Saturday, 20 January 2018

Diwani afariki dunia Kwimba



Diwani wa Kata ya Lyoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Julius Samamba (CUF), amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa kwa umma iliyotelewa leo Ijumaa (jana) na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Pendo Malebeja imeeleza kuwa diwani huyo alifariki dunia Januari 16 akiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikolazwa kwa matibabu.

“Mazishi ya marehemu yanatarajiwa kufanyika leo Januari 19 katika kijiji cha Kimiza kata ya Lyoma,” anasema taarifa hiyo.

Pamoja na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo, Malebeja amesema kifo cha diwani huyo kuwa pigo kwa halmashauri kutokana na umahiri na uwezo aliokuwa nao katika kujenga na kusimamia hoja kwenye mijadala ya masuala ya maendeleo.

Source: Mwananchi

Povu la kocha wa Simba kwa Mavugo


Laudit Mavugo.

KOCHA Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma amesema kuwa ushindi ambao timu yake iliyoupata juzi Alhamisi katika mchezo dhidi ya Singida United ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya wachezaji wake huku akimtolea ‘povu’ straika wale Laudit Mavugo.

Simba ilipata ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya wababe hao wa Singida ambapo mabao yake yalifungwa na Shiza Kichuya, Asante Kwasi na Emmanuel Okwi aliyefunga mawili. Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Djuma alisema nafasi ya Okwi kucheza ilitakiwa ichukuliwe na Mavugo lakini kwa kuwa

Mavugo hakuonyesha kiwango kizuri mazoezini ilimbidi afanye mabadiliko hayo. “Okwi amefanya mazoezi na sisi siku mbili tu kama mnavyojua hakuwepo kambini, nilipanga kumtumia Mavugo lakini nimemwambia kuwa hakuonyesha uwezo mzuri, ndiyo maana nikaamua kumpa nafasi Okwi na kweli ameitumia vizuri. “Nimeshamueleza Mavugo kuwa yeye ni ndugu yangu lakini katika hili suala la kazi anatakiwa kuonyesha uwezo na kufanya kweli, siwezi kumpa nafasi kama haonyeshi uwezo,” alisema kocha huyo.

KUHUSU KOCHA MPYA

Kuhusu kocha mpya wa Simba, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa aliyekuwepo jukwaani akifuatilia mchezo huo, Djuma alisema yeye hana tatizo na ujio wa kocha huyo, anamkaribisha na yupo tayari ku- fanya naye kazi. “Nipo tayari wala sina tatizo, namkaribisha na tutakuwa pamoja, kuhusu mfumo na maendeleo mengine nitampatia ripoti kisha yeye ndiye atakayeamua juu ya kutumia au la,” alisema. Upande wa Kocha wa Singida United, Hans van Pluijm alisema matokeo ya mchezo huo yametokana na walinzi wake kufanya makosa na Simba wakayatumia vizuri.

Mapenzi yamtesa Kajala kisa mwanaye



STAA wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja amefunguka kuwa hivi sasa anaumizwa na mapenzi ya kufichaficha kwa sababu ya kulinda heshima yake kwa mtoto wake wa kike, Paula kwa kuwa sasa amekuwa msichana mkubwa.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Kajala alisema amekuwa kwenye wakati mgumu sana wa kuwa na uhusiano wa kificho lengo likiwa ni kutomharibu mwanaye huyo ambaye ana uelewa mkubwa na anatambua kila kitu.

“Sipendi Paula anijue kiundani kuhusiana na mahusiano kwa sababu kwa umri aliofikia na darasa alilopo (Kidato cha nne) kama sitakuwa na usiri ataelewa kila kitu, sio Kajala yule tena wa zamani wa kuweka mpenzi wazi ingawa inaniumiza kwani sikuzoea, na mapenzi ya siri yanaumiza asikwambie mtu,” alisema Kajala.



Chuchu Hans afunguka kuachana na Ray


MSANII wa filamu za Kibongo, Chuchu Hans ameibuka na kusema kuwa tetesi zilizozagaa akidaiwa kuachana na mzazi mwenziye Vincent Kigosi ‘Ray’ na kwamba ndiyo sababu ya kubadili jina lake kwenye ukurasa wake wa Instagram siyo za kweli.

