Saturday, 23 December 2017

Watu 22 wahofiwa kufa maji na 115 kuokolewa Ziwa Tanganyika



Watu 22 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tanganyika katika ajali ya boti iliyotokea iliotokea leo alfajiri.
Imeelezwa miili ya watu wanne imeopolewa na imetambuliwa na ndugu zao huku watu wengine 115 wameokolewa wakiwa hai baada ya boti kugonga mtumbwi.
Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Kigoma, Amaniel Sekulu amesema ajali hiyo imetokea katika kitongoji cha Lubengela kijijini Msihezi, Kata ya Sunuka wilayani Uvinza.
Amesema mtumbwi uitwao Mv Pasaka uligongwa ubavuni na boti ya Atakalo Mola na kupasuka, hivyo kuzama ziwani.
Sekulu amesema mtumbwi ulikuwa umebeba abiria 137 waliokuwa wanakwenda kwenye mkutano wa injili katika Kijiji cha Sunuka.
Amesema boti ilikuwa ikitokea Kigoma kwenda Kalya ikiwa imebeba abiria 65.
Sekulu amesema boti na mitumbwi inayobeba abiria hairuhusu kufanya safari usiku.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Sweetbert Njewike akizungumzia ajali hiyo amesema wanaendelea kuwatafuta watu ambao hawajaonekana waliokuwa wakisafiri na vyombo hivyo.
Amesema shughuli za uokoaji zinafanywa kwa pamoja na vikosi vya Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kulikuwa na dosari zilizosababisha ajali hiyo.
Amezitaja dosari hizo kuwa ni ukosefu wa vifaa vya uokoaji, vifaa vya kuzima moto na boti kufanya safari usiku.
Diwani wa Sunuka, Athumani Chuma amesema ajali hiyo imeacha simanzi kutokana na mazingira iliyotokea.
Amesema licha ya ajali kutokea saa tisa usiku, wanakijiji wameonyesha mshikamano katika kuokoa watu wakiwa hai na hatimaye kuopoa maiti nne.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msihezi, George Gasper amesema ajali ilitokea umbali wa mita takriban 150 kutoka ufukweni, ikiwa ni muda mfupi baada ya boti la Atakalo Mola kushusha na kupakia abiria katika Kitongoji cha Lubengela.
Desemba 20, watu saba walikufa papohapo na wengine 12 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Saratoga kugongana uso kwa uso na gari ndogo la abiria.
Ajali hiyo imetokea saa 4:30 asubuhi katika Kijiji cha Kabeba katani Mwakizega wilayani Uvinza.

No comments:

Post a Comment