Sunday, 24 December 2017

Jinsi ya kudumisha Afya Bora na kuishi maisha marefu



Katika hali ya kawaida, hakuna mtu ambaye ana uhakika mkubwa wa maisha yake kwamba ni lazima afike kesho. Muda na dakika yoyote ile unaweza kuachana na mwili wako na ukafa. Swala la kufika kesho au kutofika huwa mara nyingi linabaki mikononi mwa Mungu mwenyewe.
Pamoja na kwamba binadamu huyo hana uwezo wa kujua kesho yupo au hayupo, lakini upo uwezo wa kutambua kama binadamu huyo ataishi maisha marefu au mafupi. Inawezekana unaanza kujiuliza maswali hilo linawezekana vipi? Tulia usiwe na wasiwasi nitakwambia.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya wanadai kwamba, ikiwa binadamu ataishi maisha yake ya kawaida bila kupata changamoto nyingine za nje yake kama kugongwa na gari au namna yoyote ile ya kukatisha uhai wake upo uwezo wa kujua maisha yake yataishia wapi.
Wataalamu hao wanatuonyesha viashiria ambavyo vinaonyesha kama ukiishi hivyo ni lazima uishi maisha marefu. Mambo hayo au viashiria hivyo walivyotoa, ni matokeo ya utafiti yaliyofanywa hasa kwa watu walioishi miaka 100 na kuendelea.
Kwa mfano utafiti huo ulionyesha, watu wanaokula vyakula vyenye mafuta kidogo, watu hawa wao waliishi maisha ya muda mrefu. Mara nyingi ni kweli unapokula vyakula vya mafuta kidogo hiyo inakusaidia sana katika swala zima la mwili wako kutopata magonjwa hovyo.
Pia utafiti huo uliendelea na kuonyesha kwamba, watu wanaokula vyakula vyenye wingi wa protini pia afya zao ziliimarika zaidi na kupelekea kuwa na maisha marefu. Vyakula hivyo ni kama samaki, dagaa, maharage, nyama ana vinginevyo.
Hata hivyo pia watu wanaofanya mazoezi kila siku nao pia walionyeshwa kwamba wanauwezo wa kuishi maisha ya muda mrefu kutokana na mazoezi huweza kuimarisha afya na kupunguza baadhi ya magonjwa na hali za kunenepeana hovyo.
Hivyo utaona, vyakula visivyo na mafuta sana, vyakula vyenye protini na kufanya mazoezi ni mambo ambayo yametajwa na wataalamu yanaweza kuboresha afya yako na kupelekea kuwa na uwezekano mkubwa sana wa kuishi maisha marefu.
Kumbuka siku zote, afya ni kitu cha muhimu sana katika maisha yako na safari yako ya mafanikio kwa ujumla. Kama ukiwa huna afya njema hakuna utakachokifanikisha kwenye hii dunia. Ni muhimu sana kutunza afya yako kwa ajili ya mafanikio yako.

