Saturday, 20 January 2018

Steve Nyerere: “Nimekaa Ndani Wiki 3, Nimeona Waliosema Nina Ukimwi”


January 19, 2018 Muigizaji maarufu wa Bongomovie Steve Nyerere amezungumza baada ya kuugua kwa wiki tatu Steve ameeleza kuwa alichokuwa anaumwa kuwa ni miguu na siyo VVU kama ilivyokuwa inasemwa kwenye mitandao japo hashangai watu kumsema.

Steve amesema hakuna mtu wake wa karibu aliyezusha suala la ugonjwa wake bali ni mitandao tu ndo imevujisha, alipoulizwa kama Wema Sepetu alikuwa miongoni mwa watu walioenda kumtembelea alijibu kuwa Utu haulazimishwi na kumuona mgonjwa hakulazimishwi pia.


Jenerali wa Jeshi ampa Rais Kabila siku 45 aachie Urais



Haijapita hata miezi mitatu toka tushuhudie Jeshi likiingilia kati na kumuondoa madarakani Rais aliekaa muda mrefu madarakani, Robert Mugabe wa Zimbabwe….. leo tena tunasikia huko Congo DRC Mwanajeshi mmoja ampa Rais Kabila siku 45 awe ameachia madaraka.

Tunafahamu kwamba Rais Kabila alimaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba kuwa Rais mwezi December 2016 lakini hajaachia madaraka, mengi yamesemwa na Serikali ikiwemo “hatuna pesa za kutosha kufanya Uchaguzi Mkuu”

January 19 2018 Mwandishi wa habari Byobe Malenga alieko Congo DRC ameiambia millardayo.com kwamba Jenerali mmoja wa Jeshi aitwae John Tshibangu ameasi na kutangaza vita na Rais Kabila, amempa siku 45 aachie madaraka.

Asubuhi ya Ijumaa January 19 2018 Wanajeshi walionekana kuizingira kwa wingi IKULU ya Kinshasa huku video iliyorekodiwa na Jenerali Tshibangu ikiendelea kusambaa ambapo ndani yake ameonekana kazingirwa na Wanajeshi wenye silaha.

Kwenye video hiyo Tshibangu amenukuliwa akisema “Nafahamu siri ya Rais Kabila, sasa ni muda wa kuondoa Serikali ya Mabeberu na Udikteta, na ni lazima Rais Kabila aombe msamaha kwa Wakongo kuanzia Makanisani, Shuleni na hata Raia wa kawaida kwa kosa la kushindwa kuiongoza Nchi”

“Mimi kama Mwananchi mwenye msimamo na huruma kwa mateso yenu, niliamua kujitokeza ili kumfukuza Joseph Kabila kwa nguvu za vita na kijeshi, nawahakikishia kwamba tutamuwinda na atakimbia. ” – John Tshibangu.

Tshibangu amelitaja kundi lake la Waasi kwamba linaitwa Forces Nouvel du Congo ikimaanisha NGUVU MPYA KWA AJILI YA CONGO ambapo Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kumekuwa na majaribio ya mapinduzi katika Serekali ya Congo ambapo IKULU ya Taifa imezungukwa na Wanajeshi wengi wanaoonekana kama Wageni, yaani sio Wanajeshi wa congo.

Raisi Kabila amekabiliwa na upinzani mkali kutokana na nia yake ya kutaka kugombea Urais kwa muhula wa tatu baada ya muhula wake wapili kumalizika mwezi December 2016.

John Tshibangu

Source: Millardayo

Friday, 19 January 2018

Ndege yatetemeka angani



Ndege moja ya Malaysia ililazimika kutua katika eneo la Australia ya kati baada ya tatizo la kiufundi kuifanya kuanza kutetemeka ikiwa angani, wamesema abiria.

Ndege hiyo aina ya MH122 ilikuwa inasafiri kuelekea Kuala Lumpur kutoka Sidney siku ya Alhamisi wakati iliporudi katika eneo ambalo haliko mbali na Broome, kaskazini Magharibi mwa Australia.

Ndege hiyo iliokuwa ikiwabeba watu 224 ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Alice Springs Airport.

Abiria wanasema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitetemeka na kutoa sauti kubwa.

Katika taarifa yake, kampuni ya ndege ya Malaysia Airline ilisema kuwa ndege hiyo ilibadilsha safari kutokana na tatizo la kiufundi.