Awali kwenye ukurasa wa Insta Chuchu alikuwa akijiita Chuchu Hans the Great na sasa anajiita Chuhans Kichuna, jambo lililowafanya wengi waamini safari ya mapenzi yao imefika mwisho.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Chuchu alisema kuwa yeye ameamua tu kubadili jina na wala hajaachana na Ray na kama wapo wanaosubiri penzi livunjike, watasubiri sana.

“Waniache jamani kila siku nimeachana na Ray… nimeachana na Ray…, nina sababu zangu za kubadilisha jina, haina maana kwamba tumeachana, hata hivyo sitaki kuongelea sana suala hilo kama tumeachana au la, majibu mtayapata subirini tu,”alisema Chuchu.

Serikali Yakataza Kulima Pamba kwa Mkataba


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imekataza kilimo cha pamba cha mkataba kwa sababu kinawanyonya wakulima.

Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua zahanati ya Hunyari wilayani Bunda, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.

“Ni marufuku kwa wanunuzi wa pamba kulima pamoja na wakulima kwa sababu wakulima wanakosa uamuzi wa kupanga bei. Kuanzia sasa zao hilo litauzwa kwa njia ya mnada.”

Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa kilimo cha zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Kilimo katika wilaya hiyo wawafuate wakulima vijijini kwa ajili ya kutoa elimu itakayowawezesha wakulima kulima kwa kufuata njia bora za kisasa.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo lao.“Marufuku kulisha mifugo katika mashamba ya watu.”

Amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mfugaji yeyote atakayelisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima kwani tabia hiyo huchangia migogo baina yao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Steve Nyerere: “Nimekaa Ndani Wiki 3, Nimeona Waliosema Nina Ukimwi”


January 19, 2018 Muigizaji maarufu wa Bongomovie Steve Nyerere amezungumza baada ya kuugua kwa wiki tatu Steve ameeleza kuwa alichokuwa anaumwa kuwa ni miguu na siyo VVU kama ilivyokuwa inasemwa kwenye mitandao japo hashangai watu kumsema.

Steve amesema hakuna mtu wake wa karibu aliyezusha suala la ugonjwa wake bali ni mitandao tu ndo imevujisha, alipoulizwa kama Wema Sepetu alikuwa miongoni mwa watu walioenda kumtembelea alijibu kuwa Utu haulazimishwi na kumuona mgonjwa hakulazimishwi pia.


Jenerali wa Jeshi ampa Rais Kabila siku 45 aachie Urais



Haijapita hata miezi mitatu toka tushuhudie Jeshi likiingilia kati na kumuondoa madarakani Rais aliekaa muda mrefu madarakani, Robert Mugabe wa Zimbabwe….. leo tena tunasikia huko Congo DRC Mwanajeshi mmoja ampa Rais Kabila siku 45 awe ameachia madaraka.

Tunafahamu kwamba Rais Kabila alimaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba kuwa Rais mwezi December 2016 lakini hajaachia madaraka, mengi yamesemwa na Serikali ikiwemo “hatuna pesa za kutosha kufanya Uchaguzi Mkuu”

January 19 2018 Mwandishi wa habari Byobe Malenga alieko Congo DRC ameiambia millardayo.com kwamba Jenerali mmoja wa Jeshi aitwae John Tshibangu ameasi na kutangaza vita na Rais Kabila, amempa siku 45 aachie madaraka.

Asubuhi ya Ijumaa January 19 2018 Wanajeshi walionekana kuizingira kwa wingi IKULU ya Kinshasa huku video iliyorekodiwa na Jenerali Tshibangu ikiendelea kusambaa ambapo ndani yake ameonekana kazingirwa na Wanajeshi wenye silaha.

