Tanzania\'s leading online News Edition (The National Newspaper). Get access to the most current and latest authoritative news on local issues, politics, events, celebrations, editorial, columnists, features, people and business.
Monday, 22 January 2018
Mtoto wa Navy Kenzo awa kivutio kwa watu

MTOTO wa wanamuziki wa kishua wanaounda Kundi la Navy Kenzo, Emannuel Mkono ‘Nahreel’ na Aika Mareale waliompa jina la Gold, amegeuka kivutio kwa watu mbalimbali baada ya wawili hao kuachia picha yake mtandaoni.
Wanamuziki hao ambao ni kapo ya muda mrefu walionesha picha ya mtoto huyo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na kusababisha watu wengi kuichua na kuweka katika kurasa wakimsifia.
Mama wa Gold, Aika aliiambia Over Ze Weekend, kuwa anafurahi kuona watu wengi wamefurahishwa na ujio wa mwanaye, jambo ambalo kwao ni baraka kubwa katika safari yao ya kimaisha.

Mnyeti atoa agizo mbunge wa Kiteto akamatwe

Kiteto. Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amemuagiza mkuu wa wilaya ya Kiteto, mhandisi Tumaini Magessa kumkamata mbunge wa Kiteto (CCM), Emmanuel Papian endapo atabainika kuwa anachochea migogoro ya ardhi.
Mnyeti amesema hayo Ijumaa Januari 19, 2018 wakati akihitimisha ziara yake ya siku saba alipotembelea wilaya ya Kiteto.
Amesema endapo Papian anasababisha migogoro ya ardhi kwa kuchochea wananchi walime kwenye hifadhi, anapaswa kuchukuliwa hatua.
"Mkuu wa wilaya wewe ndiye mteule wa Rais kwenye eneo hili la Kiteto. Endapo mtu mwingine hata kama ni mbunge wa jimbo akiwa anachochea migogoro ya ardhi, uwe unawakamata na kuwaweka ndani," amesema Mnyeti.
Amesema migogoro ya ardhi kwenye wilaya ya Kiteto haitaweza kumalizika endapo wanasiasa wataendelea kuwachonganisha wakulima na wafugaji.
"Mbunge asiote mapembe na kupanda kichwani kwako, wewe ndiye mtawala wa hapa. Nataka siku nyingine unipigie simu kuwa umemkamata na kumweka ndani mbunge ili asirudie hilo," amesema Mnyeti na kuongeza,
"Mkuu wa wilaya unapozungumzia mgogoro wa kijiji zungumza sehemu husika na kama mbunge akiendelea kuchochea umkamate," amesema Mnyeti.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Papian hakukubali wala kukataa juu ya yeye kuchochea na kusababisha migogoro ya ardhi, ila amesema muda utaongea.
"Hapa tunavyozungumza nipo kwenye gari, ila suala hilo uliloniuliza litajulikana huko mbeleni tunakokwenda hivyo tujipe muda tuu itabainika," amesema Papian.
TPSF yaiomba Serikali kufanya marekebisho muswada wa ardhi