Hatahivyo haikusema ni matataizo gani. Abiria Sanjeev Pandev alisema kuwa ndege hiyo ilionekana kuwa na tatizo hilo saa nne kabla ya safari kuanza.

''Ilikuwa ikitetemeka na kelele zilikuwa kubwa '', aliambia BBC.

''Watu walikuwa wakiomba na wengine walikuwa wakitokwa na machozi'', aliambia BBC.

Alisema kuwa abiria walionyeshwa njia za kubaliana na dharura na wafanyikazi wengi wao wakionekana kuogopa na kushtuka.

Simba kukutana na waliokwamisha mipango




Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC leo alfajiri wameondoka kwa ndege kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera kwaajili ya mchezo wao wa raundi ya 14.

Simba ambayo jana ilishinda mchezo wake wa raundi ya 13 kwa mabao 4-0 dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Uhuru, inakwenda kukutana na Kagera Sugar ambayo ilikwamisha mipango yake ya ubingwa msimu uliopita.

Kagera Sugar ilitibua mipango hiyo April 2 mwaka jana baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa uwanja wa Kaitaba hivyo kuinyima nafasi ya kurejea kileleni ikibaki na alama 55 katika nafasi ya pili na kuwaacha Yanga wakiwa na alama 56 kileleni.

Endapo Simba ingeshinda mchezo huo ingefikisha alama 58 hivyo huenda ingetwaa ubingwa kutokana na bingwa wa msimu uliopita kupatikana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, baada ya timu hizo mbili za Kariakoo kufungana pointi.

Simba ambayo kwasasa inaongoza ligi kwa alama 29 mbele ya Azam FC yenye alama 27, itashuka dimbani Kaitaba siku ya Jumapili.

Wenye mabasi wataka kumwona JPM



WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani, wameomba kukutana na Rais John Magufuli kumweleza matatizo yanayowakabili ikiwamo  vipengele wanavyodai kuwa ni kandamizi katika kanuni mpya za leseni za usafirishaji.

Wamefikia hatua  hiyo baada ya kutofikia mwafaka katika kikao kilichofanyika jana  jijini Dar es Salaam kati yao  na maofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa  Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na Jeshi la  Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akitangaza azimio hilo kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi hayo (Taboa), Enea Mrutu, alisema wataandika barua kuomba kukutana na Rais  Magufuli ili kumweleza matatizo yanayowasibu.

"Tukimaliza kikao hapa na kwa kuwa wote mmekubali na mnataka kukutana na Rais  Magufuli, sekretarieti itakutana tutaandika hiyo barua na tutaipeleka nyumba nyeupe (Ikulu)," alisema Mrutu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taboa , Mohammed Hood, alisema kabla ya kuandikia barua ya kuomba kukutana na Rais, watafanya utaratibu wa kuonana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

"Hatuwezi kufika kwa Rais  moja kwa moja bila  kupitia kwa Waziri, hivyo mimi  nitampigia Waziri ili nimwombe tuonane na baada ya hapo ndipo  tutakwenda  Ikulu," alisema Hood.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alisema hakuna uadui kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi na kwamba suala la faini inayotozwa kuanzia Sh. 250,000 hadi 500,000 haliwezi kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni la  kisheria.

"Jambo hili litafutiwe namna nyingine ya kuzungumza kwa sababu lipo kisheria. Hakuna mmiliki atakayeshitakiwa  au kupelekwa mahakamani kwa kosa la  gari kwenda kasi, dereva ndiye atakayeshitakiwa," alisema Kahatano.

Kahatano aliwataka Taboa kwenda Tume ya Ushindani kulalamika endapo wanaona kanuni au sheria hizo mpya zinawakandamiza.

Kuhusu  kuzuia gari kwa kosa la  dereva, Kahatano alisema sheria ya Sumatra inasema endapo gari litakamatwa, mmiliki wa gari atapewa siku 14 za kulipa faini hiyo na endapo siku hizo zikipita bila kulipa, mmiliki anaweza kufika Polisi au Sumatra na kutaka kesi iende mahakamani.

Alisema hakuna gari lolote litakalozuiwa kwa kosa alilofanya dereva na kwamba makosa ya dereva na mmiliki yametenganishwa.

