Sunday, 24 December 2017

VIDEO:Mtoto wa Babu SEYA afunguka kauli ya Magufuli, Lowasa



Mtoto wa Babu Seya aitwaye, Mbangu Nguza amesema kuwa wao kama familia wanamshukuru Rais Dk John Magufuli kutokana na kuwaachia kwa msamaha Baba yake, Nguza Viking 'Babu Seya' na mdogo wake Papii Kocha waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela katika gereza la Ukonga, siku ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu.
Pia amefunguka kuhusiana na kauli ya aliyekuwa mgombea wa Urais wa UKAWA, Edward Lowasa ambaye aliahidi kuwaachia huru endapo angeshinda urais mwaka 2015.
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI....USISAHAU KUSUBSCRIBE


Mwanamke Amfungia mumewe Ndani na Kisha Kumchoma moto - Mtwara



Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail (29) kwa tuhuma za kumuua mume wake baada ya kumfungia ndani na kisha kuichoma nyumba kwa petroli.
Taarifa hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Lucas Mkondya, ambapo amesema kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, baada ya mwanamke huyo kugundua kuwa aliyekuwa mume wake anaishi na mke mwingine, na kuamua kumvizia nyumbani kwake kisha kuichoma moto na kusababisha kifo chake.
"Ni kweli Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja ayefahamika kwa jina la Zuhura Ismail kwa tuhuma za kuichoma nyumba aliyokuwa anaishi mume wake na mwanamke mwingine, kutokana na wivu wa kimapenzi baada ya Zuhura kugundua kuwa mumewe anaishi na mke mwingine, na kuamua kwenda kuchoma nyumba hiyo moto na kuwasababishia majeraha makubwa, ambapo mumewe alipelekwa hospitali lakini kutokana na majereha hayo makubwa alifariki dunia, lakini mwanamke aliyekuwa nae anaendelea vizuri", amesema Kamanda Mkondya.
Aidha Kamanda Mkondya amesema mara baada ya tukio hilo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail alitoroka na kwenda kusikojulikana, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na pindi atakapopatikana watatoa taarifa.

Rose Muhando Awafungukia wanaomsema kuhusu kujiunga CCM



Msanii wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Rose Muhando ameamua kufunguka ya moyoni baada ya kupokea maoni mengi ya watu wakimponda kuhusu maamuzi yake ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Rose Muhando amesema wanaomponda na kumkebehi anawachukulia ni watu wa kawaida kwani hawezi kujifunza kwa watu walioshindwa huku akidai ameshazoea kusemwa.
“Watu wengine hawaelewagi nini wanachoongea, wanaongea ili waonekane nao wanaongea. Mimi ni mtu ambaye ninayejitambua sawa eehhh!! mimi hata sijali, nimeshazoea kutukanwa kwahiyo hata sihangaikagi na maneno yao. Mimi ni funzi kwa walioshindwa na nimeondoka kwa walioshinda, walioshindwa wana maneno mengi kutokana na nilishaimba uoga wako ndio umasikini wako, Mimi siwezi kuishi kwa uoga kwenye nchi yangu kwani ni maamuzi yangu na sijavunja sheria ya nchi na ningeogopa zaidi kama ingekuwa ni dhambi.”amesema Rose Muhando kwenye mahojiano yake na E-Gospel ya Radio E-FM.
Mapema mwezi huu kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma, Rose Muhando alialikwa kutumbuiza kwenye mkutano huo na kabla ya kukaribishwa Jukwaani, Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema Rose na Kundi lake wamekuja na maombi mawili likiwemo la kujiunga CCM na kutumbuiza huku akisema kuwa vyote vimekubaliwa.
Awali Rose Muhando hakuwa kwenye upande wowote wa vyama vya kisiasa na amesema kujiunga CCM au Chama chochote ni maamuzi yake na sio dhambi wala kosa kisheria.

RC Gambo ashiliki Kwenye Ujenzi Wa Hospitali ya Wilaya



Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la Njiro kontena. Shughuli ambayo ilihidhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza na wananchi hao Gambo alisema “Nina furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya watu wetu wa Arusha,kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi na tunatekeleza kwa vitendo.”
Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya mkoa ya Mount Meru kuelemewa.
 Vile vile Gambo anasema kwa sasa mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.
“Jiji la Arusha mapato yake ya ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli?? Gambo alihoji.
Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500 hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.
Naye mkurugenzi wa Jiji la Arusha Athuman Kihamia alimshukuru Mhe Gambo kwa kuweza kulipigania eneo hilo mpaka limeweza kurudi kwenye mikono ya wananchi.
“Kwakweli kama sio jitihada zako eneo hili lilishaondoka mikononi mwetu hivyo kwa niaba ya wananchi wa Arusha ninakushukuru sana, pia nikuahidi tutazingatia ushauri wako wa kulitumia eneo hili vizuri kwa kujenga majengo ya ghorofa kuanzia tano ili kulitumia eneo hili vizuri” alisema Kihamia. Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika June mwaka 2018 ambapo zaidi ya wakazi laki 4 watapata huduma ya afya karibu na

Rais Mnangagwa amteua mkuu wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ya kumng’oa Mugabe



Jenerali wa Jeshi la Wananchi Zimbabwe ambaye aliongoza mapinduzi yaliyopelekea Robert Mugabe kung’olewa madarakani, ameteuliwa kuwa naibu kiongozi wa chama tawala cha ZANU-PF.
Constantino Chiwenga ameteuliwa na Rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambapo hivi karibuni alistaafu kama mkuu wa jeshi, na kuenea kwa tetesi kuwa atapewa wadhifa wa kwenye serikali ya mpya ya Rais Mnangagwa.
Uteuzi huo unaonekana kama hatua ya kuelekea kutajwa kuwa makamu wa Rais baada ya makamu wa Makamu wa sasa wa Zanu PF, Kembo Mohadi ambaye alikuwa waziri usalama chini ya Robert Mugabe kuonekana kuelemewa.

