Friday, 3 November 2017

Anaswa na wananchi akimbaka mtoto wa miaka miwili

Anaswa na wananchi akimbaka mtoto wa miaka miwili



Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba 

Polisi wanamshikilia mkazi wa Kijiji cha Magamba wilayani hapa kutokana na tuhuma za kumbaka mtoto mwenye miaka miwili.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, tukio hilo lilitokea juzi Kitongoji cha Komkola Chang’ombe.

Wakazi wa kitongoji hicho waliozungumza na gazeti hili, walisema walisikia mtoto akilia nyumbani kwa mtuhumiwa na walipokwenda walikuta akimbaka mtoto huyo.

“Huu ni unyama umevuka kiwango kijana anathubutu kumbaka mtoto mdogo kama yule, sijui tunaelekea wapi vijana wa namna hii hawastahili kuishi na jamii,” alisema Hussen Juma.

Kamanda Wakulyamba alisema mtoto aliyebakwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni akiendelea na matibabu na kwamba, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Alitoa wito kwa wazazi kutowaacha watoto wao kuzurura mitaani, ili kuwalinda wasitendewe vitendo vya kikatili kama hivyo

Akaunti ya Twitter ya rais Trump ''yapotea kwa muda




Akaunti ya mtandao wa Twitter ya rais Donald Trump ilipotea kwa muda siku ya Alhamisi lakini, ikarudishwa baadaye , kampuni hiyo imesema.

Twitter imesema kuwa akaunti hiyo kwa jina @realdonaldtrump iliondolewa na mfanyikazi mmoja na baadaye kuelezea kuwa ilikuwa siku yake ya mwisho kazi.

Akaunti hiyo iliondolewa kwa muda wa dakika 11 na sasa kampuni ya Twitter inachunguza.
Bwana Trump ambaye ni mtumizi wa mtandao wa Twitter wa mara kwa mara akiwa na wafuasi milioni 41.7 hajatoa tamko lolote kuhusu swala hilo.

Siku ya Alhamisi jioni, wale waliotembelea akaunti ya rais Trump waliona ujumbe uliosema ''pole ukurasa huu hauko kwa sasa!''

Baada ya akaunti kurejeshwa , ujumbe wa kwanza wa bwana Trump ulikuwa kuhusu ule mpango wa Republican wa kupunguza kodi.

Hatahivyo@POTUS ambayo ndio akaunti rasmi ya rais Trump haukuathiriwa.

Twitter imesema kuwa inachunguza tatizo hilo na kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kisa kama hicho hakitokei tena.

Kampuni hiyo ilisema katika ujumbe wake kwamba wamebaini katika uchunguzi wao kwamba kisa hicho kilifanywa na mfanyikazi anayewahudumia wateja ambaye alifanya hivyo katika siku yake ya mwisho ya kazi.

Tunatathmini kisa chote kikamilifu.

Bwana trump alijiunga na mtandao wa twitter mnamo mwezi Machi 2009.

Amekuwa mtumiaji mkubwa wa mtandao huo kwa kukuza sera zake mbali na kuwashambulia wapinzani wake wakati wa kampeni za urais 2016 na hata baada ya kuchukua mamlaka mnamo mwezi Januari

Wahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mpwa wao



Mahakama moja nchini India imewahukumu watu wawili kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mpwa wao mwenye umri wa miaka 10 ambaye alijifungua mtoto wa kike mnamo mwezi Agosti.

Wanaume wote wawili walikuwa wajomba wa smichana huyo.

Walihukumiwa kwa kumbaka msichana huyo siku ya Jumanne.

Uja uzito wa msichana huo ulibainika katikati ya mwezi Julai wakati alipopelekwa hospitalini baada ya kulalamikia maumivu ya tumboni.

Mjombake wa pili alikamatwa baada ya chembechembe za DNA za mtoto huyo kutofanana na kakake mkubwa ambaye ndio mshukiwa wa kwanza .

Kesi ya mshukiwa wa kwanza ilichukua mwezi mmoja huku mjombake mdogo akihukumiwa baada ya kesi hiyo kuchukua siku 18.

Kesi hiyo ya msichana wa miaka 10 imegonga vichwa vya habari kwa wiki kadhaa nchini India na kote duniani.