Kwenye video hiyo Tshibangu amenukuliwa akisema “Nafahamu siri ya Rais Kabila, sasa ni muda wa kuondoa Serikali ya Mabeberu na Udikteta, na ni lazima Rais Kabila aombe msamaha kwa Wakongo kuanzia Makanisani, Shuleni na hata Raia wa kawaida kwa kosa la kushindwa kuiongoza Nchi”

“Mimi kama Mwananchi mwenye msimamo na huruma kwa mateso yenu, niliamua kujitokeza ili kumfukuza Joseph Kabila kwa nguvu za vita na kijeshi, nawahakikishia kwamba tutamuwinda na atakimbia. ” – John Tshibangu.

Tshibangu amelitaja kundi lake la Waasi kwamba linaitwa Forces Nouvel du Congo ikimaanisha NGUVU MPYA KWA AJILI YA CONGO ambapo Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kumekuwa na majaribio ya mapinduzi katika Serekali ya Congo ambapo IKULU ya Taifa imezungukwa na Wanajeshi wengi wanaoonekana kama Wageni, yaani sio Wanajeshi wa congo.

Raisi Kabila amekabiliwa na upinzani mkali kutokana na nia yake ya kutaka kugombea Urais kwa muhula wa tatu baada ya muhula wake wapili kumalizika mwezi December 2016.

John Tshibangu

Source: Millardayo

Friday, 19 January 2018

Ndege yatetemeka angani



Ndege moja ya Malaysia ililazimika kutua katika eneo la Australia ya kati baada ya tatizo la kiufundi kuifanya kuanza kutetemeka ikiwa angani, wamesema abiria.

Ndege hiyo aina ya MH122 ilikuwa inasafiri kuelekea Kuala Lumpur kutoka Sidney siku ya Alhamisi wakati iliporudi katika eneo ambalo haliko mbali na Broome, kaskazini Magharibi mwa Australia.

Ndege hiyo iliokuwa ikiwabeba watu 224 ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Alice Springs Airport.

Abiria wanasema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitetemeka na kutoa sauti kubwa.

Katika taarifa yake, kampuni ya ndege ya Malaysia Airline ilisema kuwa ndege hiyo ilibadilsha safari kutokana na tatizo la kiufundi.

Hatahivyo haikusema ni matataizo gani. Abiria Sanjeev Pandev alisema kuwa ndege hiyo ilionekana kuwa na tatizo hilo saa nne kabla ya safari kuanza.

''Ilikuwa ikitetemeka na kelele zilikuwa kubwa '', aliambia BBC.

''Watu walikuwa wakiomba na wengine walikuwa wakitokwa na machozi'', aliambia BBC.

Alisema kuwa abiria walionyeshwa njia za kubaliana na dharura na wafanyikazi wengi wao wakionekana kuogopa na kushtuka.

Simba kukutana na waliokwamisha mipango




Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC leo alfajiri wameondoka kwa ndege kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera kwaajili ya mchezo wao wa raundi ya 14.

Simba ambayo jana ilishinda mchezo wake wa raundi ya 13 kwa mabao 4-0 dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Uhuru, inakwenda kukutana na Kagera Sugar ambayo ilikwamisha mipango yake ya ubingwa msimu uliopita.

Kagera Sugar ilitibua mipango hiyo April 2 mwaka jana baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa uwanja wa Kaitaba hivyo kuinyima nafasi ya kurejea kileleni ikibaki na alama 55 katika nafasi ya pili na kuwaacha Yanga wakiwa na alama 56 kileleni.

Endapo Simba ingeshinda mchezo huo ingefikisha alama 58 hivyo huenda ingetwaa ubingwa kutokana na bingwa wa msimu uliopita kupatikana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, baada ya timu hizo mbili za Kariakoo kufungana pointi.

Simba ambayo kwasasa inaongoza ligi kwa alama 29 mbele ya Azam FC yenye alama 27, itashuka dimbani Kaitaba siku ya Jumapili.

Wenye mabasi wataka kumwona JPM



WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani, wameomba kukutana na Rais John Magufuli kumweleza matatizo yanayowakabili ikiwamo  vipengele wanavyodai kuwa ni kandamizi katika kanuni mpya za leseni za usafirishaji.

Wamefikia hatua  hiyo baada ya kutofikia mwafaka katika kikao kilichofanyika jana  jijini Dar es Salaam kati yao  na maofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa  Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na Jeshi la  Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akitangaza azimio hilo kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi hayo (Taboa), Enea Mrutu, alisema wataandika barua kuomba kukutana na Rais  Magufuli ili kumweleza matatizo yanayowasibu.