JPM, Mahalia Walivyoitikisa Bandari Dar Mwaka 2017



Kama kuna mashirika au taasisi za Serikali ambazo zilikuwa na wakati mgumu kwa mwaka huu unaomalizika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) huwezi kuiweka kando.
Ugumu wake haukutokana tu na ziara za kushtukiza zilizofanywa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, bali yale ambayo viongozi hao wakuu wa nchi waliyabaini; wizi, upigaji dili na ubadhirifu wa mali za umma.
Waliibua zaidi ya matukio matano kwa nyakati tofauti bandarini hapo jambo lililoashiria kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo nyeti kwa uchumi wa nchi.
Mara zote walizofanya ziara, kama si kubaini udanganyifu wa taarifa za uingizwaji mizigo, basi walikumbana na ukwepaji kodi wa bidhaa na mizigo iliyoingizwa nchini.
Miongoni mwa mambo waliyoyabaini ni kuwapo kwa vichwa 13 vya treni visivyo na mwenyewe, magari 53 aina ya Suzuki ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubebea wagonjwa yaliyohusishwa na Ofisi ya Rais, na malori zaidi ya 50 ya Jeshi la Polisi ambayo yaliingizwa tangu mwaka 2015 bila kuwa na nyaraka zinazoeleweka.
Magari yaingizwa kwa jina la Ikulu
Novemba 26, Rais Magufuli alifanya ziara bandarini hapo kuwaaga mabaharia wa meli ya Peace Arc kutoka China waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa wiki moja, lakini baada ya hafla hiyo fupi, alitembelea eneo la maegesho ya magari hayo yanayodaiwa kuingizwa na Ofisi ya Rais.
Akionekana kama wakili anayewabana mashahidi wa upande mwingine, Rais aliuliza maswali kutoka kwa waziri mmoja hadi mwingine, mtumishi mmoja wa Serikali hadi mwingine akitaka kujua aliyeyaagiza, sababu za taarifa kutotolewa kwa takribani miaka miwili, wahusika kutowafuatilia. Waliowekwa katika hali ngumu ni Dk Philip Mpango, ambaye ni waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Valentino Mlowola (Mkurugenzi Mkuu Takukuru), Simon Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi), George Mnyitafu (Kaimu Kamishna wa Forodha wa TRA) na Deusdedit Kakoko ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Wengi walionekana kupata taarifa za magari hayo wakati wa ziara hiyo, kiasi cha kumfanya Rais aonekane kutoridhishwa na utendaji wao wa kutofuatilia vizuri kazi zao na kufanya magari mengine kukaa bandarini kwa takriban miaka 10 wakati sheria inaruhusu siku 21.
“I’m sorry jamani, haya mengine ni frustration zangu. Nisameheni sana,” alisema Rais Magufuli baada ya kueleza udhaifu wa utendaji wa vigogo hao wa kutochukua hatua.
Rais, ambaye alisema ana taarifa za magari hayo na mtu aliyeyaagiza, alitoa siku saba kwa mawaziri na wakuu hao wa taasisi wawe wamempa taarifa kamili ya suala hilo.
Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli aliwahoji mawaziri na viongozi hao wa taasisi ambao kila mmoja alipewa kipaza sauti ili majibu yake yasikike.
Alianza kwa kumhoji Kakoko kuhusu uhalali wa magari hayo kukaa bandarini kwa muda mrefu na aliyeyaagiza.
Rais Magufuli: Nataka kujua haya magari ni ya nani?
Kakoko: Haya magari yameingia wakati hujaingia madarakani, ila yameingizwa na Ofisi ya Rais. Jina la aliyeyaagiza ni la Kichina au Kihindi hivi, lakini anwani ya mwingizaji ni Ofisi ya Rais ingawa na lenyewe limeandikwa vibaya vibaya na hata maneno yana utofauti. Magari yapo 50.
Rais: Kwa hiyo yameagizwa na ofisi yangu? Kuna mtu yeyote wa ofisi yangu ambaye aliagiza?
Kakoko: Hili jina si la mtu wa ofisini kwako na anuani si ya ofisi yako, bali ni lile jina la mwanzo tu.
Rais: Lakini wanasema yameagizwa na Ofisi ya Rais?
Kakoko: Ndivyo nyaraka zinavyoonyesha.
Rais: Mmeshafanya juhudi gani kama tangu mwaka 2015 Rais ameagiza magari kwa jina la Kichina na hayajachukuliwa na yamekaa hapa kwa jina la Kichina mpaka leo. Ulifanyaje? Ulimjulisha waziri? Na yeye anasema ndiyo amepata taarifa leo.
Kakoko: Utaratibu wetu baada ya siku 21 huwa unahama kwetu. Kimsingi yanakuwa yamehamia TRA.
Rais: Kamishna wa TRA yupo hapa hebu tueleze kuhusu haya magari ya Rais.
Mnyitafu: Rais ni kweli magari haya yaliingia mwaka 2015 Juni na taratibu zetu za kiforodha ilitakiwa tuyatangaze baada ya siku 21 ili yaweze kuuzwa.
Rais: Mliyatangaza?
Mnyitafu: Bado baada ya kushauriana na uongozi…
Rais: Mlishauriana na uongozi gani? Nataka jibu ndiyo maana nimewaita viongozi wote hapa.
Mnyitafu: Uongozi wa mamlaka wa wakati huo, tukashauriana, lakini sikuwepo wakati huo.
Rais: Nani ulimhusisha kwenye uongozi ule taja tu majina.
Mnyitafu: Sikuwepo.
Rais: Ulijuaje kama walishauriana wakati hukuwepo?
Mnyitafu: Nilivyouliza kwa wenzangu ambao…
Rais: Nani jina lake?
Mnyitafu: Maofisa ambao wapo bandarini.
Rais: Ulimuuliza nani, taja jina lake?
Mnyitafu: Meneja wa bandari ambaye yupo sasa hivi. Hata hivyo yeye ni mgeni anasema aliambiwa.
Rais: Nataka uwe muwazi, wewe si msomi bwana? Mimi mpaka kuja hapa nina taarifa nyingi ndiyo maana nataka uwe wazi ili nijue. Si umemuona mwenzako amesema wazi ofisi yangu ndiyo ilihusika mwaka 2015?
Mnyitafu: Sisi tunaangalia mtu wa kwanza aliyeagiza ambapo inasomeka kama imeagizwa na Ofisi ya Rais.
Rais: Ameshakuja mteja yeyote kufuata magari haya hapa?
Mnyitafu: Hajaja mteja yeyote kuchukua magari haya.
Rais: Ina maana hamjafanya upelelezi wowote kutambua kwamba haya magari ni ya nani?
Mnyitafu: Tuliamini kwamba ni ya Ofisi ya Rais.
Rais: Labda niulize swali jingine. Magari ya polisi yalikuja lini na haya pia yalikuja kipindi gani?
Mnyitafu: Yamekuja mwaka 2015 mwezi Juni.
Rais: Ndiyo maana nauliza magari ya polisi yalikuja mwezi wa sita na haya ya mtu ambaye hajulikani yamekuja Juni huyu hajayachukua? Polisi magari yenu yapo mangapi?