Saturday, 23 December 2017

Viongozi Wa Dini, Wanaharakati wakemea Vitendo vya Ubakaji



Dar es Salaam. Kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na kunajisi mwaka 2017, yamewaibua viongozi wa dini na wanaharakati, wakisema jamii inachangia kwa sehemu kubwa huku wakitaka sheria na adhabu kali zitolewe kwa wahusika watakaobainika kutenda makosa hayo.
Taarifa ya usalama wa nchi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Desemba 20 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz inaonyesha kuwa matukio hayo yameongezeka kutoka 6,985 mwaka jana hadi 7,460 mwaka huu.
Alisema makosa dhidi ya binadamu, yanayojumuisha mauaji, kubaka, kulawati, wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi pamoja na usafirishaji wa binadamu, yameongezeka kutoka 11,513 mwaka jana hadi 11,620 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la makosa 107.
Hata hivyo, DCI Boaz alibainisha kuwa makosa makubwa ya jinai yamepungua kutoka 68,204 mwaka jana hadi 61,794 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka huu.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu takwimu za matukio, Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki Bukoba mkoani Kagera, Methodius Kilaini alisema inasikitisha kuona bado kuna watu wanaendelea na vitendo vya ubakaji na kunajisi licha ya kuwepo adhabu kali.
“Sisi viongozi wa dini, kisiasa na jamii tunapaswa kukemea vitendo hivi ambavyo mara nyingi vinafanywa na watu wa karibu. Lakini kunaporipotiwa watu kutenda makosa haya adhabu kali zichukuliwe kwa haraka ili iwe funzo,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza, “Mtoto ni malaika, unapoona mtu kamnajisi halafu unamfumbia macho kisa ni ndugu yako na mnakaa ndani ili kumaliza suala hili pembeni ni hatari, mtu anapomnajisi mtoto huyo ni shetani, hivyo jamii tukemee matendo haya kwa nguvu zote.”
Askofu Kilaini aliungwa mkono na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum akisema, “Ni jambo la kusikitisha. Elimu kwa jamii juu ya madhara haya ni ndogo, adhabu ni ndogo ila kubwa ni mmomonyoko wa maadili.”
“Mavazi ya baadhi ya watoto wa kike nayo yanachangia, uhuru wa watoto kuachwa wanacheza na wavulana hadi kufikia kumbaka, hivyo sheria iwe kali kwa atakayebainika lakini somo la maadili liongezwe nguvu kwani hadi mtu anafanya hayo anakuwa hana hofu ya Mungu.”
Katika taarifa yake, DCI Boaz anasema makosa dhidi ya maadili ya jamii nayo yalipungua kutoka 20,000 mwaka jana hadi kufikia 18,971 mwaka huu ikiwa ni sawa na pungufu ya makosa 1,029.
Akichambua taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Eda Sanga alisema ongezeko hilo limechangiwa na elimu inayotolewa ambayo imesaidia waathirika kutoa taarifa huku akiomba ushirikiano wa pamoja kumaliza tatizo hilo.
“Zamani watu walikuwa hawatoi taarifa, wakikutwa na tatizo wanakaa kimya lakini unapomuelimisha mtu anaelewa na anatoa taarifa lakini pia ukiielimisha jamii kuhusu madhara haya, inasaidia kupunguza tatizo,” alisema Sanga.
Sanga alisema kama kasi hiyo ya matukio ikiendelea hivyo mwaka 2018, siku za usoni kutakuwa na Taifa lisilokuwa na maadili hivyo viongozi wa dini, Serikali na jamii wanapaswa kukemea hili kwa nguvu zote na vitendo vyao vionekane kupinga hili.
Katibu mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT), Leonard Mtaita alisema “Na mimi nimesikia lakini nanichoweza kusema ni siku za mwisho zimekaribia. Watu watatenda maovu na tutayaona mengi, kikubwa wamrudie Mungu na kuacha maovu.”