Alikuwa na uja uzito wa wiki 30 wakati mahakama moja ya Chandigarh ilipokataa ombi la kuavya mimba, kwa sababumimba hiyo ilikuwa kubwa.

Jopo la madaktari lilisema kuwa kutolewa kwa mimba hiyo ni hatari .

Baadaye mahakama ya juu ya India pia ilikataa kutolewa kwa mimba hiyo kwa sababu kama hizo za kimatibabu.

Sheria ya India hairuhusu kutolewa kwa mimba baada ya wiki 20 hadi pale daktari aweze kubaini kwamba maisha ya mama yapo hatarini.

Mtoto huyo hakujua kwamba alikuwa akibeba uja uzito na kwamba alielezewa kwamba tumbo lake likuwa na jiwe, kulingana na mwamndishi wa BBC Geeta Panday mjini Delhi.

Alijifungua mwezi Agosti na mtoto huyo kukabidhiwa mamlaka ya kuangalia watoto ili kulewa.

Awali msichana huyo aliwaambia maafisa wa polisi na wanaharakati wa maslahi ya watoto kwamba alibakwa mara kadhaa katika kipindi cha miezi saba iliopita na mjombake mkubwa ambaye yuko katika umri wake wa 40

Steve Nyerere amwagia sifa Aunt Ezekiel


Mchekeshaji maarufu Bongo, Steve Nyerere.

MCHEKESHAJI maarufu Bongo, Steve Nyerere amefunguka kuwa mwanamke anayemheshimu Bongo Muvi kwa sasa ni Aunt Ezekiel pekee.



Msanii wa Bongo Muvi, Aunt Ezekiel pekee.

Akizungumza na Star Mix Steve alisema kuwa, anamheshimu kwa sababu ni mwanamke ambaye hajabweteka na amejitahidi sana kukusanya hela anazopata kufanya mambo ya maana kama alivyojenga nyumba maeneo ya Kigamboni tofauti na mastaa wengine.

“Yaani kwa kweli Bongo Muvi kwa wanawake nampa heshima kubwa Aunt,ni mdada ametulia na mzazi mwenziye amepata watoto lakini pia ameweza kujituma mpaka kujenga nyumba tofauti na wengine,”alisema Steve

Shahidi adai kufungiwa tofali sehemu za siri


MSHTAKIWA wa pili wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri na bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, Shaibu Said (Mredii), amedai mahakamani kuwa alipelekwa Kituo cha Polisi kinachoitwa Guantamano, nje kidogo ya Jiji la Arusha na kuteswa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Pia alidai kuwa baada ya kuhamishiwa Moshi alifungiwa nusu ya kipande cha tofali kwenye sehemu zake za siri, ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la mauaji.

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi katika kesi ndani ya kesi, aliieleza mahakama hiyo kuwa wakati analazimishwa na polisi kusaini maelezo hayo akiwa Moshi, alinyweshwa pia maji ambayo yanafanya tumbo kuwaka moto na mwili mzima kuwasha.

Akitoa utetezi wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mredi alidai kuwa mateso mengine aliyokutana nayo ni kufungiwa bomba la chuma katikati ya miguu na kuning’inizwa kwenye paa la nyumba akiwa amefungwa pingu mkononi, kuchomwa na singe ya bunduki ya SMG kwenye fundo la mguu karibu na unyayo na kuchokonolewa na singe hiyo ndani yake ili akubali kosa na baadaye kuchomwa na pasi ya umeme miguuni.

Alidai mateso hayo ya polisi yamemfanya awe mlemavu mkono wake wa kushoto ambao kutokana na madhila hayo, hivi sasa anatumia dawa za mifupa na maradhi mengine tangu alipokamatwa mwaka 2013 hadi leo.

Aidha, alidai kutokana na madhila hayo, askari polisi waliokuwa wakimtesa ili akubali kutia saini maelezo ya kukiri kosa la kumuua Msuya, walikuwa wakimkanda kila siku kwa maji ya moto ili apate nafuu na kutia saini kama walivyotaka.

Akiwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, Mredii aliieleza mahakama hiyo kwamba wakati anakamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Bilionea Msuya, hakuwapo Mererani, Arusha wala Orkolili kulikofanyika mauaji hayo, kwa vile alikuwa shambani kwake mkoa wa Manyara.

Alidai kwamba hata taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi, Erasto Msuya (Bilionea), alizipata kwa njia ya simu akiwa shambani kwake baada ya kupigiwa simu na shemeji wa marehemu, aliyemtaja kwa jina moja la Shujaa.

Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kandokando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mbali na Mredii, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu.

Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Majeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Kesi hiyo ndani ya kesi iliibuliwa wiki iliyopita na Wakili wa Utetezi, Majura Magafu, baada ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, kudai aliteswa na kulazimishwa kutia saini maelezo bila ridhaa yake.

Madai hayo ya mateso yaliyosababisha afya ya mteja wake (Mredii) kuwa mbaya na kulazimika kupelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC kwa matibabu zaidi, ndiko kulikoibua mgongano wa kisheria na kuanza kesi ndani ya kesi.

Shahidi huyo wa upande wa utetezi (Mredii), aliongozwa kutoa ushahidi na Wakili wake Majura Magafu kuhusu uelewa wake tangu alipokamatwa hadi kufanyiwa mateso hayo na kisha kulazimishwa kusaini maelezo ya kukubali kushiriki mauaji ya Bilionea Msuya. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Magafu: Walipokuchukua askari kutoka Mererani kuja KIA, ulipofika hapo kulitokea kitu gani?

Shahidi: Walipaki gari chini ya mti wa mjohoro na kuniamuru nilale chini kifudifudi.

Wakili Magafu: Baada ya hapo ikawaje?

Shahidi:  Nililala hivyo hadi saa 12 jioni nikasikia wanasema twende hivi na nilihisi wanakwenda barabara ya Arusha.

Wakili Magafu: Ulijuaje uko barabara ya KIA kuelekea Arusha?

Shahidi:  Nimeizoea hiyo barabara kwa sababu naipita kila siku.

Wakili Magafu: Mlienda mpaka wapi?

Shahidi: Nilipelekwa mpaka Arusha

Wakili Magafu: Ulipofikishwa Arusha nini kilifanyika?

Shahidi: Nilikaa kwenye gari la Polisi kwa saa mbili hivi hadi waliponishusha kwa amri ya afande Samuel ambaye alitoa ushahidi
hapa mahakamani.

Wakili Magafu: Umesema Arusha ulipelekwa ukumbini, hebu tuambie ni jambo gani lilifanyika?

Shahidi: Nilimkuta RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) Arusha na baadhi ya askari wengine wenye vyeo vikubwa.

Wakili Magafu: Huyo RPC ulikuwa unamfahamu majina yake kabla?

Shahidi: Hapana, nilikuwa namfahamu kwa sura tu

Wakili Magafu: Wakati unapelekwa pale ukumbini Arusha, kulikuwa na askari wangapi?

Shahidi: Walikuwa kama sita au saba

Wakili Magafu: Tusaidie, wakati huo ulikuwa katika hali gani?

Shahidi: Nilikuwa katika hali nzuri, lakini walikuwa wamenifunga pingu za mikono na miguu.

Wakili Magafu: Ulipofikishwa ukumbini uliambiwa nini na hao uliowakuta?

Shahidi: RPC Arusha aliniambia Shaibu tunachotaka hapa ni ushirikiano wako.

Wakili Magafu: Alikwambia anaomba ushirikiano kuhusiana na jambo gani?

Shahidi:  Mauaji ya Erasto Msuya

Wakili Magafu: Huyo Erasto Msuya ulikuwa ukimfahamu?

Shahidi: Ndiyo nilikuwa namfahamu ingawa sikuwa na ukaribu naye.

Wakili Magafu: Ulipowajibu kwamba hutambui chochote kuhusiana na tukio hilo, walikuambiaje?

Shahidi: Niliwaambia kwamba sifahamu jambo hilo na siku ya tukio linapofanyika mimi sikuwapo Mererani, Kia wala Arusha.

Wakili Magafu: Baada ya kuwaambia hivyo walikujibu nini?

Shahidi: Waliniuliza taarifa za kuuawa kwa Erasto nilizipata wapi.