Wakichangia katika mkutano huo, wajumbe wa Taboa wengi wao  walilamikia kanuni zilizokuwapo katika leseni za usafirishaji kuwa zinawakandamiza, huku wakipendekeza faini za viwango vipitiwe upya pamoja na makosa ya dereva na mmiliki yatenganishwe.

Source: Nipashe

Afya ya Tundu Lissu yazidi kuimarika, sasa Anaweza Kutembea Mwenyewe, Kuoga


Afya ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.

Mbunge huyo aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano kati ya hizo zikimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili.

Vinceti Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema  jana kuwa Lissu ameanza kutembea mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo kwenda kuoga bila msaada wa mtu mwingine.

"Tunamshukuru Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri... tangu ameanza kupatiwa matibabu na mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno," alisema na kueleza zaidi:

"Maendeleo ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa maliwatoni lakini sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia mguu chini.

"Anakula mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo makubwa."

Mghwai alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo ikawa sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa matibabu na bila usumbufu wowote.

Alisema Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda kumjulia hali.

"Kwa sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari wanamfanyia mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona na ndiyo sababu anaendelea kupona haraka," alisema Mghwai.

"Ubelgiji muda wote yuko na madaktari akipatiwa matibabu hasa mazoezi ya viungo... huku ni kazi kazi tu. Na madaktari waliahidi kufanya kazi.

"Kule Nairobi wakati mwingine alikuwa akiwaambia madaktari wamuache pale anaposikia maumivu wakati wa mazoezi lakini sasa hakuna kitu kama hicho na wamemwambia avumilie apone."

Kuhusu risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na madhara kwake kiafya.

"Kule Ubelgiji kazi kubwa ni kumfanyisha mazoezi ili sasa aweze kurejea katika hali yake na ndicho ambacho wanaendelea nacho na kwa kweli tumeanza kuona maendeleo makubwa."

Kuhusu gharama za matibabu, Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100 zinatumika kila mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge halijatoa fedha na familia inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa huku na kule.

Alisema fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na wadau mbalimbali na wamekuwa wakifanya harambee kadhaa za kuchangia.

"Gharama ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali hiyo na kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi ni fedha za matibabu pekee," alisema Mghwai.

Alieleza zaidi kuwa fedha zilizochangwa hazitoshi kumtibu Lissu na kwamba kwa sasa wadau wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali inagharamia matibabu yake.

Alisema familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha matibabu yake.

"Tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa mzima."

Alisema gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya matibabu ya Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na si yeye peke yake kuzungumzia.

Lissu ambaye Januari 6 alizungumza na waandishi wa habari akiwa nje ya Hospitali ya Nairobi, ikiwa ni siku moja kabla ya kusafiri kuelekea nchini Ubelgiji, alieleza kuwa alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na 16 zilimjeruhi maeneo mbalimbali ya miguu, mikononi na kwenye nyonga.

Lissu alisema kutokana na shambulio hilo alifanyiwa operesheni 17 zilizofanikisha kuondoa risasi saba zilizoingia mwilini huku risasi moja ikisalia.

Wataalam wa afya walimshauri kuiacha risasi hiyo iliyopo kwenye nyonga wakisema kuwa inaweza kuleta madhara zaidi kama watajaribu kuitoa.



Mkuu wa kitengo cha ununuzi Muhas asimamishwa kazi




Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu wa kitengo cha ununuzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), baada ya kudai kubaini uwapo wa harufu ya ufisadi katika ununuzi wa taasisi hiyo.

Pamoja na mkuu huyo wa kitengo, Profesa Ndalichako pia aliagiza kuchunguzwa kwa watu wote watakaohusika katika sakata hilo.

Profesa Ndalichako alitoa uamuzi huo juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea chuoni hapo na kubaini matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema kabla ya kwenda chuoni hapo, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia tuhuma za ufisadi hususan kwenye masuala ya ununuzi na matokeo yalionyesha zina ukweli.

Aliongeza kuwa amebaini kuwa linapofika suala la ununuzi kwenye taasisi hiyo hakuna ushindani, badala yake kazi hizo anapewa mtu mmoja kupitia kampuni tatu tofauti. “Nimefanya uchunguzi wangu nimebaini kuna kampuni tatu ambazo zote zinamilikiwa na mtu mmoja ndizo zinazopata zabuni ya ununuzi katika chuo hiki, hakuna mchakato wa kushindanisha kampuni kama zinavyoagiza sheria za ununuzi serikalini,” alisema.