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeiomba Serikali kuondoa mabadiliko ya Sheria ya Ardhi yaliyomo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ili kuepuka madhara ya kiuchumi yanayoweza kusababishwa na mabadiliko hayo iwapo yatapitishwa.
Katika kuhimiza hilo, TPSF imemuandikia barua Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ikimtaka kuwashirikisha wadau kabla ya muswada huo kujadiliwa na Kamati ya Bunge.
Msimamo wa TPSF unafanana na wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambacho kimesema iwapo marekebisho hayo yatapitishwa na sheria kuanza kutumika, yataathiri mfumo wa rehani nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Katiba na sheria ya TLS, John Seka alisema kwa muda mrefu wananchi wengi wamekuwa wakitumia mashamba kama rehani kwenye taasisi za fedha.
Alisema wamewasilisha maoni yao Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inaouchambua muswada huo unaomtaka mmiliki wa shamba ambalo halijaendelezwa au kuendelezwa kidogo, kutumia fedha anayokopa kuliendeleza zaidi.
Jana, mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema muswada huo unapaswa kuondolewa kabisa bungeni kwani endapo kosa lolote litafanyika, madhara yake ni makubwa kwenye uchumi.
“Inawezekana Serikali ina lengo zuri, lakini hatukushirikishwa. Uwekezaji utakufa nchini kwa sababu wengi hukopa ili kuendeleza biashara walizonazo jambo linalozuiwa kwa sasa,” alisema Simbeye.
Kwa hali hiyo, alisema sekta ya kwanza kuanguka itakuwa ya benki na taasisi za fedha ambazo zitakosa wateja.
TPSF imeipongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, lakini imetoa angalizo kwa marekebisho yanayopendekezwa.
TPSF imepokea malalamiko kutoka kwa wanachama, benki na taasisi za fedha, wamiliki wa viwanda pamoja na wakulima kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa, inasema barua hiyo.
Miongoni mwa hoja zilitolewa na taasisi hiyo ni kutoshirikishwa kwa wadau katika utungaji wa mabadiliko hayo ili wawasilishe maoni yao.
Imesema kwa namna muswada huo ulivyoandaliwa, Serikali inaweza isipate mafanikio inayoyatarajia na mapendekezo ya vifungu hivyo vitatu yanaweza kuwa na athari kwa uchumi wa nchi.
“Kwa barua hii, tunaiomba wizara yako iuondoe mara moja muswada huo kabla haujajadiliwa na Kamati ya Bunge au Bunge lenyewe mpaka wadau, ikiwamo TPSF watakaposhirikishwa,” inasema barua hiyo.
Muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria tano ambazo ni Sura ya 25 ya Sheria ya Ufilisi, Sura ya 439 ya Sheria ya Bajeti, Sura ya 113 ya Sheria ya Ardhi na Sura ya 238 ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuondoa mapungufu mbalimbali yaliyomo katika utekelezaji wa sheria hizo.
Marekebisho ya Sheria ya Ardhi ambayo TPSF inapendekeza maoni yao yazingatiwe, inabadili masharti yaliyopo kwenye Kifungu cha 45 kwa kuongeza adhabu ya ukiukwaji wa masharti kwa mtu anayeweka dhamana ya miliki ya ardhi.
Kwenye sheria inayofanyiwa marekebisho, vifungu vya 120A, 120 B na 120 C vimeongezwa kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mkopo uliotolewa kwa dhamana ya miliki ya ardhi Tanzania zitumike kuendeleza sehemu ya ardhi iliyowekwa rehani kwa miliki zote ambazo hazijaendelezwa.
Marekebisho hayo yanawataka wote wawili; mkopaji na mkopeshaji, kuwasilisha taarifa kwa kamishna wa ardhi. Licha ya hilo, yanataka fedha itakayopatikana iwekezwe Tanzania.
Aidha, muswada unataka benki na taasisi zote za fedha zinazotoa mkopo husika; ndani na nje ya nchi kuwasilisha tamko kwa kamishna wa ardhi kwamba fedha hizo zitawekezwa Tanzania.
Maana yake, mkopo wa fedha zozote zitakazokopwa kwa dhamana ya ardhi ya Tanzania kisha zikawekezwa nje, utakuwa batili.
Waziri Lukuvi amewataka wadau wenye maoni kuhusu marekebisho yanayopendekezwa kwenye muswada huo kuyawasilisha kwenye kamati husika ya Bunge.
“Huo ndio utaratibu. Kama kuna malalamiko yoyote, ni vizuri yawahishwe wakati huu vikao vinapoendelea, yatachambuliwa,” alisema.
Dalali ameanza ruti kuhamasisha Simba kutwaa Ubingwa