IGP Sirro: Yapo 55.
Rais: Sirro, haya magari 50 ambayo ni ambulance yanawahusu ninyi?
IGP Sirro: Hapana kwa kweli hatuyatambui na hatujui chochote kuhusu magari haya.
Rais: Nani mwingine anayefahamu kuhusu haya magari? Waziri pia hujui chochote.
Profesa Mbarawa: Mimi sijui. Nimepata taarifa leo asubuhi.
Rais: Kwa hiyo tangu mwaka 2015 Juni aliyekuwa mkurugenzi wa pale TPA mpaka ameondoka ndugu (Madeni) Kipande hakutoa taarifa na aliyeingia naye hakutoa taarifa na wewe waziri watu wako wa TRA waliokuwepo na walioko mpaka sasa hivi hawajaeleza kuwa kuna magari hamsini na kitu ambayo yamekaa hapo kwa miaka miwili, ambayo hayana mwenyewe, yameandikwa hapa president’s office wala hata mimi sijaulizwa. Mtu wa PCB, hebu njoo hapa wewe unafahamu kuhusu hili kwa sababu wewe ndiyo mtumiaji na mpelelezi mzuri. Unafahamu chochote kuhusu haya magari?
Mlowola: Kwa sasa sijui chochote mheshimiwa Rais. Ndiyo kwanza nimepata taarifa hii.
Rais: Na wewe ndiyo umepata taarifa hii leo kwa hiyo mtu wako wa PCB anayekaa bandarini naye hajui? Sheria za TRA zinasemaje Mheshimiwa Waziri? Gari linaweza likakaa humu hata miaka 30 mnatunza tu?
Waziri Mpango: Hapana mheshimiwa Rais. Sheria zinaweka ukomo wa muda na baada ya hapo inabidi zinadiwe.
Rais: Sasa kwa nini haya hayajanadiwa wala hayajatangazwa mnada kuanzia mwaka 2015?
Waziri Mpango: Kwa kweli kama nilivyosema sijui labda kamishna wa customs (ushuru) anisaidie kwa idhini yako.
Rais: Kamishna wa customs (ushuru) kwa nini hayajanadiwa au ulipewa rushwa kusudi usinadi ili kusudi siku tutakapokuwa tunatoa magari ya Serikali na haya yatoke?
Kamishna wa Forodha: Hapana mheshimiwa kama nilivyosema kwamba haya magari yaliandikwa ofisi ya Rais na siyo ofisi ya Rais tu kwa Serikali.
Rais: Kwa nini hukuandika barua kuuliza ofisi ya Rais, na Rais yupo.
Mnyitafu: Mheshimiwa tumeunda kikosi kazi kwa sababu ya kupitia magari haya pamoja na mengine. Mengi ambayo yapo bandarini ni matatizo kama haya
Rais: Kwa hiyo yako magari mengi yaliyoandikwa Ofisi ya Rais
Mnyitafu: Hapana, magari ambayo yamepitiliza muda wa kukaa bandarini lakini hayajauzwa.
Rais: Magari ya polisi yamebaki mangapi?
Mnyitafu: Ninayoyafahamu yapo 32 yapo 28 na mengine manne.
Rais: Wewe unayafahamu mangapi?
Kakoko: Yapo ya awamu tatu, ambayo hayajachukuliwa, yaliyochukuliwa zamani, lakini hayo ambayo wamesema wanagawiwa ya awamu tatu yapo kadri 53.
Jina la Waziri Mkuu latumika
Novemba 29 ikiwa ni siku tatu baada ya ziara ya Rais, Waziri Mkuu Majaliwa naye alifika bandarini hapo na kubaini uwapo wa matrela 44 yaliyotaka kutolewa bandarini kwa jina lake.
Tukio hilo lilisababisha kutimuliwa kazi kwa maofisa kadhaa akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Lazaro Twange.
Pia, Majaliwa alimuagiza IGP Sirro kumkamata wakala wa kampuni ya Wallmark anayefahamika kwa jina la Samwel na mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Bahman kutoka kampuni ya NAS kwa tuhuma za kutaka kutoa bandarini magari makubwa 44 ‘semi trailers’ kutoka katika kampuni ya Serini ya Uturuki bila kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
Pia, aliitaka TPA kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha kutoka kwa viongozi wa juu serikalini.
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Waziri Majaliwa alisema Bahman wa kampuni ya NAS alitaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa matrela hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kampuni ya Serin ya Uturuki.
“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka, ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana hajafanya hivyo,” alisema.
Alieleza kuwa kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria; na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Alisema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhoofisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini.
Vichwa vya treni vyakosa mwenyewe
Julai 2, Rais Magufuli alishikwa na mshangao baada kukuta vichwa 13 vya treni vikiwa vimeshushwa bandarini lakini havijulikani ni vya nani. Alikumbana na hali hiyo alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
“Kuna vichwa 13 vya treni vilishushwa hapa lakini havina mwenyewe. Inawezekana vipi vichwa vya treni vinafika hapa bandarini, vinashushwa lakini mwenyewe hajulikani! Ni kwa sababu hakuna ‘coordination’, huo ni mchezo mchafu. Vyombo vya dola vianze kuwachunguza hao,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliendelea kuhoji, kwa nini wahusika hawakuuliza ni vya nani tangu awali ila baada ya meli kuondoka ndipo waulize! “Siku nyingine si watakuja kushusha hata na vifaru au makontena ya sumu,?” alihoji.
Kutoka na hilo, Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano iliiagiza TPA na TRA kuandaa taarifa kuhusu vichwa hivyo.
Sakata la makinikia
Machi 23, Rais Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo akifuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini.
Katika ziara hiyo alikuta makontena 20 ya mchanga wenye madini ambayo yalizuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2.
Kutokana na hali hiyo, alimwagiza aliyekuwa IGP, Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga huo unashikiliwa popote ulipo mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
Siku mbili baadaye, TPA ilizuia makontena 262 yenye mchanga huo yaliyokuwa kwenye bandari hiyo. Makontena hayo yalikuwa na lakiri (seal) za TRA. Kuzuiwa kwake ndio ukawa mwanzo wa Rais kuunda tume kuchunguza biashara ya madini ambako matokeo yake yalisababisha vigogo kadhaa kung’olewa katika nyadhifa zao sambamba na kubadilishwa kwa sheria za madini.