Viongozi 19 Wanusurika kwenda Rumande



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya Shinyanga (Shirecu) na Mwanza (NCU) kwenda rumande badala yake amewapa siku 23 wampe maelezo yatakayomridhisha kuhusu mahali zilipo mali za vyama hivyo viwili.
Majaliwa alifikia uamuzi huo jana wakati akifunga kikao cha wadau wa pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga.
Viongozi hao wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya ushirika.
“Nataka kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake jana.
Alisema, “Hawa nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisema.
Kuhusu tuhuma za viongozi wa NCU, Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na 2017, kiliuza mali kinyemela katika mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi.
Aliwataja viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo kuwa ni Murtazar Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU; Samson Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills); Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo); Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la Kauma); Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la Kauma); Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills); Peter Ng’hingi (aliyekuwa mjumbe wa bodi); Daniel Lugwisha (aliyekuwa mhasibu mkuu - NCU); George Makungwi (aliyekuwa ofisa miliki - NCU) na Sospeter Ndoli (aliyekuwa ofisa utumishi -NCU).
Kuhusu mali za Nyanza zinazoshikiliwa na Benki ya CRDB, Waziri Mkuu alisema benki hiyo inaidai NCU mikopo yenye thamani ya Sh2.123 bilioni na kwamba inashikilia mali 16 zenye thamani ya Sh18.132 bilioni.
Alitaka vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki.
Kwa upande wa viongozi wa Shirecu, alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi ya Sh11 bilioni ambazo wanadaiwa na Benki ya TIB yakiwamo madeni ya mishahara ya watumishi ambayo yanafikia Sh1.2 bilioni.
“Shirecu kwa sasa haina mali zozote kwa sababu zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,” alisema.
Aliwataja viongozi wa Shirecu ambao wanatakiwa kutoa maelezo kuwa ni Joseph Mihangwa (meneja mkuu); Sillu Mbogo (kaimu mhasibu mkuu); Maduhu Nkamakazi (kaimu mkaguzi wa ndani); James Kusekwa (kaimu meneja uendeshaji).
Wengine ni wajumbe wa bodi ya Shirecu Robert Mayongela (mwenyekiti); Mary Mabuga (makamu mwenyekiti); Sigu Maganda (mjumbe); Clement Bujiku (mjumbe) na Charles Lujiga.

Achomwa Moto paka Kufa baada ya kukataa kuchumbiwa



Picha ya mtu aliyevalishwa pete ya uchumba
Maafisa wa polisi katika mji wa kusini mwa India wa Hyderabad wanasema kuwa wamemkamata mwanamume mmoja baada ya mwanamke mmoja kuchomwa hadi kufa wakati wa mgogoro.
Sandhya Rani, mwenye umri wa miaka 25 alikuwa anaelekea nyumbani wakati aliposhambuliwa siku ya Alhamisi , polisi iliambia BBC.
Watu walikimbia kumsaidia bi Rani lakini alifariki akielekea hospitalini.
Mshukiwa huyo , Karthika Vanga , 28, ni mfanyikazi mwenzake wa zamani.
Alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja na bi Rani hadi miezi michache iliopita, polisi liliambia ripota wa BBC Deepthi Bathini.
Wakati alipomkaribia siku ya Alhamisi wawili hao walionekana wakijibizana kabla ya mwanamume huyo kuchukua mafiua ya taa, na kumwagia mwilini na kumchoma moto , polisi walidai.
Walisema kuwa kulikuwa na madai kwamba bwana Vanga amekuwa akitaka kumchumbia bi Rani kwa kipindi cha miaka miwili.
Alikuwa amekataa mara kadhaa kuchumbiwa na bwana huyo ijapokuwa polisi wanasema haijulikani iwapo kulikuwa na malalamishi dhidi ya mtu huyo.
Mashambulizi dhidi ya wanawake nchini India yameongezeka tangu ubakaji wa gengi la mwaka 2012 na mauaji ya mwanafunzi katika basi moja mjini Delhi, na yamesababisha kuwekwa kwa sheria kali zinazolenga kukabiliana na mashambulio kama hayo.

Mwalimu atiwa Mbaroni Kwa kubaka wanafunzi wake



Mwalimu mbaroni akidaiwa kubaka wanafunzi wake tisa
MWALIMU wa Shule ya Msingi Itiryo, Samweli Bisendo (29), amekamatwa na jeshi la polisi akituhumiwa kubaka wanafunzi tisa wa shule yake iliyopo wilayani Tarime.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe, alisema kuwa mwalimu huyo anadaiwa kutenda unyama huo kwa nyakati tofauti hadi alipobainika.
"Jeshi la polisi limefanikiwa kumkamata mwalimu wa shule ya msingi Itiryo, Samweli Mariba Bisendo (29) kwa tuhuma ya kubaka watoto wapatao tisa ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Itiryo,” alisema Kamanda Mwaibambe na kuongeza kuwa matukio hayo yalifanyika kati ya Novemba 30 na Desemba 6,mwaka huu.
“Alikamatwa wakati akiwa anajiandaa kutorokea nchi jirani ya Kenya," alisema Mwaibambe.
Aidha, Mwaibambe alipongeza ushirikiano kutoka kwa wananchi ambao ndiyo waliowezesha jitihada za polisi kuzaa matunda katika kumkamata mwalimu huyo.
"Pia mwalimu huyo, bila aibu, aliwafanyia matukio ya unyanyasaji wa kijinsia wanafunzi wengine watatu wa shule ya msingi Itiryo," alisema Mwaibambe.
Kamanda huyo alitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapobaini kuwapo kwa uvunjaji wa hseria za nchi ili watuhumiwa wakamatwe na sheria kutwaa mkondo wake.