Wakili Magafu: Ukawajibu nini?

Shahidi: Niliwaambia nilizisikia baada ya kupigiwa simu kwamba Erasto ameuawa.

Wakili Magafu: Unaweza kukumbuka ni nani alikwambia kwamba Erasto ameuawa?

Shahidi: Nilipata taarifa baada ya kupigiwa simu na shemeji yake Erasto, anaitwa Shujaa.

Wakili Magafu; Ukiwa kule ukumbini Arusha walikwambia nini hao kina RPC na askari wengine?

Shahidi: RPC Arusha aliniambia tunakuonea huruma kwa sababu tukikukabidhi kwa hawa vijana waliokuja na wewe, sijui kama utarudi salama.

Wakili Magafu: Kutokana na kauli hiyo au ushauri huo wa RPC Arusha uligundua nini?

Shahidi: Kwa sababu hao walioniambia hivyo ni viongozi wakubwa niliingiwa na hofu sana.

Wakili Magafu: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi: RCO Ramadhan Ng’anzi (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) alitoa amri kwa afande Samuel na kumwambia ondokeni naye.

Wakili Magafu: Baada ya kutolewa hapo ukumbini mlielekea wapi?

Shahidi: Tulielekea kama tunaenda Babati.

Wakili Magafu: Mlienda hadi wapi?

Shahidi: Tulienda hadi uwanja wa Ndege Kisongo, mkoa wa Arusha na tulienda tukaingia upande wa kushoto.

Wakili Magafu: Safari yenu huko iliishia wapi?

Shahidi: Tulienda hadi kwenye mashamba makubwa ambako kuna kituo cha Polisi kule.

Wakili Magafu:  Hicho kituo kinaitwaje?

Shahidi: Wao wenyewe Polisi waliniambia unaijua Guantanamo wewe?

Wakili Magafu:  Ehee mlipofika huko Guantanamo nini kiliendelea?

Shahidi: Hapo kituoni tulimkuta dada mmoja askari akiwa kaunta na akaambiwa chomoa hiyo redio ya Sub Uffer na switch yake ilete.

Wakili Magafu:  Ni nani aliomba hiyo redio ya Sub Uffer?

Shahidi: Ni askari mmoja toka Arusha aliyekuwa ameongozana na askari wa Moshi anaitwa Faustine Mafwele.

Wakili Magafu: Nini kilifuata?

Shahidi: Waliifungulia kwa sauti kubwa hiyo redio na wakanifungua pingu zote za mikononi na miguuni na kuniambia nivue nguo na kubaki kama nilivyozaliwa.

Wakili Magafu: Baada ya kuvua hizo nguo na kubaki kama ulivyozaliwa, walikufanyaje?

Shahidi: Waliniweka chini ya sakafu wakaniambia wao hawana ombi kama wale maofisa wakubwa zao ila wao wana amri tu.

Wakili Magafu: Wakafanyaje sasa?

Shahidi: Waliniambia sisi hatutaki maelezo wala kinachohusiana na mauaji ya Erasto.

Wakili Magafu: Wakati wakikueleza hayo walikuwa wana nini na nini?

Shahidi: Walikuwa na makaratasi mengi sana

Wakili Magafu: Walikuambia kitu gani kuhusiana na hayo makaratasi?

Shahidi: Waliniambia tunachotaka hapa ni sahihi yako tu.

Wakili Magafu: Baada ya kuwajibu hivyo walifanya kitu gani?

Shahidi: Nilisikia maumivu makali baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.

Wakili Magafu: Baada ya kukupiga kichwani kuna nini kingine walifanya?

Shahidi: Niliingizwa bomba la chuma katikati ya miguu na yule shahidi aliyetoa ushahidi wake jana (afande Dereck) na mwenzake afande Chilumba akanishika kiuno na kuniweka kwenye meza na kilichoendelea hapo mheshimiwa nilikuwa nakomeshwa na waliniambia hapa salama yako ni sahihi.

Wakili Magafu: Baada ya kuingizwa bomba walifanyaje?

Shahidi: Afande Chilumba alimwambia Dereck jisevie.

Wakili Magafu: Baada ya hapo walifanya kitu gani?