Leicester City pungufu yaiduwaza Manchester United



Klabu ya Manchester United jana Jumamosi usiku imeduwazwa kwa kulazimishwa sare ya goli 2-2 na klabu ya Leicester City waliocheza pungufu uwanjani, kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka England.
Manchester United walionekana kuutawala mchezo huo kuanzia kipindi cha kwanza na ingawaje hadi mapumziko timu zote mbili zilikuwa zimeshafungana goli 1-1, magoli kutoka kwa Jamie Vardy na Juan Mata.
Kipindi cha pili United walianza kuuwasha moto na kufanikiwa kupata goli la pili kupitia kwa Mata kunako dakika ya 60 na watu wengi walijua mchezo ulikuwa umeisha baada ya beki wa Leicester City, Daniel Amartey kulimwa kadi nyekundu.
Leicester wakiwa pungufu walipambana mpaka dakika nne za nyongeza walipofanikiwa kusawazisha goli la pili na kuwaduwaza mashabiki wa Man United.
Kwa matokeo hayo Manchester United bado wamepunguzwa pointi katika mbio za kuusaka ubingwa wa EPL dhidi ya vinara wa Ligi hiyo, Manchester City. Tazama msimamo wa ligi hiyo.

Wagonjwa Wa Homa ya Ini Waongezeka Itigi



DAKTARI wa magonjwa ya ndani ya watu wazima,katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari Itigi,DK.Kazaura Joseph amesema kumekuwa na ongezeko la ugonjwa wa homa ya ini katika Hospitali hiyo ambapo kati ya watu 100,watu wanane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo.
Daktari huyo aliyasema hayo wakati akiongea na kituo hiki alipokuwa akielezea madhara ya ugonjwa wa homa ya ini kwa binadamu katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari,Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida.
Aidha mtaalamu huyo aliweka bayana pia kwamba maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa zaidi ya mara kumi ya maambukizi ya VVU na kwamba kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi hayo, shirika la afya duniani lilitenga julai,28 ya kila mwaka kuwa siku ya homa ya ini duniani(World Hepatitis Day). Kwa mujibu wa Dk.Kazaura sababu zinazochangia kuongeza idadi ya watu wenye maambukizi hayo ni pamoja na njia za maambukizi yake ni rahisi sana ikiwemo kujamiiana,elimu ndogo kwa jamii na imani potofu kuhusu ugonjwa huo.
Kuhusu madhara yanayoweza kuwapata wagonjwa wa ugonjwa huo,daktari huyo aliyataja kuwa ni pamoja na ini kunyauka na kushindwa kufanya kazi,kupata saratani ya ini na kuharibika kwa viungo vingine kama figo.Hata hivyo Dk.Kazaura alisisitiza pia kwamba ili kukabiliana na ugonjwa huo alishauri elimu iendelee kutolewa kwa jamii kuhusu homa ya ini,kuendelea kutoa huduma za upimaji wa homa ya ini bure na kutoa chanjo ya homa ya ini kwa watu wote ambao hawajaambukizwa.
Kutokana na ongezeko hilo Daktari huyo wa magonjwa ya ndani ya watu wazima alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wanaopatwa na ugonjwa huo kuwahi kwenda haraka kwenye huduma za afya ili wapate matibabu.Ushauri mwingine ni jamii kuacha imani potofu kuwa ini linasababishwa na imani za kishirikina na kuongeza kuwa homa ya ini ikifikia kwenye hatua za saratani ya ini hakuna tiba lakini kuna matibabu ya kupunguza kasi ya ugonjwa huo.
Kuhusu watu ambao hawajui hali zao kama wameambukizwa au la,Dk.Kazaura aliwataka watu hao kwenda kwenye vituo vya afya ili kupima homa ya ini na kupatiwa matibabu. Homa ya ini iligunduliwa na Dk.Barack Blumberg mnamo mwaka 1963 na kwamba mwaka 1969 Dk.Brack na wenzake waligundua chanzo cha homa ya ini inayosababishwa na Hepatitis B virus.

Yanya Sc Waanza kazi kombe la Azam Sports Federation Leo



MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wanaanza kampemni yao ya kuwania Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kumenyana na Reha FC ya Daraja la Pili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Yanga itamkosa kocha wake, Mzambia George Lwandamina ambaye ataendelea kuwa kwao, Lusaka kwa muda mrefu kufuatia kufiwa na mtoto wake wa tatu jana, Mofya Lwandamina ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumanne.
Ikumbukwe Lwandamina aliondoka Dar es Salaam wiki iliyopita kwenda nyumbani kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya mwanawe wa kike, Nasanta Lwandamina aliyehitimu Stashahada ya Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha NRDC.
Wakati anajiandaa kurejea nyumbani baada ya hafla ya binti yake kuhitimu masomo NRDC, Lwandamina anakutwa na msiba na mwanawe.
Yanga wanaingia kwenye michuano ya ASFC siku mbili tu baada ya, mahasimu wao, Simba SC kuvuliwa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Warriors juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za leo, Burkina ya Morogoro wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Coastal Union ya Tanga watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Shupavu na Real Moja Moja wakati Villa Squad watacheza na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Waziri Mkuu awaonya Madiwani



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kuachana na makundi yanayoigawa Manispaa hiyo kwani yanakwamisha utekelezaji wa miradi.
Waziri mkuu ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Ruvuma wakati akizungmza na watumishi pamoja na Madiwani hao ambapo amewaambia kama watashindwa kuzimaliza tofauti zao yeye atawafukuza.
“Madiwani mnaigawa Halmashauri, pamoja na nguvu mliyonayo ya kuiendesha Halmashauri lakini mnaiendesha vibaya, miradi haijengwi vizuri, mmeingiza maslahi binafsi, wakati mwingine pesa zinatumwa mnaanza kubishana tu, sasa ni mwisho mkiendelea tutawafukuza, amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa ameongeza kuwa serikali inakusanya kodi ili wananchi wapate maendeleo lakini wao wanachelewesha miradi ya maendeleo kwa malengo ya kuikwamisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo hatakubali na atawafukuza.
Aidha amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kazi nzuri anayoifanya na kumtaka kuripoti kwake endapo pesa zitaingia kisha Madiwani kuanza kubishana bila utekelezaji ili awashughulikie hata kama ni Meya wa Manispaa hiyo.