Profesa Ndalichako alibainisha hayo mbele ya menejimenti ya Muhas na kumpa maagizo nwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Mariam Mwaffisi kufanya uchunguzi zaidi akishirikiana na wajumbe wake wa bodi ili kuwanasa wote ambao kwa namna moja au nyingine wamehusika kupindisha utaratibu wa Serikali.

“Ninaagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu huyo wa kitengo lakini si ajabu wapo wengine mapapa, mwenyekiti nitakukabidhi makabrasha yote niliyoyapata kutokana na uchunguzi wangu, fuatilieni hata kama ni makamu mkuu wa chuo, kama amehusika awajibishwe msimuogope mtu,” alisema

Pia, alitumia fursa hiyo kuagiza wakuu wa idara kuwa makini kwenye uagizaji wa vitu kulingana na mahitaji.   

Source: Mwananchi

Ujumbe wa Messi kwa Gaucho



 Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi.

LIONEL Messi wa Barcelona amemtumia ujumbe nyota wa zamani wa timu hiyo, Ronaldinho ambaye amestaafu kucheza soka la kulipwa.


Ronaldinho.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Messi ambaye bao lake la kwanza alifunga akipata basi ya Ronaldinho ameandika ujumbe huu:

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema, nimejifunza mengi kwako. Nitaendelea kukushukuru kwa kufanya mambo kuwa rahisi kwangu nilipojiunga na timu.

“Nilikuwa na bahati kuwa karibu yako, licha ya kuwa staa uwanjani lakini nje ya uwanja ulikuwa mtu mwema na hilo ndilo jambo muhimu, licha ya kuwa umeamua kustaafu, soka halitasahau tabasamu lako, nakutakia kila la kheri, Gaucho.”



Linah afunguka sababu za kunenepa


MKALI kwenye Muziki wa Bongo Fleva, Esterlina Sanga ‘Linah’ amefungukia sababu ya kuwa mnene kupitiliza ‘bonge nyanya’ kiasi cha kusababisha mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii.

 Linah ameweka wazi sababu iliyomfanya kuwa mnene ni kutokana na kutoka kwenye uzazi hali iliyomfanya mwili na nafsi yake kuridhika na kujikuta bonge nyanya.

“Nimetoka kwenye kipindi kifupi mno cha uzazi, hii ndio sababu kubwa iliyonifanya niwe bonge, baada ya kujifungua mtoto nafsi na mwili wangu viliridhika, ndio maana nimekuwa na mwili mkubwa na wenye afya,” alisema Linah.


Waziri Mkuu Majaliwa ajitwisha mgogoro wa Nyamongo


Mapokezi ya mabango yaliyobebwa na wananchi wa eneo la Nyamongo yamesababisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujitwisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 kati ya wakazi hao na Mgodi wa Dhahabu Acacia North Mara.

Serikali imeahidi kutatua mgogoro huo kati ya mgodi na wananchi wanaozunguka eneo hilo, ili kumaliza uhasama na kurejesha amani kati ya makundi hayo mawili yanayohasimiana kwa kipindi kirefu.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Majaliwa alipotembelea eneo la Nyamongo wilayani Tarime katika ziara yake ya siku saba inayoendelea mkoani Mara.

Hiyo ni baada ya kupokewa na mabango aliyosema hayapungui 400 alipofika eneo la Nyamongo, jambo alilosema ni ishara tosha ya kuwapo tatizo linalowachukiza wananchi linalohitaji ufumbuzi wa Serikali na viongozi wa ngazi zote.

Kikao cha kwanza cha kujadili na kutafutia ufumbuzi mgogoro huo kitakachohusisha wajumbe watano wa watakaowakilisha wananchi, uongozi wa mgodi, mbunge wa Tarime vijijini (John Heche) na wataalami wa Wizara ya Madini kitanatarajiwa kufanyika mjini Dodoma Januari 27.

Mambo muhimu yatakayojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni malipo ya fidia kwa mali ya wananchi, maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo, upatikanaji wa mawe (mabaki) ya dhahabu maarufu kama magwangala.