Watu 22 wahofiwa kufa maji na 115 kuokolewa Ziwa Tanganyika



Watu 22 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tanganyika katika ajali ya boti iliyotokea iliotokea leo alfajiri.
Imeelezwa miili ya watu wanne imeopolewa na imetambuliwa na ndugu zao huku watu wengine 115 wameokolewa wakiwa hai baada ya boti kugonga mtumbwi.
Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Kigoma, Amaniel Sekulu amesema ajali hiyo imetokea katika kitongoji cha Lubengela kijijini Msihezi, Kata ya Sunuka wilayani Uvinza.
Amesema mtumbwi uitwao Mv Pasaka uligongwa ubavuni na boti ya Atakalo Mola na kupasuka, hivyo kuzama ziwani.
Sekulu amesema mtumbwi ulikuwa umebeba abiria 137 waliokuwa wanakwenda kwenye mkutano wa injili katika Kijiji cha Sunuka.
Amesema boti ilikuwa ikitokea Kigoma kwenda Kalya ikiwa imebeba abiria 65.
Sekulu amesema boti na mitumbwi inayobeba abiria hairuhusu kufanya safari usiku.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Sweetbert Njewike akizungumzia ajali hiyo amesema wanaendelea kuwatafuta watu ambao hawajaonekana waliokuwa wakisafiri na vyombo hivyo.
Amesema shughuli za uokoaji zinafanywa kwa pamoja na vikosi vya Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kulikuwa na dosari zilizosababisha ajali hiyo.
Amezitaja dosari hizo kuwa ni ukosefu wa vifaa vya uokoaji, vifaa vya kuzima moto na boti kufanya safari usiku.
Diwani wa Sunuka, Athumani Chuma amesema ajali hiyo imeacha simanzi kutokana na mazingira iliyotokea.
Amesema licha ya ajali kutokea saa tisa usiku, wanakijiji wameonyesha mshikamano katika kuokoa watu wakiwa hai na hatimaye kuopoa maiti nne.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msihezi, George Gasper amesema ajali ilitokea umbali wa mita takriban 150 kutoka ufukweni, ikiwa ni muda mfupi baada ya boti la Atakalo Mola kushusha na kupakia abiria katika Kitongoji cha Lubengela.
Desemba 20, watu saba walikufa papohapo na wengine 12 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Saratoga kugongana uso kwa uso na gari ndogo la abiria.
Ajali hiyo imetokea saa 4:30 asubuhi katika Kijiji cha Kabeba katani Mwakizega wilayani Uvinza.

Hamisa Mobetto Na Zari Warushiana Vijembe



Usiku wa kuamkia leo kwenye jiji la Kampala Uganda kulifanyika Party mbili ambapo moja Hamisa Mobetto alihudhuria inaitwa Gal Power na nyingine ni ya Zari All White Party.
Sasa baada ya kumalizika kwa party hizo maneno ya Mashabiki yakaanza wengine wakiponda ya Zari na wengine wakiponda ya Hamisa kwamba ilikua na watu wachache.
Wao wenyewe wameandika vitu kwenye Snapchat zao na ikaonekana kama ni vijembe ambapo Zari ndio alianza kwa kuandika “Kuna tofauti kati ya Tembo na Mbu” ambapo Hamisa alijibu kwa kuandika “Tembo hana madhara sana kwa Binadamu ila mbu….. kila siku watu wanalazwa”