Jinsi Ambavyo Mazoezi Yanaweza Kukuongezea Afya Ya Mwili Na Akili Yako



Si wengi sana ambao wanaona umuhimu wa mazoezi katika suala zima la kuboresha afya zao. Wengi huyaona mazoezi ni kitu cha kawaida na hawayachukulii katika ule uzito wake.
Kutokana na wengi kuupuza mazoezi hapo ndipo hujikuta wapo katika matatizo mengine ya kiafya ambayo kumbe wangeyaepuka kama wangekuwa ni watu wa mazoezi.
Kwa mtu yeyote anayezingatia mazoezi ni rahisi sana kujenga afya ya mwili na akili, katika maisha yake. Inatokea hivyo kwa sababu, pia uimara wa mwili wako unategemea mazoezi.
Hebu tuangalie ni kwa jinsi gani mazoezi yanaweza kuongeza afya ya mwili na akili yako kwa ujumla ?
1. Mazoezi yanakufanya ujiamini.
Kwa mujibu wa tafiti nyingi zinaonyesha kwamba ni kitu cha kawaida sana kwamba mazoezi mara nyingi yanakufanya ujisikie vizuri. Na kwa jinsi unavyojisikia vizuri na kujiamini kunakuwa kunaongezeka ndani mwako.
Waangalie watu wote ambao ni watu wa mazoezi, utawaona ni watu ambao wa kujiamini sana. Ni mara chache sana kukuta mtu ambaye anafanya mazoezi halafu tena akawa ni mtu wa kutojiamini, wengi wanajiamini.
2. Mazoezi yanaifanya akili yako iwe ya ubunifu.
Hili linaweza kunekana ni jambo la kushangaza kidogo kwako, lakini mazoezi yana uwezo huo wa kuifanya akili yako ikawa na ubunifu wa hali ya juu sana kuliko ambavyo unaweza ukadhani.
Katika moja za tafiti zilizofanyika, zinaonyesha kwa kadri mtu anavyofanya mazoezi, anazalisha seli nyingi sana kwenye ubongo wake, matokeo yake seli hizo huongeza ubunifu. Hutaki kuamini katika hili, anza kufanya mazoezi leo uone.
3. Mazoezi yanaipa akili yako uwezo wa kukabiliana na changamoto.
Mbali na mazoezi kuifanya akili yako ikawa na ubunifu lakini pia, ni ukweli ulio wazi mazoezi yanauwezo wa kuifanya akili yako ikawa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto.
Akili yako inakuwa imekaa katika mkao wa kupambana na kila aina ya changamo inayojitokeza. Uwezo huu wa akili kuweza kupambana na changamoto hauji hivi hivi tu bali ni kwa kufanya mazoezi.
4. Mazoezi yanakupunguzia msongo wa mawazo.
Kila mtu kwa namna fulani anakuwa ana msongo wa mawazo hata kwa kidogo. Kuna ambao msongo wao wa mawazo unatokana na maisha magumu na kuna wengine unatokana na mapenzi.
Haijalishi msongo wako wa mawazo chanzo chake ni nini, lakini dawa kubwa ya kutoka kwenye msongo wa mawazo ni kufanya mazoezi. Wengi wanaofanya mazoezi kwa sehemu hupunguza sana msongo wa mawazo.
5. Mazoezi yanakupa nguvu.
Bila shaka umeshawahi kuliona hili sana na kutambua kwamba kwa wote wanaofanya mazoezi miili yao huonekana ina nguvu sana yaani ikiwa imekakamaa na huku ikiwa shupavu.
Kinachotokea kwenye mwili unapofanya mazoezi hupelekea kukujengea misuli mingi sana ndani yako. Kwa hali hiyo ni lazima mwili wako unaonekana wenye nguvu na afya ya kutosha.
6. Mazoezi yanakufanya ulale usingizi mzuri.
Kwa wale wote wanaofanya mazoezi sana, tatizo la kukosa usingizi huwa si kubwa sana kwao. Hiyo yote ni kwa sababu mara nyingi wanakuwa wamechoka na miili huhitaji kumpumzika.
Ni mara chache sana kukutana na mtu ayefanya mazoezi ya kutosha halafu akawa na tatizo la kukosa usingizi. Hicho ni kitu kigumu sana, ndio maana tunasema mazoezi ni muhimu kwa afya na akili yako pia.