Mengine ni upatikanaji wa maji safi na salama eneo la Nyamongo (vyanzo vya maji vya asili vinadaiwa kuchafuliwa na kemikali), na udhibiti wa matumizi ya nguvu kupita kiasi, ikiwamo kupiga mabomu ya machozi na risasi panapotokea mgogoro au vurugu kati ya wananchi na mwekezaji.

“Nimepokewa na mabango tangu nianze ziara mkoani Mara Januari 15; lakini mabango ya Nyamongo yametisha. Hayapungui 400 na yote yanaonyesha uhusiano mbaya kati yenu (wananchi) na mwekezaji. Nitalibeba hili na kulimaliza,” alisema Majaliwa akiamsha shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.

Licha ya amani na utulivu eneo la Nyamongo, uamuzi huo wa Serikali pia unalenga kuondoa kuviziana kati ya wananchi na vyombo vya dola vinavyotumika kudhibiti na kurejesha amani na utulivu nyakati za uvamizi unaofanywa na makundi ya watu, hasa vijana wanaoingia eneo la mgodi kuchukua mawe au mchanga wa dhahabu.

“Mgogoro huu unakwamisha juhudi za wananchi, Serikali na wawekezaji katika kujiletea maendeleo kupitia rasilimali ya madini yanayopatikana Nyamongo, lazima tuutafutie ufumbuzi wa kudumu kwa faida na masilahi ya pande zote,” alisema Majaliwa.

Alisema yeye binafsi ataongoza mazungumzo ya kutatua mgogoro huo hadi mwafaka utakapopatikana na kuagiza pande zote kuunga mkono juhudi hizo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu huku maslahi na maendeleo ya wananchi yakipewa kipaumbele.

Awali, mbunge wa Tarime vijijini, John Heche alimweleza Majaliwa kuwa uhasama kati ya wananchi na wawekezaji, kukosekana kwa huduma bora za kijamii kulinganisha na ya utajiri wa madini eneo hilo na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola dhidi ya wakazi kwa faida ya mwekezaji bila kujali uhalali wa madai ya wenyeji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabiliwa wakazi wa Nyamongo.



Mambo ambayo Trafiki atakiwi kufanya kwa Dereva



Kama ulikuwa unaudhika kila ukiona askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, angalau sasa unaweza kuwa na ujasiri wa kukabiliana nao kisheria.

Ni kwa kutumia elimu iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambaye jana alitoa ufafanuzi wa jinsi askari hao, maarufu kwa jina la Trafiki, wanavyotakiwa kufanya kazi.

Amezungumzia jinsi trafiki anavyotakiwa kufanya iwapo atasimamisha gari yako, makosa anayotakiwa kuyahoji na hatimaye kukutoza faini kulingana na wakati na hata utendaji wa polisi wanaozunguka na pikipiki, maarufu kwa jina la tigo.

Na faraja zaidi ni kauli yake kwamba si kila kosa linastahili faini na kuwataka trafiki kuwa makini ili kuondoa malalamiko ya uonevu na kuwakandamiza raia.

Mambosasa alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM na baadaye kuzungumza na Mwananchi kufafanua maelezo yake.

Alishangazwa na askari wanaokamata gari mchana kwa kosa la kutowaka taa na kutoza faini.

Alitaja makosa mengine kuwa ni askari kukamata gari bila kujua kosa la msingi na kulazimika kuanza kulikagua kwa lengo la kubaini kosa.

Pia alieleza kwamba askari wanaotumia pikipiki maarufu kama ‘tigo’, hawaruhusiwi kutoza faini baada ya kukamata gari.

Trafiki aeleze sababu

“Akisimamisha gari ni lazima akueleza sababu za kukusimamisha; kwamba anataka kukagua nini katika gari lako,” alisema Kamanda Mambosasa baada ya kuombwa na Mwananchi kufafanua kauli yake jana jioni.

“Nilichokimaanisha ni ile kusimamisha gari na kuanza kutafuta makosa bila kueleza sababu ya kukusimamisha.”

Trafiki wamekuwa na tabia ya kusimamisha gari, kuomba leseni na baadaye kuanza kukagua vitu kama stika ya bima, taa, gurudumu, mtungi wa kemikali za kuzimia moto na viakisi mwanga kwa ajili ya kuashiria gari bovu lililosimama barabarani.