Shahidi: Nilipigwa kwenye nyayo kwa juu (kwenye kifundo) na nilipiga kelele sana.

Wakili Magafu: Sasa hebu tusaidie ile redio ilikuwa na kazi gani?

Shahidi: Yule askari wa Arusha Faustine Mafwele alikuwa anaongeza sauti ili kuzima sauti yangu ibaki ya redio.

Wakili Magafu: Tusaidie ukiwa Moshi, unasema RCO aliondoka kwa hasira baada ya kuambiwa hujasaini, kwani mliondoka kuelekea wapi?

Shahidi: Mashamba ya miwa TPC

Wakili Magafu:  Mlipofika mashamba ya miwa kulitokea nini?

Shahidi: Waliniambia sali sala yako ya mwisho

Wakili Magafu:  Ulisali?

Shahidi: Nilisali kwa sababu kwenye moyo wangu nilishamwambia Mungu lolote linaweza kutokea na tayari nilikuwa nimeshaweka nadhiri.

Wakili Magafu: Baada ya wewe kumaliza kusali walifanya nini?

Shahidi: Askari mmoja alitoa kitu kama kisu kwenye ncha ya bunduki ya SMG (singe) na kunichoma nayo kwenye unyayo wa mguu.
Wakili Magafu: Walipoingiza hiyo singe kwenye mguu wakafanyaje sasa?

Shahidi: Walikuwa wanaichezesha huko ndani katikati ya mfupa na nyama huku wakiishindilia.
Wakili Magafu: Nini kiliendelea tena?

Shahidi: Walisema wananipeleka kwenye tocha ya mwisho (mateso) na walinipeleka kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu na kiwanda cha TPC

Wakili Magafu: Mlipofika kulifanyika kitu gani?

Shahidi: Waliipiga kisu suruali yangu niliyokuwa nimevaa na ikatolewa mwilini.
Wakili Magafu: Wakafanya kitu gani sasa?

Shahidi: Niliona wana kipande cha tofali za block (mchanga) kimefungwa kamba.

Wakili Magafu: Hicho kipande cha tofali kazi yake ilikuwa nini?

Shahidi: Walikichukua wakanifunga kwenye …(sehemu za siri) wakaliacha likiwa linaning’inia huku mimi nikiwa nimefungwa pingu juu ya paa la nyumba.

Wakili Magafu: Hilo zoezi lilichukua muda gani?

Shahidi: Sikuwa najielewa baada ya hapo.

Wakili Magafu: Wakati huo hizo document ulikuwa umeshazisaini?

Shahidi: Kwa sababu niliona nakufa ilibidi nisaini

Baada ya Wakili Magafu kumaliza kumwongoza shahidi huyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, alisimama na kumwomba Jaji Salma upande wa utetezi wamwite mahakamani Daktari wa Hospitali ya Mawenzi aje kuhojiwa kuhusiana na matibabu ya Mredii anayedaiwa kuteswa.

“Mheshimiwa Jaji, chini ya kifungu cha 291 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 ya Sheria ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo, Daktari Massam E ambaye ana cheo cha AMO (Assistant Medical Officer) aliyejaza fomu namba tatu ya Polisi, aletwe mahakamani kwa ajili ya cross examination (mahojiano),” alidai Chavula.

Kutokana na hoja hiyo ya upande wa mashtaka, Wakili Magafu aliiambia mahakama hiyo kwamba wanatarajia kuleta mashahidi wawili mahakamani akiwamo daktari huyo wa Mawenzi na daktari wa Magereza, hivyo wanaomba wenzao wawe wavumilivu.

Dakika chache baadaye, Wakili Chavula alianza kumhoji shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi (Mredii) na mambo yalikuwa hivi:

Wakili Chavula: Nairejesha mahakama nyuma kidogo kwenye kumbukumbu zake, tarehe 10/2/2015 wakati wa PH (Preliminary Hearing), shahidi ukiwa na mawakili wako, kwa nini ulisema ulikamatwa tarehe 15/8/2013, Je, uliidanganya mahakama?

Shahidi: Labda nilikuwa nimesahau.