"Tukimaliza kikao hapa na kwa kuwa wote mmekubali na mnataka kukutana na Rais  Magufuli, sekretarieti itakutana tutaandika hiyo barua na tutaipeleka nyumba nyeupe (Ikulu)," alisema Mrutu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taboa , Mohammed Hood, alisema kabla ya kuandikia barua ya kuomba kukutana na Rais, watafanya utaratibu wa kuonana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

"Hatuwezi kufika kwa Rais  moja kwa moja bila  kupitia kwa Waziri, hivyo mimi  nitampigia Waziri ili nimwombe tuonane na baada ya hapo ndipo  tutakwenda  Ikulu," alisema Hood.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alisema hakuna uadui kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi na kwamba suala la faini inayotozwa kuanzia Sh. 250,000 hadi 500,000 haliwezi kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni la  kisheria.

"Jambo hili litafutiwe namna nyingine ya kuzungumza kwa sababu lipo kisheria. Hakuna mmiliki atakayeshitakiwa  au kupelekwa mahakamani kwa kosa la  gari kwenda kasi, dereva ndiye atakayeshitakiwa," alisema Kahatano.

Kahatano aliwataka Taboa kwenda Tume ya Ushindani kulalamika endapo wanaona kanuni au sheria hizo mpya zinawakandamiza.

Kuhusu  kuzuia gari kwa kosa la  dereva, Kahatano alisema sheria ya Sumatra inasema endapo gari litakamatwa, mmiliki wa gari atapewa siku 14 za kulipa faini hiyo na endapo siku hizo zikipita bila kulipa, mmiliki anaweza kufika Polisi au Sumatra na kutaka kesi iende mahakamani.

Alisema hakuna gari lolote litakalozuiwa kwa kosa alilofanya dereva na kwamba makosa ya dereva na mmiliki yametenganishwa.

Wakichangia katika mkutano huo, wajumbe wa Taboa wengi wao  walilamikia kanuni zilizokuwapo katika leseni za usafirishaji kuwa zinawakandamiza, huku wakipendekeza faini za viwango vipitiwe upya pamoja na makosa ya dereva na mmiliki yatenganishwe.

Source: Nipashe

Afya ya Tundu Lissu yazidi kuimarika, sasa Anaweza Kutembea Mwenyewe, Kuoga


Afya ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.

Mbunge huyo aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano kati ya hizo zikimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili.

Vinceti Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema  jana kuwa Lissu ameanza kutembea mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo kwenda kuoga bila msaada wa mtu mwingine.

"Tunamshukuru Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri... tangu ameanza kupatiwa matibabu na mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno," alisema na kueleza zaidi:

"Maendeleo ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa maliwatoni lakini sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia mguu chini.

"Anakula mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo makubwa."

Mghwai alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo ikawa sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa matibabu na bila usumbufu wowote.

Alisema Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda kumjulia hali.

"Kwa sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari wanamfanyia mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona na ndiyo sababu anaendelea kupona haraka," alisema Mghwai.

"Ubelgiji muda wote yuko na madaktari akipatiwa matibabu hasa mazoezi ya viungo... huku ni kazi kazi tu. Na madaktari waliahidi kufanya kazi.

"Kule Nairobi wakati mwingine alikuwa akiwaambia madaktari wamuache pale anaposikia maumivu wakati wa mazoezi lakini sasa hakuna kitu kama hicho na wamemwambia avumilie apone."

Kuhusu risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na madhara kwake kiafya.

"Kule Ubelgiji kazi kubwa ni kumfanyisha mazoezi ili sasa aweze kurejea katika hali yake na ndicho ambacho wanaendelea nacho na kwa kweli tumeanza kuona maendeleo makubwa."

Kuhusu gharama za matibabu, Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100 zinatumika kila mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge halijatoa fedha na familia inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa huku na kule.

Alisema fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na wadau mbalimbali na wamekuwa wakifanya harambee kadhaa za kuchangia.