Haji Manara; kitendo cha Klabu yangu kufungwa kwa penanti ni aibu ya mwaka



Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya Simba SC, Haji Manara amefunguka na kusema kitendo cha klabu yake ya Simba jana kufungwa kwa njia ya penati na kuondolewa kwenye michuano ya Azam Sports Federation Cup ni aibu ya mwaka.
Haji Manara alisema hayo jana baada ya waliokuwa mabingwa watetezi wa (Azam Sports Federation Cup) Simba kupigwa na Green Warriors na kuondolewa katika michuano hiyo kwa penati 4-3
"Shame!! Aibu!!!Fedheha!!! Haivumiliki!!!Tumewakera fans wetu zaidi ya twenty millions... nimeumia kuliko siku zote toka nimeanza kazi Simba..Aibu ya mwaka" aliandika Haji Manara

Mtoto aliyefanyiwa upasuaji mara 10 aomba msaada kunusuru maisha yake




Uzinduzi wa kampeni ya Tuko Pamoja, Okoa Maisha ya Mariam imezinduliwa leo jijini Dar es salam huku ikilenga kuarifu Umma wakiwemo wadau kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuhusu msichana mdogo Mariam (16) anayesumbuliwa na ugonjwa ujulikanao kama ”Intestinal Obstruction”.
Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi masoko wa DataVision International, ambaye pia ni Msemaji wa Dar24, Teddy Ntemi Qirtu katika ukumbi wa Serena amesema kuwa uzinduzi huo unalenga kuokoa maisha ya Mariamu na kuwaomba watanzania kwa ujumla kuhusika katika kampeni hiyo kwa kuchangia kwa namna moja au nyingine ili pamoja kuokoa maisha ya msichana huyo.
Aidha Qirtu amewaomba wananchi na wadau kwa ujumla kumchangia mtoto Mariam ili aweze kwenda nchini India kufanyiwa matibabu, mara baada ya jitihada za madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Muhimbili kushindwa kutatua tatizo hilo na kupelekea kumfanyia oparesheni kumi bila mafanikio.
''Gharama za kuratibu shughuli nzima ya matibabu hayo akiwa nchini India ni kiasi cha shilingi milioni 44 za kitanzania'' alisema
Hivyo amewaomba wananchi kuungana na Dar24 kupigania maisha ya Mariam kwa kuchangia fedha kupitia M-lipa, tigo pesa, Airtell Money na Mpesa kwa kuandika namba ya kampuni 400700 na kumbukumbu namba 400700 au kupitia akaunti ya benki ya CRDB kwa akaunti namba 0150021209500 jina la akaunti ni Data Vision International – Tuko Pamoja.
Kupitia vyomba mbalimbali vya habari amewashukuru wale ambao tayari wamekwisha wasilisha michango yao kupitia mfumo maalumu wa M-lipa kama ambavyo imeelekezwa na kuwaomba wadau kuendelea kuchangia kampeni hiyo inayolenga kuokoa maisha ya Mariam ambae kwa sasa anashindwa kuendelea na masomo.