Wakili Chavula: Umeileza mahakama kwamba tarehe 18/8/2013 ukiwa kizuizini pale Polisi Mererani, baadaye ukapelekwa Polisi Kia, kweli si kweli?

Shahidi: Kweli
Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba shahidi wa nne, afande Dereck alikuwa miongoni mwa waliokutesa kutoka Guantanamo hadi mashamba ya TPC?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Chavula: Kwa nini jana, hamkumuuliza maswali wakati anaitwa kutoa ushahidi wake kwamba alihusikaje kukutesa?
Shahidi: Jaji ndio anajua kwa sababu alikuwa hajaruhusu hilo.

Wakili Chavula: Ni sahihi kwamba wakati Erasto anauawa haukuwa Mererani, Arusha wala Orkalili?
Shahidi: Sahihi.

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu anayemtetea mshitakiwa wa pili na wa tano, Wakili Emmanuel Safari anayemtetea mshitakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshitakiwa wanne, sita na saba.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdala Chavula.

Hadi sasa jumla ya mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Hai, (OC-CID) Joash Yohana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai (DMO) Dk. Paul Chaote (39) na Khalid Sankamula (49) ambaye ni Mganga wa Kienyeji na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora.

Wengine ni Anase Khalid (37), mkulima na mkazi wa Kaliua, Tabora, Mbazi Steven (32), mkazi wa Arusha na Ofisa Upelelezi, Kitengo cha Intelijensia ya Jinai mkoa wa Kilimanjaro, Herman Ngurukisi (40), Inspekta Samueli Maimu (45) ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya ukaguzi ya Polisi (CRT) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa wa Kilimanjaro na Ofisa Upelelezi (Detective), Sajenti Atway Omari ambaye aliyekuwa katika timu ya CRT. Kesi hiyo itaendelea tena leo

Simba watanguliza "mashushushu" Mbeya

KOCHA MKUU WA SIMBA, MCAMEROON, JOSEPH OMOG.

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kikosi chake hicho kitatua jijini Mbeya kikifahamu wazi kuwa wapinzani wao Mbeya City ni "imara" na wanatakiwa kutumia nguvu za ziada ili kuhakikisha wanapata pointi zote tatu.

Mbeya City inatarajia kuwakaribisha vinara Simba katika mechi ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu Sokoine jijini Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog, alisema kuwa mechi zote za ligi kwa Simba ni sawa na fainali, lakini za ugenini huwa ni zaidi kutokana na kubadilisha mazingira ya uwanja.

Omog alisema kuwa bado amewaandaa wachezaji wake kuendeleza kasi waliyoionyesha kwenye mechi zilizopita licha ya kupata matokeo ya sare.

"Hakuna mechi rahisi, hakuna timu ndogo, tunacheza ligi moja na hivyo tunatakiwa kupambana katika kila mchezo ili kufikia malengo, lengo letu kubwa ni kutwaa ubingwa na ikiwezekana iwe mapema kabla ya mechi ya mwisho ya msimu," alisema Omog.

Naye Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema kuwa kikosi cha Simba kitawasili Mbeya leo na kuweka kambi nje ya jiji hilo ili kuendelea na mazoezi kabla ya kuwavaa wenyeji wao.

"Mimi niko Mbeya tayari kwa ajili ya kuweka mambo sawa, tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri mechi yetu ya Jumapili na ile ya Prisons itakayofanyika Novemba 18, tunajua Mbeya ni pagumu, lakini tutapambana," alisema mratibu huyo.

Aliwataja wachezaji ambao Simba itaendelea kuwakosa kutokana na kuwa majeruhi ni pamoja na Salim Mbonde, Saidi Mohammed na Shomary Kapombe, ambaye bado anaendelea na kliniki maalumu.

Ili kujiandaa na mchezo huo, kikosi cha Mbeya City kilichoko chini ya kocha wake raia wa Burundi, Ramadhani Nsanzurwino, kiliingia kambi juzi huku wachezaji wake ambao ni majeruhi ni Haruna Shamte na John Kabanda

Mashabiki waYanga watolewa hofu

KOCHA WA YANGA, GEORGE LWANDAMINA.

LICHA ya kuwakosa nyota wake wanne, kocha wa Yanga, George Lwandamina, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwa timu yake inauwezo wa kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Singida United.