Magonjwa ya Kuku



1. Ugonjwa wa Mdondo:
Ugonjwa huu huathiri kuku katika umri wowote na unapoingia kwenye kundi huweza kuua idadi kubwa ya kuku hao hadi kufikia asilimia tisini. Ndege wakubwa hustahimili kidogo kuliko wale wadogo kwasababu ya usugu mwilini (body immunity) uliojengeka kwa muda mrefu zaidi.
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha kirusi kiitwacho Paramyxo viridae na huenezwa kwa njia ya hewa na kugusana.
Dalili zake:
Kukohoa na kuhema kwa shida
Ute hutoka mdomoni na puani
Kuku walioathirika hupata kizunguzungu.
Kuharisha uharo wa kijani na njano
Kuzubaa, kusinzia na mabawa kushuka
Baada ya siku 2 kuku hupindisha shingo
Kuvimba macho
Kuzunguka
Kuku hutaga mayai hafifu.
90% ya kuku huweza kufa
Tiba:
Ugonjwa huu hauna dawa.
Kinga:
Kuchanja; Chanja kuku wako kila baada ya miezi mitatu /na mara nne kwa mwaka.
Kuna chanjo aina mbili za ugonjwa huu, nazo ni;
1. Lasota :
Chanjo hii hutolewa katika dawa yenye umbile la kidonge kimoja kimoja ambacho kina dozi ya kuku 1000 na huwekwa kwenye maji ili kuku wanywe hiyo dawa.
Inashauriwa kuku wanaopewa dawa hii wanyimwe maji ya kunywa siku moja kabla yake
Ni vizuri kuwapa mchanganyiko maalum wa dawa wenye mchanganyiko wa vitamin na dawa ya kuwaongezea kuku nguvu. Dawa hii itolewe saa moja au zaidi baada ya kuwapa chanjo ya mdondo.
Thermostable I2 NCD vaccine :
Huwekwa katika chupa kimoja (vial) chenye dozi 400 za kuku
Chanjo hii inavumilia joto ikikaa bils nje ya jokofu kwa muda mrefu zaidi.
Imetengenezwa katika mazingira ya nchi za joto.
Na inaweza kukaa kwa siku 14-15 ikiwa itatunzwa ipasavyo hata baada ya kutumia mara ya kwanza..
2. Kuharisha Damu (Coccidiosis):
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea cha protozoa cha jamii ya Eimeria (Eimeria tenela, Eimeria maxima, na Eimeria acervulina)
Kwa kawaida wadudu hawa hupenda kuishi kwenye mazingira machafu, kama vinyesi, vyakula vilivyooza na umaji maji.(moist environments).
Dalili zake:
Kinyesi chake huchanganyika na damu
1. Wakati mwingine kuku hunya damu.
2. Kuku hudhoofika sana.
3. Kuku huteremsha mabawa yake.
4. Hatimaye vifo hutokea.
Tiba;
Ugonjwa huu hutibika kwa kutumia dawa za
(i) Kundi la suphur
Mfano: sulphonamides (ESB3) kwa siku 3-4
(ii) Amprolium
Dawa za ugonjwa huu hupatikana madukani hivyo ukipatwa na tatizo hilo fika kwenye maduka ya dawa aua muone mganga wa mifugo.
Kinga:
Zingatia usafi mara kwa mara
Kwakuwa ugonjwa huu huambatana na majimaji na uchafu wenye vimelea vya ugonjwa huu , ni vizuri kuhakikisha banda la kuku linakuwa safi na kavu wakati wote.
Tenga kuku wagonjwa kutoka kwa walio wazima.
Tumia dawa ya kinga ili kuepusha uwezekano wa kuku kuambukizwa ugonjwa huu
Dawa inayopendekezwa ni zile zinzoitwa (coccidiostat.
Tenga kuku wadogo (vifaranga) kutoka kwenye kundi la wakubwa.
3. Homa ya Matumbo(fowl typhoid):
Husababishwa na vimelea vya wadudu wa bakteria wa jamii ya Salmonella.
Kimelea hicho cha bacteria huitwa Salmonella gallinarum.
Dalili zake:
Uharo mweupe au wa kijani
Vifo hufikia kiasi cha 50%
Rangi ya minofu hugeuka kuwa ya njano
Viungo vya ndani kama maini , figo , bandama huvimba
Maini hung’aa kwenye mwanga mkali.
Tiba :
Tumia dawa za antibiotiki kama vile furazolidone ili kutibu ugonjwa huu.
KINGA: Chanja kuku wako mara kwa mara .
Fanya usafi wa banda na vyombo vya kulishia na kunyweshea maji ipasavyo.
4. Ugonjwa wa Mafua ya Ndege:
Ugonjwa wa mafua ya ndege ni ugonjwa hatari sana kwa kuku na jamii nyingine za ndege.
Pia ugonjwa huweza kuambukizwa na kusababisha vifo kwa binadamu.
Ugonjwa huu husababishwa na kirusi kiitwacho Orthomyxo virus.
Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya kugusana baina ya ndege na ndege na baina ya ndege na binadamu.
Dalili zake:
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana katika kipindi cha siku 3-7 baada ya kuku kuambukizwa.
Dalili hutofautiana kutokana na umri wa ndege.