"Gharama ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali hiyo na kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi ni fedha za matibabu pekee," alisema Mghwai.

Alieleza zaidi kuwa fedha zilizochangwa hazitoshi kumtibu Lissu na kwamba kwa sasa wadau wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali inagharamia matibabu yake.

Alisema familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha matibabu yake.

"Tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa mzima."

Alisema gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya matibabu ya Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na si yeye peke yake kuzungumzia.

Lissu ambaye Januari 6 alizungumza na waandishi wa habari akiwa nje ya Hospitali ya Nairobi, ikiwa ni siku moja kabla ya kusafiri kuelekea nchini Ubelgiji, alieleza kuwa alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na 16 zilimjeruhi maeneo mbalimbali ya miguu, mikononi na kwenye nyonga.

Lissu alisema kutokana na shambulio hilo alifanyiwa operesheni 17 zilizofanikisha kuondoa risasi saba zilizoingia mwilini huku risasi moja ikisalia.

Wataalam wa afya walimshauri kuiacha risasi hiyo iliyopo kwenye nyonga wakisema kuwa inaweza kuleta madhara zaidi kama watajaribu kuitoa.



Mkuu wa kitengo cha ununuzi Muhas asimamishwa kazi




Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu wa kitengo cha ununuzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), baada ya kudai kubaini uwapo wa harufu ya ufisadi katika ununuzi wa taasisi hiyo.

Pamoja na mkuu huyo wa kitengo, Profesa Ndalichako pia aliagiza kuchunguzwa kwa watu wote watakaohusika katika sakata hilo.

Profesa Ndalichako alitoa uamuzi huo juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea chuoni hapo na kubaini matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema kabla ya kwenda chuoni hapo, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia tuhuma za ufisadi hususan kwenye masuala ya ununuzi na matokeo yalionyesha zina ukweli.

Aliongeza kuwa amebaini kuwa linapofika suala la ununuzi kwenye taasisi hiyo hakuna ushindani, badala yake kazi hizo anapewa mtu mmoja kupitia kampuni tatu tofauti. “Nimefanya uchunguzi wangu nimebaini kuna kampuni tatu ambazo zote zinamilikiwa na mtu mmoja ndizo zinazopata zabuni ya ununuzi katika chuo hiki, hakuna mchakato wa kushindanisha kampuni kama zinavyoagiza sheria za ununuzi serikalini,” alisema.

Profesa Ndalichako alibainisha hayo mbele ya menejimenti ya Muhas na kumpa maagizo nwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Mariam Mwaffisi kufanya uchunguzi zaidi akishirikiana na wajumbe wake wa bodi ili kuwanasa wote ambao kwa namna moja au nyingine wamehusika kupindisha utaratibu wa Serikali.

“Ninaagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu huyo wa kitengo lakini si ajabu wapo wengine mapapa, mwenyekiti nitakukabidhi makabrasha yote niliyoyapata kutokana na uchunguzi wangu, fuatilieni hata kama ni makamu mkuu wa chuo, kama amehusika awajibishwe msimuogope mtu,” alisema

Pia, alitumia fursa hiyo kuagiza wakuu wa idara kuwa makini kwenye uagizaji wa vitu kulingana na mahitaji.   

Source: Mwananchi

Ujumbe wa Messi kwa Gaucho



 Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi.

LIONEL Messi wa Barcelona amemtumia ujumbe nyota wa zamani wa timu hiyo, Ronaldinho ambaye amestaafu kucheza soka la kulipwa.


Ronaldinho.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Messi ambaye bao lake la kwanza alifunga akipata basi ya Ronaldinho ameandika ujumbe huu:

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema, nimejifunza mengi kwako. Nitaendelea kukushukuru kwa kufanya mambo kuwa rahisi kwangu nilipojiunga na timu.

“Nilikuwa na bahati kuwa karibu yako, licha ya kuwa staa uwanjani lakini nje ya uwanja ulikuwa mtu mwema na hilo ndilo jambo muhimu, licha ya kuwa umeamua kustaafu, soka halitasahau tabasamu lako, nakutakia kila la kheri, Gaucho.”