Yanga ipo Singida bila ya washambuliaji wake, Donald Ngoma na Amisi Tambwe pamoja na Thaban Kamusoko na Juma Abdul.
Wakati Ngoma, Tambwe na Kamusoko wakiukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi, Abdul anakabiliwa na kadi tatu za njano zinazomfanya kukosa mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Singida, Lwandamina, alisema kuwa anaamini wachezaji wake ambao wapo ndani ya kikosi kilichoelekea Singida wanauwezo mkubwa wa kuwakabili wenyeji wao.

"Nina imani na wachezaji wangu wote, tunaenda kukabiliana na Singida United huku nikiamini tunauwezo wa kupata ushindi," alisema Lwandamina.

Alisema wamejitahidi kufanya marekebisho kwenye makosa madogo madogo aliyoyaona kwenye mchezo uliopita.

"Tumefanyia kazi suala la umaliziaji, yapo makosa madogomadogo ambayo niliyaona kwenye mchezo dhidi ya Simba, nataka
tutumie vizuri nafasi tunazozitengeneza ndani ya uwanja," aliongezea kusema Lwandamina.

Cannavaro: Hautakuwa mchezo rahisi

Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro', aliiambia Nipashe kuwa mchezo huo wa kesho hautakuwa rahisi kutokana na ubora wa kikosi cha wapinzani wao.

Alisema Singida United wamefanya usajili mzuri na wanachezaji wenye uzoefu na ligi hivyo wao (Yanga) watacheza kwa tahadhari kuhakikisha wanapata ushindi.

“Singida si timu ya kubeza… tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi," alisema Cannavaro.
Mchezo huo wa kesho utachezwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida

Nyalandu halazimiki kuandika barua bungeni: Msekwa

Nyalandu halazimiki kuandika barua bungeni: MsekwaDar es Salaam. Spika wa zamani, Pius Msekwa amesema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu hakuwa analazimika kuandika barua kwa Spika wa Bunge wala CCM kwani kuonyesha kwake nia ya kujiunga na Chadema kulitosha kuthibitisha hilo.


Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Msekwa ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM mstaafu, alisema kilichomwondoa Nyalandu CCM ni kifungu cha 13 (f) cha Katiba ya CCM kinachoeleza kuwa mtu aliyejiunga na chama kingine chochote cha siasa anapoteza sifa ya kuwa mwana CCM.

“Kilichomwondoa Nyalandu ni kujiunga na chama kingine kinyume na kifungu cha 13 (f). Kuandika barua ni utaratibu tu wa kutoa taarifa kwa chama au Bunge ili wajue,” alisema Msekwa.

Alisema mbali na katiba ya CCM, hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mtu aliyejivua uanachama wa chama cha siasa anapoteza sifa ya kuwa mbunge.

“Kuandika barua ni utaratibu tu... Chama pia kinaweza kumwandikia Spika ili ajue kwamba yule siyo mwanachama wake,” alisema.

Mbali na mazungumzo ya simu, baadaye Msekwa alituma ujumbe wa maandishi (sms) kupitia simu yake ya mkononi akisisitiza suala hilo.

“Nathibitisha tu maneno niliyoyasema kwenye simu kuhusu Nyalandu na mambo yake. Ni kwamba Nyalandu amepoteza uanachama wake wa CCM kutokana na ibara ya 13(1)(f) ya Katiba ya CCM. Na amepoteza ubunge wake kutokana na Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya nchi. Hakuna haja ya yeye kuandika barua kwa chama au kwa Spika.

Aliongeza: “Kwa mfano, wakati mimi nikiwa Spika, Mhe. (Augustino) Mrema alikuwa Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Halafu akaamua ghafla kuhamia TLP. Hakuna barua niliyoandikiwa kuhusu jambo hilo. Lakini tamko lake lilitosha kuniwezesha kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba nafasi ya Mrema bungeni ilikuwa wazi kwa hiyo Tume ikachukua hatua za kuijaza. Hakuna utata wowote kuhusu Nyalandu,” alisema Msekwa.

Utata wa barua

Msekwa ametoa ufafanuzi huo wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu barua ya Nyalandu kama imepokewa na Ofisi ya Bunge au la.