Akipata kosa, askari huandika kuanzia Sh30,000 kwa kosa, jambo ambalo limesababisha madereva wengi kuingiwa na hofu kila wanapoona askari hao barabarani.

“Akisimamisha gari ni lazima aeleze sababu za kulisimamisha,” alisema Kamanda Mambosasa kujibu swali “trafiki atatambuaje kama gari lina bima au vitu vingine vya lazima katika gari.

Trafiki atumie busara

Mambosasa pia alisema trafiki pia anatakiwa kutumia busara kumtoza faini mtu ambaye gari lake lina matatizo ya taa kwa kuwa huenda hatumii gari hilo usiku unapoingia.

“Yapo makosa ambayo askari yeyote wa usalama barabarani anayesimamia sheria anaweza kujitathmini mwenyewe na kuona haina ulazima wa kumtoza mtu faini,” alisema.

“Kwa mfano gari langu nimeamua kutembelea mchana tu, ikifika usiku naliegesha. Kuna sababu gani ya kuwa na taa?

“Kwa hiyo ukinikamata kwa kosa la kutokuwa na taa mchana, nitakushangaa kwa kuwa sijavunja sheria. Wakati mwingine askari anapaswa kufikiria uamuzi wa kumtoza faini mchana kwa sababu ya taa.”

Alisema kama ni usiku ni wazi kuwa mhusika atakuwa amefanya kosa.

“Ili tusiingie kwenye malumbano, tunaomba wananchi watii sheria na pale inapotokea udhaifu wa askari kumbambikia kosa mhusika, (mwananchi) anatakiwa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Aliwataka askari kuacha kutafuta makosa kwa madereva kwa kusimamisha magari na kuanza kuyakagua.

“Unakamata gari halafu unaanza; mara washa taa; mara zima. Tunaendelea kuwaeleza wenzetu kuwa busara inahitajika wakati wa kusimamia sheria,” alisema.

Askari wa pikipiki

Kuhusu polisi kikosi cha pikipiki, Kamanda Mambosasa alisema wana haki ya kukamata gari au chombo chochote barabarani na kukikagua, lakini kuhusu utozaji wa faini jukumu hilo si lao, bali ni la trafiki.

“Anaweza kukukagua lakini linapokuja suala la kutoza faini, hana kitabu. Lazima akupeleke kwa wahusika ambao ni trafiki,” alisema.

Katika maelezo yake Clouds, Mambosasa alisema Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya kulinda raia na mali zao, kusimamia sheria na si kukandamiza wananchi.

“Hawana mamlaka ya kutoza faini kwa mtu aliyevunja sheria za barabarani. Jukumu lao ni kumfikisha mtu huyo kwa askari wa usalama barabarani,” alisema.

Alisema kikosi hicho hakikuanzishwa kwa ajili ya kukamata na kutoza faini, bali kupambana na uhalifu. “Kutokana na foleni za Dar es Salaam, polisi ikaona busara kuwaweka askari hao tayari kwa ajili ya kuwahi kwenye matukio ya uhalifu na sio kukamata magari kama wanavyofanya sasa ingawa wanawajibika kushughulikia uvunjaji sheria unapotokea mbele yao,” alisema.

Aliwataka wananchi kutokubali kutoa fedha bila kupatiwa risiti kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kutoa rushwa.

Alisema jeshi hilo linaendelea kuwaelimisha askari wake kusimamia sheria na si kuwaonea watu.

Kauli yake imepokewa vizuri na wadau wa vyombo vya moto.

“Binafsi naona askari wa usalama barabarani wana haki ya kukagua magari kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao,” alisema mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kauli ya Mambosasa.

“Lakini nasisitiza kuwe na busara. Lengo si kuumizana, bali ni kuhakikisha sheria zinazingatiwa. Nitoe wito kwa wamiliki kuhakikisha magari yao yapo katika hali nzuri na madereva nao wasiingize magari mabovu barabarani.”

Kamanda Mambosasa pia alifafanua kuhusu tamko la kuzuia nguo fupi, akisema hilo ni kosa la kimaadili na si kisheria na hivyo Jeshi la Polisi haliwezi kulishughulikia kwa kuwa hakuna sheria inayozuia mavazi hayo. 