Vigezo anavyotumia mwanamke kupenda



Watu wengu hujisikia vizuri wanapowavutia wenzao wa jinsia nyingine. Je, unafikiri ni kitu gani kinachomfanya mwanamke aonekane wa kuvutia?
Kuna vitu vingi vinavyojulikana vizuri zaidi kwa upande wa mwanamke kama vile; mwili mzuri, sauti yenye mvuto, nywele, mikono mizuri na mengineyo mengi. Lakini, kuna vingine ambavyo siyo vya kawaida vinavyohusu mwanaume kumvutia mwanamke.
Je, ni vitu au mambo gani ya kipekee ambayo, humfanya mwanamke aguswe na mwanaume fulani na huku mwanamke mwingine akishangaa ni kwa nini mwanamke mwenzake ameguswa sana na huyo jamaa?
Inawezekana yapo mengi ambayo, huyajui. Kwa mfano, mwanamke anaweza akavutiwa na jina la kwanza au la ukoo la mwananume fulani. Hapa mwanamke hufikiri kwamba, huyo mwenye hilo jina hawezi kuwa mtu wa kawaida, na kila kitu anachofanya ni lazima kiwe cha ajabu.
Labda ni kutokana na jina hilo kuwa ni la kigeni au anatoka kwenye ukoo ambao ni bora au wa kipekee au anafikiri labda huyo mwanaume atamwezesha kile ambacho, mara nyingi amekuwa hakipati.
Lakini, inawezekana kabisa kwamba, mwanamume huyo si mzuri sana wa kuvutia au ni mbaya sana kuliko wengine. Hakuna anayejua, labda anachotaka mwanamke huyo ni kujaribu bahati yake ili aone kitakachotokea kwa uhakika ziadi.
Inawezekana pia kuwa, mwanamke anaweza kuchanganyikiwa zaidi baada ya kuona umbo la mwanamume huyo au gari lake. Pengine mambo hayo ndiyo ambayo, amekuwa akiyapenda zaidi. Inawezekana ikawa ni dalili ya bahati kwake kwamba, ametokea katika maisha yake mtu ambae, kwa muda mrefu amekuwa akitamani kumpata.
Upo uwezekano pia kwamba, mwanamke akavutiwa na mwandiko au sahihi ya mwanamume fulani. Wakati mwingine mwanamke hutokea kuwa na uhakika zaidi na kuamini yale anayoambiwa kuhusu tabia ya mwanaume huyo, bila hata kufanya uchunguzi wa kina. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, upo uwezekano wa kuisoma tabia ya mwanaume huyo kwenye sahihi au mwandiko wake.
Mwanamke pia huvutiwa na lafudhi ya mwanamume, fani yake, hobi, na kitu kingine kisicho cha kawaida ambacho mwanamume huyo anakipenda na kukifanya. Hata hivyo, mwanamke anatakiwa awe mwangalifu mno na upande wa pili wa mtu huyo ambao, yeye haujui. Hapa ikiwa na maana kuwa , pamoja na sifa zote hizo alizozibaini kutoka kwake, anapaswa kujua kwamba, mwanamume huyo kama binadamu asiyekamilika pia ana mapungufu na udhaifu mwingi.
Kuufahamu ukweli huu, kutamsaidia katika kuimarisha zaidi na kumfanya awe makini anapotafuta mwanaume wa kuishi naye. Na akumbuke kuwa, wapo wanaume ambao huficha makucha yao au kasoro zao kwa wapenzi wao.
Kuna mwanamke mwingine hupenda mwanaume mwenye vituko, kilema au mwenye kasoro nyingine za kimwili. Yote hayo hutokana na asili ya mwanamke. Na ni mambo yanayoongea ndani mwake kwamba, anataka kumjali na kumhurumia mwanaume huyo.
Kwa kawaida, mwanamke huvutiwa zaidi na kwa urahisi, pale mwanaume anapoonyesha tabia ya usikivu na utulivu. Hata hivyo, mtazamo huu kwa upande wa mwanamke, huhesabika kuwa ni ushindi kwake.
Hali kadhalika, mwanamke huvutiwa na tabia fulani ya kipekee ambayo, mwanaume anayo. Kwa mfano, jinsi mwanaume huo anavyoutumia mkono wake wa kushoto, kwani watu wengi wanatumia mkono wa kulia. Ukweli ni kwamba, labda huyo ndiye mwanaume ambae mwanamke huyo anamtaka, kwani pia wanawake wengine hawawezi kujizuia kuwapenda wanaume wenye macho ya bluu. Hilo pia ni jambo la kawaida.
Mwanamke anaweza kumpenda mwanaume kutokana na jinsi anavyofanya kazi za nguvu au kutokana na mwili wake kuwa na misuli. Ni jambo la kawaida kwa wanawake kufurahia wanaume waliojazia, na inavyoonekana wanawake huwaona wanaume ambao ni lainilaini kuwa wana haiba ya kike au ni mashoga.
Hapo ndipo mwanamke anapolazimika kufikiria kwa makini, kuhusu mwanaume anayetumia muda mwingi kujipodoa na fedha nyingi kwa mambo ya urembo na vipodozi kuliko hata mwanamke, kama kweli anamvutia na anamfaa.
Na kitu kingine ni kwamba, mwanamke humpenda mwanaume anayesaidia kufanya kazi za nyumbani. Kwa kufanya hivyo, mwanamke huamini kwamba, mwanaume huo anamjali na kumthamni.
Kwa kumalizia ni kwamba, mambo mengi yanayomchanganya mwanamke kuhusiana na mwanaume anayemtaka, kwa kweli ni ya kipekee sana na wakati mwingine huonekana kuwa ni kituko, ingawa wakati mwingine yanaweza yakaeleweka vizuri. Mara nyingi vigezo hivyo huonekana kuwa sahihi, iwapo tu mwanamke huyo atajisikia vizuri na kupata ridhiko la nafsi yake.