Wakati Ofisi ya Spika ikisema haijapokea barua hiyo, Nyalandu ameibuka na kuonyesha barua aliyoituma katika mhimili huo.

Nyalandu alimwandikia Spika Ndugai barua hiyo ambayo Mwananchi limeiona Oktoba 30, siku ambayo alitangaza kujiuzulu nafasi zote ndani ya chama hicho ukiwamo ubunge.

Lakini juzi, Ofisi ya Bunge katika taarifa yake ilisema haijapokea barua hiyo badala yake imepokea ile ya CCM Oktoba 30 ikieleza kuwa Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wake.

Siku hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alihojiwa na Azam TV na kusema kuwa alikuwa hajapokea barua ya Nyalandu lakini hakusema kama alikuwa amepokea ile ya CCM. Alisema endapo angeipata (Barua ya Nyalandu) na kuthibitisha kujiuzulu kwake, angeshauriana na wasaidizi wake kabla ya kuchukua uamuzi.

Ikinukuu barua ya CCM, Taarifa ya Bunge inasema kuwa chama hicho kimekuwa kikifuatilia vitendo na kauli za Nyalandu zisizoridhisha kinyume cha misingi, falsafa na itikadi ya CCM.

“Hivyo, Chama cha Mapinduzi kuanzia tarehe ya barua yao kimemjulisha Mheshimiwa Spika kuwa Lazaro Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa Chama cha Mapinduzi na hivyo kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa ibara ya 13 ya chama hicho,” inasema taarifa hiyo ya Bunge.

Taarifa hiyo inasema kutokana na barua hiyo, Nyalandu amekoma kuwa mbunge na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa.

Hata hivyo, mara baada ya mbunge huyo kutangaza kujiuzulu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alikaririwa akisema Nyalandu ametumia haki yake ya kikatiba inayompa haki kila Mtanzania kuwa mwanachama wa chama chochote.

“Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri inaeleza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuwa na chama. Ninachoweza kusema ni kwamba kuna jambo la kawaida kabisa lililotokea na wala siyo kubwa kama linavyodhaniwa.”

Polepole alisema wameondoka wazito kwenye chama na kimebaki kimoja na kwamba Nyalandu si sehemu ya wazito, bali ni mwananchi wa kawaida mwenye haki na si mara ya kwanza jambo hili kutokea.

Barua ya Nyalandu

Katika barua yake kwa Spika Ndugai ambayo Mwananchi imeiona pamoja na mambo mengine, alimjulisha kuwa kama alivyotangaza kupitia mkutano wake wa wananabari ameamua kujiuzulu nafasi yake ya ubunge wa jimbo Singida Kaskazini kupitia CCM.

Mwanasiasa huyo anasema licha ya kuondoka CCM na bungeni, bado anaamini kwamba Tanzania inahitaji kupata Katiba Mpya itakayoweka bayana ukomo wa mamlaka ya mihimili ya utawala (Bunge, Serikali na Mahakama) ili kuondoa mwingiliano unaonekana kufanyika kwa wazi sasa.

“Kwa sasa dola haionekani kuwa na mipaka katika dhana ya uongozi wa nchi na hivyo kufanya uwakilishi wetu wa wananchi bungeni kuwa legevu kuliko ilivyokusudiwa kikatiba.”

Nyalandu anawashukuru wabunge wenzake, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Freeman Mbowe, maspika wastaafu, Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda pamoja na Ndugai kwa ushirikiano waliomuonyesha katika vipindi vinne alivyokuwapo bungeni hapo ambako “Alifanya kazi kwa mapenzi makubwa, dhamira ya dhati na moyo mkunjufu.”

Katika barua yake hiyo, Nyalandu anadai kwamba dola imeingilia kwa kiasi kikubwa mfumo wa utendaji na uendeshaji wa CCM hadi kukosa uelekeo, jambo ambalo alisema linawaondolea au kuwapunguzia wabunge wake uwezo wa kufanya uamuzi binafsi wakati wa mijadala au katika kupiga kura kwa kadri ya dhamira zao zinavyowaongoza kama ilivyokuwa wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.

Source: Mwananchi