Samia ataka mpango wa kuiboresha Dar


Makamu wa Rais, Samia Suluhu amewataka viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia ngazi za wilaya, halmashauri kuwa na mpango mmoja wa kuboresha mazingira ili kujikinga na maafa yatakayotokana na mvua hasa mafuriko.

Mama Samia amesema hayo leo Ijumaa wakati akifungua mkutano unaokutanisha wadau wa mazingira wa jiji hili ambao una lengo la kuja na mpango kazi wa kuondoa majanga hasa mafuriko.

Mkutano huo ambao umeudhuriwa na viongozi na mawaziri mbalimbali akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na wakuu wa wilaya.

Samia amesema katika maafa yanayotokea katika jiji la Dar es Salaam kumekuwa na mipango tofauti katika wilaya zote jambo ambalo sio sawa kwani lazima kuwe na mkakati wa kunusuru jiji zima.

"Lazima tuwe na mkakati kabambe wa kufanya usafi wa mifereji na hatuwezi kusubiri maafa ndio tuanze kufanya kazi ya uokoaji sio sawa kabisa," amesema Samia.

Katika mkutano huo ambao mwenyekiti wake ni Makamba amesema kikao hicho kitatoka na azimio moja katika kukabiliana na majanga hayo.


Madiwani waliohama Upinzani kugombea tena kupitia CCM Ruangwa


Madiwani wa Kata za Namichiga na Nachingwea Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi Bakari Omari Mpanyangula na Mikdadi Ibadi Mbute, ambao walihama vyama vya Chadema na CUF na kujiunga na Chama cha Mapindizi CCM kwa kukiunga mkono Chama hicho.

Madiwani hao wananafasi kubwa ya kugombea tena nafasi hiyo kupitia CCM kwani umedhihirishwa Leo na Katibu wa CCM mkoa wa Lindi Bw, Loti Olelesele kwenye hafla ya kuwakabidhi kadi za chama hicho iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika kata za Nachinwea na Namichiga.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya Wanachama na wapenzi wa CCM katika kata hizo Olelesele alisema Mpanyangula na Mbute ndio wanachama wanaofaa kugombea nafasi hiyo tena kupitia chama hicho, kwakuwa wameonesha uwezo mkubwa wa Uongozi walipokuwa Madiwani kupitia Vyama walivyohama.

Pia Olelesele alisema licha ya kuonesha uwezo wa uongozi lakini pia wanakubalika na Wananchi hali ambayo ilisababisha wawabwage wagombea wa CCM katika uchaguzi Mkuu uliopita "Tunakubaliana na uamuzi wa Vikao halali vya Chama vya kata za Namichiga na Nachingwea vilivyopendekeza wawe wagombea wetu wakati wa uchaguzi mdogo kwenye kata hizo kwani wananchi wameendelea kuwaamini," alisema Olelesele.

Lakini pia alitumia hafla hiyo kuwahakikishia Wananchi kwamba Chama hicho kimeweza kudhibiti vitendo vya rushwa  hivyo Viongozi wanapatikana kutokana na uwezo wao na kukubalika kwao mbele ya Wananchi


Nae Katibu wa Mkoa wa Lindi wa Jumuia ya Wazazi wa Chama hicho Tatu Hamisi, ameipongeza Serikali kwa kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo ikiwamo sera ya Elimu bila malipo, alitoa wito kwa wazazi kutumia vyema fursa hiyokwa kuwapeleka watoto wao Shule.

Hata hivyo Wanachama 15 kutoka upinzani walihama vyama vyao na kujiunga na CCM na kukaribishwa na makada wa chama hicho, nae Mpanyangula akifuatwa na watu sita wa Familia yake walimuunga mkono, Mpanyangula alisema"pamoja na kuridhishwa na Serikali ya awamu ya tano lakini mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF umesababisha chama hicho kukosa muelekeokuanzia juu mpaka chini hivyo huu ni mwanzo tu wanachama wengi wanajiandaa kuhama," alisema Mpanyangula.

Madiwani hao walitangaza kuvihama vyama vyao vya awali wiki iliyopita kwa madai kwamba wamehamia CCM ili kuungana na Serikali ya awamu ya tano na Mbunge wao Mheshimiwa Kassim Majaliwa katika kuwaletea Wananchi maendeleo.