

Shahidi: Nilipata taarifa baada ya kupigiwa simu na shemeji yake Erasto, anaitwa Shujaa.

Wakili Magafu; Ukiwa kule ukumbini Arusha walikwambia nini hao kina RPC na askari wengine?

Shahidi: RPC Arusha aliniambia tunakuonea huruma kwa sababu tukikukabidhi kwa hawa vijana waliokuja na wewe, sijui kama utarudi salama.

Wakili Magafu: Kutokana na kauli hiyo au ushauri huo wa RPC Arusha uligundua nini?

Shahidi: Kwa sababu hao walioniambia hivyo ni viongozi wakubwa niliingiwa na hofu sana.

Wakili Magafu: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi: RCO Ramadhan Ng’anzi (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) alitoa amri kwa afande Samuel na kumwambia ondokeni naye.

Wakili Magafu: Baada ya kutolewa hapo ukumbini mlielekea wapi?

Shahidi: Tulielekea kama tunaenda Babati.

Wakili Magafu: Mlienda hadi wapi?

Shahidi: Tulienda hadi uwanja wa Ndege Kisongo, mkoa wa Arusha na tulienda tukaingia upande wa kushoto.

Wakili Magafu: Safari yenu huko iliishia wapi?

Shahidi: Tulienda hadi kwenye mashamba makubwa ambako kuna kituo cha Polisi kule.

Wakili Magafu:  Hicho kituo kinaitwaje?

Shahidi: Wao wenyewe Polisi waliniambia unaijua Guantanamo wewe?

Wakili Magafu:  Ehee mlipofika huko Guantanamo nini kiliendelea?

Shahidi: Hapo kituoni tulimkuta dada mmoja askari akiwa kaunta na akaambiwa chomoa hiyo redio ya Sub Uffer na switch yake ilete.

Wakili Magafu:  Ni nani aliomba hiyo redio ya Sub Uffer?

Shahidi: Ni askari mmoja toka Arusha aliyekuwa ameongozana na askari wa Moshi anaitwa Faustine Mafwele.

Wakili Magafu: Nini kilifuata?

Shahidi: Waliifungulia kwa sauti kubwa hiyo redio na wakanifungua pingu zote za mikononi na miguuni na kuniambia nivue nguo na kubaki kama nilivyozaliwa.

Wakili Magafu: Baada ya kuvua hizo nguo na kubaki kama ulivyozaliwa, walikufanyaje?

Shahidi: Waliniweka chini ya sakafu wakaniambia wao hawana ombi kama wale maofisa wakubwa zao ila wao wana amri tu.

Wakili Magafu: Wakafanyaje sasa?

Shahidi: Waliniambia sisi hatutaki maelezo wala kinachohusiana na mauaji ya Erasto.

Wakili Magafu: Wakati wakikueleza hayo walikuwa wana nini na nini?

Shahidi: Walikuwa na makaratasi mengi sana

Wakili Magafu: Walikuambia kitu gani kuhusiana na hayo makaratasi?

Shahidi: Waliniambia tunachotaka hapa ni sahihi yako tu.

Wakili Magafu: Baada ya kuwajibu hivyo walifanya kitu gani?

Shahidi: Nilisikia maumivu makali baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.

Wakili Magafu: Baada ya kukupiga kichwani kuna nini kingine walifanya?

Shahidi: Niliingizwa bomba la chuma katikati ya miguu na yule shahidi aliyetoa ushahidi wake jana (afande Dereck) na mwenzake afande Chilumba akanishika kiuno na kuniweka kwenye meza na kilichoendelea hapo mheshimiwa nilikuwa nakomeshwa na waliniambia hapa salama yako ni sahihi.

Wakili Magafu: Baada ya kuingizwa bomba walifanyaje?

Shahidi: Afande Chilumba alimwambia Dereck jisevie.

Wakili Magafu: Baada ya hapo walifanya kitu gani?

Shahidi: Nilipigwa kwenye nyayo kwa juu (kwenye kifundo) na nilipiga kelele sana.

Wakili Magafu: Sasa hebu tusaidie ile redio ilikuwa na kazi gani?

Shahidi: Yule askari wa Arusha Faustine Mafwele alikuwa anaongeza sauti ili kuzima sauti yangu ibaki ya redio.

Wakili Magafu: Tusaidie ukiwa Moshi, unasema RCO aliondoka kwa hasira baada ya kuambiwa hujasaini, kwani mliondoka kuelekea wapi?

Shahidi: Mashamba ya miwa TPC

Wakili Magafu:  Mlipofika mashamba ya miwa kulitokea nini?

Shahidi: Waliniambia sali sala yako ya mwisho

Wakili Magafu:  Ulisali?

Shahidi: Nilisali kwa sababu kwenye moyo wangu nilishamwambia Mungu lolote linaweza kutokea na tayari nilikuwa nimeshaweka nadhiri.