Baadhi ya dalili zake nihizi zifuatazo
Kuku /ndege hupumua kwa shida (dyspnoea).
Kuzubaa.
Kutokwa na machozi.
Kukohoa na kupiga chafya.
Kuharisha kinyesi chenye majimaji.
Sehemu za kichwa zisizo na manyoya huvimba.uvimbe wenye majimaji huonekana kichwani na shingoni.
Sehemu ya juu kichwani hubadilika na kuwa na rangi ya bluu iliyopauka.
Kuku hutaga mayai yenye maganda laini.
Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba .
Kinga na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu:
Toa taarifa kwa mganga (daktari wa mifugo aliye karibu ukiona dalili za ugonjwa huu.
Tenga mabanda ya kuku wagonjwa na walio wazima.
Fungia kuku wako wasitembee holela.
Acha kununua kuku kutoka eneo linalohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
Acha kusafirisha mifugo /ndege bila idhini ya daktari.
Zuia wageni kutembelea mabanda yako ya kuku.
Acha kuhamisha mbolea ya kuku kwenda shambani kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
Safisha mabanda na kuweka dawa chini ya usimamizi wa mtaalamu wa mifugo na kulipumzisha kwa siku 21kabla ya kuanza kufuga tena.
Choma moto mkali au fukia chini mbolea kutoka kwenye banda la kuku wanaoumwa ugonjwa huu.
Pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe.
5. Gumboro (infectious Bursal Disease):
Ugonjwa huu husababishwa na kirusi
Dalili zake:
Hushambulia vifaranga
Uharo mweupe
Kuchafuka (dirting of anal area)
Kuvimba
Kiwango kikubwa cha vifo
Damu hutapakaa eneo la kutolea kinyesi
Kinga:
1. Usafi
2. lishe bora
3. chanja vifaranga wakiwa na umri wa wiki tatu kwa kutumia chanjo hai (live vaccine)
6. Kifua Kikuu cha Ndege(Avian Tuberculosis-TB):
Husababishwa na kimelea aitwaye Mycobacterium avium.
DALILI ZAKE:
Kukonda na Kupungua uzito
Vidonda kwenye kishungi
Kupungua uzito/kukonda
Kuhara
Kinga:
Usafi:
Fanya usafi na vyombo , banda na mazingira .
7. Magonjwa yatokanayo na Lishe (Nutritional and Metabolic Disorders):
Dalili za magonjwa haya hutegemea aina ya virutubisho vinavyokosekana mwilini
Kwa mfano:
Kupinda miguu (rickets) husababishwa na upungufu wa Vit.D, madini ya calcium na fosforasi.
Vidonda vyenye vyenye damu husababishwa na vit.K
Kichaa cha kuku na kusinyaa kwa misuli husababishwa na upungufu wa Vit.E
Magamba ya Mayai (egg shell)kuwa laini ama umbo kuwa bovu husababishwa na upungufu wa madini ya calcium na fosforasi.
Kudonoana kusababishwa kwa njia moja au nyingine na upungufu wa chakula na madini ya fosforasi na calcium
Kuvimba macho, upungufu wa damu huletwa na upungufu wa vit.A.
Kinga:
Kuwapa kuku mlo kamili
Kuelewa kwa kina aina za chakula kwa kila rika na aina ya kuku ; vifaranga , kuku wa mayai na wa nyama. (Poultry age and classes i.e chicks, layers and broilers)
Kufanya uchunguzi wa virutubisho vilivyomo katika aina ya chakula unachotumia.
8. Minyoo (Helminthiasis):
Minyoo iko ya aina tatu kama vile minyoo kamba, minyoo bapa na minyoo ya mviringo
Dalili zake:
Kudumaa
Kuwa manyoya hafifu
Kupungua uzito
Kukonda
Minyoo huonekana kwenye kinyesi
KINGA / KUZUIA:
USAFI:
Fanya usafi wa vyombo, banda na mazingira.
Tenga vifaranga kutoka kwa wale wakubwa.
Badilisha matandazo kuondoa mazalia ya minyoo.
Badilisha matandazo kila baada ya miezi mitatu.
TIBA:
Tumia dawa zinazopendekezwa na wataalamu hasa zile zinazoua minyoo ya aina zote (mfano: piperazine citrate).
Hakikisha kila baada ya miezi mitatu unawapa kuku wako dawa za minyoo.
9. Kupe, Utitiri, Chawa na Viroboto
kupe laini waitwao Argus persicus, chawa na viroboto wanaong’ata .
Dalili zake:
Kujikung’uta.
Kupiga kelele.
Kiasi cha damu hupungua mwilini.
Utando wa ngozi ndani ya kope za macho hupauka.
Utando wa ngozi ya juu mwilini huwa mnene.
Magamba ya unga-unga hudondoka.
Kuzuia:
Tupa au choma masalia ya mayai yasiyoanguliwa na magamba ya mayai yaliyoanguliwa vifaranga.
Safisha banda mara kwa mara na kunyunyizia dawa; kuna dawa zinazopendekezwa na wataalamu za kunyunyizia kwenye banda la kuku.