Friday, 22 December 2017

Tanzania yapolomoka katika viwango vya FIFA



TANZANIA imezidi kuporomoka katika viwango vya soka vinavyotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambapo hivi sasa inashika nafasi ya 147 kutoka 142 ya mwezi Oktoba.
Jana Alhamisi, Fifa ilitoa viwango hivyo ambapo inaonyesha ndani ya miezi mitano kuanzia Julai, mwaka huu, Tanzania imeshuka kwa jumla ya nafasi 33.
Ikumbukwe kuwa, kwa siku za hivi karibuni, Tanzania ilifanya vizuri kwenye viwango vya Juni baada ya kushika nafasi ya 114 kutoka nafasi ya 139 ya mwezi Mei. Baada ya hapo, Julai ikashika nafasi ya 120, Agosti 125, Septemba 136, Oktoba 142 na sasa Novemba ni 147.
Kushuka huko kwa Tanzania kunatokana na Novemba, mwaka huu, Taifa Stars kutoka sare ya bao 1-1 na Benin katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa l’Amitie, Benin.
Katika 10 Bora ya duniani, Ujerumani inaongoza ikifuatiwa na Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Hispania, Poland, Uswisi, Ufaransa na Chile.

Waziri Kigwangalla kuwakutanisha Joketi Na Wema Sepetu





Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla jana Desemba 21, 2017 aliteua majina mengine ya Kamati ya Kitaifa ya kuandaa mwezi maalum wa maadhimisho ya Urithi wa Tanzania. Miongoni mwa wajumbe walioteuliwa ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jokate Mwegelo na Wema Sepetu ambao wataungana na wajumbe 23 aliowateua awali kuunda Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Mwezi Maalumu wa Maadhimisho ya Urithi wa Tanzania.

Mashindano Ya Miss Tanzania kutokuwepo 2017



WAANDAAJI wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, Kampuni ya Lino International Agency Limited, wamesema kwamba hakutakuwa na Fainali za Taifa za shindano la Miss Tanzania kwa mwaka 2017.
Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo leo imeeleza kuwa sababu kubwa ya kuahirishwa kwa shindano hilo ni ukosefu wa Wadhamini ambao kwa njia moja au nyingine huwezesha kufanyika kwa mashindano hayo kwa kulipa gharama mbalimbali ikiwemo zawadi za washiriki.
Aidha waandaaji hao pia wamesema kuwa kuchelewa kupata kibali cha kuanza mchakato wa Miss Tanzania 2017, ambacho kilitolewa na BASATA mwezi Septemba mwaka huu pia kimechangia kukosa kwasababu muda ulikuwa umeshaenda.
Mashindano ya kutafuta warembo wa Miss Tanzania yamekuwa yakifanyika kila mwaka na baadae kuibua mastaa mbalimbali kama Wema Sepetu, Lulu Diva, Jokate Mwegelo na wengine