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Mzee Hassan Dalali ‘Handsome Boy’, ameanza harakati za kuhamasisha wanachama wa timu hiyo kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo amepanga kutembelea Tanga na Zanzibar kabla ya mikoa mingine.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mzee Dalali alisema kuwa tayari ameshaanza kuzunguka katika matawi mbalimbali ya Mkoa wa Dar kwa ajili ya kuhamasisha umoja na mshikamano kwa lengo la kuweza kutwaa ubingwa wa msimu huu.
“Tayari nimeshaanza ziara yangu ya kuzunguka matawi ya nchi nzima, kwa hapa Dar nimeshakwenda kuongea na wanachama wa matawi ya Mabibo na leo (jana) nitakwenda Gongo la Mboto, lengo kubwa ni kuhamasisha umoja na mshikamano wa matawi ambao kama ulitoweka lakini sasa umeanza kuzaa matunda kutokana na ushirikiano wa viongozi wa juu wa timu, nawapongeza sana.
“Hili nimeamua kufanya mwenyewe kwa mapenzi ya timu yangu kwa sababu ni muda mrefu umoja na mshikamano umekuwa kama umepotea lakini wiki ijayo nitakwenda Tanga kisha Zanzibar, ikizingatiwa tulikuwepo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, muda mrefu umepita sasa bila ya kuchukua ubingwa lakini kwa mabadiliko chini ya viongozi wangu ambayo wanayafanya, naamini tutafanikiwa na kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Mzee Dalali.
Humphrey Polepole afunguka kuhusu UKAWA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa hakuna kitu kinaitwa UKAWA kwani mpango huo ulianzishwa na CHADEMA ili kuvitumia vyama vingine kisiasa.
Polepole amesema kuwa kama UKAWA ingelikuwepo hadi leo basi isingetokea baadhi ya majimbo CHADEMA kushindana na CUF ile hali vyama vyote vipo chini ya muavuli wa UKAWA.
“Hakuna kitu kinaitwa UKAWA, hii ilikuwa project ya Chadema ikivitumia vyama vingine, CUF, NCCR na NLD. Kilichobaki ni UKIWA, katika jimbo lililokuwa la CUF leo CDM na CUF wanamenyana,”ameandika Humphrey Polepole kupitia Twitter.
Hata hivyo, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kinondoni CUF kwa upande wa Prof Lipumba imesimamisha mgombea wake huku CHADEMA nao wakisimamisha mgombea wao.
Alichokisema Isha Mashauzi kuhusu mziki wa Taarabu

Msanii Isha Mashauzi maarufu kama Jike la Simba ameibuka na kusema muziki wa miondoko ya taarabu nchini hauwezi kufa kama baadhi ya watu wanavyodhani, kwa madai wao hawategemei 'kiki' katika kufanya kazi zao kama wanavyofanya wasanii wengine.
Isha amebainisha hayo wakati akitambulisha 'video' yake mpya ya wimbo 'nibembeleze' kwenye kipindi cha 'FRIDAY NIGHT LIVE' (FNL) kinachorushwa na EATV tinga namba moja kwa vijana, baada ya kuwepo minong'ono mingi kwa wapenzi na mashabiki wa nyimbo hizo wakidai huenda muziki huo umekufa, kwa maana hawasikii vijembe vya maneno wanavyopigana wasanii wenyewe kwa wenyewe kama wanavyofanya baadhi ya waimbaji wa muziki wa bongo fleva.
"Taarabu haiwezi kufa, naweza kusema ni muziki mama wa Afrika, Tanzania au hata duniani. Muziki wa taarabu ukipigwa sehemu yeyote kila mtu ataujua fika kwamba hii ni taarabu tofauti na muziki mingine kwa hiyo hauwezi kufa", alisema Isha Mashauzi.
Pamoja na hayo Isha ameendelea kwa kusema "naweza sema tu kwamba labda wanamuziki wa taarabu hawapendi zile kiki ambazo zipo kwa wanamuziki wengine, leo utasikia huyu sijui anatoka na fulani mara yule vile ndiyo mwisho wa siku aachie kazi yake mpya. Hicho kitu kwenye taarabu hamna naweza kutetea hivyo ndiyo maana wanasema hivyo"
Inasikitisha, Mashabiki Wawili wa WCB Wafariki Dunia kwa Ajali

Mashabiki hao waliopata ajali ya gari maeneo ya Chalinze wakitokea Morogoro kurudi Dar es Salaam, ni Philly Nevvo na mwingine ni Platnumz Mondi kwa majina ambayo walikuwa wanatua Instagram.
Rais wa WCB, Diamond Platnumz amesikitisha kutokea kwa ajali hiyo.
“Mbele Yenu Nyuma yetu, Siku zote tutaendela kuwakumbuka na kuthamini Mapenzi na mchango wenu Mkubwa kwa @wcb_wasafi…..Mwenyez Mungu azilaze Roho zenu mahali pema peponi….amen🙏 @philly_nevvo_msafi @,” aliandika Diamond.
Scorpion ahukumiwa miaka saba jela

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Salum Njwete ‘Scorpion‘ miaka 7 jela kwa kosa la kumjeruhi na kumtoboa macho Said Mrisho, pia mahakama imemtaka kulipa faini ya TSH. Milioni 30 kwa ajili ya fidia kwa majeruhi huyo.
Mlalamikaji amelia akidai adhabu hiyo haitoshi. Amesema atakwenda kwa Rais Magufuli kumueleza masikitiko yake.
Kagera Sugar imejiandaa kuikwamisha Simba