Wakili Magafu: Baada ya wewe kumaliza kusali walifanya nini?

Shahidi: Askari mmoja alitoa kitu kama kisu kwenye ncha ya bunduki ya SMG (singe) na kunichoma nayo kwenye unyayo wa mguu.
Wakili Magafu: Walipoingiza hiyo singe kwenye mguu wakafanyaje sasa?

Shahidi: Walikuwa wanaichezesha huko ndani katikati ya mfupa na nyama huku wakiishindilia.
Wakili Magafu: Nini kiliendelea tena?

Shahidi: Walisema wananipeleka kwenye tocha ya mwisho (mateso) na walinipeleka kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu na kiwanda cha TPC

Wakili Magafu: Mlipofika kulifanyika kitu gani?

Shahidi: Waliipiga kisu suruali yangu niliyokuwa nimevaa na ikatolewa mwilini.
Wakili Magafu: Wakafanya kitu gani sasa?

Shahidi: Niliona wana kipande cha tofali za block (mchanga) kimefungwa kamba.

Wakili Magafu: Hicho kipande cha tofali kazi yake ilikuwa nini?

Shahidi: Walikichukua wakanifunga kwenye …(sehemu za siri) wakaliacha likiwa linaning’inia huku mimi nikiwa nimefungwa pingu juu ya paa la nyumba.

Wakili Magafu: Hilo zoezi lilichukua muda gani?

Shahidi: Sikuwa najielewa baada ya hapo.

Wakili Magafu: Wakati huo hizo document ulikuwa umeshazisaini?

Shahidi: Kwa sababu niliona nakufa ilibidi nisaini

Baada ya Wakili Magafu kumaliza kumwongoza shahidi huyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, alisimama na kumwomba Jaji Salma upande wa utetezi wamwite mahakamani Daktari wa Hospitali ya Mawenzi aje kuhojiwa kuhusiana na matibabu ya Mredii anayedaiwa kuteswa.

“Mheshimiwa Jaji, chini ya kifungu cha 291 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 ya Sheria ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo, Daktari Massam E ambaye ana cheo cha AMO (Assistant Medical Officer) aliyejaza fomu namba tatu ya Polisi, aletwe mahakamani kwa ajili ya cross examination (mahojiano),” alidai Chavula.

Kutokana na hoja hiyo ya upande wa mashtaka, Wakili Magafu aliiambia mahakama hiyo kwamba wanatarajia kuleta mashahidi wawili mahakamani akiwamo daktari huyo wa Mawenzi na daktari wa Magereza, hivyo wanaomba wenzao wawe wavumilivu.

Dakika chache baadaye, Wakili Chavula alianza kumhoji shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi (Mredii) na mambo yalikuwa hivi:

Wakili Chavula: Nairejesha mahakama nyuma kidogo kwenye kumbukumbu zake, tarehe 10/2/2015 wakati wa PH (Preliminary Hearing), shahidi ukiwa na mawakili wako, kwa nini ulisema ulikamatwa tarehe 15/8/2013, Je, uliidanganya mahakama?

Shahidi: Labda nilikuwa nimesahau.

Wakili Chavula: Umeileza mahakama kwamba tarehe 18/8/2013 ukiwa kizuizini pale Polisi Mererani, baadaye ukapelekwa Polisi Kia, kweli si kweli?

Shahidi: Kweli
Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba shahidi wa nne, afande Dereck alikuwa miongoni mwa waliokutesa kutoka Guantanamo hadi mashamba ya TPC?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Chavula: Kwa nini jana, hamkumuuliza maswali wakati anaitwa kutoa ushahidi wake kwamba alihusikaje kukutesa?
Shahidi: Jaji ndio anajua kwa sababu alikuwa hajaruhusu hilo.

Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba wakati Erasto anauawa haukuwa Mererani, Arusha wala Orkalili?
Shahidi: Sahihi.

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu anayemtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, Wakili Emmanuel Safari anayemtetea mshitakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshitakiwa wanne, sita na saba.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdala Chavula.

Hadi sasa jumla ya mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Hai, (OC-CID) Joash Yohana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO) Dk. Paul Chaote (39) na Khalid Sankamula (49) ambaye ni Mganga wa Kienyeji na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora.

Wengine ni Anase Khalid (37), mkulima na mkazi wa Kaliua, Tabora, Mbazi Steven (32), mkazi wa Arusha na Ofisa Upelelezi, Kitengo cha Intelijensia ya Jinai mkoa wa Kilimanjaro, Herman Ngurukisi (40), Inspekta Samueli Maimu (45) ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya ukaguzi ya Polisi (CRT) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa wa Kilimanjaro na Ofisa Upelelezi (Detective), Sajenti Atway Omari ambaye aliyekuwa katika timu ya CRT. Kesi hiyo itaendelea tena leo