Jinsi ya kudumisha Afya Bora na kuishi maisha marefu



Katika hali ya kawaida, hakuna mtu ambaye ana uhakika mkubwa wa maisha yake kwamba ni lazima afike kesho. Muda na dakika yoyote ile unaweza kuachana na mwili wako na ukafa. Swala la kufika kesho au kutofika huwa mara nyingi linabaki mikononi mwa Mungu mwenyewe.
Pamoja na kwamba binadamu huyo hana uwezo wa kujua kesho yupo au hayupo, lakini upo uwezo wa kutambua kama binadamu huyo ataishi maisha marefu au mafupi. Inawezekana unaanza kujiuliza maswali hilo linawezekana vipi? Tulia usiwe na wasiwasi nitakwambia.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya wanadai kwamba, ikiwa binadamu ataishi maisha yake ya kawaida bila kupata changamoto nyingine za nje yake kama kugongwa na gari au namna yoyote ile ya kukatisha uhai wake upo uwezo wa kujua maisha yake yataishia wapi.
Wataalamu hao wanatuonyesha viashiria ambavyo vinaonyesha kama ukiishi hivyo ni lazima uishi maisha marefu. Mambo hayo au viashiria hivyo walivyotoa, ni matokeo ya utafiti yaliyofanywa hasa kwa watu walioishi miaka 100 na kuendelea.
Kwa mfano utafiti huo ulionyesha, watu wanaokula vyakula vyenye mafuta kidogo, watu hawa wao waliishi maisha ya muda mrefu. Mara nyingi ni kweli unapokula vyakula vya mafuta kidogo hiyo inakusaidia sana katika swala zima la mwili wako kutopata magonjwa hovyo.
Pia utafiti huo uliendelea na kuonyesha kwamba, watu wanaokula vyakula vyenye wingi wa protini pia afya zao ziliimarika zaidi na kupelekea kuwa na maisha marefu. Vyakula hivyo ni kama samaki, dagaa, maharage, nyama ana vinginevyo.
Hata hivyo pia watu wanaofanya mazoezi kila siku nao pia walionyeshwa kwamba wanauwezo wa kuishi maisha ya muda mrefu kutokana na mazoezi huweza kuimarisha afya na kupunguza baadhi ya magonjwa na hali za kunenepeana hovyo.
Hivyo utaona, vyakula visivyo na mafuta sana, vyakula vyenye protini na kufanya mazoezi ni mambo ambayo yametajwa na wataalamu yanaweza kuboresha afya yako na kupelekea kuwa na uwezekano mkubwa sana wa kuishi maisha marefu.
Kumbuka siku zote, afya ni kitu cha muhimu sana katika maisha yako na safari yako ya mafanikio kwa ujumla. Kama ukiwa huna afya njema hakuna utakachokifanikisha kwenye hii dunia. Ni muhimu sana kutunza afya yako kwa ajili ya mafanikio yako.