Klabu ya Simba SC leo inarejea kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, sehemu ambayo ina kumbukumbu ya kukwamishwa mipango yake ya kusaka ubingwa msimu uliopita.
Kocha wa Kagera Sugar Meck Mexime, amesema timu yake imejiandaa kwa muda mrefu hivyo leo inaingia uwanjani kupambana na vinara wa ligi Simba SC huku lengo likiwa ni kusaka alama tatu.
''Hali ya hewa leo hapa Bukoba ni jua tu na hali ya uwanja ni nzuri, tumefanya maandalizi kwa muda mrefu leo tuna kazi moja tu ya kucheza mpira kwaajili ya kupata alama tatu kwasababu mpira ndio kazi yetu'', amesema Mexime.
Timu hizo zinakutana kwenye mchezo wa raundi ya 14 ambapo Simba wanahitaji alama tatu ili kuweza kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi. Simba kwa sasa ina alama 29 nyuma ya Azam FC yenye alama 30.
Msimu uliopita Simba ikiwa inaelekea kwenye hatua za mwiosho za kusaka ubingwa ilitibuliwa mipango na Kagera Sugar April 2, 2017 ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 hivyo kuiacha Yanga katika mazingira mazuri ambayo mwisho wa ligi waliibuka mabingwa.
Magogo yaliyokosa mmiliki bandarini kuuzwa wakati wowote kuanzia sasa

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema magogo 938 yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yatauzwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukosa wamiliki wa mzigo huo.
Maamuzi hayo yamekuja baada ya Waziri Kigwangalla mwezi uliopita kufanya ziara ya kushitukiza bandarini hapo baada ya kupata taarifa kuwa kuna shehena hiyo ya magogo ambayo umiliki wake ulikuwa na utata.
Mhe. Kigwangalla alieleza kuwa magogo hayo yamekuwa bandarini kwa miaka 10 huku mengine yakiwa kwenye makontena 55 .
Kutokana na utata huo, Kigwangalla alitoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 kujitokeza wakiwa na nyaraka zote ili kuthibitisha kama kweli yalivunwa Zambia kama ilivyodaiwa au laah!.
“Kulikuwa na vikao mbalimbali ndani ya serikali kujadili suala hilo, na tumekubaliana kuyauza baada ya wahusika kutojitokeza kuthibitisha umiliki wake,” amesema Waziri Kigwangalla.
Waziri Kingwangalla amesema jukumu la kuyauza magogo hayo wamepewa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wanaoruhusiwa kisheria kufanya kazi hiyo, ambapo watashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS).
Kauli ya Salum Mwalimu kuhusu wanaodai kuwa sio mkazi wa Kinondoni

Mgombea ubunge wa Kinondoni kupitia Chadema, Salum Mwalimu amwajibu baadhi ya watu wanaodai kuwa yeye si mkazi wa wilaya ya Kinondoni, hivyo hana sifa za kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Akizungumza leo Januari 22, 2018 katika mahojiano na kituo cha tevisheni cha Azam, Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Zanzibar amesema ni mkazi wa wilaya hiyo na anajua matatizo ya wananchi wake.
“Nilianza maisha Kinondoni baada ya kumaliza chuo. Nimeishi kwa miaka 14 na niko Kinondoni kwa miaka zaidi ya 30. Kwa nini Kinondoni? Si kwamba fursa zimejitosheleza lakini ninaifahamu na ninayajua matatizo ya Kinondoni kuhusu barabara, afya na elimu.”
Amesema alipomaliza Chuo Kikuu mwaka 2008 aliishi mtaa wa Togo kisha akahamia Hananasif, kufafanua kwamba madai kwamba si mkazi wa Kinondoni hazina ukweli wowote.
Kuhusu suala la kugombea ubunge akiwa na wadhifa Chadema amesema, “Ninachotafuta ni uwakilishi wa wananchi, kwa sasa ni mwakilishi ndani ya chama. Hata CCM kuna wenye vyeo viwili. Tunatafuta mwakilishi madhubuti ndani ya Bunge na katika chama chetu hakuna changamoto ya kofia moja au mbili.”
“Kama ni kofia mbili au moja mbona kuna mawaziri ambao ni wabunge, ili uwe mbunge ni lazima uwe raia wa Tanzania, lakini mbona Rais John Magufuli ni mwenyekiti wa CCM, mbona Rais wa Zanzibar ni makamu mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo hilo la vyeo halitupi shida.”
Amesema yeye kiuhalisia ni mzaliwa wa Kikwajuni Zanzibar huku akigusia kwa kifupi kwamba anaungwa mkono na CUF.
Subscribe to:
Comments (Atom)

